Saturday, December 24, 2016

Mh. Zelote aagiza Nesi kuchukuliwa hatua baada ya kuwapuuza wagonjwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameagiza Muuguzi wa kituo cha Afya cha Mtowisa kuchukuliwa hatua baada ya kubainika kumpuuza majeruhi aliyeangukiwa na tofali na kupata michubuko katika maafa yaliyotokea katika kijiji cha Mwela Kata ya Mtowisa, Wilaya ya Sumbawanga. 

Muuguzi huyo ambae inasemekana baada ya majeruhi hao kuwasili katika kituo hicho cha afya saa tano usiku wakihitaji msaada, yeye aliwaandikia dawa waende kutafuta katika dawa hizo katika maduka yaliyopo nje ya hospitali.

Mkuu wa Mkoa alifika katika kituo hicho cha afya baada ya kutoka kutoa pole kwa waathirika wa maafa ya Mvua yaliyoezua nyumba 24 ili kujihakikishia na kuona kuwa kuna dawa za kutosha na hakukuwa na sababu ya muuguzi huyo kuwaelekeza majeruhi hao katika maduka yaliyopo nje ya hospitali

“Huyu Nesi achukuliwe hatua, narudia kusema ni bora tubaki na muuguzi mmoja ambaye ni mwadilifu na anayetuwakilisha vizuri, Kwasababu hiki kituo hakikuwekwa kwa bahati mbaya kimewekwa kwaajili ya hawa wenye shida wanaokimbilia huku kupata huduma” Mh. Zelote Alisisitiza.

Mh. Zelote aliongeza kuwa muuguzi huyo anaweza kuwa ni miongoni mwa watumishi ambao hawatoi huduma mpaka mwananchi ajipapase na kutoa chochote.

Kaimu Mganga wa kituo hicho cha afya Dokta Thomas Cyprian alikiri kutokea kwa tukio hilo na kumuahidi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuwa kamati ya maadili ya kituo hicho kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule watakaa na kumchukulia hatua.


“Ni kweli baada ya mimi kupata taarifa za tukio hilo, nilimwita na kumuuliza na kweli alieleza kilichotokea kuwa ndivyo hali ilivyokuwa,” Dk. Cyprian alisimulia.


No comments:

Post a Comment