Friday, November 17, 2017

“Mshirikiane na SIDO kuwa na Viwanda 25 kwa kila Halmashauri hadi Disemba 2018,” RC Wangabo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameziagiza halmashauri nne za mkoa huo kushirikiana na Shirika la viwanda vidogo nchini SIDO kuhakikisha wanakuwa na viwanda vipya 25 hadi kufikia Disemba mwaka 2018 ili kutimiza agizo la serikali la kuwa na viwanda 100 vipya kwa kila Mkoa.

Amesema kuwa SIDO ndio msaada mkubwa wa kuhakikisha kuwa ndoto hii inatimia kwani shirikia hilo limejaa wataalamu lakini pia hutoa mafunzo ya viwanda vidogo na vya kati kwa wajasiliamali hivyo hawana budi kuwa nao karibu.

“Serikali imekwishaagiza tuwe na viwanda 100 hadi kufikia Disemba mwaka 2018 na kwa mahisabu ya haraka mkoa una Halmashauri nne, 100 ukigawa kwa nne ni 25, kwahiyo hadi kufikia Disemba 2018 kila Halmashauri iwe na viwanda hivyo vipya, na msaada upo kuna SIDO hapo ambao wataalamu wamejaa na wanatoa mafunzo kila siku ya viwanda vidogo na vya kati watawasadidia na mimi nitalisismamia,” Alisema

Ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya diwani wa kata ya Mtowisa Mh. Edgar Malini. alipomkabidhi Mh. Wangabo Skafu iliyotengenezwa na kilichokuwa kiwanda cha nguo katika kata hiyo ambacho kilifungwa miaka zaidi ya 30 na kubaki majengo.

Mh. Edgar Malini alisema kuwa kiwanda hicho kilifunguliwa na Aliyekuwa Waziri Mkuu Mh. Rashid mfaume Kawawa lakini kwa sasa uzalishaji wake umekwama kwani pamba haipatikani kwenye maeneo yao na hivyo kuwa na mazingira magumu ya uzalishaji wa nguo katika kiwanda hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule akitoa maelezo ya Kumtambulisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa wananchi wa kijiji cha Zimba kata ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga. wakati walipofika kwenye kijiji hicho kuona kiwanda cha kukamulia alizeti. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akisalimiana na Mzee Gabriel Joseph wakati wa kujitambulisha kwa wananchi wa kijiji cha Zimba Wilayani Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu kutoka kulia) akiuliza swali kwa mhandisi wa maji wa Wilaya Patrick Ndimbo (wa kwanza kushoto) wakati walipotembelea mradi wa maji wa kutumia umeme wa jua mji mdogo Laela Wilayani Sumbawanga wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.8. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akivishwa Skafu na Diwani wa Kata ya Mtowisa Mh. Edgar Malini, Skafu hiyo ni mabaki ya miongoni mwa skafu zilizokuwa zikitengenezwa na kiwanda cha nguo kilichokuwepo katika kata hiyo na hivi sasa kimebaki majengo tu.


Kwa sasa Mkoa wa Rukwa una jumla ya viwanda 950 huku kukiwa na kiwanda kikubwa kimoja, viwanda vya kati 2 na viwanda vidogo 947. 

No comments:

Post a Comment