Tuesday, March 10, 2015

WAKUU WA MIKOA YA RUKWA NA MBEYA WAMTEMBELEA MTOTO BARAKA COSMAS MLEMAVU WA NGOZI ALIYEKATWA KIGANJA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya, Dk. Mpoki Ulisubisya (kulia) akiwaongozwa Wakuu wa Mikoa ya Mbeya (Mhe. Abbas Kandoro) na Rukwa (Mhe. Eng. Stella Manyanya) kuelekea Wodini kumjulia hali Mtoto Baraka Cosmas (6) Mlemavu wa ngozi  aliyekatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao Ikonda tarafa ya Chipeta usiku wa kuamkia juzi tarehe 08/03/2015.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akimuangalia kwa jicho la huruma Mtoto Baraka Cosmas aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana na kutokomea nacho akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Wakuu wa Mikoa ya Mbeya na Rukwa wakimjulia hali Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao Chipeta juzi usiku tarehe 8/03/2015.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya (kushoto) akiongoza sala pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro kuwaombea walemavu wa ngozi  sambamba na viongozi wa Chama cha Albino Mkoa wa Mbeya wakiwa wameinamisha nyuso zao huku wakisali kuwaombea watu wenye ulemavu wa ngozi ili wasipate madhara baada ya kumtembelea  Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi.
Mama mzazi wa mtoto Baraka,Prisca Shabani akiwa na jeraha kichwani baada ya kupigwa na watu waliomkata kiganja mtoto wake kiganja cha Mkono wa kulia, akiwa anawasikiliza wakuu wa mikoa ya Mbeya na Rukwa waliomfika kuwajulia hali katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya wanakopatiwa matibabu.
Mtoto Baraka aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana kijijini kwao juzi akiwa amelala kitandani akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Mbeya.
Waandishi wa habari wakichukua maelezo katika tukio hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akikabidhi zawadi ya pole ya kwa mama wa Cosmas, Zawahi hiyo hiyo ya fedha ilitolewa na wakuu hao wa Mikoa ya Mbeya na Rukwa.
Wakuu wa Mikoa ya Rukwa na Mbeya wakiagana.


 

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kumtembelea Mtoto Baraka Cosmas Mlemavu wa ngozi baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi kufuatia kitendo cha kukatwa kiganja cha mkono na watu wasiojulikana na kutokomea nao.

Mtoto huyo mkazi katika kijiji cha Ikonda kata ya Chitepa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa alihamishiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kukatwa kiganja chake akitokea kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa mama wa mtoto huyo, Prisca Shaban(28) alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa saba usiku tarehe 8/03/2015 alipokuwa anarudi ndani akitokea nje kujisaidia ambapo alivamiwa na mtu ambaye hakumfahamu na kisha akamsukumia ndani kabla ya kumpiga kichwani kwa rungu na kisha kupoteza fahamu.

Alisema akiwa amepoteza fahamu mtu aliyekuwa amemvamia ndipo alipata nafasi ya kuingia ndani na kutekeleza adhma yake ya kumkata kiganja mtoto huyo ambaye ni mmoja kati ya  watoto watatu wenye ulemavu wa ngozi katika familia hiyo na kuondoka nacho.

Alisema wakati hayo yakitokea mumewe aliyemtaja kwa jina la Cosmas Lusambo alikuwa amekwenda kulala nyumbani kwa mke mdogo kwani ilikuwa zamu ya kwenda kulala huko kwa usiku huo lakini baada ya kusikia mayowe ya kuomba msaada alikwenda kuungana na familia yake na kumpeleka mtoto kituo cha afya cha Kamsamba kutokana na kuwa jirani na kijiji chao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya, Akizungumza baada ya kumtembelea Mtoto huyo katika wodi ya watoto kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya, alioneshwa kusikitishwa na tukio hilo na kuahidi kulifanyia kazi usiku na mchana kwa kushirikisha vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili wahusika wapatikane na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema ni tukio ambalo linasikitisha ambalo linazidi kuendeleza vitendo vya aibu kwa kuwafanyia ukatili wa kinyama albino kwa ujinga wa watu wachache wanaowadanganya watu kuwa viungo vyao ni bahati ya kuleta utajiri, Aliongeza kuwa kama viungo vya Albino ni utajiri basi Albino wenyewe wangekuwa matajiri zaidi.

Mhandisi Manyanya mbali na kuzungumza na familia ya waathirika wa janga hilo pia aliongoza sala fupi ya kuwaombea walemavu wa ngozi hospitalini hapo akioynesha pia kusikitishwa na mwenendo wa mashitaka ya watu waliofanya ukatili dhidi ya albino akisema mahakama zimekuwa na milolongo mirefu inayokatisha tamaa wadau wa kupinga ukatili huo.

Mkuu huyo wa mkoa alishauri pia kuangaliwa upya kwa sheria inayohusu masuala ya hukumu za kifo akisema ikibidi inapaswa kubadilishwa ili iweze kutoa haki kwa watu wanaofanya ukatili dhidi ya wenzao.

Alisema sheria ya sasa kumtaka rais pekee kuwa mtu wa mwisho kutoa uamuzi kunyongwa kwa mtu aliyehukumiwa inakosa nguvu ya kutekelezwa kutokana na jukumu hilo kuwa mikononi mwa mtu mmoja ambaye Mhe. Rais ambaye anatakiwa kusaini hukumu hiyo kabla ya utekelezaji na kushauri kuwa ni vyema vyombo vya sheria vipewe mamlaka ya mwisho ya kutekeleza adhabu hiyo.

Ushauri mwingine alioutoa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ni kujengwa kwa vituo maalum kwa ajili ya kuwahifadhi walemavu wa ngozi ambao wanaonekana kuwepo katika mazingira hatarishi waweze kupatiwa ulinzi ambapo wananchi pamoja na Serikali yao na wadau mbalimbali wa maendeleo watachangia katika kuendesha vituo hivyo.

Alimalizia kwa kusema kuwa tatizo kubwa ni elimu kwa wahusika wa vitendo hivo ambapo amewaasa wananchi na wadau husika kupiga vita imani hizo na kutoa elimu zaidi kwa jamii jamii kufuta imani hizo za kishirikina.

No comments:

Post a Comment