Tuesday, May 22, 2018

Wanarukwa watolewa mashaka kuhusu Ebola.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatoa mashaka wanarukwa
juu ya kutokuwepo kwa ugonjwa wa Ebola katika Mkoa na kutahadharisha yeyote anaejaribu
kuleta hofu ya ugonjwa huo katika Mkoa na kuwataka wananchi wasijengewe hofu
bali waendelee kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema kuwa Mkoa unaendelea kushirikiana na sekta
mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya udhibiti ikiwemo
kutoa taarifa na elimu kwa jamii kwa kadiri itakavyohitajika ili ugonjwa huo
usiingie katika mkoa.

“Katika kipindi hiki ambacho tunatakiwa kuchukua tahadhari
kubwa, wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa ni lazima tuwe na mshikamano, umoja na
tahadhari kubwa sana na hasa maeneo yale ya Ziwa Tanganyika ambako kuna
muingiliano wa watu kutoka Zambia, DRC, Rwanda na Burundi. Lakini pia
wanaotokea maeneo mengine ya nchi, la muhimu ni kuchukua tahadhari kubwa sana,”
Alisema

 Ameongeza kuwa
wenyeviti wa vijiji wajizatiti katika kuboresha taarifa za wakazi wao kwenye madaftari
yao na kuwa makini na wageni wanaoingia kwenye maeneo yao pamoja na kuitaka
idara ya uhamiaji kuhakikisha wageni wote wanaingia katika njia zilizo rasmi.

Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa afya
Mkoa kilichoitishwa na Mganga Mkuu wa mkoa ili kutoa elimu kwa wawakilishi wa
makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo waandishi wa habari juu kusambaza ujumbe
huo wa kujihadhari na ugonjwa huu hatari wa Ebola.

Mmoja wa wadau hao akiwakilisha kundi la wazee, Zeno Nkoswe
amesema kuwa serikali ya Mkoa haina budi kuhakikisha elimu hiyo inafikishwa kwa
viongozi wote wa dini kwani wao wanauwezo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi na
kwa muda ufupi na ujumbe hatimae kutimiza malengo ya kufisha ujumbe huo kwa
wananchi.

Akichangia mjadala huo mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila amesema kuwa serikali haina
budi kutumia redio zilizopo Mkoani Rukwa ili kufikisha ujumbe huo kwa watu wote
na maeneo yote ya Mkoa na mikoa ya jirani ili watu waweze kujikinga na ugonjwa
huo.

Ugonjwa wa Ebola upo katika nchi ya jirani ya Jamhuriya watu
wa Kongo katika mji wa Biroko, jimbo la Equator na kwa taarifa za shirika la
afya duniani, hadi kufikia tarehe 17 Mei, 2018 watu 44 walikuwa wamebainika
kuwa na ugonjwa huo na watu 23 kufariki.


No comments:

Post a Comment