Friday, October 14, 2016

Mkuu wa Mkoa aahidi Milioni Moja kwa Shule ya Kwanza Kimkoa mtihani wa Darasa la Saba.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameahidi kutoa Shilingi Milioni Moja kwa Shule itakayokuwa ya Kwanza Kimkoa katika Mitihani ya darasa la saba iliyokuwa imeshafanyika.
Aliyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba mbele ya
waalimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika maadhimisho ya siku ya Mwalimu Duniani (tarehe 5.10.2016) yaliyofanyika katika Viwanja va Nelson Mandela ambapo Mkuu wa Mkoa aliuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa aliwakumbusha waalimu wao kuacha uvivu na kuona aibu kwa kuwa mkoa wa 22 kati ya 26 katika mitihani ya darasa la saba, wakati Mkoa wa Katavi ambao ni mtoto wa Mkoa wa Rukwa ni wa Kwanza kitaifa.
"Kama mimi ndio ningekuwa mwalimu na nasikia matokeo kama hayo, ningekuwa najificha kwa aibu...aaaahhhhaaaa... hivi ninyi hamuoni aibu?," Mkuu wa Mkoa alieleza kwa masikitiko.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Kamisna Mstaafu Zelote Stephen
Lakini pia Kamisna Mstaafu Zelote Stephen aliwashukuru walimu kwa kuona juhudi za serikali kushughulikia uozo uliokuwepo serikalini kwani bila kuchukua hatua ya kuondoa uovu serikalini watumishi hawawezi kupata maslahi hayawezi kuwa mazuri kwani mapato yataendelea kupita katika mikono isiyo salama na kufujwa.

Aliwataka walimu kujichunguza kama hawamo katika makundi waliyoyataja ya ufisadi, utumishi hewa na uzembe kazini na kama wakibaini kuwa wako safi wachape kazi serikali inawaandalia mambo mazuri sana.
Kama hamko katika makundi ya mafisadi, wazembe, watumishi hewa na yanayofanana na hayo, basi nawaomba mchape kazi kwa nguvu zenu zote bila hofu serikali inayafanyia kazi mnayoyahitaji”. Alisema Zelote
Mkuu wa mkoa aliwaomba walimu kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika juhudi zake za kuleta maendeleo hasa kwa wananchi wa kipato cha chini na kuwahakikishia kuwa kero za watumishi wote zitatatuliwa mapema iwezekanavyo kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu zilizopo.


Katika kupiga vita vya ukatili dhidi ya walimu vinavyofanyika katika baadhi ya maeneo hasa ya vijijini, mkuu wa mkoa alimuagiza kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa kushughulikia ipasavyo malalamiko ya walimu kufanyiwa ukatili popote ndani ya mkoa wa Rukwa.
Akisoma risala ya walimu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna Mstaafu Zelote Stephen  Katibu wa chama cha walimu Manispaa ya Sumbawanga, Polycarp Mwanahanja alisema hatua zinazochukuliwa na serikali zinaungwa mkono na walimu mkoani hapa na kuwa wanaamini zoezi hilo linalenga kujenga uwezo kwa serikali kuboresha maslahi ya watumishi.
Aidha walimu hao wameipongeza serikali kwa kuanzisha tume ya utumishi wa walimu (TSC) ambayo wameomba iwe na majukumu yote ya mwajiri kwa lengo la kupunguza idadi ya waajiri wanaomuhudumia mwalimu na hivyo wameomba tume ipewe meno zaidi kuliko ilivyo hivi sasa kwa tume ya utumishi wa walimu nchini (TSD).
Kwa kutumia fursa hiyo waliwasilisha baadhi ya changamoto kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa wanazokabiliana nazo walimu katika halmashauri, mkoa na taifa zima ambazo walidai ni kuwa na kipato duni kisichoendana na mfumuko wa bei nchini hali ambayo imepelekea baadhi ya walimu kuingia katika mikopo yenye riba kubwa inayoishia kuwadhalilisha walimu hao.
Wameleza suala la kuchelewa kuwapandisha madaraja walimu kuwa ni kikwazo kwa serikali kufikia malengo ya kulipa madeni ya walimu kwani mrundikano unakuwa mkubwa wakati wa kuwapandisha madaraja unapofanywa kwa kundi kubwa lililolimbikizwa mfano katika Manispaa ya Sumbawanga zaidi ya walimu 745 wanadai kupandishwa madaraja kwakuwa hawakupandisha madaraja mwaka 2015/16, 2016/17 hivyo wote wanalazimika kuingizwa katika bajeti ya 2016/17.
Walimu hao walimuomba mkuu wa mkoa kuwafikishia maombi yao serikali ya posho za mazingira magumu na usafiri kurejeshwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma pamoja na kuanza mikakati ya kuondoa uhaba wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu ili mazingira ya uwajibikaji kwa mwalimu yawe rafiki.

No comments:

Post a Comment