Tuesday, August 30, 2016

Mkuu wa Mkoa adhamiria kumaliza malalamiko ya ardhi Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amedhamiria kumaliza kabisa malalamiko yanayotolewa na wananchi wa mkoa wa Rukwa katika migogoro ya ardhi iliyopo katika Mkoa wake.

Alionesha dhamira hiyo pale alipotembelea ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuangalia zoezi linaloendelea la kusikiliza walalmikaji wamiliki wa ardhi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.

Zoezi hili lilianza baada ya maafisa wa Ardhi wa Mkoa na wa Manispaa ya Sumbawanga kupewa agizo na Waziri Mkuu Mh. Kasim Majaliwa alipofanya ziara tarehe 24, August, 2016 katika mji wa Sumbawanga na kubaini ukubwa wa tatizo la migogoro ya ardhi katika mkoa wa Rukwa.

Wakati anatoa maagizo hayo Waziri Mkuu, aliwapa maafisa ardhi hao siku mbili kuanza kusikiliza malalamiko hayo.

Mwenyekiti wa kamati ya kusikiliza malalamiko ambae pia ni mkuu wa idara ya Miundombinu kutoka katika ofisi ya Mkuu wa  Mkoa wa Rukwa Seti George Mwakyembe amesema kuwa zoezi hilo lilianza tarehe 26, August na linatazamiwa kuisha tarehe 2, Septemba, 2016 kwa Wakazi 300 wa Manispaa ya Sumbawanga.

Ndugu Mwakyembe alieleza kuwa kutokana na maagizo ya Mkuu wa Mkoa, watatangaza ratiba ya kuweza kuzungukia wilaya na Halmashauri zilizobaki ili kuweza kumfikia kila mlalamikaji wa migogoro ya Ardhi katika Mkoa wa Rukwa.


“Tunataka ifikie hatua tuseme migogoro ya ardhi kwa Mkoa wa Rukwa sasa basi, Maana majibu ya maswali yote ya wananchi yapo” Mkuu wa Mkoa alisema.

No comments:

Post a Comment