Thursday, April 2, 2015

WADAU WA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA MATIBABU MKOANI RUKWA WAPEWA ELIMU YA UTARATIBU WA MIKOPO MBALIMBALI INAYOTOLEWA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akichangia na kufunga Semina maalum ya siku moja iliyoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwaelimisha wadau wa vituo mbalimbali vya kutolea huduma za matibabu Mkoani Rukwa juu utaratibu wa Mfuko huo katika kutoa mikopo ya vifaa tiba, dawa na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za matibabu. Lengo kuu la utaratibu huo ulioanzishwa na Mfuko wa Bima ya Taifa ni kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake na watanzania kwa ujumla. Semina hiyo imefanyika leo tarehe 02/03/2015 katika ukumbi wa RDC Mkoani Rukwa, Ndugu Pangisa amewaasa wadau hao kuchangamkia fursa hiyo kuimarisha huduma katika vituo vyao.
 Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Rukwa Ndugu Abdiel Mkaro akizungumza katika semina hiyo. Ndugu Mkaro alisema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeanza utaratibu wa kuwakopesha wadau mbalimbali wanaotoa huduma za matibabu Mkoani Rukwa, lakini jambo la kushangaza wengi wao wamekuwa hawatumii fursa hiyo vizuri kwani baadhi yao wamediriki hata kutofuatilia maombi yao na kutelekeza barua zao ambazo wameshakubaliwa. Aliwaasa wadau hao kutumia fursa hiyo ili kuboresha huduma katika vituo vyao.
Mtoa mada mkuu katika Semina hiyo ndugu Yesaya Irira (Kulia) ambaye ni Afisa Mipango na Uwekezaji Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Makao Makuu akizungumza katika Semina hiyo ambapo amesema mikopo hiyo inatolewa kwa vituo vyote vya Serikali, vya Binafsi na vya Kidini kwa kigezo kikuu kuwa kituo hicho kiwe kimesajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutoa huduma kwa wanachama wake. Aliongeza kuwa miongoni mwa taratibu za kupewa mkopo ni pamoja na Mkopaji kujaza fomu ya maombi ambapo kiwango cha Mkopo kitategemea wastani wa madai ya kituo kwa huduma zitolewazo kwa wanachama wa Bima ya Afya ambayo pia yatakuwa dhamana kuu ya Mkopo husika katika madai ya kila mwezi. Kwa Mkopo unaozidi Milioni tano Mkopaji atatakiwa kuweka dhamana yenye thamani ya mkopo na kwa upande wa mkopo wa kifaa tiba hufanyika kuwa dhamana ya mkopo mpaka marejesho ya Mkopo yatakapokamilika.
 Dkt. Dunstan Tendwa, Afisa Mhakiki wa Ubora wa Huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Rukwa akiwa na wadau wengine walishiriki semina hiyo.
 Wadau kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia semina hiyo.
 Bi Safi Julius, Afisa Mipango na Uwekezaji Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na wajumbe wengine waliohudhuria semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa RDC Mkoani Rukwa.
 Sehemu ya wajumbe katika semina hiyo.
Sister Helena Katebela wa Kituo cha Afya Katandala akiuliza swali katika Semina hiyo. Alitaka kujua endapo dawa anazohitaji Mkopaji hazipo kwa wakala wa usambazaji ambaye ni MSD itakuwaje? Alipata jibu kuwa mkopaji huyo ataelekezwa kwa msambazaji mwingine aliyejiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afta tofauti na MSD.

No comments:

Post a Comment