Sunday, July 23, 2017

"Wananchi tujitolee Damu" Dk. Kigwangala

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Dk. Hamis Kigwangala amesikishwa na hali ya hospitali ya mkoa wa Rukwa kukosa damu ya kutosha kusaidia wagonjwa pindi dharura inapotokea.

Masikitiko hayo aliyatoa baada ya kufanya ukaguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika ziara yake ya siku moja ambapo alitembelea hospitali hiyo pamoja na vituo vya afya vitatu vya Laela Wilayani Sumbawanga, Wampembe na Nkomolo vya Wilaya ya Nkasi.
Dk. Hamis Kigwangala (kushoto) akiongea na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mh. Julieth Binyura pamoja na watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa. 

“Nimesikitishwa na changamoto ya upatikanaji wa damu, kwanza mna units chache mlipaswa kuwa na units karibu 120 ili kuendana na idadi ya watu milioni 1.2 wa mkoa mzima, lakini kwa bahati mbaya hamna hata damu moja ambayo imekuwa “screened” na tayari kwa matumizi, hii inasikitisha sana lakini kwa ujumla maabara iliyopo ni nzuri sana, kuna mapungufu machache sana kwenye “theatre” na pia nimefurahishwa na “labour ward” iko vizuri sana.

Dk. Kigwangala alibainisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa damu ipo katika kanda ya nyanda za juu kusini na kuahidi kulishughulikia jambo hilo huku akiwaasa wananchi kuweza kujitokeza kwa wingi kuchangia damu na si kukaa vipembeni na kulalamika pindi wanapokosa damu hospitali wakati wanashindwa kujitolea damu.

“Mimi binafsi najitolea damu mara tatu kwa mwaka, wananchi tunatakiwa kujitolea damu ili kuweza kuwasaidia wale wanaohitaji, huwezi jua inaweza kumsaidia ndugu, jirani ama rafiki, hivyo tuwe na moyo wa kujitolea.” Alisema.

Katika ziara yake hiyo mambo aliyoyapa kipaumbele ni kuangalia huduma za maabara, vyumba vya upasuaji, vyumba vya kuzalia pamoja na akiba ya damu salama, ambapo vituo hivyo vilionekana kufanya vizuri katika maeneo hayo.

Huduma ya maji katika vituo hivyo ilioneka kuwa ni kikwazo katika upatikanaji wa huduma bora hivyo Dk. Kigwangala aliwaagiza wakurugenzi wa Sumbwanga Vijijini pamoja na Halmashauri ya Nkasi kuhakikisha jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi wa haraka kwa kutambua umuhimu wa maji na ubora wa huduma za afya.

Dk. Kigwangala hakutaka ziara hiyo iwe ya kiutendaji pekee hivyo alikutana na wananchi wa maeneo ya Laela pamoja naWampembe na kuwapa nafasi ya kueleza vikwazo wanavyokutana navyo katika kupata huduma bora ya afya.

Ndipo alipojitokeza ndugu Nassoro Ibrahim na kutaka kufahamu nafasi ya walemavu katika kupata huduma bure kama ilivyo katika makundi ya wazee, watoto na wajawazito, “Naomba Serikali ituangalie na sisi walemavu tunnapata shida sana maana wenzetu wazee, watoto na kinamama wanasaidiwa,”Alisema.


Katika kujibu swali hilo Dk. Kigwangala alimtaka mlemavu huyo kuonana na uongozi ili aweze kufuata taratibu za kuweza kutibiwa bure lakini alimuahidi kuwa serikali ipo katika mkakati kuona namna ambayo wanaweza kuwasaidia walemavu katika kupata huduma bure.

No comments:

Post a Comment