Thursday, November 15, 2018

Vijana, wanawake na walemavu wala neema Manispaa ya Sumbawanga


Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga imetoa shilingi milioni 70.5 kwa vikundi 21 vya vijana, wanawake na walemavu ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa hundi kwa moja ya vikundi vilivyopewa Mkopo katika manispaa ya Sumbawanga. 
Manispaa ya Sumbawanga imedhamiria kutekeleza maelekezo ya serikali kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuwezesha vikundi hivyo ambapo tangu mwaka wa fedha 2018/2019 uanze mwezi Julai hadi mwezi Novemba Halmashauri tayari imeshakusanya Shilingi bilioni 1.1 ambayo ni nusu ya makusanyo ya malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu.

Fedha hizo zilitolewa katika hafla fupi ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliyekabidhi hundi kwa vikundi hivyo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule, Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na vikundi husika.

Akisoma taarifa ya kukabidhi fedha hizo kwa vikundi Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisisitiza kuwa Ili dhamira ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati na Tanzania yenye Viwanda itimie shughuli utoaji wa mikopo lazima iwe endelevu na kuwa halmashauri imejiimarisha katika kukusanya mapato yake ya ndani ili kuleta matunda kwa kutoa mikopo.

“Vikundi hivi  vinajishughulisha na Usindikaji mafuta, chakula,vinywaji, Useremala, Utengenezaji wa Chaki na ushonaji, ufumaji na utengenezaji wa Mabatiki na Ufugaji wa kuku na ngombe wa maziwa. Pia Halmashauri inatarajia kutoka kiasi cha mkopo kilichobakia kwa mwezi Januari, 2019 kitakachokuwa kimekusanywa kutokana na makusanyo ya ndani.” Alisema.

Aliongeza kuwa ili kuona vikundi hivyo vinakuwa kiuchumi maafisa maendeleo ya jamii  ngazi ya kata na halmashauri kuhakikisha wanakuwa na orodha ya vikundi vilivyokopeshwa, kwaajili kufuatilia shughuli za vikundi na kuwajengea uwezo pamoja na kubaini mwendo wa urejeshaji wa mikopo kwa vikundi  na kufanya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo.

KWa upande wake Mh. Wangabo aliipongeza Manispaa ya Sumbawanga na kwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri zizlizopo Mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kuweza kukuza kipato cha mwananchi wa Mkoa kwa kuwawezesha kiuchumi na hatimae kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi wa viwanda.

Pi aliwapongeza wale waliofanikiwa kupata mikopo hiyo na kuwasihi waweze kurudisha kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya kukopeshwa na kujikwamua na kuwaonya kutotumia fedha hizo kwa matumizi ambayo yako tofauti na walichoombea.

“Serikali haitafurahishwa kuona fedha zilizokopwa zinatumika kwa malengo ambayo hayakukusudiwa kama vile anasa, aidha, nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote ndani ya Mkoa wetu kupitia hafla hii, kuweka mipango na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na wadau mbalimbali wa maendeleo  ndani na nje ya Mkoa kwa kadiri itakavyowezekana.”Alisisitiza.

Kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018 fedha zilizopaswa kuchangiwa na Halmashauri yetu kama asilimia 10 ya mapato ya ndani ni shilingi 684,055,823. Hata hivyo hadi kufikia Juni 2018 jumla ya shilingi 50,000,000 zilitolewa kwa vikundi 43 sawa na asilimia 7.3 ya lengo. kiasi cha shilingi 634,055,823 hakikutolewa kutokana na mwenendo wa makusanyo.

Thursday, November 8, 2018

RC Wangabo afika kwenye ghala la TFC na kukuta patupu

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametembela ghala la kuhifadhia mbolea la Kampuni ya Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Company – TFC) na kutokuta hata mfuko mmoja wa mbolea huku wakulima wakijiandaa na msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 huku mvua zikitarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga na Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga walipotembelea moja ya maduka ya wauzaji wa mbolea yaliyopo mjini Sumbawanga. 

Mh. Wangabo amefanya ziara fupi katika maghala kadhaa ya wafanyabiashara binafsi pamoja na makampuni yaliyopo mjini sumbawanga na kukuta shughuli za uletaji wa mbolea ukiendelea kwa maandalizi yam simu wa kilimo huku Kampuni ya Mboleaa Tanzania (TFC) ikikosa hata mfuko mmoja katika ghala lao jambo lililowashanga walioambatana na Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo.
“Tutawasiliana na viongozi wa TFC ili tuweze kujua kwanini hawaleti mbolea ya kutosha wakati hii ni kampuni ya serikali inaweza ikaleta mbolea nyingi kuliko hata hao wengine lakini badala yake “godown” (ghala) kubwa lakini hakuna kitu, nini manufaa ya TFC sasa,” Alihoji.
Awali akisoma taarifa ya kampuni hiyo msimamizi wa ghala hilo Jelio Mahenge alisema kuwa msimu wa kilimo wa mwaka 207/2018 kampuni ilifanikiwa kusambaza tani 1082 na kuwa msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 kampuni imejipanga kuleta jumla ya tani 2500 kwa awamu ya kwanza.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kampuni inafanya jitihada zote za hali na mali kuhakikisha uletaji wa mbolea unatekelezeka ndani ya mwezi huu wa kumi na moja ili kuendana na msimu wa kilimo na kuleta tija kwa wakulima na nchi kwa ujumla,”
Msimu wa Kilimo wa mwaka 2017/2018 Mkoa ulitumia zaidi ya tani 24,000 za Mbolea ya kupandia (DAP) na mbolea ya kukuzia (UREA) na msimu wa kilimo wa mwaka 2018/2019 mkoa unatarajiwa kutumia zaidi ya tani 34,000 na mpaka mwanzoni mwa mwezi huu Mkoa umepokea tani 363.75 ambazo tayari zikiwa ndani ya maghala ya wafanyabiashara wa mbolea na nyingine zikiwa njiani.

RC Wangabo asisitiza upandaji miti kuzuia maafa huku wa mabondeni wakiamuliwa kuhama.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri kuhakikisha wanatekeleza sheria ya upandaji miti kwa kila nyumba ili iwe ngao dhidi ya upepo mkali unaosababisha maafa na kuwafanya wanachi hao kukosa mahala salama pa kukaa na wengine kuharibikiwa na vyombo vyao.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyenyoosha kidole) akionyesha moja ya nyumba zilizoathirika na upepo mkali na mvua kubwa zilizonyesha mapema mwezi huu katika kijiji cha Kichangani, kata ya kirando Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa, alipokwenda kutoa pole kwa waathirika hao. 

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiingia katika moja ya nyumba zilizoathiriwa na upepo mkali ulioambatana na mvua pamema mwezi huu katika kijiji cha Kichangani, kata ya kirando Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa.

Miongoni mwa nyumba zilizoathiriwa na upepo mkali ulioambatana na mvua pamema mwezi huu katika kijiji cha Kirando, kata ya kirando Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa.

Ameyasema hayo alipokwenda kuwatembelea walioathiriwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa iliyoezua paa za nyumba zipatazo 27 na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni 26 katika Tarafa ya kirando, Wilayani Nkasi.

“Mh. DC tuwe wakali katika hili, kuhakikisha kwamba nyumba ambayo haina miti inayozunguka lile eneo la makazi tuhakikishe kwamba tunachukua hatua stahiki za mazingira, halmashauri mnajua hata kwenye vibali vya ujenzi huwa mnasema lazima muwe na miti angalau minne kama sio mitano lakini hakuna anaefuatilia kwamba hiyo miti ipo? Sadsa ni wakati muafaka wa kufuatilia taratibu zote,” alisisitiza.

Mh. Wangabo aliongeza kuwa wale wote waliojenga kwenye mabonde ya mpunga wajue kwamba maeneo hayo si salama na kama watapatwa na maafa yoyote wasiitegemee serikali kuwahudumia kwasababu serikali imeshatoa onyo juu ya uhatari wa makazi hayo na kuwataka wananchi wasiishi kwenye maeneo hatarishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amesema kuwa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi inaendelea kutoa elimu ya ujenzi wa nyumba bora na katika kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa kamati za ujenzi za vijiji zinaendelea kuundwa katika kila kijiji ikimabatana na jukumu la kuhamasisha upandaji wa miti.


DC Nkasi aonya wanaotishia hali mbaya kiuchumi.


Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda amewaonya wale wote wanaowatia hofu wananchi wa mwambao wa ziwa Tanganyika juu ya ugumu wa maisha baada ya kufanyika oparesheni ya kukamata wavuvi haramu katika mwambao huo.

“kuna kikundi kidogo cha watu kazi yao kuwajaza wananchi hofu, baada ya suala la (operesheni ya) Samaki kuanza tulipokea kama simu sita saba hivi wengine wakitoka hapa kirando, tukafuatilia, tukawaita wale maafisa wanaofanya oparesheni, tukakaa nao, tulikuwa tunaambiwa huruhusiwi hata kusafirisha samaki hata kama ni mmoja, tukajua hali ni mbaya, tuliuliza nia ya operesheni tukaambiwa ni kudhibiti uvuvi haramu sio kuzui biashara ya samaki,” Alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda

Ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wavuvi hao walizozielekeza  kwa Mkuu wa Mkoa akiwa ziara fupi kata ya kirando ili kujionea maafa yaliyotokea siku chache zilizopita yalisababishwa na mvua kali na kuharibu nyumba 27 na kutia hasara ya shilingi milioni 26.

Ameongeza kuwa wavuvi hao walikuwa wanalalamika kutozwa kuanzia milioni tano kama faini ya kukiuka sheria za uvuvi lakini baada ya mkuu wa Wilaya huyo kutangaza aliyetozwa kiasi hicho ajitokeze ili arudishiwe fedha yake, hakutokea hata mwananchi mmoja.

Aliwataka watu kuacha hofu na wengine kuacha kuwapa wenzao hofu kwa kuwaambia kuwa shughuli za uvuvi hivi sasa hakuna na kwamba watu wanaotegemea shughuli hizo watalala na njaa jambo ambalo si la kweli.

Mmoja wa wavuvi hao Ali Seif alisema kuwa wavuvi wamekuwa wakitozwa faini kubwa kuliko kawaida ikiwemo faini ya shilingi milioni tano na milioni kumi huku mvuvi mwingine Rashid Huseni aliongeza kuwa wakazi wa Kijiji cha Kirando kwa asilimia 99 wanategemea ziwa Tanganyika kwaajili ya vipato vya vya kuendesha maisha hivyo operesheni hiyo inawakosesha vipato hivyo na kusababisha watu wajiingize kwenye uhalifu.

Akitoa maelekezo ya Serikali katika utekelezaji wa zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alisisitiza kuwa aliapa kuitetea na kuilinda sheria ya nchi na hana mpango wa kwenda kinyume na sheria ambayo ilishapitishwa ila ataendelea kusisitiza utekelezaji wake hadi hapo itakapobadilishwa na vyombo husika.

RC Wangabo atembelea kituo cha Afya na kukuta madudu


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza mkurugenzi wa halmasshauri ya Wilaya ya Kalambo kuhakikisha anampatia taarifa ya kila wiki juu ya maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Kanyezi, kilichopo kata ya Kanyezi wilayani Kalambo.

Maesema kuwa tangu kuanza kwa miradi ya upanuzi na ujenzi wa vituo vya afya katika halmashauri hiyo kumekuwa na ubabaishaji hasa wa kuchelewa kununua vifaa vya ujenzi pamoja na malipo kwa mafundi ambapo ujenzi huo unatumia mfumo wa “Force Account” kutekeleza kazi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa mbele) akiongoza ukaguzi wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Kanyezi, Wilayani Kanyezi, Wilaya ya Kalambo. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wanne toka kushoto) akiwa na wataalamu wa ofisi yake na wa halmashauri pamoja na wananchi wakikagua ujenzi wa kituo cha afya cha Kanyezi. 

Moja ya majengo ya Kituo cha Afya cha Kanyezi katika kijiji cha kanyezi, kata ya Kanyezi Wilayani Kalambo. 

“Sasa wewe afisa mipango, Mkurugenzi, kuanzia sasa hivi nataka muwe mnanipa taarifa “on weekly basis” (za kila wiki) kwamba nini kinachoendelea katika ujenzi huu, nisingependa tabia hii ya kusua sua iendelee, muiache mara moja, mnaumiza hawa wajenzi, halafu hamuwezi kuwalipa fidia, ingekuwa hawatimizi wajibu wao ingekuwa kitu kingine, kama ilivyotokea kule Kijiji cha Legeza mwendo fundi akakimbia ni kwasababu ya namna hii ubabaishaji wa malipo, mjipange,” Alisisitiza.

Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kimepandishwa hadhi kutoka kuwa zahanati ya kijiji cha Kanyezi na kukuta zimebaki siku 15 kutakiwa kukabidhi majengo hayo lakini bado wapo katika hatua ya linta.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa halmashauri hiyo Bw. Erick Kayombo aliahidi kuwa pamoja na kucheleweshewa kupata fedha lakini halmashauri tayari imeshaagiza vifaa vyote vinavyotakiwa kwaajili ya kumalizia ujenzi.

Kauli hiyo ya Mh. Wangabo ilikuja baada ya mmoja wa vibarua bw. Hamisi Pesambili kumlalamikia Mkuu wa Mkoa juu ya kucheleweshewa vifaa kwaajili ya kuendelea na ujenzi hali inayowafanya waishi kwa taabu huku wakiwa wameacha familia zao mjini sumbawanga na kwa siku kulipwa shilingi 10,000 fedha ambayo hawaridhiki nayo.

Katika kulirekebisha hilo, Mh. Wangabo alimuagiza mhandisi wa Halmashauri ambaye pia ni msimamizi wa jengo hilo kuhakikisha kuwa wanasimamia malipo ya mafundi wadogo kutoka kwa mafundi wao na sio kuishia kuwalipa mafundi huku hawajui kama vibarua hao wanalipwa kama walivyokubaliana na mafundi wao na kuongeza kuwa kutolipwa vizuri kwa vibarua kunaweza kupelekea majengo kutokuwa na ubora unaotarajiwa.

Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kujenga vituo vitatu vya afya katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na kutumia zaidi ya shilingi bilioni moja kwaajili ya ujenzi na utanuzi huo huku ikielekeza shilingi bilioni 1.5 kwaajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.

RC Wangabo atoa njia mbadala kuwanufaisha wavuvi


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewashauri wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi na Kalambo kuchangamkia fursa ya kibiashara iliyojitokeza baada ya operesheni ya kukamata wavuvi haramu na wasafirishaji wa samaki wanaotumia magari ya abiria kuzuiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003.

Amesema kuwa sheria hiyo hairuhusu mabasi ya abiria kupakiza samaki wanaozidi kilo 20 ambao katika hali ya kawaida ni samaki wa kitoweo nyumbani tofauti na hapo ni samaki wa biashra ambao mwananchi anatakiwa kulipia ushuru na kuongeza kuwa bidhaa hizo zinakuwa na magari yake maalum kwaajili ya kazi hiyo ambayo kwa sasa hayapo katika kusafirishia samaki kutoka mwambao hadi sumbawanga mjini.

“Kuna mazingira ambayo lazima sisi wenyewe tuanze kuyawekea utayari na watu wengine wachukulie kama fursa, kama unaambiwa samaki wasafirishwe kwa chombo fulani kilicho maalum, basi wafanyabiashara wengine chukueni hiyo ni fursa kwenu, nunueni hilo gari, sio kwamba wote ni wafanyabiashara wadogo hapa wapo wenye uwezo, lakini pia mnaweza kuungana mkakopa hilo gari na sisi tutawadhamini,” Alisisitiza.

Alitoa kauli hiyo baada ya wavuvi kumlalamikia Mkuu wa Mkoa kuhusu kuzuiwa kusafirisha samaki kwa kutumia magari ya abiria jambo ambalo ni kinyume na sheria.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiongea na wananchi wa kijiji cha Kirando, Wilayani Nkasi chini ya mwembe maarufu kwa jina la "kijiwe cha BBC"