Wednesday, May 14, 2014

TAARIFA KWA UMMA


1.    UTANGULIZI:

Kufuatia kutokea madhara makubwa ya watu kupoteza maisha na kuharibu
miundombinu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Taasisi ya
Wahandisi Tanzania iliitisha mkutano wa wazi wa wahandisi tarehe 17
Aprili, 2014 jijini Dar es Salaam ili kujadili hatua za dharura za
kupunguza madhara ya mafuriko hayo.

 Mkutano huo ambao ulifanyika kwenye
ukumbi wa Luther House, vile vile ulijadili  msongamano wa magari jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kushauri namna ya kupunguza madhara ya
msongamano huo kwenye uchumi wa nchi na kero kwa wakazi wa jiji. Baada ya
majadiliano ya kitaalamu, washiriki walizingatia mambo yafuatayo na
kuyatolea mapendekezo.

2.    MAFURIKO KUTOKANA NA MVUA
2.1    Mambo ya kuzingatia

è    Washiriki wamesikitishwa sana na madhara yaliyotokana na mvua na
kusababisha vifo vya watu na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.
Aidha wahandisi walitoa pole kwa wafiwa na waathirika wengine na mafuriko
hayo.

è    Washiriki walizingatia  na kupongeza juhudi zinazofanywa na viongozi na
wahandisi wa TANROADS na Shirika la Reli katika kuhakikisha kwamba madhara
ya mafuriko yanapunguzwa kwa kiasi kikubwa ili kunusuru maisha ya watu na
uchumi kwa ujumla.

è    Ingawa mafuriko makubwa ya mvua ni tukio la asili, vitendo vya wanadamu
vinaweza kuongeza au kupunguza madhara yake. Hii ina maana kwamba madhara
ya mafuriko yanayoendelea kuikumba nchi yetu yanaongezeka kutokana na
vitendo vya watu katika maeneo yafuatayo;

    Kilimo kwenye miteremko na ukataji miti ovyo.

    Ujenzi holela kwenye mikondo ya asili ya maji.

    Usanifu hafifu wa miundombinu na hasa barabara na madaraja ambayo
wakati mwingine hujengwa bila matoleo ya maji.

    Ukosefu wa matengenezo ya kinga (preventive maintenance) kwenye
miundombinu.

    Utupaji taka na/au uchimbaji mchanga kwenye mito hasa sehemu za
madaraja.

    Uzuiaji wa maji ya mvua kuingia baharini kutokana na ujenzi
holela kwenye fukwe.

2.2    MAPENDEKEZO

Njia bora ya kukabiliana na matukio ya asili ni kujiweka tayari kupambana
wakati wote. Hivyo basi, madhara ya mafuriko yanayoendelea yanaweza
kupunguzwa kwa kufanya yafuatayo;

è    Kutoa elimu kwa wananchi wote juu ya umuhimu wa kulinda mazingira.
Inatakiwa tufike mahali ambapo hata wale wasioishi mabondeni wajue kwamba
kuzibwa kwa njia za asili za maji kutawaathiri pia. Kama jamii haitapata
mwamko huo, watu wataendelea kulima kiholela kwenye miteremko, kutupa
takataka kwenye mito na mitaro ya kusafirisha maji na kujenga makazi na
majumba ya biashara kwenye njia za asili za kupeleka maji baharini.

è    Sheria ziheshimike na kila mtu na zisimamiwe ipasavyo na wahusika.
Hakuna shaka kwamba zinapojengwa barabara, wakorofi wanaokaidi kupisha
ujenzi huo kuvunjiwa nyumba zao bila huruma. Lakini wale wanaojenga kwenye
mabonde ya kupitisha maji na kutozingatia michoro ya mipango miji,
hawaguswi isipokuwa kuombwa tu na inapofika wakati wa mvua serikali
hutumia fedha nyingi kuwahudumia.

è    Miiko ya kazi na taaluma vizingatiwe. Wahandisi na mafundi kote nchini
wafanye kazi kwa uadilifu na kuzingatia mahitaji ya taaluma na utunzaji wa
mazingira. Wahandisi na mafundi wasikubali kujenga majengo kwenye mikondo
ya asili ya maji na kwenye maeneo ya fukwe za bahari yanayozuia kutiririka
kwa maji kuingia baharini.

è    Wahandisi wa miji na wale wa halmashauri za Wilaya wajengewe uwezo siyo
tu wa kitaaluma na vifaa, bali pia nyenzo za kupambana na majanga ya asili
kama mafuriko, vimbunga na kadhalika.

è    Serikali za mitaa na vijiji ziwajibike kusimamia mipango miji na usafi
wa mazingira. Uzoefu unaonyesha kwamba kwa kiasi kikubwa viongozi wa
serikali hizo ndiyo mawakala wakubwa wa wakorofi wachache wanaovamia
maeneo ya wazi na hivyo kusababisha misongamano ya makazi. Misongamano ya
makazi huzuia mtiririko wa maji na hatimaye kusabisha mafuriko.

è    Waandishi wa habari wana machango mkubwa katika masuala haya. Badala ya
kutangaza kwa nguvu na kwa wingi matukio ya mafuriko peke yake, waandishi
wajitahidi  vile vile kutangaza kwa nguvu na wingi ule ule njia
zinazopendekezwa na wataalamu za kuepukana na matukio hayo.

3.    AZIMIO

Katika maadhimisho ya WIKI YA WAHANDISI mwaka huu (Septemba 21 - 26,
2014), wahandisi kote nchini watashirikiana na wataalamu wa mipango miji
na wale wa ardhi kutembelea maeneo mbalimbali ili kupata ufumbuzi kuzibwa
kwa mikondo ya maji KAULI MBIU YA MWAKA HUU NI UTUNZAJI WA MAZINGIRA
KUEUPUSHA MAJANGA.

4.    MSONGAMANO WA MAGARI JIJINI DAR ES SALAAM

Washiriki walizingatia kukithiri kwa msongamano wa magari jijini Dar es
Salaam na madhara yake kwenye maisha ya watu na uchumi wa taifa. Baada ya
majadiliano, washiriki waliazimia kama ifuatavyo ;

è    Wahandisi kupitia Taasisi ya Wahandisi Tanzania watawasilliana na
kushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani ili kuimarisha namna bora
zaidi ya kuongoza magari kwa lengo la kupunguza makali ya msongamano.

è    Wizara ya Ujenzi iungwe mkono na kila madau wa maendeleo kuhakikisha
kwamba barabara za mzunguko (Ring roads) zinajengwa haraka iwezekanavyo.

è    Wizara ya Ujenzi itenge dawati la taaluma ili afisa wa dawati hilo aweze
kupokea na kuwasilisha kwa viongozi wakuu wa Wizara mapendekezo mbali
mbali ambayo hutolewa na taasisi za kitaaluma kukabiliana na matatizo
mbali mbali. Taasisi hizo ni pamoja na IET, ERB, CRB, TARA, AQRB, TIQS na
kadhalika. Aidha afisa huyo atakuwa kiungo kati ya Wizara na Taasisi hizo
katika masuala ya kitaaluma.


Taarifa imetolewa na;
Eng. Dkt. Malima M.P. Bundara
Rais, IET
11 Mei 2014

No comments:

Post a Comment