Tuesday, January 31, 2017

Matokeo ya Kidato cha Nne 2016Shule 10 Bora Kitaifa 

Shule 10 za Mwisho Kitaifa 
Bonyeza Hapa 
🔻

Mh. Zelote Stephen aungana na wananchi ujenzi wa Shule ya Sekondari Milundikwa


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Kasu Wilayani Nkasi katika ujenzi wa shule ya Sekondari Milundikwa baada ya shuke hiyo kuhamishwa utoka katika Kijiji cha Milundikwa ili kupisha kambi ya jeshi la kujenga taifa.

Katika zoezi hilo Mkuu wa Mkoa alishirikiana na wakuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule, na Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na ya Wilaya ya Nkasi.


"Nawashukuru sana, najua mnaratiba zenu na shughuli zenu mmeziacha ili kuja kushiriki kwenye ujenzi huu wa shule yetu ya sekondari ya Milundikwa, Jeshi walikuwa waungwana wakatuachia eneo lile na sasa wamerudi wamelihitaji, na wao ni amri tu," Mh. Zelote alisema.

"Katika kuboresha elimu, serikali ya awamu ya tano imehakikisha kwamba hakuna mwanafunzi anakayekaa chini na atakaekosa darasa la kusomea," Mh. Zelote aliongeza.

Katika kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa katika darasa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amesema kuwa Wilaya yake ina mpango wa kujenga madarasa matatu kwa kila shule, madarasa ambayo yatakuwa yakijengwa kwa nguvu za wananchi na kumaliziwa na serikali.

"Mpaka sasa kila kijiji kina benki ya matofali kwaajili ya ujenzi wa madarasa ya shule zilizopo katika maeneo yao, tunawahamasisha wananchi wajitahidi kuzalisha matofali mengi ikiwezekana kujenga madarasa zaidi ya hayo, nawashukuru wananchi wanaendelea kuitikia wito huo," Mh. Mtanda alifafanua.
Monday, January 30, 2017

Mh. Zelote Stephen azungukia shule kujua changamoto za wanafunzi na waalimu mwanzo wa mwaka.
HALMASHAURI ZIFANYE KAZI KWA WELEDI-MAJALIWA


           *Azitaka zisiwe pango la wezi, wazembe
WAZIRI MKUU Kassm Majaliwa amesema wakati umefika wa kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha kwenye Halmashauri zote nchini na pia hazitakiwi kuwa pango la wezi, wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu walioshindikana kwingineko.

Aidha, Waziri Mkuu amesemma Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini zinatakiwa zianze kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi kuona ni kwa namna gani zitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda vinavyotarajiwa.
WAZIRI MKUU Kassm Majaliwa

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 30, 2017) wakati akifungua Kikao cha Baraza la Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma. Amesema kikao ni chombo muhimu na endapo kitatumika vizuri kitaweza kusaidia kusukuma maendeleo ya Mkoa na kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.

Amesema Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Halmashauri zote nchini kwa kadiri uwezo utakavyoruhusu na kusisitiza kwamba fedha hizo lazima zisimamiwe vizuri na zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi.

“Endapo itabainika kwamba kuna baadhi ya Sheria zinazokwamisha utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatutasita kuzifanyia mapitio na hatimaye kuzibadili ili ziendane na azma yetu ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema.

Amesema Serikali ina maslahi makubwa kwa Serikali za Mitaa, sio tu kwa kuwa ni Serikali kamili katika ngazi hiyo, bali pia kutokana na ukweli kwamba kero nyingi za wananchi ziko katika ngazi hiyo.

Waziri Mkuu amesema vyanzo vingi vya mapato ya Serikali vinapatikana kwenye Halmashauri huku changamoto kubwa ikiwa ni kulegalega kwa  Halmashauri nyingi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi jambo linalozorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hivyo Waziri Mkuu ametoa rai kwa Halmashauri hizo kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kutatua kero zao kikamilifu na kwa wakati pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.

Pia zihakikishe malipo yote yanafanyika kwa njia za kielektoniki na zihamasishe vijana na akina mama wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji mali na kuwapatia stadi za kazi na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuwa chanzo cha mapato hapo baadaye.

Amesema watendaji wa Halmashauri wanatakiwa  kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na uzembe kazini na watakaobainika kufanya vitendo hivyo  wachukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.

“Someni taarifa ya CAG (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali) na kutoa majibu ya kina ya namna mtakavyodhibiti mianya ya rushwa na ubadhilifu kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hizo,” amesema.

Hata hivyo amesema kila Halmashauri iandae mpango wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye maeneo makubwa ya kipaumbele kama vile ujenzi wa miundombinu ya shule,  maboresho kwenye sekta ya afya (ujenzi wa hospitali, zahanati na vituo vya afya).

“Endeleeni kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwenu, mfanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.  Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atimize wajibu wake na kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni migogoro, matusi, dharau, bezo na vitisho. Mshirikiane na jamii ione mpo wamoja,” amesema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JANUARI 30, 2017


Saturday, January 28, 2017

Mh. Zelote Stephen awacharukia Wakurugenzi kuhusu TASAF

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewaagiza wakurugenzi, waratibu wa Tasaf, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji Mkoani humo kuhakikisha kwamba haki inapatikana katika kufanya mchujo kwa zile kaya ambazo hazistahili kuingizwa katika mpango wa kuzinusuru kaya masikini (TASAF)

Ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara yake ya siku ya nne katika wilaya za kalambo na Nkasi Mkoani humo kwa kuzitembelea kaya za walionufaika na mpango wa TASAF ambao bado wanaendelea kunufaika na wale ambao waliondolewa katika mpango huo baada ya kukosa vigezo na hatimae kutakiwa kurudisha pesa hizo.

“nimezunguka nimebaini kuwa zoezi hili limekuwa likifanyika hovyo hovyo, hakuna umakini, hakuna usimamizi, hakuna ufuatiliaji, matokeo yake kwenye mradi wameingizwa watu wenye sifa na wasio na sifa, Wakurugenzi na waratibu wasimamie zoezi hili, wasiwaachie wenyeviti na watendaji wa vijiji peke yao katika hili,”

Zelote Stephen alifanya ziara hiyo ili kujiridhisha kuwa kaya ambazo hazistahili kuingizwa katika mpango wa TASAF wanatendewa haki katika kuondolewa kwenye mpango huo lakini pia kujua sababu zilizopelekea kaya hizo kuingizwa kwenye mpango bila ya kuwa na vigezo na kuachwa kaya zenye vigezo.

“Wale wote ambao hawana vigezo na kweli ionekane kwamba hawana vigezo vya kuwepo basi watolewe kwasababau sehemu zingine utakuta kwenye mpango huo wameingizwa wastaafu, mke wa mwalimu, mjumbe wa smc yumo humo humo, hii haifai,” Zelote alifafanua.

Katika ziara yake hiyo iliyolenga kufuatilia mchujo wa kaya hizo, Zelote Stephen alibaini kuwa wakurugenzi pamoja na waratibu wa TASAF wilaya wanakosa umakini katika kuzifanya shughuli zao na hatimae kubaki maofisini kusubiri ripoti zitokazo vijijini bila ya kufuatilia kwa kina kwa kufika katika maeneo husika ili kujua hali halisi.

“Mimi nina taarifa kwamba fedha za ufuatiliaji wa TASAF zikifika tu katika Ofisi ya Mkurugenzi, kama zimefika asubuhi basi mchana tu hakuna senti tano, zote zimeshanyanganyiwa na hatimae makusudio ya fedha zile hayatimii na ufuatiliaji haufanywi,” Alisisitiza.

Nae mratibu wa TASAF Mkoa wa Rukwa, James Kapenulo aliongeza kuwa kaya zote ambazo zilinufaika na TASAF kwa kuwa na mashamba na nyumba nzuri ambazo kabla ya TASAF hawakuwa nazo, familia hizo ndio ziwe za mfano na ziendelee kuwezeshwa ili tathmini itakapokuja kufanywa ioneshe hali halisi ya mafanikio ya mpango huo.

“Hatuwezi tukaendelea kuwaweka wale ambao wakipewa pesa za TASAF wanaishia kwenye vilabu vya pombe na kumuacha yule ambae akipewa pesa hizi ananunua kuku au mbuzi au bati na kuwapeleka watoto shuleni, hayo sio madhumuni ya mpango huu, huyu aliyefanikiwa baada ya TASAF ndiye ametoka weye umaskini.

Naye mnufaika wa TASAF aliyetolewa kwenye mpango huo Mathias Mwanakatwe alimshukuru Mkuu wa wa Mkoa kwa kuweza kuliona hilo na kulishughulikia kabla hali haijawa mbaya zaidi kwa wale wananchi wenye wivu na chuki kwa wale waliofanikiwa kutokana na kuwepo kwa mpango huo wa TASAF.

Kaya a 550 mbazo hazistahili kuwepo katika mpango huo kwa Mkoa wa Rukwa.WALIOTAFUNA ZAIDI YA SH. BILIONI 1 ZA USHIRIKA WASHUGHULIKIWE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika na upotevu zaidi ya sh. bilioni moja za vyama vya ushirika.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa

 
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Januari 27, 2017) alipozungumza na watumishi wa Mkoa wa Njombe wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani hapa.

Alisema kati ya fedha hizo sh. milioni 532.736 zilipotea katika SACCOS ya Kurugenzi  Njombe pamoja na sh. milioni 900 zilizopotea katika Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kiitwacho Wafanyabiashara Njombe SACCOS.

“Maofisa Ushirika nchini mmeendelea kudhoofisha jitihada za Serikali katika kuimarisha ushirika. Katika eneo hili ninahitaji Mkuu wa Mkoa ufuatilie suala hili na kuwachukulia hatua wahusiuka wote,” alisema.

Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wote wa Wilaya kuwatumia warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika Mkoani Njombe.”Tunataka ushirika ulete tija kwa wananchi na hatutaki ushirika ulioambatana na harakati za kugawa watu. Endeleeni kuwashughulikia wanaushirika wasio waaminifu,”.

Aidha, Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi wa umma wote nchini kuzingatia uadilifu, uaminifu, kutojihusisha na rushwa na kutumia ipasavyo fedha za umma Serikali itachukulia hatua kali dhidi ya watumishi wote wanaotumia nafasi zao kujinufaisha binafsi.

Alisema anataarifa za Watendaji wa Wakuu wa Wilaya ya Makete akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Francis Namsumbo, Mweka Hazina Bw. Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi, Bw. Nicodemas Tindwa na Mkaguzi wa Ndani Bw. Michael Shija kuhusika na upotevu wa sh. milioni 71 zikiwemo sh milioni 41 za UNICEF.

Waziri Mkuu alisema kuwa watumishi hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa kwa vyombo mbalimbali ili kuficha ubadhilifu huo. “Mkuu wa Mkoa hakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kuhusiana na matukio haya,”.

Pia alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kuhakikisha kuwa ……..wa Wanging’ombe Bw. Edwin Kigoda anachukuliwa hatua stahiki kwa ubadhilifu wa sh. milioni 37.9 zilizotolewa kwa ajili ya kuwajengea uwezo Walimu katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Mbali na watumishi hao pia Waziri Mkuu alimtaka Bw. Ole Sendeka kumchunguza na kumchukulia hatua Ofisa Ardhi wa Mji wa Njombe, Bw. Addo Kabange ambaye anatuhumiwa kuuza viwanja mara mbili, kuchukua rushwa na kujipatia viwanja vingi kwa bei nafuu na kuviuza kwa wananchi kwa bei ya juu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema atawaelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Msajili wa Hazina na Mrajisi wa Ushirika kuanza kufuatilia malalamiko kuhusu umiliki wa kiwanda cha chai cha Lupembe pamoja na kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa hisa za kiwanda hicho.

Alisema alipotembelea kiwanda cha chai cha Lupembe ambapo alifarijika kukuta kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi baada ya kusimama kwa takriban miaka nane kutokana na mgogoro uliopo baina ya mwekezaji wa Kiwanda hicho na Umoja wa Wakulima wa Chai Muvyulu.

Waziri Mkuu alisisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa wananchi, hivyo aliahidi kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo mbili na kutafuta njia ya kutatua mgogoro uliopo.

Alisema baada ya kusomewa taarifa ya kiwanda na kwa upande mwingine taarifa ya wanaushirika alibaini kuwepo kwa mgogoro unaohitaji kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za kiwanda kuendelea kwa amani na usalama.

Aidha, Waziri Mkuu alielekeza shughuli za ulimaji na uvunaji wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na kupeleka katika kiwanda hicho iendelee na kiwanda kisisimamishe kazi ili kulinda soko la wakulima na ajira za watumishi wa kiwanda hicho,” alisema.

Alisema kwa kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia, alimwelekeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kuhakikisha kuwa wanaweka wawakilishi wawili au watatu wa wanaushirika katika Bodi ya Kiwanda hicho.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga, ambapo alisema ucheleweshaji huo si wa makusudi bali ni mpango wa Serikali wa kujiridhisha na vipengele mbalimbali vya mkataba ili uwe wa manufaa kwa Watanzania.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema baada ya kutembelea eneo ambalo uchimbaji utakapofanyika, na kujionea maendelezo ya wananchi yaliyopo, alipata mashaka na kiasi cha sh. bilioni 13 kilichotengwa na wawekezaji kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.

Alisema Serikali haina budi kufanya tathmini ya kina na kujiridhisha. “Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge (Deo Ngalawa-Ludewa) na Mwenyekiti wa NDC kujiridhisha na wahusika wanaotarajiwa kupata fidia hiyo,”.

Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Bodi ya Motisha na Mishahara inaendelea kufanya tathmini ya uzito wa kazi ili kupanga upya viwango vya motisha na mshahara kwa watumishi wote.

Pia aliwasisitiza waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya likizo, masomo na uhamisho, kuandaa leave roster na mipango ya mafunzo kwa watumishi.


(Mwisho)

Thursday, January 26, 2017

MCHUCHUMA NA LIGANGA KUANZA UZALISHAJI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali lazima ijiridhishe ni kwa namna gani itafaidika na uwekezaji katika miradi ya makaa ya mawe na chuma kabla haijaanza.
 
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa
Amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na muwekezaji kabla ya kuanza uzalishaji kwenye miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga. 

Miradi hiyo inatekelezwa kwa ubia kati ya  Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Ltd (SHG) ya China.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 26, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mundindi baada ya kukagua eneo la mradi wa chuma cha Liganga.

“Madini haya yana viwango vya juu  vya ubora, hivyo ni lazima tuwe makini kabla ya kuanza kwa uzalishaji wake. Kwani chuma chetu ni bora na tutachimba kwa zaidi ya miaka 50,”.

“Hivyo maeneo haya ni nyeti na lazima Serikali ijipange vizuri na kujiridhisha kama  vipengele vyote vya mkataba vimetengamaa ndipo mradi huo uanze,” amesema.

Hata hivyo amesema mradi huo hautachukua muda mrefu utaanza hivyo wananchi wawe na subira. “Hatutaki kusikia tena suala la mikataba mibovu tunataka mikataba itakayoleta tija.

Akizungumzia suala la fidia kwa wananchi wanaopisha mradi, amesema kabla haujaanza lazima walipwe fidia zao na tayari fedha zipo muwekezaji anasubiri ruhusa ya Serikali.

Amesema kuna baadhi ya watu wamejipenyeza na kutaka kuiibia Serikali kupitia suala la ulipaji wa fidia. Serikali haiko tayari kuona wananchi hao wakitumika kama madaraja ya wizi.

Waziri Mkuu amesema watu hao ambao hawahusiki na eneo hilo wamesababisha gharama za fidia kuwa kubwa, hivyo wataalam wanatathmini ili kubaini wahusika kabla ya kulipa.

“Tunataka wananchi wenyewe waliokuwa hapa ndiyo tuwalipe fidia yao kwa mujibu wa tathmini husika. Fidia yenu mtalipwa baada ya kuwaondoa wezi wote waliojipenyeza.

“Kuna watu wanataka kuiibia Serikali kwa mgongo wenu, hili hatutakubaliana nalo. Tupo makini vumilieni inalifanyia kazi suala letu. Hakuna haki ya mtu itakayopotea,” amesema.

Naye Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Ltd (TCIMRL) Bw. Eric Mwingira amesema miradi ya Liganga na Mchuchuma inatekelezwa kwa mfumo unganishi ambayo ina vipengele vitano kikiwemo cha mgodi wa chuma cha Liganga.

Amesema mgodi huo wa chuma una uwezo wa kuzalisha tani milioni 2.9 kwa mwaka huku kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma Liganga kitazalisha tani milioni 1.1 kwa mwaka.

Bw. Mwingira amesema kipengele kingine ni mgodi wa makaa ya mawe Mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka.

“Kipengele cha nne ni kituo cha kufua umeme cha megawati 600 huko Mchuchuma. Kati ya hizo megawati 250 zitatumika Liganga katika kuchenjua na kuzalisha chuma cha pua na megawati nyingine 350 zitaingizwa kwenye msongo wa Taifa ili kuiuzia TANESCO,” amesema. 

Pia kutakuwa na njia ya msongo wa umeme wa kilowati 220 kati ya Mchuchuma na Liganga na barabara ya mkato kutoka Mchuchuma hadi Liganga.

Amesema gharama za uwekezaji katika mradi huo unganishi ni Dola bilioni tatu, ambapo dola milioni 600 ni mtaji wa muwekezaji na mkopo utakuwa dola bilioni 2.4.

Awali Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mheshimiwa Deo Ngalawa alimuomba Waziri Mkuu kuwaeleza wananchi hao ni lini watalipwa fidia za kupisha mradi wa chuma Liganga na mradi huo utaanza lini.


(Mwisho)
       


Tuesday, January 17, 2017

Mh. Zelote Stephen asema Mkoa wa Rukwa hauna njaa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amesema kuwa Mkoa hauna njaa baada ya kufanya ziara katika maghala mbalimbali ya wajasiriamali pamoja na kiwanda cha Unga cha Energy Mills vyote vilivyopo katika mji wa Sumbawanga.

“Mmejionea wenyewe, Katika Manispaa ya Sumbawanga suala la kwamba hakuna chakula ama kuna njaa ni maneno hewa, hakuna kitu kama hicho, Chakula kipo cha kutosha nafaka karibu zote zipo,” Mkuu wa Mkoa alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akiwa ameshika kisado cha mahindi wakati alipopita kwenye soko la mandela ili kujua hali ya chakula Mkoani Kwake, akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule (kuliani kwake)

Ameongeza kuwa wakulima wengi wameonekana kuuza mazo yao kwa wachuuzi na kusababisha wafanyabiashara wa masokoni kwenda kununua mazao hayo kwa bei kubwa na matokeo yake nao ili wapate faida nao wanaongeza bei jambo linalosababisha wananchi kushindwa kununua na wao kulalamika kuwa hakuna wateja. 

Katika suala la malalamiko ya wananchi kuosa pesa Zelote Stephen alifafanua “malalamiko yaliyokuwepo kuwa pesa hakuna, nami nakubali, kipindi hiki tulichopo ni wakati wa kilimo na wakati wa kilimo maana yake kila mtu yupo shambani, na mwezi ujao (Februari) kuanzia tarehe 20, kuna taarifa kwamba watu wataanza kuvuna maharage, kwahiyo ni dhahiri kwamba suala la njaa na bei hakuna mtu ambae atalizungumzia.”

Katika kulishuhudia hilo mmiliki wa kiwanda cha Energy Mills, Aziz Tawakali alisema kuwa mpaka sasa katika ghala lake ana tani 30 na mifuko 3400 ya unga wa sembe wenye kilo 50 kwa kila mfuko, na kuongeza kuwa kwa idadi hiyo kiwanda chake kinaweza kufanya biashara hadi mwezi wa tatu mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akiwa ametembelea kiwanda cha Energy Mills kujua hali ya Chakula Mkoani kwake.
“Sio kwamba kuna njaa, na katika mwaka mzima hatujawahi kukosa stock ya chakula, na wa stock hii niliyonayo nina uwezo wa kuuza mpaka mwezi wa tatu” Azizi alithibitisha
Nae mmoja wa wamiliki wa mashine za mpunga Mathias James amethibitisha kuwa katika Mkoa wa Rukwa hakuna shida ya chakula bali shida iliyopo ni ya wateja wa kununua chakula hicho, hivyo aliwaasa wale wote wanaosema kuwa hawana chakula cha kununua wafike katika ofisi yake.

“Kusema kuwa kuna njaa, hiyo si kweli, maana sisi tunahangaika kutafuta wateja, na wateja tunaowategemea ni kutoka Mbeya na Tunduma na wengine kutoka nchi za jirani kama Zambia na Kongo, hivyo tunawaasa wale wanaotafuta mchele, kwetu upo, tuna magunia ya mpungaya kilo 90 zaidi ya 18,000 hayana wateja, mpunga upo, mahindi yapo, waohitaji watuone,” Mathias alisisitiza.
Nao baadhi ya wajasiriamali wadogo wadogo wanouza kwa visado nao pia waliendelea kulalamikia upungufu wa fedha katika mifuko yao na kuongeza kuwa shida za wananchi si chakula kwa sasa bali pesa ndio ngumu na ndio inayotusababishia njaa.

“Njaa yetu pesa hakuna chakula kipo ila hela ya kununulia hayo mahindi ndio hakuna, kutokana na mzunguko wa biashara hela hakuna ila chakula kipo,” Deus Malonga alisema
Nae Agness Palakata alisema “Tokea asubuhi tunauza hilo gunia halijaisha, sasa namna hii hatuwezi kurudi nyumbani uawalisha watoto, pesa hakuna, chakula kipo ila pesa ndio tatizo, shida yetu na njaa yetu ni pesa.”

Kwa kuthibitisha kutokuwepo kwa njaa  Zelote Stephen aliongeza kuwa wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) wana jumla ya tani 15,500 ambazo zipo kwenye magala yao.

Sunday, January 15, 2017

Watumishi wa Manispaa ya Sumbawanga waanza kampeni kwa kupanda miti 600

Afisa Mazingira wa Manispaa ya Sumbawanga Hamidu Masare amewaongoza watumishi pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kupanda Miti katika chanzo cha maji kilichopo katika kijiji cha Malonje.

Hamidu Masare amewaomba wananchi waendelee kupanda miti katika maeneo yao ya nyumbani pamoja na maeneo ya vyanzo vya maji kwaajili ya kutunza vyanzo hivyo kwa manufaa ya vizazi hivi na vizazi vijavyo.


"Tupande miti ili Mkoa wetu upendeze, miti ni uhai, miti ni mali, miti ni biashara, miti ni ukombozi," Mh. Zelote


Wananchi wa Rukwa na Katavi wakosa mawasiliano baada ya Daraja kukatika


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aagiza TANROAD kutengeneza barabara ya dharura baada ya daraja kubebwa na maji na kusababisha kutokuwa na mawasiliano kati ya Mkoa wa Rukwa na Katavi katika Kijiji cha katete barabara ya kuelekea kibaoni ikitokea Namanyere na kusababisha abiria kushindwa kuendelea na safari zao. 

Watumishi wa Rukwa wajiimarisha kimichezo


Mh. Zelote Stephen alipokutana na RUREFA kujadili maendeleo ya mchezo huo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen alikutana na viongozi wa Chama cha Mpira wa miguu cha Mkoa wa Rukwa RUREFA ili kujadili maendeleo ya mchezo huo katika Mkoa wa Rukwa.


Tixon Nzunda ahimiza utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kupanda miti


Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Tixon Nzunda amewaasa wakulima kuacha kulima au kufanya shughuli za kibinaadamu kwenye vyanzo vya maji na matokeo yake waimarishe vyanzo hivyo kwa kupanda miti.

Mh. Zelote Stephen awahimiza Tanesco Rukwa kufikisha Umeme katika gereza la MolloMkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemhimiza Meneja wa Tanesco Mkoa wa Rukwa kufikisha umeme katika Gereza la Mollo lililopo katika Mji wa Sumbawanga ili kusukuma shughuli za kiuchumi zinazofanywa na gereza hilo ikiwemo uzalishaji wa mbegu za mahindi ambao unatazamiwa kuja kuwa uzalishaji mkubwa wa kuweza kutumika na wanarukwa na kuacha kuagiza mbegu zinazotoka nje ya mkoa. 

"Hadi kufikia mwezi Machi tatizo a maji ni Historia katika mji wa Sumbawanga" SUWASA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen aliambiwa maneno hayo baada ya kutembelea mradi wa maji unaondelea kumaliziwa katika makao yao kata ya majengo,

Baada ya kusikia hayo Mh.Zelote Stephen aliwaagiza Mamlaka ya maji safi mji wa Sumbawanga (SUWASA) kumpa taarifa kila siku asubuhi juu ya maendeleo ya Mradi huo, na kuwahimiza wakandarasi wa mradi huo kuhakikisha kuwa hiyo iwe mara ya mwisho kutoa ahadi. 


Sunday, January 8, 2017

Waziri Mkuu aagiza maafisa wanne wakamatwe

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU AAGIZA MAAFISA WANNE WAKAMATWE
*Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000
* Wapelekwa Masasi chini ya ulinzi wakajibu tuhuma zinazowakabili

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.

Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. We
ngine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana jioni (Jumamosi, Januari 7, 2017) baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO - Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.

Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa an wanunuzi wa mnda wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw.  Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.

“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.

Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.

Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.

Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara wananchi.

Tuhuma nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).

Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.

Mapema, wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero nyingi sana kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.

“Makubaliano yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa. Pia kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye pia ni mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.

Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli.

Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.

(mwisho)

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JANUARI 8, 2017.

Mh. Zelote Stephen awaonya wanaoingiza mifugo Mkoani Rukwa bila ya utaratibu aliouweka

Mkuu wa mko wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewaagiza wakuu wa Wilaya kutokubali kupokea mifugo kutoka katika wilaya nyingine bila ya mifugo hiyo kuipa kibali maalum cha kuhamia katika wilaya zao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen

Ameyasema hayo katika amri halali namba 1/2017 kuhusu kupokea, kuingiza, kuihamisha, kusafirisha na kupitisha mifugo ndani ya mkoa wa rukwa kwa mamlaka aliyopewa na kifungu cha 7 cha sheria Nambari 19 ya mwaka 1997 ya Tawala za Mikoa Sura Namba 97 mapitio ya mwaka 2002, kwa lengo la kusimamia na kutekeleza maagizo ya waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2002 unaokataza kabisa usafirihaji kiholela wa mifugo.

“Mifugo isihamishwe kutoka katika Kijiji, Wilaya ama Mkoa kabla ya kupata kibali cha Kijiji, Wilaya ama Mkoa inakopelekwa. Hivyo Kijiji, Wilaya na Mkoa itatoa kwanza idhini ya kupokea mifugo hiyo ndipo kibali cha kusafirisha mifugo kitolewe,” Zelote Stephen alisema.

Zelote Stephen alisisitiza kuwa Vijiji, Wilaya na Mkoa usitoe vibali vya kupokea mifugo kabla ya kujiridhisha kwamba wanayo maeneo ya kutosha ya malisho ya mifugo, yaliyopimwa na kuthibitishwa na wataalamu kama yanafaa kwa malisho na maji ya kutosha na majosho ya kuoshea mifugo.

Vile vile Mkuu wa Mkoa aliwaagiga maafisa mifugo kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya na Mkoa kusisimamia na kuhakikisha hakuna mifugo inayosafirishwa kutoka Kijiji, Wilaya na Mkoa kwenda Mkoa mwingine au kuingia katika Kijiji, Wilaya au Mkoa bila ya kupimwa na kuchanjwa chanjo lengo likiwa ni kuthibiti uenezaji wa magonjwa ya mifugo nchini.

“Kabla ya kutoa vibali vya kusafirisha mifugo, madaktari wa mifugo wa Wilaya ama wawakilishi wao wahakikishe kwamba mifugo inaogeshwa na kuchanjwa dawa za kuzuia magonjwa husika kabla ya kuiruhusu mifugo hiyo kusafirishwa ili kuzuia uenezaji wa magonjwa ya mifugo,” Zelote Stephen alifafanua.

Aidha Mkuu wa Mkoa amewatahadharisha maafisa mifugo ambao sio waaminifu wanaotumia njia ya kuingiza mifugo kwenye wilaya kwa njia ya biashara za minada na matokeo yake mifugo hiyo kubaki eneo husika bila ya kufuata taratibu zozote.


Amri hii itafanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 9 January, 2017 hadi tarehe 31 Desemba, 2017.

Mh. Zelote Stephen ameagiza kila mtumishi kuwa na mpango kazi wa mwaka 2017Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna Mstaafu Zelote Stephen ameagiza kila mtumishi wa serikali katika Mkoa wa Rukwa Kuwa na Mpango kazi, kuanzia siku ya kwanza ya mwaka mpya hadi siku ya mwisho, mpango kazi ambao utaonesha kila siku shughuli zake atakazokuwa anazifanya.