Tuesday, July 11, 2017

RC Rukwa awatoa wasiwasi wakulima kuhusu suala la barabara vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstafu Zelote Stephen Zelote amewatoa wasiwasi wakulima wanaolalamikia ubovu wa barabara vijijini kwa kusisitiza mpango wa serikali kuanzisha wakala wa barabara mijini na vijijini ili kuondoa kero hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa (katikati), akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen(kushoto) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Gen. Mstaafu Rafael Muhuga (kulia) pamoja na wadau wa usindikaji wa mafuta ya alizeti wa mikoa hiyo.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu hoja ya mmoja wa wakulima Frank Enock aliyeilalamikia serikali kushindwa kuboresha miundombinu vijijini ili kupata urahisi wa kusafirisha mazao kwa kipindi chote cha mwaka.

Hoja hiyo iliibuka wakati wa majadiliano katika mkutano wa uzinduzi wa mradi wa Taasisi ya Kuendeleza Mifumo ya Kimasoko katika Kilimo AMDT uliofanyika Mkoani Songwe na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi ambapo mgeni rasmi wa uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa. 

Mbali na wakuu wa Mikoa mkutano huo pia ulijumuisha wakurugenzi wa Halmashauri, mafisa kilimo wa mikoa na halmashauri, wakulima, pamoja na wasindikaji wa mafuta ya alizeti huku lengo kuu likiwa ni kuboresha zao la kilimo cha alizeti ili kumkomboa mkulima mdogo.

“Kuhusu suala la miundiombinu serikali imeliona hilo tatizo na ndio maana kimeanzishwa kitu kinaitwa TARURA wakala wa barabara mijini na vijijini kwaajili ya kuboresha barabara kuona kuwa zinatengenezwa na zinapitika, kwahiyo msiwe na wasiwasi, barabara hizo zimelenga kuwainua wakulima kwa kuwawezesha kusafirisha mazao yao kwa urahisi na hatimae bei za mazao kupungua kutokana na kurahisishwa kwa njia za kusafirishia,” Mh. Zelote alisisitiza.

Na kuongeza kuwa uanzishwaji wa wakala huo utaondoa ubabaishaji uliokuwa katika halmashauri ambazo hudanganya katika utekelezaji wao wa kujenga barabara za uhakika na ama kuzichelewesha.
Katika kukazia suala la maendeleo na nia ya serikali ya awamu ya tano katika kumkomboa mwananchi, Mh. Zelote alisisitiza msimamo wa Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kuhakikisha wananchi wa kipato cha chini ndio wanaoangaliwa kwa jicho la pekee ili anyanyuke, Mh. Zelote alisema,

“Tukitaka kuendelea katika taifa hili tufate yale rais wetu anayosema kila siku kwamba tusihangaike na mtu ambaye ameshasonga mbele, tuhangaike na mtu ambaye anataka kusonga mbele, mwananchi wa kawaida”

Pamoja na hayo Mh. Zelote aliahidi kuwa balozi mzuri katika kuwafikishia ujumbe wananchi juu ya umuhimu wa zao la alizeti katika kujikomboa katika umasikini.

“Tukirudi katika mikoa yetu tutakwenda kuhangaika na yule mwananchi ambae anataka kujikomboa ili tumkomboe na mkombozi mmoja wapo ni alizeti kwani hatujajitosheleza kwenye suala la mafuta lakini tunaweza kujitosheleza kwasababu tuna kila kitu kwenye jambo hili, watu wapo, nguvu ipo, ardhi ipo, wataalamu wapo na mahitaji yapo”.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa amewasisitiza watumishi kufanya kazi kwa umoja kuanzia kwa maafisa ugani hadi kwa wakuu wa idara na kusisitiza kuwa Hakuna anayemiliki miradi na kuwa miradi yote ni ya serikali.

“Utamkuta afisa ugani anasema mradi huo haunihusu unasimamiwa na Fulani, tukimkuta kama huyo tutamshughulikia na wakulima wanakijiji wote mkikutana na afisa ambaye hatoi ushirikiano kwenye miradi ya serikali badi nyie tupigieni simu ili tumshughulikie, haiwezekani alipwe mshahara halafu asifanye kazi, wakati wote anavizia posho tu,” Mh. Galawa alisema

No comments:

Post a Comment