Thursday, January 17, 2019

Ujumbe wa “Niache Nisome” kutawala katika “T-shirt” za wananfunzi Rukwa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wananfunzi wa shule zote za serikali katika halmashauri za mkoa huo zinaandikwa ujumbe wa “Niache Nisome” kwa herufi kubwa mbele ya flana zao za shule ili kuufikisha ujumbe huo kwa wale wote wenye nia na dhamira ya kukwamisha masomo ya wanafunzi hao kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto nyuma) katika picha ya pamoja na viongozi wa kiserikali na wawakilishi wa wananchi pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kate waliovalia flana zilizoandikwa "Niache Nisome"

Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutapunguza idadi ya wanafunzi wa kike kupata mimba pamoja na kumaliza utoro kwani ujumbe huo utawalenga wazazi pamoja na vijana wenye tabia ya kuwanyemelea wanafunzi wa kike na kuwalaghai kwa kuwanunulia chipsi pamoja na kuwapakiza bure katika usafiri wa pikipiki maarufu kama Bodaboda ili waweze kuwapa mimba na hatimae kukatisha masomo yao.


“shule zote ziandikwe maneno “niache Nisome” Mkurugenzi kama kuna “T-shirt” imeandikwa maneno mengine zifutwe, ziandikwe “Niache Nisome” tena ziwe na herufi kubwa nzuri, ujumbe huu ufike mbali, ujumbe kwa watanzania, ujumbe wa watu wote wa mkoa wa Rukwa “Niacheni Nisome” Msitusumbue, vichipsi chipsi vile hakuna kwa Watoto wa kike, sijui bodaboda, utoro utoro, “Niacheni Nisome””, Alisema.

Aliyasema hayo alipotembelea katika shule ya sekondari Kate, iliyopo Kata ya Kate, Wilayani Nkasi na kupokea taarifa ya shule hiyo iliyoonyesha ufaulu mzuri kwa wananfunzi wa kidato cha sita na ufaulu mbovu kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne jambo lililopelekea Mkuu wa Mkoa kushtushwa na hali hiyo ya wanafunzi kuwa katika shule moja na kuwa na ufaulu tofauti.

Halikadhalika alielezea kuwa kitendo cha wanafunzi wa kidato cha kwanza kushindwa kufika shuleni kwa wakati na kuwa watoro ni sababu mojawapo ya kupelekea kushindwa mitihani ya kidato cha pili kutokana na kuwakuta wanafunzi wenzao wakiwa wamekwishapiga hatua katika masomo na ukizingatia kuwa lugha ya kufundishia ni ya kigeni hivyo hupelekea mwanafunzi huyo kushindwa kuwa sawa na wanafunzi wenziwe na hatimae kukata tamaa, hali inayopelekea kushindwa kidato cha nne.

Kwa upande wake makamu mkuu wa shule ya sekondari Kate alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 katika shule hiyo, wa kiume ni 144 na wa kike ni 155 na kufanya jumla yao kuwa 299 huku walioripoti wa kiume wakiwa 27 na wa kike 19 na kufanya jumla yao kuwa 46 na hivyo wanafunzi 253 bado kuripoti shuleni hapo tangu shule kufunguliwa tarehe 7.1.2019.

Wiki ya Kwanza ya Ufunguzi wa Shule za Sekondari na mahudhurio ya Kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari alizozitembelea Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.

Shule
Waliopangiwa
Walioripoti
1.
Shule ya Sekondari Kate
299
46
2.
Shule ya Sekondari Chala
100
37
3.
Shule ya Sekondari Korongwe beach
50
17
4.
Shule ya Sekondari Kala
153
38

No comments:

Post a Comment