Thursday, April 18, 2019

Wananchi wajitetea kwa RC Wangabo baada ya kuishambulia gari ya Serikali
Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya wananchi wa Kijiji cha Nankanga, Kata ya
Nankanga, Wilayani Sumbawanga kuacha tabia ya kuharibu mali za serikali ili
kutafuta suluhu ya migogoro iliyopo baina yao na askari wa hifadhi ya Pori la
Akiba Uwanda katika bonde la ziwa Rukwa huku akimuagiza kamanda wa polisi Mkoa
kuwasaka na kuwakama wote waliohusika na uharibifu huo.

Ametoa
maagizo hayo baada ya gari ya hifadhi hiyo kushambuliwa na wavuvi waishio
katika kambi ya uvuvi ya Kijiji cha Nankanga kilichopo pembezoni mwa ziwa
Rukwa, tukio lililotokea tarehe 10.4.2019 ambapo wavuvi hao walivunja vioo vya
gari, kuchomoa tairi pamoja na kuchukua vitu vilivyokuwamo ndani ya gari huku
dereva wa gari hiyo kukimbia na kuicha gari hiyo.

Alisisitiza
kuwa wananchi hawawezi kufanya uhalifu ili kuhalalisha madai yao na  uhalifu haulipwi kwa uhalifu na kuongeza kuwa mahali
popote penye uhalifu, sheria huchukua mkondo wake, sio kuanza uharibifu na
vitendo vingine vya uvunjifu wa amani mpaka kutishia uhai wa watu hivyo
aliwataka wana Nankanga kujitafakari kwa kina na kujitambua.

“Hebu
fikiria hiyo gari kama ingechomwa moto na uvunjifu mwingine wa amani mkubwa
ungetokea mnadhani mngelala kwenye Kijiji chenu hiki, wengine mngetumbukia
kwenye maji, wengine mngepanda mlima bila ya kujua na wengine msingekaa kurudi
hapa, kwahiyo mimi ninawaonya na ninawakanya iwe ni mara ya kwanza na ya
mwisho, ninyi kama wanakijiji kuleta uvunjifu wa amani ndani ya Kijiji, msije
mkagusa tena mali ya serikali, bahati mbaya sikujua gharama za uharibifu
mlioufanya mngechanga Kijiji kizima kulipa huo uharibifu ambao mmeshaufanya,” Alisisitiza.

Kwa upande
wake Meneja wa Pori la Akiba la Uwanda Jovine Nachihangu alisema kuwa mgogoro
huo ulitokana na askari wa hifadhi hiyo kukamata mitumbwi sita na wavuvi 18
waliokuwa wakivua katika eneo la hifadhi ndani ya ziwa Rukwa ambapo hifadhi
hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 5000 huku eneo la nchi kavu likiwa na
kilomita za mraba 490.

“Wakati nipo
Mbeya, nilipokea simu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya kwamba kuna watu wanataka
kuvamia kambini kwahiyo nichukue tahadhari, kwahiyo nilianza kuwasiliana na
watu waliomo humu kuwa kuna jambo hili na hili linataka kutokea, gari ilipata
pancha Kijiji kwasababu tunakawaida ya kumchukua mwenyekiti wa Kijiji ili
kuwatambua watu wake lakini muda huo dereva alinipigia simu kunambia hali siyo
nzuri na ameiacha gari kijijini, hivyo tuliwasiliana na polisi ili kuomba
msaada,” Alieleza.

Wakati
akifafanua tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule alisema
kuwa mahusiano baina ya wananchi na askari wa hifadhi hiyo sio mazuri lakini
kitendo cha wananchi kuvamia gari ya serikali kuipiga mawe na kuiba hakifai na
kuongeza kuwa hifadhi hiyo ina mipaka ya muda na mipaka ya kudumu bado
infanyiwa tathmini na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamis Kigwangala.

“Waziri
Kigwangala mwaka jana alikuwa hapa na miongoni mwa matatizo tuliyomueleza ni
mgogoro wa mpaka kati ya hifadhi na wavuvi, nchi kavu huku tunashukuru alama
zimewekwa na zimepunguza migogoro iliyopo kati ya wananchi na hifadhi, bado
tuna changamoto ya mifugo nae neo la wavuvi bado wavuvi wanaingia hifadhini,”
Alisema.

Wakati huo
huo Diwani wa Kata ya Nankanga Anyisile Kayuni alisema kuwa tukio lililotokea
limetokana na chuki kati ya wavuvi na wahifadhi na kudai kuwa wavuvi wanahisi
wanaonewa wakati wahifadhi wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.

“Mgogoro huu
nimeukuta tangu naingia udiwani umepitia hatu anyingi sana hadi kufikia Waziri
Dkt. Kigwangala kuwasimamisha watumishi 27 wa wanayapori lakini mgogorio huu
bado haujaisha, Mh. Mkuu wa Mkoa wakazi hawa wa Nankanga wamepungua idadi
uliyoikuta wakati ule wa masika sio hii asilimia kubwa wamekimbilia forodha ya
masuche jirani hapo (wilaya ya) Momba (Mkoani Songwe) wakitokea mwalo huu
hapa,” Alieleza.

Katika hatua
nyingine Mh. Wangabo aliwatahadharisha askari wa wanayamapori kutotumia sheria
vibaya na hatimae kuwaonea wananchi kwa kuwapiga bila ya mpangilio na huku
akiwataka wananchi hao kuhakikisha wanatii sheria na inapotokea wanakiuka
sheria hizo basi waache ubishi wakati wanapokamatwa.

Katika
kipindi cha mwezi Novemba mwaka 2018 hadi Machi 2019, Wanyama walioonekana
katika pori hilo la Akiba la Uwanda lililopo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) Wanyama walioonekana ni Nyati, Swala, Fisi na
Tembo.

Wednesday, April 17, 2019

Mwenge wa Uhuru waacha maumivu kwa Ma-DC – RukwaMkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku
tatu kwa wakuu wa wilaya wanaosimamia halmashauri ambazo Mwenge wa Uhuru
umekataa kuweka mawe ya msingi au kuzindua miradi iliyopitiwa na Mwenge huo
kutoa maelezezo ya kina juu ya sababu ya kukataliwa kwa miradi hiyo yenye
tamani ya shilingi 1,248,489,871.

“Napenda nitoe
maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wenye miradi iliyokataliwa kunipa
taarifa ya kwanini miradi yao haikuzinduliwa/kuwekewa mawe ya msingi. Maelezo
hayo niyapate ndani ya siku tatu kuanzia tarehe ya leo hadi tarehe 14, April,
2019,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo muda mfupi kabla ya kukabidhi Mwenge wa
Uhuru kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mh. Amos Makalla huku Mwenge huo ukiwa
umekimbizwa katika halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa zikichukua umbali wa
kilemeta 832.5 na kutembelea miradi 35 na vikundi 11 ikiwa na tamani ya
shilingi 45,404,104,489.59

Aidha, kutokana na mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kubeba
kauli mbiu isemayo “Maji ni haki ya Kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke
kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa,” hivyo alitoa wito kwa wananachi
kuendela kutunza vyanzo vya maji, kuimarisha jumuia za watumia maji pamoja na
kufanya maandalizi thabiti ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na
kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2019
Ndugu Mzee Mkongea Ali aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Rukwa kwa kumpa
ushirikiano wa Kutosha tangu wanawasili katika mkoa huo hadi kuondoka na
kuelekea katika mkoa wa Katavi na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa
kufikisha asilimia 55 ya wananchi wa Mkoa huo kupata maji safi na salam.

“Mimi nikupe hongera kwasababu takwimu zinaonyesha katika
mkoa wako wa Rukwa umejitahidi kwa asilimia 55 kuhakikisha wananchi woyte
wanapata maji ya uhakika na salama sambamba na hilo katika kupambana na Rushwa
katika TAKUKURU kuna malalamiko 64 na kesi 59 wanazifanyia kazi, endeleeni
kufanya kazi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote,” Alisema.

Kutokana na mapungufu yaliyobainika Mwenge wa Uhuru
haukuzindua amakuweka mawe ya msingi kwenye miradi mitatu, Halmashauri ya
Manispaa ya Sumbawanga mradi mmoja vyumba vitano vya madarasa wenye thamani ya
shilingi 76,250,000, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mradi mmoja wa ujenzi
wa nyumba ya waalimu “6 in 1” wenye thamani ya shilingi
174,977,775
na
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mradi mmoja wa maji wenye thamani ya shilingi
997,262,096.