Friday, June 28, 2019

RC Wangabo atoa ushauri baada ya Taifa Stars Kufungwa
Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo ametoa
ushauri kwa wadau wa michezo nchini kuona namna ya kuimarisha mbinu za kuibua
vipaji vya wanamichezo kuanzia ngazi ya shule za msingi katika mashindano ya
UMITASHUMTA na UMISETA ili kuweza kuwa na vijana watakaoweza kubeba jina la
Tanzania katika michezo.

Amesema kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliochelewa
kulala ili kuangalia mechi baina Tanzania maarufu kama Taifa Starts na jirani
zetu Kenya maarufu kama Harambee Strars ambapo hadi kumalizika kwa mchezo huo Harambee
Stars iliibuka kidedea kwa kuilaza Taifa Stars mabao 3 kwa 2.

“Kuna ambao wamelala alfajiri na wengine wapo humu
ambao wamelala leo, tunaomboleza kufungwa huku, tungeshinda jana tungekuwa na
mwanga wa kusonga mbele, sasa ni kinyume na yalivyokuwa matarajio yetu lakini
ndugu wana Rukwa tusikate tamaa, tuendelee kuiunga mkono timu yetu hii ya
Taifa, Kufungwa ni kujifunza, tuendelee kujipanga vizuri hasa kwa vijana
kuanzia UMISHAMTA huku mpaka UMISETA na kwenye “academy” hizi,” alieleza.

Aidha, alibainisha kasoro kadhaa zinazojitokeza
katika ligi yetu ya Tanzania hasa kwa upande wa timu vinara zinazopata nafasi
za kwenda kucheza makombe ya Kalbu Bingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho
kuona namna ya kutoa fursa kwa wachezaji wa kitanzania ili wapate ujuzi wa kimataifa
na sio kuwajenga wachezaji wa nje ambao wanakwenda kutumikia nchi zao.

“Hizi timu zetu za Yanga na Simba pamoja na Azama
zinafanya vizuri kwasababu zina wachezaji wengi wa kigeni matokeo yake timu ya
Taifa inapokwenda kwenye mashindano wachezaji wetu wanabaki wenyewe, angalieni
Emanuel Okwi anavuma kule Uganda lakini tumemuwezesha sisi hapa Tanzania,”
Alisema.Afisa Utamaduni Sumbawanga atoa kibao cha Kusifu Kasi ya Maendeleo nchini
Katika kuunga mkono na kuieleza jamii juu ya juhudi
zinazofanya nwa serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Dkt. John Pombe
Magufuli, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Sumbawanga Kiheka Charles a.k.a K
Chars ameibuka na wimbo wa kuelezea mazuri yanayofanywa na serikali ya
Tanzania.

Katika kueleza malengo ya kutunga wimbo huo alioupa jina
la Mchaka Mchaka na kumshirikisha msanii Mackpaul Sekimanga a.k.a Makamua, K
Chars alisema kuwa kama kiongozi na mshauri wa wasanii ni jukumu lake
kuwaonesha wasanii mada mbalimbali za kuimba na sio kujikita kuyaimbia mapenzi
wakati wanaweza kuimba kuhusu kuhamasisha lishe bora, kuhimiza kilimo cha mazao
mbalimbali na faida zake, kukemea mimba za mashuleni, ndoa za utotoni,
kuboresha huduma za afya nakadhalika.

"Hakuna msanii wa nje atakayekuja kusifu nchi yetu
isipokuwa sisi wenyewe kusifia maendeleo yetu na kuyatangaza kwa wengine, hivyo
nikaona niyaweke katika wimbo mazuri yaliyofanywa na serikali ambayo jamii
inapaswa kuyafahamu, msanii ana nafasi kubwa ya kusikilizwa na jamii na yapo
mengi ya kuyazungumzia katika maisha yetu, hivyo ni vyema wasanii wakajielekeza
katika kuhamasisha mambo ya kimaendeleo, kuyaimba mazuri ya serikali na kuyaibua
yale ambayo wanaona serikali inahitaji kuyafahamu ili yafanyiwe kazi,"
Alisema

Halikadhalika, alisifu juhudi za Mkurugenzi wa Manispaa
ya Sumbawanga, James Mtalitinya, kwa kumuunga mkono katika juhudi za kuibua
vipaji vya wasanii wa Sumbawanga tangu kuanzishwa shindano la "Sumbawanga
Talent Search" lililowahusisha wasanii wa kuimba, hadi kumalizika kwa
shindano hilo.

Katika Shindalo hilo ambalo fainali yake ilifanyika usiku
wa mkesha wa Mwenge wa Uhuru 2019 na mshindi wa kwanza alipata shilingi 300,000/=,
wa pili 200,000/= na wa tatu 100,000/= na walioingia kwenye kumi bora wamepewa
fursa ya kurekodi wimbo wa kuelezea fursa za uwekezaji zinazopatikana katika
Mkoa wa Rukwa pamoja na kusifu ukarimu wa watu wa mkoa huo, kibao
kinachotarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi July,2019.

K Chars ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi mbalimbali
wa mkoa kuwasaidia na kuwaunga mkono wasanii wachanga wanaoutangaza mkoa.