Monday, April 30, 2018

Mufti wa Tanzania aiombea dua Rukwa

Mwananchi ashangazwa na visanduku vya maoni serikalini


Mwananchi wa Kijiji cha Mtowisa, Kata ya Mtowisa, Tarafa ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga Pius Wapinda ameshangazwa na kitendo cha taasisi mbalimbali za kiserikali kuweka visanduku kwaajili ya kukusanyia maoni ya wananchi lakini hakuwahi kupata mrejesho wa maoni hayo kufanyiwa kazi.
Mwananchi huyo aliiomba serikali kuyafanyia kazi maoni hayo na kufanya mrejesho kupitia mikutano na vikao mbalimbali vinavyofanywa na serikali katika ngazi tofauti ili wananchi wawe na moyo wa kuendelea kutoa maoni hayo pindi wanapoona yanafanyiwa kazi.
“ukipita kwenye maofisi ya kiserikali kuna masunduku mbalimbali pale, yale masanduku ya maoni mimi huwa sioni kama yana maana yoyote na sijui yanatusaidia kitu gani maana sioni mrejesho wake, ningependelea kwenye mikutano kama hii wangekuwa wanatuambia kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa kumi tumepokea maoni kadhaa na mrejesho wake ni huu hapa,” Alieleza.
Nae Afisa utumishi wa Halamashuri ya Wilaya ya Sumbawanga Hamis Mangale alisema kuwa ni mwezi mmoja tu tangu akabidhiwe ofisi hiyo na hakufahamu kama utaratibu wa dawati la malalamiko halifanyiwi kazi hivyo aliahidi mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kulichukua hilo na kuhakikisha wanalifanyia kazi ili kukata kiu ya wananchi ambao wengi wamekuwa na malalamiko yanayohusu masuala ya mapenzi.
Katika Kusisitiza hilo Mh. Wangabo alisema kuwa maoni hayo ni vyema yakachukuliwa na taasisi husika ikiwa ni hospitali kuna kamati ya afya, yajadiliwe katika kamati hiyo na hatimae wananchi wapatiwe mrejesho katika vikao mbalimbali kuanzia ngazi ya Kijiji hadi kata.  

Friday, April 20, 2018

Wenyeviti wa vijiji wapewa onyo kali kuhusu vitambulisho vya NIDA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya vikali wenyeviti wa vijiji wananojihusisha na kuwajazia watu wasio raia wa Tanzania fomu za mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) ili kuhalalisha uwepo wao katika nchi na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria.
Pia aliwaasa wananchi kuwa macho na wale wanaopewa fomu hizo hali ya kuwa sio raia na hawastahili kupewa vitambulisho hivyo na kuwasisitiza kuwa walinzi wa kwanza wa taifa la Tanzania ili wananchi ambao ni raia wa Tanzania wanaostahili kupata fomu hizo ndio wapatiwe.
“Mwenyekiti yoyote wa Kijiji akibainika amemwandikisha mtu amabae sio raia, ambae hastahili na hana vibali husika vinavyomruhusu apate kitambulisho cha taifa, ukibainika tunakukamata tunakuweka ndani, halafu tunakufungulia mashataka kwasababu utakuwa msaliti na unalisaliti taifa letu, na nyie wananchi ndio macho yetu yeyote mnaeona sio raia na amepewa fomu muwekeeni kipingamizi, kwasababu sheria inaruhu,” Alisema.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha mtowisa, kata ya mtowisa, wilayani Sumbawanga alipokwenda kutemebelea na kuijionea miradi kadhaa ya kimaendeleo inayoendelea kutolewa katika ukanda  wa bonde la ziwa Rukwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya taifa (NIDA)Mkoani Rukwa Emanuel Mjuni amesema kuwa katika kata ya Mtowisa wanatarajia kuwaandikisha wananchi 5,430 na kusisistiza kuwa wale wasiokuwa wakazi wa kata hiyo hawana vigezo vya kupata fomu na hatimae kukosa vigezo vya kupata vitambulisho hivyo vya taifa.
“Kama tukiwaandikisha wananchi ambao hawaishi kwenye maeneo yetu wale wananchi ambaotumewaandalia fomu hizo watakosa, kama Mh. Mkuu wa Mkoa alivyosema wale wenyeviti na watendaji wa vijiji wasimamie kwa makini kuhakikisha yule anaepata fomu ni mkazi halali wa eneo husika na zoezi hili linafanyika nchi nzima hivyo basi wale ambao wapo huku kibiashara ama kwa mambo mengine warudi kwenye maeneo yao ili waandikishwe, ili wasikose vitambulisho,” Alisisitiza.
Majibu hayo yaliibuka baada ya maswali kadhaa kutoka kwa wananchi Pius Wapinda na Paulo Chipeta waliotaka kujua endapo ni ruhusa kwa wafanyabiashara kuchukua fomu za maombi ya vitambulisho vya taifa katika eneo ambalo zoezi hilo limemkuta ili aweze kuchukua fomu na kupata kitambulisho na hatimae kuwa na utambulisho wa uraia wa nchi yake na pia hatua zitakazochukuliwa kwa wenyeviti watakaokiuka taratibu za kutoa fomu.

Mti wamshangaza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Thursday, April 19, 2018

wasichana zaidi ya 26,000 kupata Chanjo ya HPV, Rukwa
Zaidi ya Wasichana 26,000 wenye umri wa miaka 14 wanatarajia
kupatiwa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi mkoani Rukwa ikiwa ni
juhudi za serikali ya mkoa kuwakinga wasichana hao kutokana na madhara makubwa
yanayoweza kuwapata pindi wanapofikia umri wa utu uzima.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa chanjo ngazi ya mkoa kwaajili ya
maandalizi ya utoaji wa chanjo mpya ya kinga dhidi ya saratani ya mlango wa
kizazi kwa wanawake mkoani Rukwa.
 “Kwa Mkoa
wetu wa Rukwa, jumla ya wasichana 26,234 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hii
muhimu, Wazazi na Walezi, wahakikishe kuwa watoto wa umri
wa miaka 14 wanaenda katika vituo vya kutolea huduma za chanjo kupata chanjo.
Naomba kuwahakikishia wananchi kuwa chanjo zinazotolewa katika vituo vyetu ni
salama na zinatolewa na wataalamu wenye uzoefu waliopatiwa mafunzo,” Alisema.

Nae Mganga mkkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu amesema
kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuanza katika wiki ya mwisho wa mwezi wanne ambayo
itakuwa ni wiki ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa nchi nzima ambapo
uzinduzi wake ulifanyika tarehe 10, Aprili mwaka huu.

 Pia ametaja sababu
kadhaa zinazosababisha ugonjwa huo ikiwemo watoto wa kike kushiriki tendo la
ndoa wakiwa katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, uvutaji wa sigara na
kuonya kuwa dalili zake hujitokeza baada ya saratani hiyo kusambaa mwilini.

“Baadhi ya dalili za saratani ya
mlango wa kizazi ni pamoja na kutokwa damu ya hedhi bila mpangilio, kutokwa
damu baada ya tendo la ndoa, maumivu
ya mgongo, miguu na/au kiuno, kuchoka,
kupungua uzito, kukosa hamu ya kula, kutokwa
uchafu wa rangi ya kahawia au wenye damu ukeni na kuvimba miguu,”Alisema.

Kwa upande wao mwakilishi wa viongozi wa dini ambae ni
katibu wa Bakwata Mkoani Rukwa Mohamed Adam amesema kuwa kama viongozi wa dini
watahakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha waamini wao
kujiunga na juhudi za serikali katika kupunguza vifo vinavyosababishwa na
saratani ya mlango wa kizazi.

Imeelezwa kuwa, nchini Tanzania zaidi ya asilimia 36 ya
wagonjwa wa saratani wanaugua saratani ya mlango wa kizazi ikiwa na wastani wa
wagonjwa 51 kwa kila kinamama 100,000, na kuongoza kwa kusababisha vifo
ikifuatiwa na saratani ya matiti ambazo kwa pamoja husababisha zaidi ya
asilimia 50 ya vifo vyote vya akina mama vitokanavyo na saratani.

Monday, April 9, 2018

RC Wangabo afanikisha kupatikana Ekari 3 kujenga nyumba za polisi Mtowisa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amefanikisha kupatikana
kwa ekari 3 ili kujengwa kwa nyumba za askari polisi katika eneo la karibu na
kituo cha polisi kipya kinachomaliziwa kujengwa katika kata ya Mtowisa,
Wilayani Sumbawanga na kurahisisha makazi ya polisi katika bonde la ziwa Rukwa.
Hayo yamejiri ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya wananchi wa
kata ya Mtowisa kwa Mkuu wa Mkoa waliyoiahidi tarehe 13.11.2017 Mh. Wanagabo
alipofanya ziara katika eneo hilo na kudai kuwa usalama wa bonde hilo sio mzuri
kwa kukosa kituo bora cha polisi na makazi yao na kupelekea kuanzisha ujenzi wa
kituo na hatimae kuomba nguvu ya Mkuu wa Mkoa kuweza kumalizia ujenzi huo.
“Nilipokuja mwaka jana tuliwekeana agano na mkasema
mtatafuta eneo kwaajili ya ujenzi wa nyumba za polisi ya kwangu nimekamilisha
Milioni 5 mlizohitaji kumalizia ujenzi wa kituo cha polisi sasa bado zamu yenu,”
Mh. Wangabo alisema.

Mtendaji wa Kata ya Mtowisa Paulo Katepa alimuhakikishia MKuu
wa Mkoa kuwa eneo hilo limeshapatikana na tayari kwa kukabidhi kwa askari
polisi kwaajili ya taratibu nyingine za kisheria na kumuhakikishia kuwa eneo
hilo halihitaji fidia ya aina yoyote na kwamba wananchi wa Kijiji cha Mtowisa
wameridhia bila ya kusukumwa, na kufanya yote kwaajili ya usalama wao na wa
mali zao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoawa Rukwa ACP George
Kyando amekiri kupokea eneo hilo la ekari 3 na kuahidi kuwatuma vijana wake ili
waanze maandalizi ya kuweka alama zinatakazobainisha eneo hilo na maeneo
mengine ili waendelee na taratibu nyingine za kisheria ili kumiliki eneo hilo
kihalali.

RPC Rukwa atahadharisha mauaji kwa wivu wa mapenzi