Sunday, December 3, 2017

Waziri Tizeba aagiza wanaouza mbegu feki wafungiwe maduka yao

Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba ameiagiza Taasisi ya Uthibitishaji Rasmi wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kufanya ukaguzi wa duka kwa duka kwenye maduka ya wafanyabiashara wa pembejeo ili kuwabaini wanaouza mbegu feki na na kuwafungia biashara zao ikibainika wanafanya hivyo.

Amesema kuwa kuwa suala la mbegu feki linawakatisha tamaa wakulima ambao wanategemea kilimo kwaajili ya kuendesha maisha yao na kuwa serikali ya awamu ya tano haitalivumilia jambo hilo na itaendelea kumtetea mkulima nae afaidike kwa kazi anayoifanya.

“Mkulima badala ya kupata gunia 15 hadi 20 anaambulia gunia tano na wananchi wengi hawana uwezo wa kugundua kwamba kinachomsababisha asivune ni mbegu feki, yeye atadhani labda ni hali ya hewa kumbe ni mwizi mmoja kwa tamaa zake amekwamisha maendeleo ya mkulima huyu,” Mh. Tizeba alisisitiza.

Ameyasema hayo alipotembelea shamba la msipazi lililopo katika Kijiji cha china, Wilayani Nkasi na kulalamikiwa na mmiliki wa shamba hilo Salum Sumry aliyeuziwa mbegu feki na Johanes Sanga mwenye duka linaloitwa Gadu Store na kumfungulia kesi mahakamani, kesi ambayo inaendelea hadi leo.

Mh. Tizeba amesema kuwa kesi hizo hazifai kuendeshwa na mkulima badala yake watu wa TOSCI wanatakiwa kuingilia kati ili kupambana na wauzaji hao wa mbegu feki ili kulimaliza tatizo hilo.

Aidha, Waziri Tizeba ameagiza watu wa udhibiti wa mbolea kushughulikia suala la bei elekezi katika mbolea kuhakikisha maduka yote ya pembejeo nchini wanabandika mabango ya bei elekezi za mbolea nje ya maduka yao ili kila mkulima na mnunuzi aweze kuelewa bei hizo na kuongeza kuwa bei hizo elekezi ni kwaajili ya mnunuzi wa mwisho kijijini na sio makao makuu ya Mkoa au Wilaya.

“Huu mzaha wa bei elekezi kuuzwa kwa jumla Mkoani au Wilayani likome, wafuatilie watu waweke matangazo kwenye maduka yao, kwamba bei za Mkoani na Wilayani sio zile zilizotangazwa za mkulima, hizo za mkulima ni kijijini ndipo ananunua ile bei iliyotangazwa na serikali, sio Namanyere kule anatakiwa kuuza chini yah apo,” Mh. Tizeba alifafanua.

Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Lazaro Kitandu amefafanua kuwa mfumo ulioanzishwa na serikali wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja unarahisisha upatikanaji wa mbolea nyingi kwa wakati mmoja na hivyo mbolea kuwa na bei ya chini.

“Mfumo huu unadhibiti ununuzi wa mbolea kutoka kwenye chanzo usafirishaji wake, gharama za bandari, gaharama za usafirishaji ndani ya nchi na ile faida anayotaka kuweka mfanyabiashara, kwahiyo hakuna tena nafasi kwa mfanyabiashara kujiongezea bei pasipokjuwa na uhalali, hakuna tena kumnyonya mkulima pasipo halali,” Kitandu alifafanua.

Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba (katikati) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (Wa pili kushoto) Kaimu Mkurugenzi wa Mazao Wizara ya Kilimo Beatus Malema (wa kwanza Kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule (wa pili kulia) Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa David Kilonzo (wa Kwanza Kulia) katika picha ya pamoja. 

Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba (kaunda suti ya blu) akimsikiliza mmoja wa wakulima wa maharage katika kijiji cha Ilambila, Wilayani Kalambo akiwa na Naibu Waziri wa OR - TAMISEMI Mh. Josephat Kandege (kaunda suti nyeupe).

Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba (kushoto) akimuelekeza mmoja wa wakulima wa maharage katika kijiji cha Ilambila, Wilayani Kalambo (katikati)  akiwa na Naibu Waziri wa OR - TAMISEMI Mh. Josephat Kandege (kulia).


Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba (kulia) akimsikiliza mkurugenzi wa shamba la msipazi  Salum Sumry (kushoto) kati kati ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda. 
Waziri wa Kilimo Mh. Charles Tizeba akitoa maelekezo.

Gari kwaajili ya Kilimo cha Kisasa lililopo katika Shamba la Msipazi, Wilayani Nkasi. No comments:

Post a Comment