Tuesday, May 8, 2018

Miradi ya Tsh. Bilioni 20 kupitiwa na Mwenge wa Uhuru Rukwa.
Mwenge wa Uhuru wa Tanzania unaratajiwa kuweka mawe ya
msingi, kukagua na kuzindua miradi yenye thamani ya shilingi 20,499,194,866 Mkoani
Rukwa ikiwemo miradi ya maendeleo 43 na vikundi 48 katika kutekeleza malengo ya
serikali ya awamu ya tano nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo alipokuwa akisoma hotuba ya mapokezi ya mwenge huo wa Uhuru katika Kijiji
cha Kizi mpakani na Mkoa wa Katavi.

Mh. Wangabo alibainisha kuwa katika fedha hizo wananchi
wamechangia shilingi 654,373,600, halmashauri zikiwa zimechangia shilingi
323,187,500, na serikali kuu nayo ikiwa imechangia 15,958,184,766 huku wadau
wengine wakiwa wamechangia shilingi 3,563,499,000.

Aidha Mh. Wangabo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa
kumaliza kukimbiza mwenge ukiwa salama na kuwatunza wakimbiza mwenge na kuingia
katika MKoa wa  Rukwa wakiwa na afya
nzuri na kumuhakikishia kuukimbiza mwenge huo wa uhuru kwa amani na usalama
katika kipindi chote ukiwepo katika Mkoa wa Rukwa

“nikuhakikishie kuwa Wakimbiza Mwenge wote wa Kitaifa
mliotukabidhi tutawalea, tutawatunza na kuwaenzi na kuhakikisha kuwa
wanahitimisha Mbio za Mwenge katika Mkoa wetu kwa amani na utulivu.” Alisema.

Mwenge wa uhuru wa mawaka huu ukiwa umebeba kauli mbiu ya
‘Elimu ni ufunguo wa maisha; Wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu’ Mh.
Wangabo amesema kuwa wanafunzi waliojiunga na darasa la kwanza kwa shule za
msingi wamevuka maoteo ambapo wanafunzi 50,887 sawa na asilimia 106, huku
wanafunzi wa shule ya awali wakifikia 39,486 ambayo ni sawa na asilimia 92 ya
maoteo.

Mkoa wa rukwa ni mkoa wa sita kutembelewa na mwenge wa
uhuru tangu kuwashwa kwake mkoani Geita mwanzoni mwa mwezi wan ne mwaka huu, na
kutegemewa kukimbizwa kwa zaidi ya kilomita 721 katika Halmashauri nne ndani ya
mkoa wa Rukwa.


No comments:

Post a Comment