Wednesday, October 10, 2018

Viwanda 54 vyaanzishwa Rukwa kabla ya kuisha mwaka 2018


Katika kufikia malengo ya kampeni ya serikali ya “Mkoa Wetu, Viwanda Vyetu” inayolenga ujenzi wa viwanda vipya 100 ikiwemo vikubwa, vya kati na vidogo. Mkoa wa Rukwa hadi kufikia June, 2018 tayari imefikisha nusu ya idadi ya viwanda hivyo huku kila halmashuri ikiwa inakaribia kufikia lengo lake.

Katika kutekeleza kampeni hiyo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliitaka kila Halmashauri kuhakikisha inaanzisha viwanda 25 ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia Desemba 2018 ili kutimiza viwanda 100 katika Mkoa wenye Halmashauri nne.

Kabla ya kampeni hiyo ya viwanda iliyozinduliwa na Waziri wa OR – TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo, Mkoa ulikuwa na jumla ya viwanda 901. Lakini tangu kutolewa kwa agizo la Waziri pamoja na Mkuu wa Mkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imeongeza viwanda vidogo 19, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, viwanda 11, Halamshauri ya Wilaya ya Nkasi, Viwanda 11 na Manispaa ya Sumbawanga, viwanda 13.

Kutokana na ongezeko hilo, sasa Mkoa wa Rukwa una jumla ya viwanda 955. Kupitia kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa rukwa kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu wa kumi Mh. Wangabo alitumia fursa hiyo kuendelea kuwahamasisha wajasiliamali na wafanyabiashara waliopo ndani nan je ya mkoa kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo mkoani Rukwa kuanzisha viwanda.
Mmoja wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Energy Sembe Kilichombo Manispaa ya Sumbawanga akiendelea na kazi yake. 

“Mkoa unaendelea kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye masuala mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa viwanda na tayari baadhi ya wadau wanaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika ujenzi wa Viwanda katika Mkoa wetu. Hivyo basi, nitoe wito kwenu tuendelee kushirikiana na kuhamasisha wadau mbalimbali kuja kuwekeza katika Mkoa wetu.” Alisema.

Katika Kuchangia hilo mbunge wa Kwela Mh. Ignus Malocha alimtoa hofu Mkuu wa mkoa na kueleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni kutokuwepo kwa nishati ya umeme katika maeneo mengi ya mkoa wa Rukwa. Na kumuahidi kuwa endapo umeme utapatikana basi kuna wakulima na wafanyabiashra ambao wapo tayari kuanzisha viwanda katika bonde la ziwa Rukwa.

“Katika jambo hili tunapozungumzia masuala ya viwanda, tuanze kuangalia kipaumbele cha kusukuma umeme katika maeneo ambayo yanaweza yakaleta tija na ikaonekana kwa mkoa mzima, kila mtu anataka atumie umeme katika kuzalisha, shida umeme umechelewa lakini wateja wetu wameshatanguliza vifaa vyao kama kujenga magodown na mashine mbalimbali kwaajili ya mpunga, mahindi na samaki, wanasubiri umeme,” Alibainisha.

Kwa upande wake meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Rukwa Frank Chambua amesema kuwa kikazo kikubwa cha kuchelewesha kufikisha umeme kwenye maeneo 1274 ni bajeti kutoka serikalini na kuwaomba wabunge wa mkoani humo kuendelea kuiomba serikali kuwapatia bajeti ya kutosha ili kufikia maeneo yote ya mkoa.

“Mkoa wa rukwa upo tofauti sana na mikoa mingine, zamani mkoa haukuwa na miundombinu, kwahiyo vijiji vingi havikuendelea sana kuhitaji umeme, sasa baada ya barabara hizi kuisha, vijiji vimekuwa na uhitaji wa umeme ni mkubwa mno, sidhani kama kuna mkoa Tanzania amnbao uhitaji wa umeme ni mkubwa kuliko Rukwa,” Alisema.

No comments:

Post a Comment