Saturday, December 24, 2016

"Nawatakia wanarukwa Heri ya Christmas na Mwaka Mpya 2017, lakini....," Mh. Zelote Stephen

SALAMU ZA CHRISMASS NA MWAKA MPYA KUTOKA KWA MKUU WA MKOA WA RUKWA MHESHIMIWA ZELOTE STEPHEN ZELOTE KWA WANANCHI WOTE WA MKOA WA RUKWA 

Ndugu Wananchi,
Tunapokaribia kumaliza Mwaka 2016 napenda nichukue nafasi hii kwa dhati na moyo mkunjufu kuwashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba amani na utulivu inatawala muda wote katika Mkoa wa Rukwa.  Ni imani yangu na matarajio yangu kwamba mwaka unaofuata Mwenyekzi Mungu akituvusha salama tutaendelea ama tutazidisha ushirikiano uliokuwepo.

Pili, nachukua nafasi hii kuwatakia sikukuu njema na baraka tele toka kwa Mwenyezi Mungu.  Katika siku hizo nawaomba kila mmoja asherehekee kwa mipaka yenye kujali amani, utulivu, kuzingatia sheria ikiwa ni pamoja na kulinda maisha na mambo mengine yote muhimu yanayotuzunguka.  Natumaini vyombo vinavyohusika kuhakikisha ulinzi na usalama ndani ya Mkoa vitavitimiza majukumu yake kwa weledi mkubwa. 

Ndugu Wananchi,
Katika Mwaka unaomalizika yapo mambo mengi tuliyoyafanya kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya Mkoa wetu ndani yake kukiwemo lengo la kunyanyua maisha ya kila mwananchi kiuchumi.  Nawaomba sana tuendelee kushirikiana na Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye nia na dhamira ya hali ya juu ya kuleta mabadiliko kwa manufaa ya kila Mtanzania.  Binafsi nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa utumishi na uongozi wa namna ya pekee katika Taifa letu la Tanzania

Tumuunge mkono katika kupiga vita vitendo vya Rushwa, Ufisadi, Ubadhilifu na Kutowajibika ipasavyo kwa baadhi ya Watumishi wa Umma sehemu za kazi.  Naamini tukiungana naye tutafanikiwa kuondosha mambo yote hayo mabaya.  Vilevile napenda kuhimiza kila mtu ajitume kufanya kazi.

Ndugu Wananchi,
Kumekuwepo na matukio mbalimbali; wengine wamepoteza ndugu zao kwa matukio mbalimbali ikiwepo ajali, moto, hali ya hewa, maradhi na kadhalika.  Nachukua nafasi hii kuwapa pole.

Ndugu Wananchi,
Hali ya hewa ambayo ndio msingi tunaoutegemea sana kwa ajili ya kilimo katika Mkoa wetu inayumba.  Mvua hazinyeshi kwa kawaida yake.  Kutokana na hali hiyo natoa rai kama ifuatavyo:-

i.                   Wananchi watunze akiba ya chakula waliyojiwekea.  Kisitumika kwa kuuza ama kutengeneza pombe badala yake wahifadhi ili ituvushe kipindi ambacho kipo mbele yetu.
ii.                Sambamba na hilo natoa wito watu walime mazao yanayoweza kuhimili ukame mfano Viazi vitamu, Mihogo, Ulenzi na Mtama.  Naagiza Halmashauri zote kusimamia agizo hili.

iii.              Natambua kwamba Pembejeo za Ruzuku zilichelewa kidogo lakini jambo hilo limerekebishwa na usambazaji wa Pembejeo hizo unaendelea vizuri zoezi ambalo tunafuatilia kwa karibu sana.  Hata hivyo hata wale ambao sio wanufaika wa pembejeo hizo wamekuwa wakipata huduma hiyi katika maduka ya pembejeo za Ruzuku kwa bei ya kawaida.  Serikali inajitahidi kuhakikisha pembejeo hizo zinakuwa zenye ubora na sio feki.

Ndugu Wananchi,
Napenda nimalizie salamu zangu kwa kuwatakia wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kila la Kheri kwa sherehe zote zijazo ikiwa ni pamoja na kuaga Mwaka wa 2016 na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2017 katika hali ya Amani na Utulivu.

Asanteni kwa kunisikiliza


Zelote Stephen Zelote
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa


No comments:

Post a Comment