Wednesday, May 30, 2018

RC Wangabo kutumia nguvu ya dola kukomesha Kipindupindu


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema atalazimika kuwatumia polisi kusimamia zoezi la usafi na ujenzi wa vyoo salama katika Kijiji cha Namasinzi, kata ya Kapenta, bonde la ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga baada ya wananchi hao kushindwa kujenga vyoo hivyo mbali na elimu ya umuhimu wa vyoo waliyopewa kwa muda mrefu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akikabidhi tenki la lita 5000 kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Liweliyamvula, Kijiji cha Lumbesa, Kata ya Kapenta, Wilayani Sumbawanga Paulo Maufi, ikiwa ni miongoni mwa juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama na kuhifadhiwa sehemu salama, kuepukana na kipindupindu. 


Amesema kuwa ikifikia hatua hiyo Kijiji hicho kitafungiwa na hakuna atakayetoka wala kuingia na hatimae kusitisha shughuli za kiuchumi za Kijiji hicho ambacho ni maarufu kwa kilimo cha mpunga hali itakayopelekea maisha magumu kwa wananchi hao jambo ambalo asingependa litokee.

Katika kuhakikisha hali hiyo haitokei Mh. Wangabo alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule na timu yake ya usafi ya halmashauri kuhakikisha wanapita kaya kwa kaya ili kuzibaini kaya zisizopenda usafi na zisizokuwa na vyoo na kuzichukulia hatua za kisheria kwani kwa kushindwa kufanya hivyo kipindupindu hakitamalizika katika bonde hilo.

“Sasa tutatumia nguvu ya dola, ili kuhakikisha kwamba kila mtu anaishi katika maisha ya usafi wala sio uchafu, na kila mtu ahakikishe kwamba anakuwa na kiboko Fulani ambacho ni kigumu amuone mtu anachemsha maji, anayaweka maji yake yanapoa akienda shambani anakwenda na maji mbayo yamekwisha poa, lakini mkilea lea hivi, waswahili wanasema ukicheka na nyani unavuna mabua, mabua ambayo tunayavuna ni vifo.” Alisisitiza.

Aliyasema hayo katika Mkutano wa hadhara alioufanya katika  kijiji cha Namasinzi, Kata ya Kapenta, Wilayani Sumbawanga, kijiji ambacho wananchi watatu wamefariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine wakiendelea kupatiwa huduma. 

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hlamshauri ya Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Fani Musa aliendelea kuishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka misaada katika bonde hilo ili kuhakikisha wanakabiliana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa wataendelea kutoa elimu bila ya kuchoka akiamini kuwa wananchi hao wataelewa wakiendelea kusimamiwa.

“Serikali imekuwa ikifanya kazi tatu kwa wakati mmoja, tumekuwa tukitoa elimu ya ugonjwa huu kwa lengo la kuzuia haya yasitokee, lakini yakitokea tunatumia nguvu kubwa ya kukabiliana na tatizo hili lakini pia serikali inatoa dawa za kutosha ili kuweza kuponya pia, ugonjwa wa kipindupindu ni kitendo cha kula kinyesi ambacho ni kibichi, hivyo watu ni muhimu kujenga vyoo salama,” Alimalizia.

Tangu kulipuka kwa ugonjwa huo tarehe 6 Mei, 2018 watu 14 wameshafariki na wengine 221 wakiendelea na kupatiwa matibabu katika kambi za wagonjwa hao katika bonde la ziwa Rukwa.

Wednesday, May 23, 2018

Watendaji wanaochangia kuenea kipindupindu Rukwa kushughulikiwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema
hatamvumilia mtendaji wa serikali atakaechangia kuenea kwa ugonjwa kipindupindu
katika mkoa kwani elimu ya ugonjwa huo imeshatolewa kwa muda mrefu hivyo ni
jukumu la kila mtendaji kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa.

Amesema kuwa kumekuwa na tabia iliyojengeka ya watendaji
kuanza kufanya majukumu yao baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kutokea na kuonya
kuwa kaya ambayo haitakuwa na choo katika ngazi ya Kijiji basi mtendaji wa Kijiji
atawajibishwa.

“Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa, tukikidhibiti
kipindupindu halafu kikatokea tena hapo mahali ambapo kimetokea hatutapaelewa, watendaji
wetu wakitilia maanani  wakahakikisha
kaya zetu zina vyoo na kuchemsha maji hatuwezi kuwa na kipindupindu, sasa
kinatokea kipindupindu halafu kaya haina choo, mtendaji wa Kijiji hicho hana
sababu ya kuwa mtendaji,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo alipokuwa akifunga kikao cha dharura
kilichoitishwa na kamati ya afya ya mkoa ili kujadiliana juu ya mbinu za
kutokomeza ugonjwa huo ambao umeathiri zaidi ya watu 600 tangu kulipukwa kwake
mwezi November mwaka 2017 na kutoweka mwezi Machi mwaka 2018 na hatimae kuibuka
tena tarehe 6, Mei mwaka 2018.

Kikao hicho kilichojumuisha, Wakuu wa ilaya, Wakurugenzi wa halmashauri,
Wenyeviti wa halmashauri, madiwani, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya,
Maafisa Afya wa mkoa na halmashauri, wataalamu wa afya pamoja na waganga wakuu
wa wilaya na mganga mkuu wa mkoa kiliazimia kutokomeza ugonjwa huo na kuweka
mikakati ya kutorejea tena wa ugonjwa huo.

Akisoma baadhi ya maazimio Katibu Tawala wa Mkoa Benard
makali amesema kuwa kamati ya afya za vijiji na vitongoji zisimamiwe kutenda
majukumu yake kwani wao ndio wanaojuana zaidi katika utekelezaji wa maagizo na
sheria za serikali kuanzia ngazi hizo na kuitaka kamati za afya za Wilaya kuwa
na mbinu za kudumu za kuthibiti ugonjwa huo na kutaka elimu zaidi iendelee
kutolewa.

Tangu kulipuka tena kwa ugonjwa huo tarehe 6, Mei mwaka 2018
wagonjwa 9 wamefariki na wengine 214 wakiendelea kupatiwa matibabu katika vituo
mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambayo imeathirika zaidi
huku wananchi wake wakiwa na asilimia 36 ya umiliki wa vyoo bora.

Mganga Mkuu Rukwa atoa elimu ya kina ya Kipindupindu Rukwa

Tuesday, May 22, 2018

Saba Wafariki kwa kipindupindu Rukwa.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule
amethibitisha kufariki kwa wagonjwa saba wa kipindupindu katika Wilaya ya
Sumbawanga huku wagonjwa wengine 44 wakibaki wodini kuendelea kupatiwa matibabu
na wagonjwa 115 wakiruhusiwa kurudi nyumbani.

Amesema kuwa ugonjwa huo umelipuka tarehe 6 Mei, 2018 katika
Kijiji cha Mayenje, kata ya Milepa katika bonde la ziwa Rukwa na kusambaa
katika meneo mengine ya Wilaya na hatimae kupatikana kwa wagonjwa wawili katika
hospitali ya rufaa ya mkoa.

“Sasa hivi katika bonde la ziwa Rukwa kuna shughuli za
uvunaji wa mpunga na hivyo watu wengi hutokea huku juu kwenda bondeni kutafuta
vibarua vya kuvuna mpunga kwenye maeneo hayo yaliyoathirika na kipindupindu,
maji yanayotumika huko ni machafu kutoka katika madimbi na mito nawaomba
viongozi wa dini watoe tahadhari kwa waumini hasa katika maeneo yale
yalioathirika zaidi,” Alisema.

Alisema hayo alipopewa nafasi ya kutoa taarifa hiyo ya
ugonjwa wa kipindupindu na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wakati wa
Mkutano uliowakutanisha wadau wa afya Mkoani hapa kwaajili ya kuzungumzia
tahadhari ya ugonjwa wa Ebola uliopo katika nchi ya jirani ya Kongo.

Kwa upande wake Mh. Wangabo alisema kuwa elimu ya tahadhari
itatolewa kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara ya wakuu wa wilaya,
madiwani pamoja na wakurugenzi ili ifikie hatua ya kusema “kipindupindu sasa
basi”.


Wanarukwa watolewa mashaka kuhusu Ebola.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatoa mashaka wanarukwa
juu ya kutokuwepo kwa ugonjwa wa Ebola katika Mkoa na kutahadharisha yeyote anaejaribu
kuleta hofu ya ugonjwa huo katika Mkoa na kuwataka wananchi wasijengewe hofu
bali waendelee kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema kuwa Mkoa unaendelea kushirikiana na sekta
mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya udhibiti ikiwemo
kutoa taarifa na elimu kwa jamii kwa kadiri itakavyohitajika ili ugonjwa huo
usiingie katika mkoa.

“Katika kipindi hiki ambacho tunatakiwa kuchukua tahadhari
kubwa, wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa ni lazima tuwe na mshikamano, umoja na
tahadhari kubwa sana na hasa maeneo yale ya Ziwa Tanganyika ambako kuna
muingiliano wa watu kutoka Zambia, DRC, Rwanda na Burundi. Lakini pia
wanaotokea maeneo mengine ya nchi, la muhimu ni kuchukua tahadhari kubwa sana,”
Alisema

 Ameongeza kuwa
wenyeviti wa vijiji wajizatiti katika kuboresha taarifa za wakazi wao kwenye madaftari
yao na kuwa makini na wageni wanaoingia kwenye maeneo yao pamoja na kuitaka
idara ya uhamiaji kuhakikisha wageni wote wanaingia katika njia zilizo rasmi.

Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa afya
Mkoa kilichoitishwa na Mganga Mkuu wa mkoa ili kutoa elimu kwa wawakilishi wa
makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo waandishi wa habari juu kusambaza ujumbe
huo wa kujihadhari na ugonjwa huu hatari wa Ebola.

Mmoja wa wadau hao akiwakilisha kundi la wazee, Zeno Nkoswe
amesema kuwa serikali ya Mkoa haina budi kuhakikisha elimu hiyo inafikishwa kwa
viongozi wote wa dini kwani wao wanauwezo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi na
kwa muda ufupi na ujumbe hatimae kutimiza malengo ya kufisha ujumbe huo kwa
wananchi.

Akichangia mjadala huo mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila amesema kuwa serikali haina
budi kutumia redio zilizopo Mkoani Rukwa ili kufikisha ujumbe huo kwa watu wote
na maeneo yote ya Mkoa na mikoa ya jirani ili watu waweze kujikinga na ugonjwa
huo.

Ugonjwa wa Ebola upo katika nchi ya jirani ya Jamhuriya watu
wa Kongo katika mji wa Biroko, jimbo la Equator na kwa taarifa za shirika la
afya duniani, hadi kufikia tarehe 17 Mei, 2018 watu 44 walikuwa wamebainika
kuwa na ugonjwa huo na watu 23 kufariki.


Monday, May 14, 2018

RC Wangabo aagiza DED kuchunguzwaMkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza Katibu Tawala
wa Mkoa kuanzisha mchakato wa kinidhamu na uchunguzi mara moja dhidi ya
Mkurugenzi wa Halamashauri ya Wialaya ya Kalambo kutokana na utendaji kazi wake
usioriddhisha.

Amesema kuwa mkurugenzi huyo amekuwa akichelewesha juhudi za
serikali baada ya kushindwa kumaliza ujenzi wa upanuzi wa kituo cha afya cha Mwimbi
kwa wakati na kuchelewa kuanza ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Legeza mwendo
hata baada ya kupatiwa Shilingi Bilioni 1.1 na serikali kwaajili ya vituo vyote
viwili vilivyopo katika halmashauri hiyo.

“Huyu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo
utendaji wake siridhwi nao hata kidogo katika mazingira ya sekta ya afya kwa
ujumla wake, ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika kituo cha afya cha
Mwimbi ulianza mwezi wa nane mwaka 2017 mpaka leo naongea hapa mwezi wa tano
mwaka 2018 kituo cha afya kile bado hakijakamilika,” Alisema
Ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wauguzi katika siku yao
ya wauguzi duniani iliyoadhimishwa kimkoa katika kata ya Laela, Wilaya ya
Sumbawanga.

Tuesday, May 8, 2018

Miradi ya Tsh. Bilioni 20 kupitiwa na Mwenge wa Uhuru Rukwa.
Mwenge wa Uhuru wa Tanzania unaratajiwa kuweka mawe ya
msingi, kukagua na kuzindua miradi yenye thamani ya shilingi 20,499,194,866 Mkoani
Rukwa ikiwemo miradi ya maendeleo 43 na vikundi 48 katika kutekeleza malengo ya
serikali ya awamu ya tano nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo alipokuwa akisoma hotuba ya mapokezi ya mwenge huo wa Uhuru katika Kijiji
cha Kizi mpakani na Mkoa wa Katavi.

Mh. Wangabo alibainisha kuwa katika fedha hizo wananchi
wamechangia shilingi 654,373,600, halmashauri zikiwa zimechangia shilingi
323,187,500, na serikali kuu nayo ikiwa imechangia 15,958,184,766 huku wadau
wengine wakiwa wamechangia shilingi 3,563,499,000.

Aidha Mh. Wangabo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa
kumaliza kukimbiza mwenge ukiwa salama na kuwatunza wakimbiza mwenge na kuingia
katika MKoa wa  Rukwa wakiwa na afya
nzuri na kumuhakikishia kuukimbiza mwenge huo wa uhuru kwa amani na usalama
katika kipindi chote ukiwepo katika Mkoa wa Rukwa

“nikuhakikishie kuwa Wakimbiza Mwenge wote wa Kitaifa
mliotukabidhi tutawalea, tutawatunza na kuwaenzi na kuhakikisha kuwa
wanahitimisha Mbio za Mwenge katika Mkoa wetu kwa amani na utulivu.” Alisema.

Mwenge wa uhuru wa mawaka huu ukiwa umebeba kauli mbiu ya
‘Elimu ni ufunguo wa maisha; Wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu’ Mh.
Wangabo amesema kuwa wanafunzi waliojiunga na darasa la kwanza kwa shule za
msingi wamevuka maoteo ambapo wanafunzi 50,887 sawa na asilimia 106, huku
wanafunzi wa shule ya awali wakifikia 39,486 ambayo ni sawa na asilimia 92 ya
maoteo.

Mkoa wa rukwa ni mkoa wa sita kutembelewa na mwenge wa
uhuru tangu kuwashwa kwake mkoani Geita mwanzoni mwa mwezi wan ne mwaka huu, na
kutegemewa kukimbizwa kwa zaidi ya kilomita 721 katika Halmashauri nne ndani ya
mkoa wa Rukwa.


Tuesday, May 1, 2018

Mufti wa Tanzania apongeza ushirikiano baina ya waislamu na serikali ya ...


Shekhe Mkuu na Mufti wa Tanzania Aboubakar Bin Zuber Bin Ali amepongeza ushirikiano uliopo baina ya baraza la waislamu la Mkoa  pamoja na serikali ya Mkoa wa Rukwa katika kutatua kurekebisha au kuyaweka sawa masuala mablimbali kwa maslahi ya watanzania.
“siku zote huwa nawaamnbia viongozi wangu hawa wa baraza kwamba wafanye kila wanachokifanya lakini wahakikishe kuwa wanajenga mahusiano mazuri na serikali ya mahala walipo, baada ya kujenga mahusiano na wananchi wa dini zote basin a serikali pia na katika eneeo hili ninapowauliza panaonesha pana mashirikiano mazuri, cha kusema ni kwamba ushirkinao na uhusiano uendelee na udumu vizuri kwasababu ndio utakaoweza kujenga nchi yetu katika masuala yote ya maendeleo,” alisema.
Wakati akisoma taarifa ya Mkoa, mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na waislamu katika kuiletea nchi maendeleo na kumuomba mufti wa Tanzania kuikumbuka Rukwa katika mipango yao mbalimbali ya uwekezaji katika sekta ya afya, maji, elimu na viwanda.
“Baada ya serikali kutangaza elimu bure kuna mafuriko ya wanafunzi huko mashuleni, hii inaonesha kwamba bado miundombinu ya elimu bado haitoshelezi hivyo tunahitaji kwenye eneo hilo ushirikinao wa kujenga shule za msingi, sekondari na hata vyuo, sisi ni eneo la pembezoni lakini tunapenda kuliita eneo la kipaumbele hivyo kwenye mipango yako basi utuweke kwenye eneo la kipaumbele,” Alisema.
Mufti wa Tanzania atafanya ziara ya siku mbili katika Wilaya ya Sumbawanga pamoja na Nkasi, akizindua na kuweka mawe ya msingi katika misikiti pamoja na kituo cha afya kilichopo kata ya kirando, Wilayani Nkasi.