Wednesday, October 31, 2018

Jazia kupunguza uhaba wa Dawa Rukwa


Serikali kupitia ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeanzisha mfumo wa Jazia Prime vendor kwaajili ya kupata dawa na vifaa tiba pale vinapokosekana katika Bohari ya Dawa (MSD), mfumo ambao unakuwa na mzabuni mmoja atakayesambaza dawa na vifaa tiba ndani ya mkoa mzima.

Kupitia utaratibu huo Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kupitia katibu tawala wa mkoa Bernard Makali wamewekeana saini na mzabuni ambaye ni kampuni ya Maranatha Pharmacy Ltd,  atakayesambaza dawa na vifaa tiba hivyo kuanzia katika ngazi ya zahanati katika halmashauri nne za mkoa, ili kuongeza upatikanaji wake.

Akifungua hafla hiyo fupi ya kuwekeana saini mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa mfumo huo utawezesha na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu pale ambapo vitakuwa havipatikani MSD.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Bernard makali (Kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy Ltd. Bw. Stephen Lengeni (kushoto) wakiweka saini katika mkataba wa kusambaza dawa na vifaa tiba kwa mkoa wa Rukwa. 

“Mfumo huu unaendeshwa kwa kumlipa mzabuni fedha mara tu baada ya vituo husika kuchukua dawa na vifaa tiba na si kwa mkopo. Maana yake vituo vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kuhakikisha vina fedha kabla ya kupeleka mahitaji yao kwa mzabuni,” Alisema.


Aidha alitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanasimamia vyema mapato na matumizi ya fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha fedha zilizotengwa kwaajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba zinatumika kwa mujibu wa miongozo iliyopo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Maranatha Pharmacy Ltd alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuiamini kampuni yake ambayo hadi sasa imeingia mikataba na mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya pamoja na Rukwa ambapo mara ya mwisho kufanya kazi na serikali ilikuwa mwaka 2006 wakati ambao mifumo ilikuwa haiku sawa.

Mbali na kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa mfumo huu unatarajiwa kuboresha huduma kwa wazee, ambapo mkoa una jumla ya wazee 14,832 waliopatiwa vitambulisho vya kupatiwa matibabu bure.


No comments:

Post a Comment