Sunday, September 14, 2014

MKUU WA MKOA WA RUKWA ENG. STELLA MANYANYA AIBUKA NA MBINU MPYA KUPUNGUZA VIFO VYA KINAMAMA WAJAWAZITO MKOANI HUMO

WATENDAJI wa Serikali kuanzia ngazi za wilaya, tarafa na kata mkoani Rukwa wamekula kiapo mbele ya mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Stella Manyanya kwamba wapo tayari kuwajibika iwapo katika maeneo yao ya utawala kitatokea kifo cha mama mjamzito kitakachosababishwa na uzembe
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya akisisitiza jambo jana katika kikao cha kuweka mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito, sambamba na kuhimiza jamii kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) kilichowajumuisha wananchi, wakunga wa jadi,watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya kata, tarafa, wilaya na mkoa ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga. 

Kiapo hicho wamekula jana mara baada ya kikao cha siku nzima kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito, sambamba na kuhimiza jamii kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) kilichowajumuisha baadhi ya wananchi, wakunga wa jadi na watendaji hao wa serikali kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga mjini hapa

Watendaji wa Serikali waliokula kiapo hicho ni wakurugenzi wa halmashauri, maofisa tarafa na watendaji wa kata ambao wana jukumu la kuhakikisha hakuna mama mjamzito ambaye itatokea anafariki dunia kutokana na sababu ambazo zinaweza kuzuilika kwenye maeneo yao

"tumedhamiria kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito.....na hilo linawezekana sasa kuna mikakati tumejiwekea kama mkoa ya kuhakikisha tunafuta vifo vyote vinavyotokana na uzembe wa watawala wa eneo husika au wataalam wa idara ya afya, hatutaki kusikia mama mjamzito ameshindwa kufikishwa kituo cha afya au hospitali kwa sababu ukosefu wa gari ya kubeba wagonjwa au kitu kingine ambacho kipo ndani ya uwezo wa utawala" alisema Manyanya

Baadhi ya viongozi wa Serikali na wadau wengine wa maendeleo wakifuatilia kwa makini mada katika kikao hicho.

Manyanya aliongeza kuwa iwapo kitatokea kifo uchunguzi utafanyika na ikibainika kulikuwa na uzembe uliosababishwa na mtendaji yoyote kati ya hao waliokula kiapo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufukuzwa kazi ili we fundisho kwa watendaji wengine

Pia Manyanya alisema kuwa mkoa unajipanga kuona uwezekano wa kuwapatia simu za mkononi wakunga wa jadi ambao watawasiliana na wataamu wa afya na watawala wa eneo husika ili wafike kuwachukua wajawazito wanakwenda kwao kujifungulia badala ya kwenye vituo vinavyotoa huduma ya afya

Awali, Kaimu Mganga mkuu wa mkoa, Emmanuel Mtika alisema kuwa tangu januari 2014 hadi mwezi agosti kumeripotiwa kutokea vifo vya wajawazito 33 hali ambayo inasababishwa na changamoto kadhaa ikiwemo matumizi ya dawa za asili kwa wajawazito ili kuongeza uchungu wakati wa kujifungua hivyo kusababisha kizazi kufumuka na kupasuka sambamba na upungufu wa wataalamu wenye ujuzi

Naye, Gasper Materu ambaye ni mratibu wa mradi wa Wazazi na Mwana ulio chini ya mashirika ya Africare, Jhpiego na Plan International wenye lengo la kupunguza vifo vya wajawazito katika mkoa huo kwa asilimia 75 ifikapo mwakani
Mratibu wa mradi wa Wazazi na Mwana ulio chini ya mashirika ya Africare, Jhpiego na Plan International, Gasper Materu akitoa mada katika hicho.

Alisema kuwa  mradi huo umefanya kazi kubwa ikwemo kutoa elimu kwa wahudumu wa afya vijijini wapatao 3032 katika vijiji 288 ambao wanawajibu wa kutembelea kaya zilizopo katika maeneo yao ili kuwaelimisha wakina mama wajawazito kuhusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki kwa ajili ya kupata elimu ya afya ya uzazi kabla na baada ya kujifungua

Materu aliongeza kuwa kupitia mradi huo umetoa gari la wagonjwa katika vituo vya afya Mtowisa na Wampembe maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki kirahisi hivyo wajawazito wengi kupoteza maisha kutokana na umbali ili waweze kufikia hospitali kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua

Takwimu zinaonyesha kwamba kwa mkoa wa Rukwa wakinamama wajawazito 138 kwa wastani wa 100,000 ufariki kila mwaka kutoka na matatizo ya uzazi. (Habari hii ni kwa hisani ya pembezoni kabisa blog)

No comments:

Post a Comment