Wednesday, July 31, 2019

“Ushiriki wa Kinababa ni muhimu katika wiki ya Unyonyeshaji” RC Wangabo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa mkoa wa Rukwa hasa kinababa kushiriki katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yanayofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 ya Mwezi wa Nane ambapo Tanzania huungana na nchi nyingine duniani katika maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akiogea na Waandishi wa habari katika maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji Mkoani Rukwa. 

Amesema kuwa wiki hiyo ya unyonyeshaji itumike katika mapambano dhidi ya udumavu ambao mkoa wa Rukwa unaongoza kitaifa kwa kuwa na udumavu wa asilimia 56.3 na hivyo kuwataka wananchi kushiriki kwa ukamilifu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika vijiji 339 vya mkoa huo ili kupata elimu stahiki itakayowawezesha kuwaepusha watoto na udumavu.

‘Msingi Mkubwa kabisa wa kupambana na udumavu uko hapa kwenye unyonyeshaji, ni lazima mama anyonyeshe mtoto wake ipasavyo, kina mama huwa wanapuuza wengine kufanya jukumu hili kwasababu labda ya masuala ya kiuchumi lakini pia hata kijamii na kimazoea, sasa hii elimu ndio inapswa kuitoa ndani ya siku hizi saba,kwasababu inakwenda katika vijiji vyote, kinamama wakisikia huu ujumbe pamoja na jamii kwa ujumla na kinababa wote tutaweza kupambana na udumavu,” Alisisitiza.

Aidha amevitaka vyombo vya habari kushiriki katika kufuatilia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazolinda haki za uzazi na ulishaji wa watoto kwa kufanya tafiti, kuandika au kuripoti matukio mbalimbali kama vile utekelezaji wa haki mbalimbali ikiwemo haki ya kupata likizo ya uzazi.

Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo tarehe 31.7.2019 katika maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo kimkoa itafanyika katika Kijiji cha Kisumbakati, Wilayani Kalambo ambapo maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na siku ya Afya ya Kijiji katika vijiji vyote vya mkoa.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika alisisittiza kuwa mradi wa Lishe Endelevu ambao unalenga kupunguza udumavu katika Mkoa wa Rukwa umekuja kuongeza kasi ya juhudi za mkoa katika kupambana na udumavu na kuongeza kuwa maadhimisho hayo yanalenga kujenga uelewa wa pamoja katika unyonyeshaji wa mtoto.

“Siku 1000 za makuzi ya mtoto, ukikosea kwenye eneo la unyonyeshaji kuna uwezekano mkubwa sana wa kumuweka mtoto kwenye mazingira magumu, kwahiyo hii inalenga sit u kutoa elimu ya unyonyeshaji lakini pia juu ya maandalizi ya vyakula vya watoto hawa,” Alisema.

Halikadhalika Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa Asha Izina alizitaka sekta binafsi kuwapa muda wafanyakazi kina mama wenye watoto ili aweze kuwanyonyesha watoto wao, “Serikali inatia msisitizo kwamba waajiri wahakikishe nao pia wanatoa nafasi au wanatengeneza mazingira ambayo yanakuwa ni Rafiki pale kazini ambapo mama analetewa kazini mtoto wake na kuhakikisha kwamba anamnyonyesha, tukitambua kwamba maziwa ya mama ni ya muhimu kwa afya na maendeleo ya mtoto”.

Kauli mbiu ya mwaka huu 2019 ni: Mwezeshe mama aweze kunyonyesha. Ambayo inasisitiza kuwa kwa pamoja tushirikiane kumwezesha mama aweze kunyonyesha ipasavyo.


Tuesday, July 30, 2019

RC Wangabo atoa wito kwa Wizara kuhusu ukarabati wa MV LIEMBA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa wito kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu kuharakisha ukarabati wa meli ya MV Liemba ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na wananchi wanaoishi katika mwambao wa Ziwa Tanzganyika.

Mh. Wangabo amesema kuwa wananchi hao wamekuwa wakiweka maisha yao hatarini kwa kutumia vyombo kama mitumbwi na boti ambavyo usalama wake ni mdogo ukilinganisha na meli kubwa ya MV Liemba ambayo usalama wake ni wa uhakika.

“Nitoe wito kwa wizara husika hii meli ya MV Liemba nimeambiwa hapa kwamba ikipita kwenda Zambia inaitwa ‘Our Baby’ mtoto wetu, sasa huyu mtoto wetu anaulizwa yuko wapi, Zambia wanauliza, sasa Wizara husika twende haraka isimamie hili jambo, MV Liemba itengenezwe, watu maisha yao yapo kwenye hatari kubwa ndani ya hili ziwa Tanganyika”

Mh. Wangabo ameyasema hayo alipotembelea mradi wa usanifu na ujenzi wa bandari ya Kabwe iliyopo kata ya Kabwe katika Wilaya ya Nkasi ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo ulioanza tarehe 1 Aprili,2018 ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 52 katika miezi 14 na unatarajiwa kukamilika tarehe 1 Aprili 2020 na kugharimu Shilingi Bilioni 7.49 ambazo ni fedha za Mamlaka ya Bandari nchini.

Eneo la gati ya Bandari ya Kabwe ikiendelea kujengwa katika Ziwa Tanganyika Wilayani Nkasi. 

Naye Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini Mh Ali Kessy alieleza kuwa meli hiyo ya MV Liemba ilitakiwa kukamilishwa ukarabati wake tangu mwaka wa fedha 2017/2018 lakini fedha za ukarabati hazikutengwa na kudai kuwa Waziri wa Fedha Mh. Filipo Mpango amemuhakikishia kuwa fedha za ukarabati wa meli hiyo zimetengwa katika bajeti yam waka 2018/2019.  

Kwa upande wake Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika Pasivo Ntetema amesema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa gati, jengo la kupumzikia abiria, jengo la mgahawa, ofisi, ghala la kuhifadhia mizigo, nyumba za wafanyakazi na uzio na kuongeza kuwa kwa Bandari ya Kabwe peke yake wastani wa usafirishaji kwa mwezi ni tani 1500 hadi 2000 na mwaka wa fedha 2018/2019 zimesafirishwa tani 20,000

“Pamoja na changamoto za miundombinu lakini utaona kuna ‘access’ nzuri ya watu kupita hapa kwahiyo kukishaboreshwa bandari hii ikakamilika lakini pia miundombinu ya barabara ya kuingia hapa ikakamilika ni Imani yetu watu wa bandari ya kwamba kupitia uongozi wako, kupitia mheshimiwa mbunge na mamlaka zote zinazotawala mkoa wa Rukwa pamoja na serikali kuu, tutaangalia sasa uwezekano wa kuboresha barabara hii kwa kiwango cha lami ili shehena kubwa iweze kupita hapa.

Mamlaka ya Bandari inatekeleza miradi mitatu katika Mkoa wa Rukwa ambayo ni Mradi wa uboreshwaji wa bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo, Ujenzi wa barabara katika Bandari ya Kipili na Mradi wa Usanifu na Ujenzi wa Gati Bandari ya Kabwe zilizopo katika Wilaya ya Nkasi ambapo miradi yote itagharimu shilingi bilioni 12.7