Friday, May 10, 2019

RC Wangabo aendesha ukaguzi maalum ujenzi wa hopsitali za Wilaya

RC Wangabo awataka ma-DED kununua vifaa vya ujenzi wa hospitali za Wilaya

Fundi abishana na RC Wangabo nae ampa maagizo

RC Wangabo abeba zege kusaidia ujenzi wa hospitali ya Wilaya Kalambo

Fundi ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi awekwa kitimoto

Balozi wa Kenya ‘ayapigia debe’ Maporomoko ya kalambo.


Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu amewaomba wawekezaji kutoka kila pande ya dunia kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwa kujenga hoteli na nyumba za kupumzikia wageni katika eneo linalozunguka maporomoko ya Kalambo (Kalambo Falls) yaliyopo katika Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa.
Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu (mbele kulia) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mbele kushoto) wakati wakiteremka ngazi za kuelekea kwenye kina cha maporomoko ya Kalambo. (Kalambo Falls)

Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu (kushoto) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) wakati walipofika kwenye sehemu ya kwanza ambapo maporomoko hayo hayaonekani kwa ufasaha (nyuma yao).

Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu baaada ya kufika eneo ambalo unaweza kuyaona maporomoko hayo vizuri. 

Sehemu ya maporomoko ya kalambo (Kalambo Falls) 

Amesema kuwa eneo hilo ni zuri kwa wanafamilia kulitumia katika siku za mapumziko, siku za sikukuu na pia kujitokeza ili kuyaona maajabu hayo ambayo yametambuliwa na Shirika la umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni urithi wa dunia.

“Tunaomba wawekezaji waje hapa kwa wingi, hapa kuna kivutio ambacho kimejulikana na umoja wa mataifa UNESCO kama hifadhi ya urithi wa dunia, mje wawekezaji hapa, pahali ambapo siku za mwisho wa wiki watu wanaweza kuja kujipumzisha ama siku za sikukuu kuja na familia yao kwaajili ya “picnic”, wanajenga “lodges” lakini tunaomba “lodges” zijengwe nyingi zaidi za hadhi ya ubora wa juu zaidi ili tufurahie na familia zetu,” Alisema.

Balozi Kazungu ameyasema hayo alipotembelea maporomoko ya kalambo katika ziara yake ya siku moja Mkoani Rukwa iliyolenga kutafuta fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huku akitembelea kiwanda cha Nyama cha SAAFI pamoja na ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga.

Aidha, Balozi Kazungu alitoa ushauri kwa wakala wa misitu Tanzania wanaoshughulika na uhifadhi wa msitu wa Kalambo pamoja na kuimarisha miundombinu ya maporomopko hayo kuona uwezekazo wa kuweka nyaya pamoja na vigari vitakavyopita kwenye nyaya hizo ili watalii waweze kuyaona maporomoko hayo vizuri zaidi pamoja na msitu huo.

Wakati akisoma taarifa ya maporomoko hayo ya Kalambo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Kalambo Helman Ndanzi amesema kuwa pindi ujenzi wa ngazi za kushukukia kutoka maporomoko yanapoanzia hadi kufikia sehemu maji yanapodondokea utakapokamilika, ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 1277 na kugharimu shilingi 852,789,066.70.

“Changamoto zilizopo ni kutotangazwa vya kutosha maporomoko hayo hali inayopelekea kutojitokeza kwa wawekezaji katika eneo hilo ambalo mawasiliano ya simu pia bado ni tatizo na hivyo tunaiomba mitandano mbalimbali ya simu kujitokeza kuweka minara katika maeneo haya ili mawasiliano yawe rahisi,” Alisema.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alimhakikishia Balozi huyo kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha unakamilisha miundombinu inayohitajika ili kuwarahisishia wawekezaji kutekeleza shughuli zao kwa urahisi na hatimae kuinua uchumi wa wananchi katika mkoa lakini pia uchumi Tanzania kwa ujumla.

“Sisi tupo kwenye mpango ule wa viwanja vya ndege vile vinne, kuna kiwanja hiki cha Sumbawanga, Tabora, Shinyanga pamoja na Kigoma, karibu kila kitu kipo tayari kimazingira, vitu vyote vinavyotakiwa kufanyika kabla ya kuanza upanuzi wa uwanja tayari vimekwishafanyika, mhandisi mshauri yupo, mkandarasi yupo, mikataba tayari, fidia kwa wananchi waliohusika nae neo la upanuzi tayari, kila kitu kipo tayari, bado serikali haijaruhu lakini bila ya shaka wakati wowote ruhusa itatoka,” Alisisitiza.

Maporomoko ya Kalambo ni maporomoko ya pili kwa urefu kutoka maji yanapoanzia kumwagika hadi yanapodondokea kwa mita 235 na upana wa mita kuanzia 3.6 hadi mita 18 (single drop waterfall) ambapo maporomoko ya kwanza ni ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yenye urefu wa mita 947.Mapato ya Manispaa ya Sumbawanga kupaa kwa 46% kutokana na ujenzi Stendi ya Kisasa.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amepongeza juhudi zinazofanwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga katika kukusanya mapato pamoja na kuwa mbunifu wa kuongeza vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuweza kutatua na kukamilisha miradi mbali mbali ya manispaa hiyo.
Muonekano wa Stendi ya Manispaa ya Sumbawanga pindi itakapomalizika mwezi Disemba 2019

Amesema kuwa kukamilika kwa stendi hiyo ya kisasa kutaongeza ukusanyaji wa mapato wa karibu asilimia 46 ya mapato ya sasa ambapo manispaa hiyo ilikisia kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ikusanye shilingi 2,212,104,000 na hadi kufikia mwezi machi 2019 ilikuwa imekusanya shilingi 2,424,032,802.71 ambayo ni sawa na asilimia 110 ya makusanyo.

“Hii stendi ikimalizika mapato ya kutoka hapa itakuwa bilioni 1, sasa hii ni karibu asilimia 46 ya mapato yote ya manispaa kwa sasa hivi, hamuoni kwamba mapato ya manispaa yataongezeka kwa kasi kubwa sana na kwa hali hiyo hata waheshimiwa madiwani wataweza kutekeleza mipango yao vizuri na kwa ukamilifu sana na watakaonufaika ni sisi wananchi wote ndani ya Manispaa, “Alisema.

RC Wangabo ametoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa kituo kipya cha kisasa cha mabasi kitakachojengwa katika eneo la Katumba azimio lililopo kilomita 12 kutoka Sumbawanga mjini, ambapo mradi huo ukikamilika utaiingizia manispaa ya Sumbawanga Shilingi 1,027,800,000 kwa mwaka.

Aidha, Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri nyingine za mkoa huo kuipa kipaumbele miradi ya kimkakati, miradi ambayo huleta fedha nyingi kwa wakati mmoja kwani kwa kufanya kutazifanya halmashauri hizo kuweza kutatua kero nyingi za wananchi pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya alisema kuwa miundombinu itakayojengwa katika eneo hilo ni pamoja na Eneo la kuegeshea mabasi ya ndani na nje ya mkoa, bajaji, bodaboda, taksi na baiskeli, vyumba vya maduka, jengo la utawala, kituo kidogo cha polisi, mama lishe, choo cha kulipia, uzio, Taa, mifereji, vyumba kwaajili ya benki na ATM’s na vyumba vya mazoezi (Gyms)

“Mzabuni aliyepatikana kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Kisasa cha Mabasi Katumba azimio ni Sumry Enterprises Ltd. Eneo ambalo litatumika kwaajili ya Ujenzi wa Stendi ni ekari 10 na ekari 12 zitakuwa ni kwaajili ya mipango ya halmashauri ya hapo baadae. Mradi huu ni chanzo cha mapato ambacho kitaweza kutuingizia fedha itakayotumika kujenga au kumalizia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo ndani ya Manispaa na Kuboresha huduma mbalimbali.” Alisema.
  
Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Manispaa ya Sumbawanga iliweka bajeti ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi Katumba Azimio kupitia fedha za Mradi wa Uimarishaji miji (ULGSP) na kumpata mkandarasi Sumry Enterprises Ltd ambaye atahusika na ujenzi huo utakaogharimu shilingi 5,955,363,986 bila ya VAT

Wafanyakazi Rukwa waaswa kupunguza matumizi ya simu za mikononi muda wa kazi.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wafanyakazi mkoani Rukwa kupunguza matumizi ya simu za mikononi kwaajili ya shughuli binafsi nje na majukumu ya kazi hasa muda wa kazi wanapokuwa ofisini wakiendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesema kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya tano ni kumtumikia mwananchi kwa nguvu zote hivyo kila mfanyakazi anapaswa kuongeza bidii katika kufanya kazi, lakini kutumia simu na kuacha kuwahudumia wananchi kwa wakati mfanyakazi anakuwa anapata mshahara ambao hausmtahili kutokana na kutotumia muda wake alioajiriwa kwa ufanisi.

“ Ndugu wafanyakazi, hizi simu zimekuwa ni changamoto kubwa sana sehemu zetu za kazi, unakuta mtu badala ya kufanya kazi, hata kutoa huduma kwa mwananchi yeye “ana-chat” kwenye simu, vidole viko kwenye simu, yeye na simu, simu na yeye, kazi haziendi na kama zinakwenda basi zinakwenda kwa mapungufu, kunakuwa hakuna ufanisi na umakini, suala hili la simu tuliangalie sana ndugu waajiri pamoja na waajiriwa,” alisisitiza

Ameongeza kuwa wafanyakazi wamekuwa wakidai maslahi kuliko kupima uwajibikaji wao katika kazi ambazo wanapaswa kuzitekeleza na hali inayopelekea kuzorota kwa kazi nyingi kutokana na wafanyakazi kujishughulisha na matumizi ya simu za mkononi kuliko kuwajibika.

Ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kimkoa katika mkoa wa Rukwa yalifanyika katika viwanja vya mpira mji mdogo wa Laela, Wilaya ya Sumbawanga alipokuwa akitoa ufafanuzi wa maeneo nane yenye kulenga kuimarisha utendaji wa kazi ili kuleta maslahi kwa wananchi pamoja na wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi, ikiwemo uwajibikaji, kushughulikia kero za wananchi, uadilifu, usimamizi wa miradi, ubunifu, ushirikiano,kupambana na Rushwa,na kuunda mabaraza ya kazi.

Wakati akisoma risala ya wafanyakazi kwa mgeni rasmi katibu wa shirikisho la vyama huru vya wafanayakazi (TUCTA) Mkoani Rukwa Nashoni Kabombwe alisema kuwa kuna baadhi ya waajiri hawataki kabisa zoezi la kupata wafanyakazi bora kwenye taasisi zao lifanyike kwa kisingizio kwamba hawana fedha wala zawadi yoyote ya kuwalipa.

Katika kushinikiza hilo alisema, “kiwango cha zawadi kwa wafanyakazi bora zinazotolewa na baadhi ya waajiri ni kidogo na hakiendani na mabadiliko ya kiuchumi TUCTA inawataka waajiri kuanzia sasa kiwango cha chini cha zawadi kiwe shilingi 500,000 au kitu chenye thamani isiyopungua fedha hiyo.”

Kwa upande wake Afisa mfawidhi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mikoa ya Rukwa na Katavi Oscar Ngaluka katika mwaka wa fedha 2017/2018 Tume ilipokea jumla ya migogoro ya kikazi 127, wakati iliyomalizwa katika hatua ya usuluhishi ni 93, na inayoendelea na migogoro ni 10 na kuongeza kuwa sekta inayoongoza kwa migogoro mahala pa kazi katika mikoa ya Rukwa na Katavi ni ujenzi wa barabara.

“Sababu zinazoweza kumfanya mfanyakazi afungue mgogoro wake katika Tume ni pamoja na kuachishwa kazi bila ya kuwepo sababu ya kufaa na utaratibu wala kosa, mwajiri kuzuia vyama vya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ya kichama, madai ya stahili mbalimbali na manyanyazo sehemu za kazi,” Alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (aliyevaa skafu) pamoja na viongozi wengine ngazi ya mkoa wa Rukwa katika siku ya wafanyakazi Mei Mosi 2019. 

Kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi ni “Tanzania ya Uchumi inawezekana, wakati wa mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa” ambapo Tanzania nzima ina vyama vya wafanyakazi 31 huku Mkoa wa Rukwa ukiwa na vyama vya wafanyakazi 9.

Monday, May 6, 2019

RC Wangabo awasihi watakaoongeza bei za bidhaa mwezi mtukufu wa RamadhaniMkuu wa Mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wafanyabiashara wa vyakula katika masoko
ya Mkoa huo kuwa na moyo wa huruma kwa wale watakaofunga mwezi mtukufu wa Ramadhani
kwani ni mwezi wa toba ambao waumini hujinyima kwaajili ya watu wengine.

Amesema kuwa
mwezi wa ramadhani ni kipindi ambacho waumini humrudia Mwenyezi Mungu kwa nguvu
zote, hivyo sio kipindi cha wafanyabiashara hao kujinufaisha kwa watu
wanaofunga, kwani waumini wamekuwa wakijidunduliza ili kusaidia wasiojiweza
lakini wafanyabiashara hao wanaona ni fursa ya kujinufaisha.

 “Hiki ni Kipindi ambacho wanawasaidia watu
mbalimbali kwa nguvu zao zote, sasa akamsaidie mtu mwingine na wakati huo huo
akusaidie wewe ambaye unataka kujinufaisha kwa manufaa yako mwenyewe ukijua
kabisa kwamba hiki ni kipindi maalum cha kumrudia Mwenyezi Mungu niwasihi sana
wafanyabiashara wote msiongeze bei ya vyakula mbalimbali ten asana sana mshushe
bei za vyakula, nisinikie bei zimepanda sijui ongezeko la bei ya sukari sijui
ya unga, maharage sitaki kusikia nataka kusikia bei zimeshuka, “ Alisisitiza.

Aidha,
amewatakia mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhani Waislamu wote Tanzania pamoja na
wale waumini wa dini mbalimbali watakaosindikiza mwezi huo na kumuomba Mwenyezi
Mungu atupe baraka kutokana na mwezi huo ndani ya Mkoa wa rukwa na Tanzania kwa
ujumla.Waislamu wote
wa Tanzania wanatarajia kuungana na waislamu wengine duniani kufunga mwezi
mtukufu wa Ramadhani huku waumini wa Tanzania wakianza kufunga kuanzia tarehe
7.5.2019. 

Thursday, April 18, 2019

Wananchi wajitetea kwa RC Wangabo baada ya kuishambulia gari ya Serikali
Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya wananchi wa Kijiji cha Nankanga, Kata ya
Nankanga, Wilayani Sumbawanga kuacha tabia ya kuharibu mali za serikali ili
kutafuta suluhu ya migogoro iliyopo baina yao na askari wa hifadhi ya Pori la
Akiba Uwanda katika bonde la ziwa Rukwa huku akimuagiza kamanda wa polisi Mkoa
kuwasaka na kuwakama wote waliohusika na uharibifu huo.

Ametoa
maagizo hayo baada ya gari ya hifadhi hiyo kushambuliwa na wavuvi waishio
katika kambi ya uvuvi ya Kijiji cha Nankanga kilichopo pembezoni mwa ziwa
Rukwa, tukio lililotokea tarehe 10.4.2019 ambapo wavuvi hao walivunja vioo vya
gari, kuchomoa tairi pamoja na kuchukua vitu vilivyokuwamo ndani ya gari huku
dereva wa gari hiyo kukimbia na kuicha gari hiyo.

Alisisitiza
kuwa wananchi hawawezi kufanya uhalifu ili kuhalalisha madai yao na  uhalifu haulipwi kwa uhalifu na kuongeza kuwa mahali
popote penye uhalifu, sheria huchukua mkondo wake, sio kuanza uharibifu na
vitendo vingine vya uvunjifu wa amani mpaka kutishia uhai wa watu hivyo
aliwataka wana Nankanga kujitafakari kwa kina na kujitambua.

“Hebu
fikiria hiyo gari kama ingechomwa moto na uvunjifu mwingine wa amani mkubwa
ungetokea mnadhani mngelala kwenye Kijiji chenu hiki, wengine mngetumbukia
kwenye maji, wengine mngepanda mlima bila ya kujua na wengine msingekaa kurudi
hapa, kwahiyo mimi ninawaonya na ninawakanya iwe ni mara ya kwanza na ya
mwisho, ninyi kama wanakijiji kuleta uvunjifu wa amani ndani ya Kijiji, msije
mkagusa tena mali ya serikali, bahati mbaya sikujua gharama za uharibifu
mlioufanya mngechanga Kijiji kizima kulipa huo uharibifu ambao mmeshaufanya,” Alisisitiza.

Kwa upande
wake Meneja wa Pori la Akiba la Uwanda Jovine Nachihangu alisema kuwa mgogoro
huo ulitokana na askari wa hifadhi hiyo kukamata mitumbwi sita na wavuvi 18
waliokuwa wakivua katika eneo la hifadhi ndani ya ziwa Rukwa ambapo hifadhi
hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 5000 huku eneo la nchi kavu likiwa na
kilomita za mraba 490.

“Wakati nipo
Mbeya, nilipokea simu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya kwamba kuna watu wanataka
kuvamia kambini kwahiyo nichukue tahadhari, kwahiyo nilianza kuwasiliana na
watu waliomo humu kuwa kuna jambo hili na hili linataka kutokea, gari ilipata
pancha Kijiji kwasababu tunakawaida ya kumchukua mwenyekiti wa Kijiji ili
kuwatambua watu wake lakini muda huo dereva alinipigia simu kunambia hali siyo
nzuri na ameiacha gari kijijini, hivyo tuliwasiliana na polisi ili kuomba
msaada,” Alieleza.

Wakati
akifafanua tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema
kuwa mahusiano baina ya wananchi na askari wa hifadhi hiyo sio mazuri lakini
kitendo cha wananchi kuvamia gari ya serikali kuipiga mawe na kuiba hakifai na
kuongeza kuwa hifadhi hiyo ina mipaka ya muda na mipaka ya kudumu bado
infanyiwa tathmini na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamis Kigwangala.

“Waziri
Kigwangala mwaka jana alikuwa hapa na miongoni mwa matatizo tuliyomueleza ni
mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wavuvi, nchi kavu huku tunashukuru alama
zimewekwa na zimepunguza migogoro iliyopo kati ya wananchi na hifadhi, bado
tuna changamoto ya mifugo nae neo la wavuvi bado wavuvi wanaingia hifadhini,”
Alisema.

Wakati huo
huo Diwani wa Kata ya Nankanga Anyisile Kayuni alisema kuwa tukio lililotokea
limetokana na chuki kati ya wavuvi na wahifadhi na kudai kuwa wavuvi wanahisi
wanaonewa wakati wahifadhi wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.

“Mgogoro huu
nimeukuta tangu naingia udiwani umepitia hatu anyingi sana hadi kufikia Waziri
Dkt. Kigwangala kuwasimamisha watumishi 27 wa wanayapori lakini mgogorio huu
bado haujaisha, Mh. Mkuu wa Mkoa wakazi hawa wa Nankanga wamepungua idadi
uliyoikuta wakati ule wa masika sio hii asilimia kubwa wamekimbilia forodha ya
masuche jirani hapo (wilaya ya) Momba (Mkoani Songwe) wakitokea mwalo huu
hapa,” Alieleza.

Katika hatua
nyingine Mh. Wangabo aliwatahadharisha askari wa wanayamapori kutotumia sheria
vibaya na hatimae kuwaonea wananchi kwa kuwapiga bila ya mpangilio na huku
akiwataka wananchi hao kuhakikisha wanatii sheria na inapotokea wanakiuka
sheria hizo basi waache ubishi wakati wanapokamatwa.

Katika
kipindi cha mwezi Novemba mwaka 2018 hadi Machi 2019, Wanyama walioonekana
katika pori hilo la Akiba la Uwanda lililopo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) Wanyama walioonekana ni Nyati, Swala, Fisi na
Tembo.

Wednesday, April 17, 2019

Mwenge wa Uhuru waacha maumivu kwa Ma-DC – RukwaMkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku
tatu kwa wakuu wa wilaya wanaosimamia halmashauri ambazo Mwenge wa Uhuru
umekataa kuweka mawe ya msingi au kuzindua miradi iliyopitiwa na Mwenge huo
kutoa maelezezo ya kina juu ya sababu ya kukataliwa kwa miradi hiyo yenye
tamani ya shilingi 1,248,489,871.

“Napenda nitoe
maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wenye miradi iliyokataliwa kunipa
taarifa ya kwanini miradi yao haikuzinduliwa/kuwekewa mawe ya msingi. Maelezo
hayo niyapate ndani ya siku tatu kuanzia tarehe ya leo hadi tarehe 14, April,
2019,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo muda mfupi kabla ya kukabidhi Mwenge wa
Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mh. Amos Makalla huku Mwenge huo ukiwa
umekimbizwa katika halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa zikichukua umbali wa
kilemeta 832.5 na kutembelea miradi 35 na vikundi 11 ikiwa na tamani ya
shilingi 45,404,104,489.59

Aidha, kutokana na mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kubeba
kauli mbiu isemayo “Maji ni haki ya Kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke
kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa,” hivyo alitoa wito kwa wananachi
kuendela kutunza vyanzo vya maji, kuimarisha jumuia za watumia maji pamoja na
kufanya maandalizi thabiti ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na
kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2019
Ndugu Mzee Mkongea Ali aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Rukwa kwa kumpa
ushirikiano wa Kutosha tangu wanawasili katika mkoa huo hadi kuondoka na
kuelekea katika mkoa wa Katavi na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa
kufikisha asilimia 55 ya wananchi wa Mkoa huo kupata maji safi na salam.

“Mimi nikupe hongera kwasababu takwimu zinaonyesha katika
mkoa wako wa Rukwa umejitahidi kwa asilimia 55 kuhakikisha wananchi woyte
wanapata maji ya uhakika na salama sambamba na hilo katika kupambana na Rushwa
katika TAKUKURU kuna malalamiko 64 na kesi 59 wanazifanyia kazi, endeleeni
kufanya kazi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote,” Alisema.

Kutokana na mapungufu yaliyobainika Mwenge wa Uhuru
haukuzindua amakuweka mawe ya msingi kwenye miradi mitatu, Halmashauri ya
Manispaa ya Sumbawanga mradi mmoja vyumba vitano vya madarasa wenye thamani ya
shilingi 76,250,000, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mradi mmoja wa ujenzi
wa nyumba ya waalimu “6 in 1” wenye thamani ya shilingi
174,977,775
na
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mradi mmoja wa maji wenye thamani ya shilingi
997,262,096.

Saturday, March 23, 2019

Waganga wa kienyeji Kufyagiwa Sumbawanga baada ya Mauaji ya Watoto wawili.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako
wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa
kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.

Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati
wa mkutano ulifanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi
waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika
hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha
katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana
wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na
kuwajulisha wananchi kilichotokea.

Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike
katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu
ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika
kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu
uliopo katika mkoa.

“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani
ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni n
ani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama
kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi,
kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe
hapa kote, opresheni ipite ya kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,”
Alisisitiza.

Wakati wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo wa mkoa,
wananchi hao walisema kuwa vifo vya watoto hao vinahusishwa na Imani za
kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la vijana wanaoonekana wakila, wakinywa na
kuvaa vizuri bila ya kujulikana shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo
limekuwa likiwaumiza kichwa wananchi hao na kukosa majibu.

Mmoja wa wananchi hao Debora Maenge alisema “ Nasikitika
kwa tukio hili lililotokea mtaa wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae jirani sana,
tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu ambae sio mwema na hafai kabisa katika
jamii, cha kushanga alikuwa na vibali ambavyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye
ni mganga wa jadi, vibali hivi vinatolewa serikalini, Je serikali yetu
mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu waendelee kuuawa kiasi hiki? serikali
angalieni mnapotoa vibali je ni waganga Kweli?” Aliuliza.

Mh. Wangabo alitembelea eneo la nyumba ya mganga huyo wa
kienyeji ambayo gari alilowafichia watoto ilikuwamo na kukuta nyumba hiyo ikiwa
imevunjwa na gari la mganga huyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.

Watuhumiwa James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake Michael
Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na
Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali
ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya
gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo
kufungwa.Thursday, January 17, 2019

RC Wangabo azihamasishaTaasisi na wananchi kufika Msitu wa mbizi kuchuku...

Maafisa Kilimo na ugani watakiwa kuwafuata wakulima mashambani kutoa elimu ya viwavi jeshi vamizi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza maafisa ugani wote wa mkoani humo kuhakikisha wanawafikia wakulima kwenye mashamba yao na kuwapa elimu ya kukabiliana na wadudu aina ya viwavijeshi vamizi ambao wanaonekana kuanza kuleta athari katika wilaya ya Nkasi.
Amesema kuwa wakulima wengi hawana elimu ya kukabiliana na wadudu hao hasa kujua aina ya dawa ya kutumia ili kuwaua na wasiendelee kuharibu mazao na kuongeza kuwa ni wakati wao sasa maafisa ugani kufanya kazi ya kuwasaidia wananchi kupata matokeo bora ya mavuno kwa kutoa elimu ya kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa.
“Kitu cha kufanya ni maafisa ugani wote na maafisa kilimo wote washuke kwenda kwenye mashamba, wakague na kutoa ushauri wa moja kwa moja, dawa zipo zinapatikana wanaanzia dawa gani inayofuata ni ipi, ili tuweze kuwasaidia wakulima waweze kuokoa haya mahindi, DC hawa watu wasimamiwe washuke asibaki mtu kwenye ofisi zao,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo baada ya kuona athari ya viwavi jeshi alipotembelea shamba la mkulima wa mahindi Alex Ndenge katika ziara yake ya kuangalia maendeleo ya kilimo kwa wakulima na changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo pamoja na mashambulizi ya wadudu na magonjwa ya mazao Wilayani Nkasi.
Mkulima wa Zao la Mahindi, Namayere Wilayani Nkasi Alex Kwandenge (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (wa pili toka kulia) pamoja na timu ya ke ya wataalamu wa Mkoa na Wilaya juu ya athari ya viwavijeshi vamizi katika shamba lake.

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alifafanua namna ya kupambana na wadudu hao na kutoa tahadhari kwa wakulima kuwa na tabia ya kupanda kwa kipindi kimoja na sio kupishana kwani hali hiyo hupelekea wadudu hao kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kufuata mimea teke.

“Kuna sumu nyingine ukipiga inakuwa kwenye mmea, kwasababu huyu (mdudu) anatoa kinyesi kwahiyo ile sumu inaingia kwenye mmea kwahiyo anapokula anapata madhara anakufa, kwahiyo katika hatua za kwanza tunashauri (dawa aina ya) Duduba na hatua ya pili tunashauri dawa inaitwa “systemic” japo zina majina tofauti tofauti ni amjina ya kibiashara ila itumike hiyo baada ya kuona kwamba wameshaanza kutoa huu uchafu” Alieleza.
Kwa mujibu wa Afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi Emanuel Sekwao amesema kuwa viwavijeshi vamizi hao wameshaathiri kwa asilimia 2 mpaka 5 kutegemea eneo lakini bado haijafikia hatua ya wadudu hao kuharibu mimea kiasi cha kushindwa kuzaa.
Katika kipindi cha mwaka 2018/19 mkoa unalenga kulima jumla ya hekta 599,345.45 za mazao mbalimbali, kati ya hizo hekta 517,482.15 ni za mazao ya chakula na hekta 81,863.3 za mazao ya biashara.  Kutokana na eneo hilo mkoa unategemea kuzalisha jumla ya tani 1,817,171.84 za mazao ya chakula na biashara. Katika kiasi hicho tani 1,680,701.6 ni za mazao ya chakula na tani 136,470.25 ni za mazao ya biashara.

Wanafunzi watoro na wazazi wao kusakwa na kukamatwa huku hostel ikibadilishwa matumizi.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha anawatumia watendaji wa kata na vijiji pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuhakikisha wanawasaka na kuwakamata wanafunzi watoro pamoja na wazazi waoili kuhakikisha wanafunzi wote wanafika shule.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa fundisho kwa wazazi ambao kwa makusudi wanaacha watoto wao kutokwenda shule huku akipigia mfano faida ya elimu kwa kuwataja viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo yeye mwenyewe pamoja na wataalamu waliozingatia elimu na matokeo yake wamefanikiwa kimaisha.
“Kuna wanafunzi 173 watoro, hawajafika shuleni, sasa Mkurugenzi fuatilia shule yako, mkuu wa wilaya tumia watendaji wa vijiji, wa kata, kamati yako ya ulinzi, sakeni wanafunzi wote kamateni wazazi wao mpaka walete watoto wao shule, hatubembelezani hapa,”Alibainisha.
Ameyasema hayo alipotembelea shule ya sekondari Korongwe Beach katika Kijiji cha korongwe, kata ya Korongwe Wilayani Nkasi ili kujionea mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza pamoja na ujenzi wa madarasa ambapo wanafunzi 50 wamepangiwa kuanza kidato cha kwanza huku 17 tu wakiwa wameripoti na shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 383.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Awali akitoa taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu wa shule Nicomedi Ntepele amezitaja changamoto za shule hiyo ikiwemo utorowa rejareja na wa kudumu, ukosefu wa madarasa na nyumba za waalimu, ofisi za waalimu na maji.
“miongoni mwa changamoto tulizonazo hapa shule ni pamoja na utoro wa wanafunzi wa reja reja na wa kudumu, ukosefu wa madarasa, pia wazazi kutokuwa na uelewa kuwaleta Watoto wao kuishi hostel, uhaba wa maji eneo la shule, ofisi za walimu kutokamilika hivyo tunaomba changamoto hizi kufanyiwa kazi ili tufanye kazi kwa ufanisi,” Alimalizia.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangula aliamua kubadilia matumizi ya hosteli ya wanafunzi wa kike kutumiwa na wanafunzi wa kiume baada ya Mh. Wangabo kumtaka ajibu maombi ya mwanafunzi Ibrahimu Musa ambaye pia ni kaka mkuu wa shule hiyo juu ya kujengewa hosteli  baada ya Mkuu wa Mkoa kutoa nafasi kwa wanafunzi kuuliza maswali.
“Wanafunzi tunatembea umbali mrefu hasa Watoto wa jinsia ya kiume, sisi tulikuwa tunaomba ndugu Mkuu wa Mkoa uweze kutujengea sisi pia hosteli ili na sisi tuweze kukaa bweni nasi tuweze kufanya vizuri katika masomo yetu,”Alisema
Katika shule hiyo ya Korongwe Beach Sekondari kuna hosteli ya wanawake iliyojengwa kwa msaada wa watu wa Japan (JAICA) pamoja na serikali ya Tanzania, hosteli ambayo kwa mujibu wa taarifa ya mwalimu mkuu wa shule haijawahi kutumika tangu kumaliziwa kwake, ndipo Mkurugenzi aliposema.
“Hosteli ile ilipojengwa ilikuwa ni kwaajili ya kuawasaidia Watoto wa kike kwasababu ndio wanachangamoto zaidi, lakini kwasababu hosteli ile hawaingii walengwa ambao wako hapa, tuna uwezo tu wa kuibadilisha matumizi na uiandika hosteli ya wavulana kuliko kujenga hosteli nyingine, tutakapobadili matumizi ninyi Watoto wa kike msige kuidai tena wakati ipo sasa hamuingii,” Alimalizia.
Shule ya Sekondari Korongwe Beach ina wanafunzi 383 na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018. Na wanafunzi 50 wamepangwa kuanza kidato cha kwanza huku 17 wakiwa wameripoti shuleni.

RC Wangabo asisitiza ushirikiano baina ya watendaji wa ngazi zote kutatua changamoto za elimu.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi, kuhakikisha kila mtumishi kwa nafasi yake na majukumu yake anashirikishwa katika kutatua changamoto za wananchi ikiwemo elimu, afya, maji na kilimo pamojana kushirikiana na wananchi kutatua chnagmoto hizo.

Amesema kuwa ili kutatua hayo halmashauri inapaswa kuongeza vyanzo vya mapato ikiwemo kuzidisha malengo ya makusanyo kwa mwaka ili kuweza kukabiliana na changamoto anazokuwa anasomewa kila anapofanya ziara katika shule mbalimbali za halmashauri na kumuomba achangie kutatua changamoto zao.

“Mpige hesabu zote muwarudishie huko jamii ili jamii iguswe kwamba alaa! Kumbe kuna changamoto kubwa sana zisingoje sisi viongozi ambao pengine hatuna nafasi ya kuzunguka sekondari zote, lakini kama tutafanya hivi tutaondoa changamoto zote hizi na matatizo na haya yote mliyoyasema yako chini ya uwezo wenu, sio mambo ya mkuu wa mkoa haya, ni mambo ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi, kata na vijiji vyenu, kama ni “support” tunatoa ya kuhamasisha,naweza kusema nanunua bati mbili tatu, je, ninatatua matatizo yote hayo?”Alibainisha.

Ameongeza kuwa kazi ya shule ni kuandaa taarifa nzuri na kuikabidhi kwa watendaji wa halmashauri kuanzia Mtendaji wa kata na vijiji pamoja na viongozi wa kisiasa akiwemo diwani wa kata husika ili taarifa hizo ziwafikie wananchi watambue kupitia vikao vya kamati ya maendeleo ya kata ambao ni mfumo mzuri uliowekwa na serikali katika kutambua changamoto na kuzitatua.

Ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya shule ya sekondari Chala, iliyopo kata ya Chala Wilayani Nkasi na mkuu wa shule hiyo Fatma Mchomvu aliyemuomba kufanya harambee ya haraka kutoka kwa msafara alioambatana naoi li kuweza kukarabati nyumba ya “Matron” ambapo hadi wanafikisha ombi hilo waalimu walikwishajichangisha shilingi 50,000/-.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wananfunzi wa Shule ya Sekondari Chala. 

“Walimu wamejitolea kuchangia 50,000/- kusaidia kukarabati nyumba moja ya mwalimu ya “matron” kwasababu kule wanafunzi wako peke yao hakuna ulinzi kwahiyo nao wakaomba kupitia msafara wako, na wewe ndio kiongozi wetu tupate harambee ya haraka ili angalau tuanze kufanya ukarabati wa jengo hilo ili angalau wanafunzi wawe salama kwasababu wanakaa mbali na hakuna mlezi wa kukaa nae kule,” Alifafanua.Nkasi waitikia wito wa serikali katika kukikuza kilimo cha kahawa Mkoani wa Rukwa.


Wakulima katika halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wameitikia wito wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza zao la kahawa mkoani Rukwa na kuhakikisha wanalima zao hilo kwa wingi ili kubadili kipato chao na hatimae kushawishi wawekezaji wa kuchakata zao hilo kuwekeza Mkoani humo ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Zao la kahawa ni miongozi mwa mazao matano ya kimkakati yanayohimizwa na serikali ya awamu ya tano katika kuinua kipato cha wananchi pamoja na pato la nchi kwa ujumla.

Wakulima hao wakiongozwa na mkulima mzoefu wa zao hilo Elias Mwazembe alisema kuwa zao la kahawa linastawi katika mkoa mzima wa Rukwa hivyo aliushukuru uongozi wa Wilaya pamoja na Mkoa kwa kuendelea kuwasaidia pale wanapokwama mbali na changamoto aliyoipata mara ya kwanza alipolima katika hifadhi yam situ wa mfili na kuondolewa na serikali.

“Nilipoona kwenye Mkoa inakubali na kwenye wilaya ikabidi nije huku (Kijiji cha) Kalundi nikaanzisha kulima mwezi wa tatu nikaona ile kahawa inastawi vizuri kwahiyo nikaona hapa sio pa kuachilia niendelee na zao la kilimo lakini sikutulia niliendeleza hamasa kwa watu wengine kuwaambia kuwa zao la kahawa mkoani Kwetu linakubali ingawa changamoto ikawa mtu alikuwa anahitaji avune kwa mwaka huo huo nikasema mbegu iliyopo ni miaka miwili unaweza kuvuna kahawa na kwa umri nilionao nitavuna mpaka vitukuu,” alisema.

Nae Afisa kilimo wa Kijiji cha Kalundi Jiasi Muyunga alikiri kuwa kitendo cha mkulima huyo Elias Mwazembe kufika katika Kijiji hicho kumepelekea wakulima wengi kutaka kujihusisha na kilimo hicho cha kahawa baada ya kuona kuwa kinastawi vizuri katika Kijiji hicho na hivyo kutoka wito kwa maafisa ugani wenzie juu ya kuwasaidia wakulima na kuwakikishia kuwa zao hilo ndilo litakalokuwa mkombozi.

Kwa upande wake Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi alisema kuwa baada ya kubaini kwamba kata 18 zilizopo ufipa ya juu zenye eneo la hekta 48,000 kuwa zinafaa kulima zao hilo hal,mashauri ilianisha maeneo ya kuanza nayo huku wakishirikiana na kituo cha utafiti cha Tacri kilichopo Mbimba Wilaya ya Mbozi, ili kujua mbegu inayofaa katika maeneo hayo na hatimae kuwapeleka wataalamu na wakulima kwenda kujifunza.

“Mkulima ambaye tumemtembelea leo ndugu Mwazembe ni mmoja wa wakulima hao ambao nae alikwenda kujifunza Mbimba na baada ya kutoka huko aliendeleza juhudi za kufanya kilimo hiki cha kahawa na tunae mkulima mwingine yupo Kijiji cha Kakoma kata ya Namanyere nae pia mepanda kahawa karibu miche 500 na kitaluni ana miche karibu 12,000 na kuna taasisi zaidi ya sita ambazo tumepa miche iliyotokana na kilo 100 za mbegu ambapo kila kilo moja inatoa miche 4000, hivyo tunaamini baada ya miaka mitatu halmashauri itaanza kuona faida yake,” Alisisitiza.

Aidha Afisa kilimo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ocran Chengula aliwashauri wakulima wote wanaotarajia kuanza kilimo hicho cha kahawa kuhakikisha kuwa wanaandaa mashimo mapema na kuweka mbolea ili iweze kuchangayikana na udongo.

“Tunatakiwa kuandaa mashimo mapema, kama unategemea kupanda mwaka huu maana yake unaze kuandaa mashimo mwezi wa nane ama wa tisa kwa kuchimba mashimo na kuweka mbolea ili mbolea iweze kuchanganyikana na udongo ikishaanza mvua mwezi wa kumi na moja ile miche inatakiwa ihamishwe kwenye mashamba ili mvua itakavyonyesha iweze kushika na kuwa na nguvu zaidi ya kuweza kukua,” Alifafanua.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwa amesimama katikati ya kitalu cha miche ya mikahawa katika shamba la mkulima Elias Mwazembe wa kijiji cha Kalundi, kata ya Myula, Wilayani Nkasi. 

Mkoa wa Rukwa unategemea kuwa na miche 1,040,000 ifikapo mwakani inayotokana na kilo 260 za mbegu za kahawa inayopandwa kwenye vitalu mwaka huu ili kuweza kuisambaza kwa wakulima na taasisi mbalimbali ikiwa ni kuhamasisha kilimo cha zao hilo pamoja na kuinua kipato cha wananchi, mkoa na taifa kwa ujumla.

Ujumbe wa “Niache Nisome” kutawala katika “T-shirt” za wananfunzi Rukwa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wananfunzi wa shule zote za serikali katika halmashauri za mkoa huo zinaandikwa ujumbe wa “Niache Nisome” kwa herufi kubwa mbele ya flana zao za shule ili kuufikisha ujumbe huo kwa wale wote wenye nia na dhamira ya kukwamisha masomo ya wanafunzi hao kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto nyuma) katika picha ya pamoja na viongozi wa kiserikali na wawakilishi wa wananchi pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kate waliovalia flana zilizoandikwa "Niache Nisome"

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutapunguza idadi ya wanafunzi wa kike kupata mimba pamoja na kumaliza utoro kwani ujumbe huo utawalenga wazazi pamoja na vijana wenye tabia ya kuwanyemelea wanafunzi wa kike na kuwalaghai kwa kuwanunulia chipsi pamoja na kuwapakiza bure katika usafiri wa pikipiki maarufu kama Bodaboda ili waweze kuwapa mimba na hatimae kukatisha masomo yao.


“shule zote ziandikwe maneno “niache Nisome” Mkurugenzi kama kuna “T-shirt” imeandikwa maneno mengine zifutwe, ziandikwe “Niache Nisome” tena ziwe na herufi kubwa nzuri, ujumbe huu ufike mbali, ujumbe kwa watanzania, ujumbe wa watu wote wa mkoa wa Rukwa “Niacheni Nisome” Msitusumbue, vichipsi chipsi vile hakuna kwa Watoto wa kike, sijui bodaboda, utoro utoro, “Niacheni Nisome””, Alisema.

Aliyasema hayo alipotembelea katika shule ya sekondari Kate, iliyopo Kata ya Kate, Wilayani Nkasi na kupokea taarifa ya shule hiyo iliyoonyesha ufaulu mzuri kwa wananfunzi wa kidato cha sita na ufaulu mbovu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne jambo lililopelekea Mkuu wa Mkoa kushtushwa na hali hiyo ya wanafunzi kuwa katika shule moja na kuwa na ufaulu tofauti.

Halikadhalika alielezea kuwa kitendo cha wanafunzi wa kidato cha kwanza kushindwa kufika shuleni kwa wakati na kuwa watoro ni sababu mojawapo ya kupelekea kushindwa mitihani ya kidato cha pili kutokana na kuwakuta wanafunzi wenzao wakiwa wamekwishapiga hatua katika masomo na ukizingatia kuwa lugha ya kufundishia ni ya kigeni hivyo hupelekea mwanafunzi huyo kushindwa kuwa sawa na wanafunzi wenziwe na hatimae kukata tamaa, hali inayopelekea kushindwa kidato cha nne.

Kwa upande wake makamu mkuu wa shule ya sekondari Kate alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 katika shule hiyo, wa kiume ni 144 na wa kike ni 155 na kufanya jumla yao kuwa 299 huku walioripoti wa kiume wakiwa 27 na wa kike 19 na kufanya jumla yao kuwa 46 na hivyo wanafunzi 253 bado kuripoti shuleni hapo tangu shule kufunguliwa tarehe 7.1.2019.

Wiki ya Kwanza ya Ufunguzi wa Shule za Sekondari na mahudhurio ya Kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari alizozitembelea Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Shule
Waliopangiwa
Walioripoti
1.
Shule ya Sekondari Kate
299
46
2.
Shule ya Sekondari Chala
100
37
3.
Shule ya Sekondari Korongwe beach
50
17
4.
Shule ya Sekondari Kala
153
38

Wananchi kata ya Kala wamlilia RC baada ya kukosa mawasiliano ya simu na radio.


Wananchi wa kata ya Kala yenye vijiji vitano iliyopo katika wilaya ya Nkasi wamefikisha kilio chao cha kukosa mawasiliano ya simu kwa mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ili aweze kuwasaidia kutatua kero hiyo ambayo inakwamisha maendeleo ya kata.

Kilio hicho kimetolewa wakati wa kusoma risala ya maendeleo ya kata na msoma risala Felix Kapoze alipokuwa akielezea changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo kwa muda mrefu jambo linalokwamisha utendaji kazi pamoja na kufanya mawasiliano kuwa magumu.

“Changamoto nyingine kubwa ilipo hapa Kijijini kutokuwapo kwa mtandao wa simu, hii inapelekeana kukwama kwa taarifa nyingi hasa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo hivyo tunaiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa itusaidie kupatikana kwa mtandao wa simu ili kurahisisha mawasiliano,” Alifafanua.

Halikadhalika jambo hilo liliungwa mkono na mbunge wa jimbo la Nkasi Kusini Mh. Desderius Mipata wakati akielezea changamoto hiyo na hatua alizochukua kuhakikisha kuwa mawasiliano hayo yanapatinaka na hatimae kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za maendeleo katika kata hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipokea risala ya Kata ya Kala, muda mfupi baada ya kusomewa risala hiyo na msomaji Felix Kapoze (kushoto)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akizungumza na wananchi wa kata ya kala wilayani Nkasi.

“Hawa wananchi ni pekee ambao hawazungumzi na wenzao katika taifa na katika jimbo, juhudi nilizozifanya kama kiongozi wa jimbo ni kuitaka wizara ihakikishe kwamba tunapata mtandao, tunashukuru mungu wametusikiliza na sasa wanajenga minara miwili katika Kijiji cha kilambo cha mkolechi na Kijiji cha Kala, wanasema Kala itazungumza wantuambia katika kipindi kisichozidi miezi miwili,” Alibainisha.

Nae Mh. Wangabo aliwahakikishia wananchi wa kata hiyo kuwa mawasiliano yataimarishwa “Tutaimarisha hayo mawasiliano na juzi nilikuwa naongea na waziri wa ujenzi alikuja pale ofisini na tuliongea swala hili la minara ya mawasiliano, uzuri wameshaanza kufanyia kazi, kwahiyo tutaongeza nguvu kule ili mitandao ya mawasiliano ifanye kazi n ahata radio nkasi iweze kuwafikia huku,” Alisema.