Saturday, May 20, 2017

Serikali Mkoa wa Rukwa yawatahadharisha wananchi na Ugonjwa wa Ebola

Serikali ya Mkoa wa Rukwa imetoa tahadhari kwa wananchi kupitia kikao cha madiwani wa Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kilichoitishwa na Sekretarieti ya Mkoa ili kupewa mafunzo ya kupitia taarifa za fedha na tathmini ya utekelezaji wa programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha katika sekta ya umma awamu ya nne.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Tixon Nzunda

Tahadhari hiyo ilianza kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wakati alipokuwa akimalizia hotuba yake iliyolenga kuwaasa madiwani hao kuwa wasimamizi wa matumizi ya fedha katika Halmashauri zao na kuwafikishia ujumbe wa ugonjwa huo hatari wananchi katika kata wanazoziwakilisha.

Taarifa za Ugonjwa huo wa Ebola zimetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto baada ya kupata taarifa kutoka “International Helath Regulation – National Focal Point” kuhusu mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) uliotangazwa na Shirika la Afya Duniani siku ya tarehe 12 Mei, 2017.
Ugonjwa wa Ebola umethibitishwa kwa kupitia vipimo vya maabara baada ya kutokea wagonjwa 9 ambpo kati yao 3 wamepoteza maisha na wengine 6 wanaendelea na matibabu katika kituo kilichoandaliwa. Ugonjwa huo umetokea katika jimbo la North – East Basuele, Afrika ya Kati.

“Ebola ni ugonjwa wa kumuomba Mungu apitishie mbali sana na Mkoa wa Rukwa, ni ugonjwa mbaya, Rukwa ni Mkoa wa Mpakani na dalili zake zimeshaanza kutokea kwa jirani zetu DRC, sasa wako wengine wanaotoka kwenye mitumbwi kwenye mialo yetu wanaopanda mabasi na wanaoleta biashara zao, pamoja na mambo mazuri mtakayokwenda kuyafanya ondokeni na hilo mkatoe tahadhari kwa wananchi,” Mh. Zelote alifafanua.

Nae kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika alipata nafasi ya kuelezea dalili anazopata mgonjwa ili kujua kuwa mgonjwa ameathirika na Ebola na kuongeza kuwa ugonjwa huo hauna tiba wala kinga na endapo utakupata kupona si rahisi.
“Miongoni mwa dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu makali ya misuli, kuumwa kichwa na vidonda kooni, kuhara na kutapika na mara nyingine kutokwa na damu nyingi ndani na nje ya mwili na kujikinga kwake ni kumuepuka mgonjwa aliyeathirika na ugonjwa huo,” Dkt. Mtika alifafanua.

Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Tixon Nzunda kwa kulisisitiza hilo aliwakumbusha kuwa kinga ni bora kuliko tiba na kuweka wazi kuwa ugonjwa huo hauna tiba na kuwaasa walichukue jambo hilo na kulisambaza kuanzia kazi ya kijiji, hadi mtu kwa mtu.

“Tulichukue kama jambo la dharura na la kimkakati, tulifanyie kampeni kuanzia ngazi ya kijiji, kitongoji na tukienda mbali zaidi hadi ngazi ya mtu kwa mtu wa maana ya ngazi ya familia, tusisubiri yatukute,” Nzunda alibainisha.

Ugonjwa wa Ebola ni kati ya magonjwa yenye hatari ya kusambaa na kuleta madhara makubwa ya kiafya duniani, ingawa hadi sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa ama kuthibitishwa kuwa ana virusi vya ugonjwa wa Ebola.


No comments:

Post a Comment