Saturday, September 3, 2016

Mkuu wa Mkoa amuonya afisa elimu msingi Manispaa ya Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuonya afisa elimu shule ya msingi wa Manispaa ya Sumbawanga kwa kutofuatilia mahudhurio ya ufundishaji wa waalimu katika shule za Msingi za Manispaa.

Alitoa onyo hilo wakati alipoitisha kikao cha dharura leo (jumamosi tarehe 3/09/2016) kwa maafisa wa elimu, Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na watu wa idara ya afya katika ofisi yake ili kupata majibu ya matatizo aliyokumbana nayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika shule ya Msingi malagano, iliyopo katika kata ya Pito, Wilaya ya Sumbawanga.

Katika ahadi zake za kuimarisha elimu katika mkoa wake,Siku ya Ijumaa (tarehe 2/09/2016), Mkuu wa Mkoa alitembelea shule ya Msingi malagano na kubaini mahudhurio hafifu ya walimu darasani na katika juhudi za kujiridhisha na fikra hiyo ndipo alipowahoji wanafunzi wa darasa la tano ambao walikiri kuwa baadhi ya masomo kama Tehama, Stadi za Kazi na Uraia hawafundishwi kabisa.

Pamoja na kufanya mahojiano na wanafunzi, Mkuu wa Mkoa alifanya mapitio ya Daftari la mahudhurio ya walimu darasani na kugundua kuwa idadi ya vipindi vilivyofundishwa kuanzia tarehe 4 Julai, 2016 hadi 2 September, 2016 ni 31 badala ya 248 kwa masomo 7 ambayo ni Hisabati, kiingereza, Kiswahili, Jiografia, Haiba na Michezo, Sayansi na Historia.

Kwa kuonesha ukubwa wa tatizo taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza ilitangaza utafiti ilioufanya katika sekta ya elimu ambao matokeo yake yanaonyesha kuwa walimu watatu kati ya 10, sawa na asilimia 31 wa shule za msingi ni watoro kazini.


Vilevile, katika utafiti huo wa Sauti za Wananchi uliofanyika kati ya Aprili na Mei, 2014 ukihusisha shule za msingi za Serikali 1,309, kaya 16,013 na wanafunzi 32,694 katika mikoa yote nchini, uliitaja mikoa inayoongoza kwa utoro baada ya Singida na asilimia zake kwenye mabano kuwa ni Mbeya (53), Geita (44), Tanga (41), Simiyu (40), Iringa 39 na Rukwa (36). Mikoa mingine mbali ya Manyara na Ruvuma isiyo na idadi kubwa ya walimu watoro kwa mujibu wa utafiti huo ni Kilimanjaro (19), Arusha (20), Katavi (20), Tabora (22) na Mtwara (22).


 “Hii ni mfano wa shule moja tu, hii ni dalili kuwa shule nyingine za Manispaa na Mkoa mzima zina hali kama hii ama Zaidi” Mkuu wa Mkoa alisema.

Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa aliwasisitiza Maofisa wa elimu kuwakumbusha na kuwaelimisha wazazi wa watoto hao kuwapa walau uji watoto wao kabla ya kwenda shule.

“Wazazi wakumbushwe mtoto anapokwenda shule apate japo uji, katika Mkoa huu uji sio shida, mtoto hataelewa masomo kama tumbo liko tupu,ndio chanzo cha vidonda vya tumbo” Mkuu wa Mkoa alisisitiza.

Katika kuhakikisha kasoro hiyo ya mahudhurio inarekebishwa, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga D. Halfan Haule aliahidi kuwa kutaandliwa timu ya kuweza kuzunguka shule zote za msingi za Sumbawanga ili kuyabaini mapungufu na kuyatafutia dawa.

Pamoja na kupitia kwenye shule ya Msingi Malagano Mkuu wa Mkoa pia aliweza kupita katika Zahanati ya Kijiji cha malagano na kukumbana na hali isiyoridhisha kama vile Hospitali kutokuwa na “Gloves”, Kituo hakikuwa na dawa za kutosha, idadi ndogo ya wananchi waliojiunga CHF na watumishi wachache. Hivyo amewaagiza watu wa Afya kutafuta suluhisho haraka.

No comments:

Post a Comment