Tuesday, June 12, 2018

Kamati ya watu wenye ulemavu Rukwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu.


Kamati ya watu wenye ulemavu Mkoa wa Rukwa imeaswa kuhakikisha inawatambua watu wenye ulemavu na kubaini mahitaji yao pamoja na kuona namna ya kutatua changamoto zao ili kuweza kuwasaidia katika kufikia malengo yao katika sekta mbalimbali za kimaendeleo.
“Katika Mkoa wa Rukwa tunachamoto kubwa juu ya namna ya kuwahudumia watu wenye ulemavu, kwani mara nyingi watu hawa wamekuwa wakileta malalamiko yao katika ofisi hii, hivyo uwepo wa kamati hii utapunguza sana changamoto wanazokabiliana nazo ndugu zetu hawa.”Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipokuwa akizindua kamati ya watu wenye ulemavu ngazi ya Mkoa.
Ameongeza kuwa ni matumaini ya serikali kuwa kamati hiyo itazisimamia kamati zote zilizopo chini yake kuanzia ngazi ya halmashauri, mitaa na vijiji ili kujua idadi ya watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kufikia ngazi ya halmashauri na kupeleka taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Kwa upande wake akisoma taarifa ya kamati katibu wa kamati ya watu wenye ulemavu mkoa Godfrey Mapunda amezitaja changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na taarifa sahihi juu ya haki zao, kutokuwepo kwa miundombinu isiyozingatia hali za watu wenye ulemavu zinazowapelekea kushindwa kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na Imani potofu kwa jamii inayowapelekea kushindwa kupata elimu na mahitaji muhimu.
Na kueleza majukumu ya kamati hiyo ikiwa ni pamoja na “Jukumu la kwanza itakuwa ni kutambua haki na uwezo wa watu walio na ulemavu katika mkoa lakini pia kuwasaidia watu wenye ulemavu na familia zao na kupanga mipango yenye ufanisi ili kupunguza umasikini kupitia shughuli za kujiingia kipato, kuratibu shughuli zote za watu wenye ulemavu katika mkoa, kulinda na kukuza ustawi wa watu wenye ulemavu katika Mkoa,” Alisema.
Hadi kamati hiyo inazinduliwa na Mkuu wa Mkoa asilimia 42 ya kamati za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya Kijiji hadi halmashauri zilikuwa zimeshaundwa na walemavu 774 wamebanika huku maazimio ya kamati hiyo ikiwa ni kuhakikisha kamati zinaundwa kwa asilimia 100 na walemavu wote kutambulika na kuwa na takwimu sahihi ili kuweza kuwafikishia huduma stahiki.
Hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa alilolitoa alipohudhuria hafla ya chakula cha mchana kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee mapema mwezi wa pili mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment