Tuesday, November 1, 2016

Mkuu wa Mkoa atoa maelekezo ya mgao wa Pembejeo msimu huu

Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikoa 25 ya Tanzania Bara itakayonufaika na ruzuku ya pembejeo kwa maana ya Mbolea na Mbegu bora itakayotolewa na Serikali katika Msimu wa Mwaka 2016/2017. Ruzuku hii itatolewa kwa mazao mawili tu ya Mahindi na Mpunga kwa maana ya kufidia asilimia 30 ya bei ya soko kwa Mbolea na Mbegu bora za Mazao hayo.

Katika Msimu huu, ruzuku ya Pembejeo haitatolewa kwa mfumo wa Vocha kama ilivyokuwa imezoeleka, badala yake Mkulima atanunua moja kwa moja Pembejeo kutoka kwa Msambazaji kwa bei elekezi itakayopangwa na Wilaya. Kampuni ya Mbolea TFC, Wakala wa Mbegu ASA pamoja na Makampuni mengine ya Mbegu kupitia mawakala wao walioko Wilayani watakuwa na jukumu la kusambaza pembejeo kwa bei yenye ruzuku ya asilimia 30 hadi kwa Mkulima.

Mfumo huu wa utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo unalenga kuongeza tija katika mazao ya Kilimo na kuhakikisha kuwa Mkoa unajitosheleza kwa chakula kwa kumuwezesha hata Mkulima mwenye kipato cha chini sana ambaye hawezi kupata pembejeo kwa bei ya soko aweze kupata mbolea na mbegu bora. Kwa kuzingatia hilo Mkoa wa Rukwa Msimu huu umepata mgao wa Tani 2,444 za Mbolea ya Kupandia, Tani 2,444 za Mbolea ya kukuzia na Tani 489 za Mbegu bora za Mahindi.

Natambua kwamba kiasi hiki cha pembejeo hakitoshi kwa mahitaji ya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wapatao Kaya 250,952. Kiasi hiki cha Pembejeo kinatosha tu kunufaisha Kaya zipatazo 48,880 sawa na asilimia 19.47 ya kaya zote. Pia natambua kwamba sio maeneo yote ya Mkoa wa Rukwa yanafaa kwa kilimo chenye tija cha zao la Mahindi.


Kwa kuzingatia ratiba ya Kilimo natambua kwamba Mkoani Rukwa Mvua zitaanza kunyesha Mwanzoni mwa Mwezi Novemba kuanzia tarehe 10 hadi 15. Na pia Wataalam wa hali ya hewa wametuambia kwamba Mvua za Msimu huu zitakuwa kidogo. Hivyo, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba taratibu za maandalizi ya kufikisha Pembejeo kwa Mkulima zinafanyika haraka sana kuanzia sasa. Kwa sababu hiyo napenda kuwaagiza Wakuu wa Wilaya wote Mkoani Rukwa Kuhakikisha Vikao vya Kamati za Pembejeo za Wilaya vinafanyika kati ya Tarehe 1-4 Novemba, 2016 kwa ajili ya maandalizi,

Kuhakikisha kwamba Vikao vya Kamati za Pembejeo za Vijiji Vinafanyika kati ya Tarehe 5-8 Novemba, 2016 hususan kuainisha Majina ya Wanufaika,Kuhakikisha kwamba hadi kufikia Tarehe 10 Novemba, 2016 Taarifa za Vikao vya Kamati za Pembejeo katika Ngazi za Vijiji zinawasilishwa Wilayani,Kuhakikisha kwamba hadi kufikia Tarehe 12 Novemba, 2016 Taarifa za Kamati ya Pembejeo ya Wilaya zinawasilishwa katika Ngazi ya Mkoa.

Kusimamia kikamilifu zoezi la usambazaji wa Pembejeo za Kilimo na kuhakikisha kwamba Wanufaika walioainishwa na Kamati za Pembejeo za Vijiji ndio wanatumia Pembejeo zenye ruzuku na sio wajanja wachache wenye pesa kushambulia pembejeo hizo.
Kuhakikisha kuwa elimu kwa wananchi juu ya uwepo wa mvua kidogo kwa mwaka huu inatolewa ili wakulima wetu waweze kuitumia vizuri na kuzalisha mazao ya kutosha. 

Wakulima wetu ambao hawatafikiwa na pembejeo hizo kuhakikisha wanajiunga katika Vikundi mbalimbali vya Kilimo kama AMCOS, SACCOS na Vikundi vinginevyo, ili kupitia Vikundi hivyo waweze kujipatia Mikopo ya Pembejeo zitakazotosheleza mahitaji yao badala ya kutegemea pembejeo zenye Ruzuku ambazo hazitoshelezi. Lengo ni kuona kwamba kila Mkulima anapata pembejeo ili Kilimo chetu kiwe na tija kwa maisha ya Wakulima wetu na taifa kwa jumla.

zaidi angalia video


No comments:

Post a Comment