Tuesday, January 31, 2017

Mh. Zelote Stephen aungana na wananchi ujenzi wa Shule ya Sekondari Milundikwa


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Kasu Wilayani Nkasi katika ujenzi wa shule ya Sekondari Milundikwa baada ya shuke hiyo kuhamishwa utoka katika Kijiji cha Milundikwa ili kupisha kambi ya jeshi la kujenga taifa.

Katika zoezi hilo Mkuu wa Mkoa alishirikiana na wakuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule, na Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na ya Wilaya ya Nkasi.


"Nawashukuru sana, najua mnaratiba zenu na shughuli zenu mmeziacha ili kuja kushiriki kwenye ujenzi huu wa shule yetu ya sekondari ya Milundikwa, Jeshi walikuwa waungwana wakatuachia eneo lile na sasa wamerudi wamelihitaji, na wao ni amri tu," Mh. Zelote alisema.

"Katika kuboresha elimu, serikali ya awamu ya tano imehakikisha kwamba hakuna mwanafunzi anakayekaa chini na atakaekosa darasa la kusomea," Mh. Zelote aliongeza.

Katika kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa katika darasa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amesema kuwa Wilaya yake ina mpango wa kujenga madarasa matatu kwa kila shule, madarasa ambayo yatakuwa yakijengwa kwa nguvu za wananchi na kumaliziwa na serikali.

"Mpaka sasa kila kijiji kina benki ya matofali kwaajili ya ujenzi wa madarasa ya shule zilizopo katika maeneo yao, tunawahamasisha wananchi wajitahidi kuzalisha matofali mengi ikiwezekana kujenga madarasa zaidi ya hayo, nawashukuru wananchi wanaendelea kuitikia wito huo," Mh. Mtanda alifafanua.
No comments:

Post a Comment