Wednesday, May 23, 2018

Watendaji wanaochangia kuenea kipindupindu Rukwa kushughulikiwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema
hatamvumilia mtendaji wa serikali atakaechangia kuenea kwa ugonjwa kipindupindu
katika mkoa kwani elimu ya ugonjwa huo imeshatolewa kwa muda mrefu hivyo ni
jukumu la kila mtendaji kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa.

Amesema kuwa kumekuwa na tabia iliyojengeka ya watendaji
kuanza kufanya majukumu yao baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kutokea na kuonya
kuwa kaya ambayo haitakuwa na choo katika ngazi ya Kijiji basi mtendaji wa Kijiji
atawajibishwa.

“Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa, tukikidhibiti
kipindupindu halafu kikatokea tena hapo mahali ambapo kimetokea hatutapaelewa, watendaji
wetu wakitilia maanani  wakahakikisha
kaya zetu zina vyoo na kuchemsha maji hatuwezi kuwa na kipindupindu, sasa
kinatokea kipindupindu halafu kaya haina choo, mtendaji wa Kijiji hicho hana
sababu ya kuwa mtendaji,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo alipokuwa akifunga kikao cha dharura
kilichoitishwa na kamati ya afya ya mkoa ili kujadiliana juu ya mbinu za
kutokomeza ugonjwa huo ambao umeathiri zaidi ya watu 600 tangu kulipukwa kwake
mwezi November mwaka 2017 na kutoweka mwezi Machi mwaka 2018 na hatimae kuibuka
tena tarehe 6, Mei mwaka 2018.

Kikao hicho kilichojumuisha, Wakuu wa ilaya, Wakurugenzi wa halmashauri,
Wenyeviti wa halmashauri, madiwani, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya,
Maafisa Afya wa mkoa na halmashauri, wataalamu wa afya pamoja na waganga wakuu
wa wilaya na mganga mkuu wa mkoa kiliazimia kutokomeza ugonjwa huo na kuweka
mikakati ya kutorejea tena wa ugonjwa huo.

Akisoma baadhi ya maazimio Katibu Tawala wa Mkoa Benard
makali amesema kuwa kamati ya afya za vijiji na vitongoji zisimamiwe kutenda
majukumu yake kwani wao ndio wanaojuana zaidi katika utekelezaji wa maagizo na
sheria za serikali kuanzia ngazi hizo na kuitaka kamati za afya za Wilaya kuwa
na mbinu za kudumu za kuthibiti ugonjwa huo na kutaka elimu zaidi iendelee
kutolewa.

Tangu kulipuka tena kwa ugonjwa huo tarehe 6, Mei mwaka 2018
wagonjwa 9 wamefariki na wengine 214 wakiendelea kupatiwa matibabu katika vituo
mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambayo imeathirika zaidi
huku wananchi wake wakiwa na asilimia 36 ya umiliki wa vyoo bora.

No comments:

Post a Comment