Wednesday, March 1, 2017

TAARIFA YA POLISI YA MKOA WA RUKWA

OFISI YA,
KAMANDA WA POLISI MKOA,
RUKWA,
SLP 82,
SUMBAWANGA
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA RUKWA
KWA VYOMBO VYA HABARI.

PRESS RELEASE TAREHE 01.03.2017

KIJANA MMOJA AFARIKI BAADA YA KUPIGWA NA RADI HUKO MPUI.

Mnamo tarehe 27.02.2017 majira ya saa 02:00 usiku huko katika kitongoji cha Nankanga, kijiji cha Mkima, kata na tarafa Mpui, wilaya ya Laela, mkoa wa Rukwa.
Kijana wa miaka 26, Mkulima, Mkazi wa Mkima,Mnyika, aitwaye HIKA NAKATALE .Alikutwa akiwa amekufa baada ya kupigwa na radi wakati akiwa njiani kurudi nyumbani akitokea shambani akiwa ameongozana na na wake zake wawili ambao ni AGRIPINA KAUZENI, Miaka 23,Mfipa,Mkulima,na HURUMA MWANANJELA, Mfipa, Miaka 21,Mkulima, wote wakiwa ni wakazi wa Mkima.
Aidha katika tukio hilo mmojawapo kati ya wale wanawake wawili ambaye ni HURUMA MWANANJELA amelazwa zahanati ya kijiji cha Mkima baada ya kupigwa na radi kwa matibabu na anaendelea vizuri.
Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Polisi GEORGE SIMBA KYANDO anatoa rai kwa wananchi kuwa makini na kuepuka kukaa sehemu zenye miinuko au chini ya miti kwani hayo ndo mazingira hatarishi ya radi.

KIJANA MMOJA AUAWA KWA KUCHOMWA NA KISU KIFUANI HUKO MTOWISA.

Mnamo tarehe 28/02/2017 majira ya saa 08:00 mchana huko kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Lwanji, kata ya Zimba, tarafa ya Mtowisa, wilaya ya Sumbawanga mkoa wa Rukwa.
Kijana wa miaka 38, Msukuma, Mkulima, Mkazi wa Mtakuja, aitwaye MASUNGA KASINJE, Aliuawa kwa kuchomwa na kisu kifuani upande wa kushoto chini ya titi na kaka yake mwenye umri wa miaka 40, Msukuma, mkazi wa Mtakuja.
Chanzo cha mauaji ni ugomvi wa kugombania vyombo vya kupikia.
Aidha marehemu anaishi nyumbani kwa mtuhumiwa na aliazimishwa vyombo vya kupikia na ugomvi ulizuka pindi mtuhumiwa akidai vyombo vyake na hatimaye mtuhimwa kumchoma kisu marehemu.
Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari wa kituo cha afya Mtowisa na kubaini kuwa kifo cha marehemu kimetokana na kuvuja damu nyingi.
Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.
Mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Polisi GEORGE SIMBA KYANDO anatoa rai kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani suala lao lilikuwa dogo ambapo lingepelekwa hata katika ngazi za familia lingepatiwa ufumbuzi kuliko maamuzi aliyoyachukua kwani ni kinyume cha sheria za nje na ni kosa la jinai.

MWANAMKE MMOJA AFA MAJI HUKO NKASI

Mnamo tarehe 27/02/2017 majira ya saa 07:15 mchana huko katika Mto Tembwa, kijiji cha Mwinza, kata na tarafa ya Wampembe, wilaya ya Nkasi na mkoa wa Rukwa.
Mwanamke wa miaka 24, Mfipa, Mkulima, aitwaye GELISTAD NGALIKO, Alikufa maji baada ya kusombwa na maji wakati akivuka mto Tembwa.
Aidha marehemu alikuwa amembeba mtoto wake wa kike mgongoni aitwaye NAOMI mwenye umri wa miezi kumi ambaye hadi sasa mwili wake haujapatikana na juhudi za kuutafuta mwili wa mtoto huyo zinaendelea.
Chanzo cha kifo ni kukosa hewa baada ya kunywa maji mengi.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Polisi GEORGE SIMBA KYANDO anatoa rai kwa wananchi kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha masika. Aidha anatoa ushauri kwa wananchi kuwa makini pale wanapovuka mito kwa kina cha maji hakipimwi kwa macho pia watumie vivuko vilivyo rasmi. Pia anatoa wito kwa wananchi kwa yeyote atayeuona mwili au kumuokota mtoto kike waweze kutoa taarifa katika vituo vya polisi.

Imesainiwa na;
(G.S. KYANDO -ACP )
KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUKWA

No comments:

Post a Comment