Sunday, July 27, 2014

MKUU WA MKOA WA RUKWA ENG. STELLA MANYANYA AFUTURISHA WAISLAMU MKOANI HUMO

Tunaomba radhi kwa ubora hafifu wa picha hii. Kulia ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kupitia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Rashid Akililimali akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya kushoto muda mfupi baada ya futari iliyoandaliwa na Mkuu huyo wa Mkoa katika viwanja vya ofisi yake Mjini Sumbawanga tarehe 26/07/2014.

Katika salamu zake Sheikh huyo alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi wake wa kuwaunganisha Waislamu wa Mjini Sumbawanga katika futari hiyo ambayo ilihudhuriwa na waumini zaidi ya 70. Aliwaomba wabunge wa Bunge Maalum la Katiba waliosusia bunge hilo kupitia kiongozi huyo wa Mkoa kurudi bungeni kwa ajili ya kuwatengenezea wananchi Katiba wanayoisubiri kwa hamu.

"Toka mmeanza bunge hili la katiba naskia Serikali tatu, Serikali mbili mara moja mara mkataba lakini sjaskia mkijadili mambo ya kiuchumi au ya kijamii ambayo yanamgusa mwananchi moja kwa moja......" Alisema Sheikh Akilimali kumwambia Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya.

Aliwaomba wabunge wote wa UKAWA kurejea bungeni kutengeneza katiba ambayo itabadilisha maisha ya watanzania waweze kuondokana na umaskini na kupata maisha bora tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo wamekua wakijadili mivutano ya kisiasa pekee.

Kwa upande mwingine shekhe huyo aliwataka wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuishi kwa amani, ushirikiano na upendo baina yao katika kuuletea Mkoa maendeleo kwa kuweka pembeni tofauti zao za kiitikadi za kisiasa, dini hata ukabila.

 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya alishukuru kwa ushirikiano anaoupata kutoka kwa viongozi wa dini Mkoani humo na kuwataka waendelee kuudumisha kwa maslahi ya Mkoa na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment