Wednesday, July 31, 2019

“Ushiriki wa Kinababa ni muhimu katika wiki ya Unyonyeshaji” RC Wangabo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi wa mkoa wa Rukwa hasa kinababa kushiriki katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yanayofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 ya Mwezi wa Nane ambapo Tanzania huungana na nchi nyingine duniani katika maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akiogea na Waandishi wa habari katika maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya Unyonyeshaji Mkoani Rukwa. 

Amesema kuwa wiki hiyo ya unyonyeshaji itumike katika mapambano dhidi ya udumavu ambao mkoa wa Rukwa unaongoza kitaifa kwa kuwa na udumavu wa asilimia 56.3 na hivyo kuwataka wananchi kushiriki kwa ukamilifu katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika vijiji 339 vya mkoa huo ili kupata elimu stahiki itakayowawezesha kuwaepusha watoto na udumavu.

‘Msingi Mkubwa kabisa wa kupambana na udumavu uko hapa kwenye unyonyeshaji, ni lazima mama anyonyeshe mtoto wake ipasavyo, kina mama huwa wanapuuza wengine kufanya jukumu hili kwasababu labda ya masuala ya kiuchumi lakini pia hata kijamii na kimazoea, sasa hii elimu ndio inapswa kuitoa ndani ya siku hizi saba,kwasababu inakwenda katika vijiji vyote, kinamama wakisikia huu ujumbe pamoja na jamii kwa ujumla na kinababa wote tutaweza kupambana na udumavu,” Alisisitiza.

Aidha amevitaka vyombo vya habari kushiriki katika kufuatilia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazolinda haki za uzazi na ulishaji wa watoto kwa kufanya tafiti, kuandika au kuripoti matukio mbalimbali kama vile utekelezaji wa haki mbalimbali ikiwemo haki ya kupata likizo ya uzazi.

Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo tarehe 31.7.2019 katika maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo kimkoa itafanyika katika Kijiji cha Kisumbakati, Wilayani Kalambo ambapo maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na siku ya Afya ya Kijiji katika vijiji vyote vya mkoa.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika alisisittiza kuwa mradi wa Lishe Endelevu ambao unalenga kupunguza udumavu katika Mkoa wa Rukwa umekuja kuongeza kasi ya juhudi za mkoa katika kupambana na udumavu na kuongeza kuwa maadhimisho hayo yanalenga kujenga uelewa wa pamoja katika unyonyeshaji wa mtoto.

“Siku 1000 za makuzi ya mtoto, ukikosea kwenye eneo la unyonyeshaji kuna uwezekano mkubwa sana wa kumuweka mtoto kwenye mazingira magumu, kwahiyo hii inalenga sit u kutoa elimu ya unyonyeshaji lakini pia juu ya maandalizi ya vyakula vya watoto hawa,” Alisema.

Halikadhalika Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa Asha Izina alizitaka sekta binafsi kuwapa muda wafanyakazi kina mama wenye watoto ili aweze kuwanyonyesha watoto wao, “Serikali inatia msisitizo kwamba waajiri wahakikishe nao pia wanatoa nafasi au wanatengeneza mazingira ambayo yanakuwa ni Rafiki pale kazini ambapo mama analetewa kazini mtoto wake na kuhakikisha kwamba anamnyonyesha, tukitambua kwamba maziwa ya mama ni ya muhimu kwa afya na maendeleo ya mtoto”.

Kauli mbiu ya mwaka huu 2019 ni: Mwezeshe mama aweze kunyonyesha. Ambayo inasisitiza kuwa kwa pamoja tushirikiane kumwezesha mama aweze kunyonyesha ipasavyo.


No comments:

Post a Comment