Wednesday, August 6, 2014

UONGOZI WA MKOA WA RUKWA WADHAMIRIA KUFUNGUA UTALII "KALAMBO FALLS"

Kaimu Afisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Kalambo Ndugu Makwasa Biswalo (katikati) akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya eneo lililopimwa katika kijiji cha Kapozwa kwa ajili ya kuendeleza Utalii katika Kijiji hicho ambacho kina maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls), maporomoko ambayo ni ya pili kwa urefu barani Afrika yakiwa na urefu wa mita 235. 

Uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Eng. Stella Manyanya umeonyesha jitihada za makusudi kuhakikisha unafungua fursa za utalii katika maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls) ambayo ni maporomoko ya pili kwa urefu barani Afrika yakiwa na urefu wa mita 235.

Maporomoko hayo ambayo yanahitaji kuwekewa mazingira mazuri kuvutia watalii wa nje na wa ndani yapo mpakani mwa Tanzania na Zambia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na yanafikika katika umbali usiozidi Km 110 kutoka katikati ya makao makuu ya Mkoa wa Rukwa ambayo ni Manispaa ya Sumbawanga.  

Zipo jitihada kadhaa zilizokwishafanywa na uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Eng. Stella Manyanya katika kuhakikisha eneo la maporomoko hayo linaimarishwa na kuwa kivutio kikubwa cha utalii na chanzo cha mapato kwa halmashauri husika na taifa kwa ujumla. 

Jitihada hizo ni pamoja kuwahamasisha wananchi wa kijiji cha Kapozwa na wadau wengine katika kutambua umuhimu wa maporomoko hayo ambapo mpaka hivi sasa wananchi hao wameshashiriki kufyatua matofali kwa ajili ya kujenga kituo cha utalii katika eneo hilo.

 Jitihada zingine ni zile za kupima viwanja na kuandaa michoro katika eneo hilo ambapo ramani imeshaidhinishwa na tathmini ya kuwafidia wananchi maeneo yao imeshafanyika. 

Aidha zimekuwepo jitihada za kutafuta fedha kutoka Serikalini na kwa wahisani mbalimbali katika kusaidia kujenga na kuimarisha utalii katika maporomoko hayo (Kalambo Falls). Wakala wa Misitu Taznania (TFS) wamesaidia upatikanaji wa kiasi cha fedha (Tsh. Mil. 10) ambazo zitasaidia kufungua baadhi ya mitaa katika eneo liliopimwa na shughuli zingine zitakazohitajika katika eneo hilo.  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya anawaomba wadau wote wa utalii nchini ikiwemo Serikali, Mashirika binafsi, Wawekezaji na Wahisani mbalimbali kuwa na jicho la pamoja katika kuona Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls) yanachukuliwa umuhimu wa pekee wa kuendelezwa na kutangazwa kwa nguvu kwani ni miongoni mwa kivutio kikubwa cha utalii nchini na barani Afrika kwa ujumla. 

Kutokana na maporomoko hayo kuwa mpakani nchi ya Zambia imekuwa ikitumia fursa ya mpaka huo kuendeleza eneo lao la mpakani na kuitangaza Kalambo Falls jambo ambalo likiachwa kwa muda mrefu bila Tanzania kuchukua hatua kama hiyo itapelekea dunia kubaki na picha isiyo sahihi kuwa maporomoko hayo yapo nchini Zambia wakati sehemu kubwa ipo Tanzania na hata muonekano mzuri unapatikana kutokea Tanzania na maji ya mto huo yanatokea Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akiangalia ramani ya viwanja vilivyopimwa katika kijiji cha Kapozwa kwa ajili ya kuendeleza utalii katika kijiji hicho cha mpakani na nchi ya Zambia yalipo maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). Mkuu huyo wa Mkoa alikabidhiwa ramani hiyo na Kaimu Afisa Ardhi na Maliasili Wilaya ya Kalambo Ndugu Makwasa Biswalo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya na Meneja wa Misitu Wilaya ya Sumbwanga na Kalambo Ndugu Martin Hamis wakipanda mti wa kumbukumbu katika eneo lililopimwa la kijiji cha kapozwa kwa ajili ya kuendeleza utalii wa maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya na wapimaji wa ardhi kutoka chuo cha Ardhi Morogoro walioshiriki na wataalamu wa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kupima ardhi ya kijiji cha Kapozwa kwa ajili ya kuendeleza utalii wakiangalia Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls).
  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akifurahia jambo na Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Bi. Mapinduzi Severian katika maporomoko ya mto Kalambo. Nyuma yao anaeimarisha usalama ni WP Lucy. 
Sehemu ambayo ni nusu ya maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). 
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akiangalia bonde la maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls).
Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Bi. Mapinduzi Severian akiangalia bonde la maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls).
Sehemu ya jitihada za wananchi wa kijiji cha Kapozwa ambao wamefyatua matofali kwa ajili kujenga kituo cha utalii kwa ajili ya maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls).
Sehemu ya mchoro kwa ajili ya kujenga kituo na geti la utalii katika maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls). Jitihada hizi zimefanywa na uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Eng. Stella Manyanya.
Vijana wa nchi jirani ya Zambia wakiwa wanapunga upepo kandokando ya maporomoko ya mto Kalambo. Upande wa nyuma zinaonekana ngazi maalum ambazo ni sehemu ya miundombinu iliyojengwa na Serikali ya Zambia kuwavutia watalii katika eneo hilo. Serikali ya Tanzania ina changamoto kubwa ya kuhakikisha eneo hilo muhimu la utalii linaendelezwa ili kulijengea umiliki halali tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo inaonekana limetelekezwa kwa muda mrefu.
Mara baada ya wanahabari hawa kupata picha za habari ilikua ni fursa mwanana kwao kupata picha za viganjani (simu) kwa ajili ya matumizi ya whatsapp, facebook, twiter n.k. Kama inavyoonekana pichani Bwana Brown Tawa akimpiga picha kwa kutumia simu ya mkononi mwandishi mkongwe nchini ambaye pia hujiita Askofu wa Kanisa la kujitegemea Ndugu Nswima Errrrrrrrnest wa TBC Rukwa. 
Sehemu ya bonde ambalo ni maangukio ya maji ya mto Kalambo yanapotengenezwa maporomoko (Kalambo Falls).

No comments:

Post a Comment