Friday, May 10, 2019

RC Wangabo aendesha ukaguzi maalum ujenzi wa hopsitali za Wilaya

RC Wangabo awataka ma-DED kununua vifaa vya ujenzi wa hospitali za Wilaya

Fundi abishana na RC Wangabo nae ampa maagizo

RC Wangabo abeba zege kusaidia ujenzi wa hospitali ya Wilaya Kalambo

Fundi ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi awekwa kitimoto

Balozi wa Kenya ‘ayapigia debe’ Maporomoko ya kalambo.


Balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu amewaomba wawekezaji kutoka kila pande ya dunia kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwa kujenga hoteli na nyumba za kupumzikia wageni katika eneo linalozunguka maporomoko ya Kalambo (Kalambo Falls) yaliyopo katika Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa.
Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu (mbele kulia) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mbele kushoto) wakati wakiteremka ngazi za kuelekea kwenye kina cha maporomoko ya Kalambo. (Kalambo Falls)

Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu (kushoto) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) wakati walipofika kwenye sehemu ya kwanza ambapo maporomoko hayo hayaonekani kwa ufasaha (nyuma yao).

Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Dan Kazungu baaada ya kufika eneo ambalo unaweza kuyaona maporomoko hayo vizuri. 

Sehemu ya maporomoko ya kalambo (Kalambo Falls) 

Amesema kuwa eneo hilo ni zuri kwa wanafamilia kulitumia katika siku za mapumziko, siku za sikukuu na pia kujitokeza ili kuyaona maajabu hayo ambayo yametambuliwa na Shirika la umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni urithi wa dunia.

“Tunaomba wawekezaji waje hapa kwa wingi, hapa kuna kivutio ambacho kimejulikana na umoja wa mataifa UNESCO kama hifadhi ya urithi wa dunia, mje wawekezaji hapa, pahali ambapo siku za mwisho wa wiki watu wanaweza kuja kujipumzisha ama siku za sikukuu kuja na familia yao kwaajili ya “picnic”, wanajenga “lodges” lakini tunaomba “lodges” zijengwe nyingi zaidi za hadhi ya ubora wa juu zaidi ili tufurahie na familia zetu,” Alisema.

Balozi Kazungu ameyasema hayo alipotembelea maporomoko ya kalambo katika ziara yake ya siku moja Mkoani Rukwa iliyolenga kutafuta fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huku akitembelea kiwanda cha Nyama cha SAAFI pamoja na ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga.

Aidha, Balozi Kazungu alitoa ushauri kwa wakala wa misitu Tanzania wanaoshughulika na uhifadhi wa msitu wa Kalambo pamoja na kuimarisha miundombinu ya maporomopko hayo kuona uwezekazo wa kuweka nyaya pamoja na vigari vitakavyopita kwenye nyaya hizo ili watalii waweze kuyaona maporomoko hayo vizuri zaidi pamoja na msitu huo.

Wakati akisoma taarifa ya maporomoko hayo ya Kalambo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Kalambo Helman Ndanzi amesema kuwa pindi ujenzi wa ngazi za kushukukia kutoka maporomoko yanapoanzia hadi kufikia sehemu maji yanapodondokea utakapokamilika, ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 1277 na kugharimu shilingi 852,789,066.70.

“Changamoto zilizopo ni kutotangazwa vya kutosha maporomoko hayo hali inayopelekea kutojitokeza kwa wawekezaji katika eneo hilo ambalo mawasiliano ya simu pia bado ni tatizo na hivyo tunaiomba mitandano mbalimbali ya simu kujitokeza kuweka minara katika maeneo haya ili mawasiliano yawe rahisi,” Alisema.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alimhakikishia Balozi huyo kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha unakamilisha miundombinu inayohitajika ili kuwarahisishia wawekezaji kutekeleza shughuli zao kwa urahisi na hatimae kuinua uchumi wa wananchi katika mkoa lakini pia uchumi Tanzania kwa ujumla.

“Sisi tupo kwenye mpango ule wa viwanja vya ndege vile vinne, kuna kiwanja hiki cha Sumbawanga, Tabora, Shinyanga pamoja na Kigoma, karibu kila kitu kipo tayari kimazingira, vitu vyote vinavyotakiwa kufanyika kabla ya kuanza upanuzi wa uwanja tayari vimekwishafanyika, mhandisi mshauri yupo, mkandarasi yupo, mikataba tayari, fidia kwa wananchi waliohusika nae neo la upanuzi tayari, kila kitu kipo tayari, bado serikali haijaruhu lakini bila ya shaka wakati wowote ruhusa itatoka,” Alisisitiza.

Maporomoko ya Kalambo ni maporomoko ya pili kwa urefu kutoka maji yanapoanzia kumwagika hadi yanapodondokea kwa mita 235 na upana wa mita kuanzia 3.6 hadi mita 18 (single drop waterfall) ambapo maporomoko ya kwanza ni ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yenye urefu wa mita 947.Mapato ya Manispaa ya Sumbawanga kupaa kwa 46% kutokana na ujenzi Stendi ya Kisasa.


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amepongeza juhudi zinazofanwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga katika kukusanya mapato pamoja na kuwa mbunifu wa kuongeza vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuweza kutatua na kukamilisha miradi mbali mbali ya manispaa hiyo.
Muonekano wa Stendi ya Manispaa ya Sumbawanga pindi itakapomalizika mwezi Disemba 2019

Amesema kuwa kukamilika kwa stendi hiyo ya kisasa kutaongeza ukusanyaji wa mapato wa karibu asilimia 46 ya mapato ya sasa ambapo manispaa hiyo ilikisia kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ikusanye shilingi 2,212,104,000 na hadi kufikia mwezi machi 2019 ilikuwa imekusanya shilingi 2,424,032,802.71 ambayo ni sawa na asilimia 110 ya makusanyo.

“Hii stendi ikimalizika mapato ya kutoka hapa itakuwa bilioni 1, sasa hii ni karibu asilimia 46 ya mapato yote ya manispaa kwa sasa hivi, hamuoni kwamba mapato ya manispaa yataongezeka kwa kasi kubwa sana na kwa hali hiyo hata waheshimiwa madiwani wataweza kutekeleza mipango yao vizuri na kwa ukamilifu sana na watakaonufaika ni sisi wananchi wote ndani ya Manispaa, “Alisema.

RC Wangabo ametoa kauli hiyo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa kituo kipya cha kisasa cha mabasi kitakachojengwa katika eneo la Katumba azimio lililopo kilomita 12 kutoka Sumbawanga mjini, ambapo mradi huo ukikamilika utaiingizia manispaa ya Sumbawanga Shilingi 1,027,800,000 kwa mwaka.

Aidha, Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri nyingine za mkoa huo kuipa kipaumbele miradi ya kimkakati, miradi ambayo huleta fedha nyingi kwa wakati mmoja kwani kwa kufanya kutazifanya halmashauri hizo kuweza kutatua kero nyingi za wananchi pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga James Mtalitinya alisema kuwa miundombinu itakayojengwa katika eneo hilo ni pamoja na Eneo la kuegeshea mabasi ya ndani na nje ya mkoa, bajaji, bodaboda, taksi na baiskeli, vyumba vya maduka, jengo la utawala, kituo kidogo cha polisi, mama lishe, choo cha kulipia, uzio, Taa, mifereji, vyumba kwaajili ya benki na ATM’s na vyumba vya mazoezi (Gyms)

“Mzabuni aliyepatikana kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Kisasa cha Mabasi Katumba azimio ni Sumry Enterprises Ltd. Eneo ambalo litatumika kwaajili ya Ujenzi wa Stendi ni ekari 10 na ekari 12 zitakuwa ni kwaajili ya mipango ya halmashauri ya hapo baadae. Mradi huu ni chanzo cha mapato ambacho kitaweza kutuingizia fedha itakayotumika kujenga au kumalizia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo ndani ya Manispaa na Kuboresha huduma mbalimbali.” Alisema.
  
Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Manispaa ya Sumbawanga iliweka bajeti ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi Katumba Azimio kupitia fedha za Mradi wa Uimarishaji miji (ULGSP) na kumpata mkandarasi Sumry Enterprises Ltd ambaye atahusika na ujenzi huo utakaogharimu shilingi 5,955,363,986 bila ya VAT