Tuesday, March 31, 2015

TUME YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (TCRA) KUZIMA MFUMO WA ANALOJIA LEO MACHI 31, SUMBAWANGA TELEVISION (STV) KUTOONEKANA TENA KUPITIA ANTENNA

Uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ya mfumo wa analojia kwa awamu ya kwanza ulianza kutekelezwa nchini tarehe 31/12/2012 saa sita kamili usiku katika jiji la Dar es Salaam kwa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Uzimaji ulindelea hadi mwisho wa mwezi wa nne 2013 katika miji ya Dodoma, Tanga, Mwanza, Moshi, Arusha na Mbeya. Uzimaji huu ulikuwa ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya uzimaji mitambo ya analojia kulingana na ratiba iliyotolewa na Serikali mnamo mwezi Desemba 2012 kuhusu mji saba tajwa hapo juu.
Baada ya kukamilisha utekelezaji wa awamu ya kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikamisheni kwa wataalam wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya tathmini ya mchakato mzima wa uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa kidijiti pamoja na uzimaji wa mitambo hiyo kwenye miji saba tajwa hapo juu kabla ya kuanza awamu ya pili.
Matokeo ya tathmini hii yameonyesha wananchi wameupokea vyema mfumo wa utangazaji wa kidijiti na hivyo kupelekea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Serikali kuridhia kufanyika kwa awamu ya pili ya uzimaji mitambo ya analojia.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Serikali mnamo mwezi February, 2014, Awamu ya Pili ya uzimaji wa mitambo ya analojia ulianza kwenye miji ya Singida na Tabora mwishoni mwezi wa tatu wa tarehe 31 Machi, 2014 wakati ambapo miji mingine mitatu ilifata katika zoezi la uzimaji wa mitambo ya analojia ambayo ni Musoma, Bukoba, na Morogoro. Miji ya Kahama na Songea ilihusika katika uzinduzi wa mitambo ya dijitali ikizingatiwa kuwa miji hiyo haikuwa na matangazo ya televisheini ya mfumo wa analogia.
Maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia ya utangazaji wa televisheni kwa Mji wa Sumbawanga yamekamilika kwa kuwashirikisha wadau wa sekta ya utangazaji. Mitambo itazimwa saa sita kamili usiku wa tarehe 31 Machi, 2015. Vigezo vinavyotumika kuzima mitambo ya analojia ni pamoja na kuwepo utangazaji wa mfumo wa analojia pamoja na kidijiti kwenye eneo husika, upatikanaji ving’amuzi na uwepo wa chaneli tano za kitaifa kwenye mfumo wa kidijiti.
Elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali kuhusu kuhamia katika teknolojia ya mfumo wa utangazaji wa dijitali imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Matangazo ya dijitali yanawafikia watu asilimia zaidi ya 20% kati ya watu asilimia 24% waliokuwa wanapata matangazo ya televisheni ya analojia.
Kama ilivyoelezwa tangu awali, utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwa maeneo yenye matangazo ya dijitali tu. Maeneo ambayo hayana miundombinu ya dijitali hayatazimwa kwa sasa hadi yapate dijitali.
Mabadiliko haya hayahusu matangazo kwa njia ya utangazaji wa satelaiti, waya (cable) na redio. Tunawataka wananchi wa Mji wa Sumbawanga wasizitupe TV zao za analojia bali wanunue ving’amuzi ili kupata matangazo ya dijitali.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeagiza watoa huduma za kusambaza ving’amuzi walioko Sumbawanga kuhakikisha kuwa kunakuwa na ving’amuzi vya kutosha. Tumefanya ukaguzi katika mji wa Sumbawanga na tumehakikisha viko ving’amuzi vya kutosha na tumehakikishiwa kuwa vingine viko njiani kuja mjini Sumbawanga
Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni wa mfumo wa analojia hapa ili kufanikisha zoezi hili.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Machi, 2015 – Sumbawanga

No comments:

Post a Comment