Tuesday, October 4, 2016

Katibu Tawala wa Mkoa atoa siku saba idara ya kilimo kuwa na mpango wa kuwawezesha wakulima.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa ametoa siku saba kwa idara ya kilimo kuandaa mpango unaotekelezeka wa kuwawezesha wakulima kulima chakula chenye tija na chenye kuwaondoa kwenye umasikini.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Nixon Nzunda.
Katibu Tawala aliyasema hayo walipofanya kikao maalum kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen cha kujua maendeleo na mipango ya kilimo kabla ya kuanza kwa mvua mwezi wa 11 mwaka huu.

Kabla ya Katibu tawala kuweza kuongea lolote Mkuu wa Idara ya Kilimo Hamza aliweza kutoa taarifa fupi iliyoelezea changamoto wanazopambana nazo pamoja na namna ya kuweza kukabilina nazo ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Katibu Tawala alisisitiza kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na mipango ambayo ni mizuri lakini haitekelezwi inavyostahili kwa lengo la kuwafaidisha wananchi wanaotegemea kilimo ili kujiendesha maisha yao.

“Mipango ni mizuri sana lakini kama ingetekelezwa walau kwa asilimia 10 basi mkoa wetu ungekuwa mbali” Katibu Tawala alifafanua.

Katibu Tawala aliongeza kuwa maafisa ugani wengi wamekuwa hawafanyi kazi zao kwa ufanisi, hivyo aliagiza kila afisa ugani kuwa na mpango kazi utakaomwongoza kufanya kazi zake za kila siku ikiwa ni pamoja na kuwajua wazalishaji wakubwa na wadogo wa mazao mbalimbali na kuweza kuwa na ratiba ya kuwafuatilia.

“Tunafahamu kwamba serikali imepoteza pesa nyingi sana kuwawezesha mafia ugani lakini hawafanyi kazi zao walizopangiwa kwa usahihi, hivyo kila afisa ugani lazima awe na idadi maalum ya kuwafikia na kuwahudumia tena kwa muda maalum na ofisi ya Mkoa ifanye kazi ya kuthibitisha kwamba afisa ugani huyu anafanya hayo aliyopangiwa” Katibu tawala alisisitiza.

Mbali na kusisitiza hayo Katibu tawala pia aliwataka waweze kubainisha mazao ya kipaumbele ili mkulima ajue mazao yenye tija na yenye kumpa kipato kitakachomtoa kwenye umasikini, na kuwakumbusha kitengo cha ushirika kuweza kutafuta masoo kwa mazao hayo, ili wakulime wasipate tabu ya kuuza mazao yao.

“Ukifanya biashara bila ya kujua soko la bidhaa unayoiuza linapatikana wapi ni sawa na hakuna, maana yake kama mkulima hajui soko kilimo haiwezi kumfaidisha na kumtoa kwenye umasikini, Hivyo bwana ushirika una wajibu wa kuyatambua masoko na kuweza kuwaunganisha wakulima na masoko hayo.” Katibu tawala alimalizia.

Katika kulikazia suala hilo na kuliunga mkono Mkuu wa Mkoa aliongeza, “katika awamu hii ya tano wananchi wanamatumaini makubwa na serikali yao na kila ninapokwenda wananchi wanataka kusaidiwa katika kilimo na wataalamu tunao mpaka ngazi ya kata, na wanafahamu kinachostawi na kisichostawi, hivyo nataka waanchi wafaidike na wataalamu wa Halmashauri na wa ofisi ya Mkoa.”

Mkuu wa Mkoa alisisitiza uzalendo na umoja katika kuwawezesha wananchi tangu kuandaa mashamba, kuotesha, kukuza, kupalilia, pembejeo, kuvuna kuhifadhi, kuongeza thamani, kufanya biashara, na kutafuta masoko.


Pia mkuu wa Mkoa alisisitiza wataalamu wa kilimo kuwa na uhusiano wa karibu sana na watu wa hali ya hewa, na kufafanua kuwa mtaalamu pekee ndie anaeweza kutambua mbegu feki na kuweza kuwafahamisha wakulima. 

No comments:

Post a Comment