Thursday, December 29, 2011

TAARIFA YA USIMAMIZI WA UKARABATI WA LAMBO LA MIFUGO LA KACHECHE HALMASHAURI YA WILAYA YA NKASI

1. UTANGULIZI
Lambo la Mifugo la kacheche ni mradi ulioibuliwa na Wananchi wa Kijiji cha Kacheche kwa lengo la kukidhi mahitaji ya maji kwa matumizi ya mifugo  wakati wa upungufu wa maji  (miezi ya Julai hadi Octoba).

Ujenzi wa Bwawa hili ulianza Mwaka 2009 kwa kuingia Mkataba wa Ujenzi kati ya  Halmashauri na  Mkandarasi ajulikanae Kama Kafurusu Enterprises Chini ya usimamizi wa Ofisi ya Kanda ya Umwagiliaji Mbeya kwa gharama ya shilingi za Kitanzania 137,500,000/=. Fedha hizi zilitolewa na Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya kilimo wa Wilaya (DADPs) kiasi cha Shilingi 110,000,000/=, mchango wa  Halmshauri ya wilaya ulikuwa ni  shillingi 22,000,000/=  na mchango wa wananchi ni shillingi 5,500,000/=.Mkandarasi alishindwa kumaliza Ujenzi wa lambo la Mifugo  kwa wakati kulingana na Mkataba alioingia na Halmashauri hivyo  kupelekea tuta la bwawa  kutokamilika na kumeguliwa na mvua za Mwaka 2010.Taratibu za kimkataba zilifuatwa juu ya Mkandarasi Kafurusu Enterprises kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji H/shauri ya Wilaya ya Nkasi.

Uwezo wa Lambo kuhifadhi maji ni mita za ujazo 24,000 na uwezo wa kunywesha mifugo 5,000 kwa siku katika kipindi cha kiangazi. Lambo hili la Mifugo litakapokamilika litakuwa na mabirika 2 kwa ajili ya kunyweshea mifugo, kitorosha maji (spilly way) chenye uwezo wa kupitisha maji ya mita za ujazo 12 kwa sekunde (flow rate) ,tuta la kukinga maji lenye urefu wa mita 125,kina kirefu cha mita 5 na upana wa mita sita juu ya tuta.


2. UKARABATI WA LAMBO LA MIFUGO
2.1 UINUAJI NA UPANUAJI WA TUTA .
Kazi ya uinuaji na upanuaji  wa Lambo la Kacheche ilianza tarehe 9/11/2011 kupitia  ‘Force Account’ na Mitambo ya kufanyia kazi kama vile (Excavator) Kijiko,(Compactor/Roller) Kishindilia  na (Damp Track) Lori vilikodiwa toka kwa kampuni ya wachina ya ujenzi (CHCEG GROUP) iliyoweka kambi  Paramawe Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, kwani fedha zilizokuwepo zisingetosha kuweka Mkandarasi.Fedha iliyotengwa ilikuwa ni Shilingi 45,000,000/=(Milion arobaini na tano).
Kazi ya  ukarabati ilikuwa ni kuongeza upana wa tuta toka mita tatu (3m) mpaka mita sita (6m) na kuongeza urefu wa tuta kwa mita moja (1m) toka tuta lilipokuwa awali (existing level of the embarkment), kwa kuweka kwanza udongo usiozuia maji kupita (Impervious Materials ) na baadaye ule unaoruhusu maji kupita(Pervious Paterials) na kushindilia  kutumia  kishindilia ( Compactor/Roller), kutokana na hali ya hewa, kazi ya kushindilia ilianza kufanyika kwanza na kijiko (Excavator) ili kutengeneza barabara ya kishindilia (Compactor) isizame .
Baada ya kazi ya uinuaji na upanuaji wa tuta kukamilika kama ilivyo hapo juu tuta liliongezwa kwa urefu wa mita moja na upana wa mita sita, hata hivyo kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya maeneo mengine upana wa mita sita haukufikiwa hasa eneo la mto, hata hivyo ubora na uhimara wa tuta haujaathirika.
Aidha kazi hii ilianza kwa kuchelewa kutokana na utaratibu wa kuhamisha fedha kutoka Wilayani kwenda kwa wanufaika kuchelewa.Ucheleweshaji huu ulisababisha kazi kuanza katika mazingira magumu kwani mvua zilitukuta katika eneo la lambo.Hivyo kufanya Mitambo na malori yaliyokuwa yakisomba udongo usiozuia maji kupita (Impervious Materials) na ule unaoruhusu maji kupita( Pervious Materials) kukwama na mengine kuharibika kabisa kwa kuvunja difu,  kama inavyoonekana kwenye picha No.2,3,4,  hapa chini:-

No.1 Eneo la tuta liloaribika kabla ya ukarabati.

No. 2  Kijiko (excavator ) ikiwa imezama kwa sababu ya mvua zilizonyesha mara baada ya kazi kuanza  na kusababisha ucheleweshaji wa uinuaji na upanuaji  wa tuta.
N0.3  Kijiko (excavator) kikiwa kimezama na Bull Dozer ikikivuta bila mafanilkio.

 
No.4 Kijiko ( excavator-CAT) ikikwamua kijiko (excavator-COMAST’U) kilichozama na kufanikiwa kukikwamu ndipo kazi ya uinuaji na upanuaji wa tuta ikaendelea.

No.5 Kijiko kikiwa kimekwamuliwa tayari kuendelea na kazi ya ukarabati wa tuta

Aidha pamoja na hali ya hewa kuwa mbaya kazi ya uinuaji na upanuaji wa tuta iliendelea kufanyika   mchana kwa siku sita na usiku kwa masaa zaidi ya nane kwa siku tano.Kazi hii ya uinuaji na upanuaji ilikamilika kama inavyoonekana kwenye picha hapa chini:-

No.6. Tuta likiwa limepanuliwa kwa upana wa mita sita na kuinuliwa urefu wa mita moja ,na kazi ya kumwaga kifusi inaendelea.
No.7 Kazi ya kushindilia udongo na kumwaga kifusi ikiendelea.

No.8 Tuta likiwa limeongezwa urefu na upana na kazi ya kumwaga kifusi inaendelea.
No.9 Kazi ya kumwaga kifusi, kusambaza na kushindilia inaendelea .
No. 10  Kazi ya kuongeza tuta kwa urefu wa mita moja ikiwa kwenye hatua ya mwisho.

 
2.2  UJENZI WA UKUTA WA KITOROSHA MAJI (SPILLY WAY)
Ujenzi wa ukuta wa kitorosha maji ulienda sambamba na uinuaji na upanuaji  wa tuta.Ukuta wa kitorosha maji umeongezwa kwa nusu  mita (0.5m) ,kama inavyoonekana kwenye picha hapa chini:-

No.11   Kazi ya kuongeza tuta inaendelea kwa kuweka kifusi (Pervious Materials), kusambaza na kushindilia kwa kutumia kishindilia (Roller) , aidha kazi ya kuongeza ukuta wa kitorosha maji (Spilly wall) kwa urefu wa nusu mita (0.5m) imekamilika kama inavyoonekana kwenye picha.

2.3 UJENZI WA MAWE KWENYE TUTA NA MABIRIKA YA KUNYWESHEA MIFUGO
Kazi ya Ujenzi wa mawe kwenye tuta kwa sehemu ya tuta iliyoongezeka (stone pitching) , pamoja na ujenzi wa Mabirika ya kunyweshea Mifugo (Cattle Troughs) haijakamilika kutokana na bajeti kuwa ndogo ,hata hivyo mawe, mchanga na saruji (Mifuko 15) vipo eneo la Lambo, aidha nashauri yafuatayo ili kukamilisha ujenzi huu na Lambo kuwa endelevu na liweze kufanya kazi iliyokusudiwa:-
1.   Nguvu ya wanananchi (Wanufaika) itumike kuonyesha umiliki wa Mradi na Mchango wa wanufaika :-
a.    kwa ajili kazi ya kusogeza mchanga, mawe na kupanga mawe  kwenye eneo la tuta lililoongezwa ili kazi ya ujenzi iendelee, aidha mawe, mchanga vinapatikana eneo la lambo.
b.    kusambaza udongo juu ya tuta na kuchimba mfereji wa kuzuia maji yasifanye uharibifu juu ya tuta ili kulifanya tuta kuwa endelevu.
c.    Kurudishia majani yaliyopandwa upande wa juu wa tuta (upstream) na kuyatunza ili kufanya tuta kuwa endelevu.
d.    Kulinda lambo juu ya watu waharibifu au mifugo na kufanya usafi kwa kutoa magugu ndani ya lambo.
2.   Wafugaji wote (wanufaika) waliopo kijiji cha Kacheche Halmashauri ya wilaya ya Nkasi na vijiji vya jirani hasa wa kabila la Wasukuma washirikishwe ili wachangie ujenzi na ukamilishaji wa mabirika ya kunyweshwa mifugo, kwani wao ndio wanufaika wakubwa wa lambo.
3.   Elimu iendelee kutolewa kwa wananchi juu ya wajibu wao wakuchangia asilimia 20 (20%)  kwa miradi wanaoiibua ili kuonyesha umiliki wa miradi hiyo na kuifanya kuwa endelevu.
4.   Namba moja hapo juu(No.1), ifanyiwe kazi kwa kushirikiana na Mtaalam wa Umwagiliaji Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na mapema kabla mvua hazijaanza kuwa nyingi kwani isipotekelezwa mapema mvua zinaweza kufanya uharibifu mkubwa wa lambo, kwani mwaka huu kama walivyotoa taarifa mapema  wataalam wa hali ya hewa kuwa mvua zitakuwa nyingi.
5.   Halmashauri ifanye utaratibu wa kupeleka vifaranga vya samaki katika Bwawa kukamilisha lengo mojawapo la uwepo wa Bwawa ,kwa wananchi kupata lishe bora kwa uvuvi wa samaki.
6.   Aidha kutokana na usumbufu uliopatikana wakati wa ukarabati wa lambo uliosababishwa na mvua, nashauri Halmashauri kuwa na mipango ya kutekeleza shughuli za umwagiliaji kwa kuzingatia hali ya hewa.

Imetolewa na:
Eng.  Eliabi .J. Mashingia
Agro-Engineer

Sunday, December 25, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake jana.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ofisini kwake. Kulia ni Mussa Mwangoka (Mwananchi-Rukwa), Sammy Kisika (Star TV na RFA-Rukwa), na Petty Siame (Daily News/ Habari Leo- Rukwa) Kushoto ni Kaimu Mkurugenza wa Manispaa ya Sumbawanaga, Bw. Maulid.

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya wakisikiliza swali kutoka kwa waandishi wa habari.

PRESS CONFERENCE
24/12/2011
Viongozi wote wa serikali,
Watumishi wote wa serikali,
Vyama vya siasa,
Taasisi za Dini, wazee wetu wa mkoa wa Rukwa,
Akina mama na vijana bila kuwasahau kwa namna ya pekee waandishi wetu wa Habari

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wanajamii wa Mkoa wa Rukwa na Mkoa tarajiwa wa Katavi kwa jinsi ambavyo mmenipa ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toka kuteuliwa kwangu kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
1.   Salam za Krismas na Mwaka Mpya

v Kesho tarehe 25/12/2011 ni Sikukuu ya Krismas ambapo Wakristu Duniani kote watasherehekea kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristu. Sikukuu hiyo inakuja sambamba na Sherehe za Mwaka mpya 2012.

v Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia wakazi na wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa heri ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya wenye mafanikio (2012).

v Nawaomba wananchi wote pamoja na wageni wa Mkoa wa Rukwa kusherehekea msimu huu wa  Sikukuu kwa amani na utulivu kwa kujiepusha na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani.

v Nawahakikishia wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama katika mkoa wetu vimejipanga vizuri katika kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa Mali na Raia wakati wote huu wa Sikukuu.

v Aidha nitoe tahadhari kwa wale wote watakaohusika na vitendo vya uvunjifu wa amani kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria, na hivyo tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi katika utoaji wa taarifa za matukio mbalimbali yanayoashiria uvunjifu wa amani.

v Natoa wito kwa madhehebu yote ya dini katika Mkoa wa Rukwa kuendeleza ushirikiano na Serikali katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu wa Rukwa.
2.   Hali ya Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Rukwa

*     Nichukue fursa hii Kuungana na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwapa pole wananchi wote wa Jiji la Dar es Salaam waliopatwa na maafa au kuathirika kwa namna moja ama nyingine na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha kwa muda wa siku tatu mfululizo.

*     Kwa taarifa iliyotolewa tarehe 22-23/12/2012 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Dkt. Agnes Kijazi inaonyesha kuwa maeneo ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa) yanatarajiwa kuendelea kuwa na mvua katika kiwango cha juu ya wastani pamoja na vipindi vya mvua kubwa.

*     Hali ya mvua katika Mkoa wetu wa Rukwa inaendelea kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha. Mpaka sasa hakuna taarifa zozote za maafa ya mvua hizo katika mkoa wetu.

*     Kufuatia agizo la hivi karibuni la Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwataka wananchi wote wanaoishi katika maeneo hatarishi kwa mvua zinazoendelea kunyesha hasa mabondeni waondoke, Napenda kuwaagiza wale wote wanaoishi kwenye maeneo hayo katika Mkoa wetu waondoke mara moja ili kuepusha madhara yanayoweza kuletwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Aidha Idara ya Ardhi ihakikishe inawapimia viwanja salama wale wote watakaobainika kuwa na ulazima wa kuhama katika maeneo hayo hatarishi.

3.   Hali ya Barabara

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wetu baadhi ya maeneo korofi ya barabara ni mbaya hasa barabara ya Tunduma-Ikana, Majimoto-Inyonga, Mpanda-Inyonga, Mpanda-Karema na Mpanda-Kigoma, Hivyo basi nawaagiza Tanroads kuhakikisha maeneo hayo yanarekebishwa ili yaweze kupitika bila usumbufu wowote.

Aidha ni marufuku kwa magari ya mizigo kuzidisha uzito uliopangwa kisheria. Kwa ufahamu wangu uzito huo usizidi tani 30.
4.   Usafi wa Mazingira

·        Hali ya usafi wa mazingira katika miji yetu siyo ya kuridhisha sana. Napenda kutoa agizo kwa wananchi na wakazi wote wa mkoa wa Rukwa kushiriki katika usafi wa mazingira ili kuepukana na Magonjwa ya Mlipuko hususan Kipindupindu.

·        Usafi ni jukumu la kila mwananchi hivyo kila kaya ihakikishe inafanya usafi katika eneo lake kuweka mazingira safi na ya kuvutia kuweza kuuletea mkoa wetu sifa na heshima.

·        Viongozi wote wa serikali katika mkoa kuanzia ngazi ya wakuu wa wilaya hadi wenyeviti wa vijiji na mitaa wawe ni mfano katika usafi wa mazingira na wasimamie  zoezi la usafi wa mazingira kikamilifu katika maeneo yao.

·        Natoa agizo kwa Viongozi wa Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha barabara zote za lami katika Manispaa  zinakuwa safi kwa kufagia mara kwa mara mchanga ambao unatuama kwenye barabara hizo.

·        Wahakikishe pia miundombinu ya maji safi na maji taka katika Manispaa hususan mitaro ya maji taka inazibuliwa na kusafishwa mara kwa mara.

·        Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kutumia fursa hii ya mvua zinazoendelea kunyesha kupanda miti kuhifadhi mazingira na vyanzo vya Maji. 

5.   Bei ya bidhaa:

Nimesikitishwa kuona bei ya petrol kufikia Tshs. 8,000/= na cement kufikia mfuko Tshs,22,000/= wakati inatoka hapa jirani Mkoa wa Mbeya. Hali ya mafuta naamini itaboreka hivi karibuni kwani tayari malori yapo njiani kuleta bidhaa hiyo. Kuhusu cement nawataka wafanya biashara washushe mara moja, bei ya cement isizidi elfu 18,000/=. Zaidi ya hapo TRA wafuatilie mahesabu yao na kuona kama kweli wanapata hasara.
Napenda kuwaambia wananchi wangu wa Mkoa wa Rukwa kuwa; nawapenda sana, na ombi langu kwao ni ushirikiano wa hali na mali katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya mkoa huu. Naahidi kutoa ushirikiano wangu wote kwao bila kubagua dini, rangi, kabila, maskini au matajiri.

Nashkuru kwa kunisikiliza.
 Eng. Stella Martin Manyanya
MKUU WA MKOA
RUKWA

MASISTA WA MARIA MTAKATIFU MALKIA WA AFRIKA NA ZAWADI YA KRISMAS NA MWAKA MPYA KWA MKUU WA MKOA WA RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akipokea zawadi ya Keki na Kadi ikiwa ni zawadi ya Krismas na Mwaka Mpya kutoka kwa Masista wa Kanisa la Maria Mtakatifu Malkia wa Afrika lililopo Katandala katika Manispaa ya Sumbawanga.

Keki na Kadi aliyopewa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kama zawadi ya Krismas na Mwaka Mpya 2012.

HERI YA KRISMAS NA MWAKA MPYA

Saturday, December 24, 2011

MKUU WA MKOA WA RUKWA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KATIKA HOSPITALI KUU YA MKOA HUO, ABAINI MAPUNGUFU MBALIMBALI NA KUYATOLEA MAAGIZO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali Kuu ya Mkoa huo kufuatia malalamiko yaliyokuwa yamejitokeza kuhusu huduma mbovu inayotokana na upungufu wa vifaa katika Wodi ya wazazi.

Kufuatia malalamiko hayo Mkuu huyo wa Mkoa akiambatana na Kamati kuu ya Chama Tawala katika Mkoa huo waliamua kufanya ziara ya kushtukiza  kujionea hali halisi ya huduma katika hospitali hiyo.


Katika ziara yake hiyo alibaini mapungufu mbalimbali yakiwemo upungufu wa vyandarua kwenye baadhi ya vyumba katika wozi za wazazi ambapo aliagiza kamati ya Hospitali hiyo kuondoa mapungufu hayo katika kipindi cha wiki moja ijayo, kinyume na hivyo wajiandae kuwajibika.


Uhaba wa gloves kwa ajili ya kusaidia kinamama wajawazito pia ni tatizo kubwa katika hospitali hiyo ya Mkoa. Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Marwa alisema MSD ndio wanaohusika na usambazaji wa gloves hizo na kwamba kuna tatizo katika uzalishaji na usambazi unaopelekea uhaba mkubwa wa vifaa hivyo, alisema gloves zilizopo ni kwa ajili ya dharura tu.


Hali hiyo inapelekea kina mama wajawazito kulazimika kwenda hospitalini hapo na gloves zao wenyewe. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya alitolea tamko suala hilo na kusema ni bora MSD wawe wazi kama wameshindwa kugawa gloves hizo ili Mkoa utafute njia mbadala ya kuweza kupata vifaa hivyo badala ya kuwategemea wao.


Mapungufu mengine ni idadi ndogo ya madaktari na manesi katika hospitali hiyo, Mkuu wa Mkoa alisema kutokana hospitali hiyo kuwa na vibali vya ajira 47 na manispaa vibali 20, yeye pamoja na kamati husika kwenye hospitali hizo wataenda kuziona mamlaka husika ili vibali hivyo viweze kufanyiwa kazi haraka na watumishi hao waweze kupatikana.


Aliendelea kusema kuwa kwa wale watumishi wa hospitali 16 waliomba mkataba baada ya kustaafu kuna haja ya wao kupewa nafasi kama bado wanahitajika katika nafasi zao za kutoa huduma. Mkuu wa Mkoa alisema "hatuwezi kuitupa hi nguvu kazi tuliyonayo, itabidi tuendelee kuitumia kama bado inatusaidia huku tukiendelea kutafuta nguvu mpya".


Injinia Manyanya alitoa wito kwa wale wahitimu wa sekta ya afya wanaochaguliwa kuja kufanya kazi Rukwa kuwa wasiogope kuja kwani hakuna tatizo lolote na yote mabaya yanayosemwa kuhusu Rukwa hayana ukweli wowote. "Mimi nimekaa Rukwa nimeona maisha ya hapa ni mazuri hakuna tatizo lolote" alisema Injinia Manyanya. 


Kutokuwepo kwa mtaalam wa kuendesha mashine ya kutolea dawa na kumsaidia mzazi kupumua baada ya kutoka kwenye dawa ya usingizi ni pungufu jingine katika hospitali hiyo. Injinia Manyanya ameiomba Wizara husika kuleta mtaalam wa mashine hiyo au kumpeleka mtumishi mmojawapo kutoka katika hospitali hiyo kwenye mafunzo ya jinsi ya kuendesha mashine hiyo.


Mapungufu mengine yaliyobainika ni kwenye vitanda vya kuhifadhia watoto wachanga (Incubators) kuwa havifanyi kazi vizuri. Alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kutoa mashine moja (Incubator) kwa hospitali ya Mkoa katika tatu walizopewa na Kampuni ya uwekezaji ya TPM Mining kutoka Uturuki iliyowekeza kwenye uyeyushaji na ununuzi wa madini ya shaba Wilayani Mpanda. 


Kwenye upande kuna mapungufu kuwa baadhi ya manesi hawajalipwa posho zao za muda wa ziada na hivyo Mkuu wa Mkoa kuagiza malipo hayo yafanyike mara moja kutokana na fedha za malipo hayo kuwa zilishatumwa katika Mfuko wa hospitali kuwezesha malipo hayo. 


Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa alitoa muda wa siku tisa (9) kwa kamati ya hospitali kuhakikisha kuwa mapungufu aliyoyatolea maagizo yawe yamekwisha fanyiwa kazi. Alisema "nitakuja tena kukagua baada ya siku tisa nikikiuta hali bado ipo hivi nikute mmeshaandika barua ya kujiuzuli maana kazi itakuwa imewashinda"

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akisalimiana watumishi wa Hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akisaini Kitabu cha wageni kwenye Ofisi ya Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.

Mhe. Eng. Manyanya akiwaeleza watumishi na viongozi wa Hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa lengo la ziara yake ya kushtukiza kuwa na taarifa kuwa huduma katika wodi ya wazazi ni ya kusikitisha.

Wajumbe wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati akitoa maelekezo mbalimbali.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akihutubia watumishi wa hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa katika ofisi ya Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.
Hapo akizungumza na baadhi ya ndugu za wagonjwa walikua hospitalini hapo kutembelea ndugu zao, aliwaasa ndugu hao kuonyesha upendo wa dhati kwa ndugu zao hasa katika kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na maradhi.


Msafara ukielekea kwenye wodi ya wazazi hospitalini hapo


Kaimu Mganga Mkuu Hospitali Kuu ya Mkoa Rukwa Dkt. Marwa akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya.
Kamati kuu ya Chama Tawala Mkoa wa Rukwa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya, Mbunge wa Sumbawanga Mjini CCM Mhe. Aeshi Hillal wa pili kushoto, Bi Maufi ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mhe. Sabas Katepa wakifuatilia mwenendo wa huduma ya afya katika katika Hospitali Kuu ya Mkoa Rukwa.  


Mtoto huyu anaitwa Rachel Richard, alizaliwa nyumbani katika maeneo ya Majimoto wilayani Mpanda akiwa na uvimbe unaopelekea mguu wake wa kulia kujikunja, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa uvimbe na mguu ili aweze kuondokana na matatizo hayo. Kwa yeyote mwenye uwezo anaweza kuwasiliana na uongozi katika hospitali ya Mkoa na kutoa msaada wowote kufanikisha upasuaji huo. Mama wa mtoto huyo anaitwa Miriam Nassoro.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akiwa amemshika mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Stella mara tu baada ya kuzaliwa hospitani hapo.


Mashine ya kumsaidia mama mzazi kupumua baada ya kutoka kwenye dawa ya usingizi katika hospitali ya Mkoa Rukwa, Mashine hii haina mtaalam ya kuiendesha, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameziomba mamlaka husika kuleta mtaalam wa kuendesha mashine hiyo au kumpeleka mafunzoni mtumishi katika hospitali hiyo aweze kuendesha mashine hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na msafara wake wakiwasalimia wazazi waliokuwa mapumziko baada ya kujifungua.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitoa maagizo kwa Kamati ya Hospitali ya Mkoa wa Rukwa.

Thursday, December 22, 2011

YALIYOJIRI KATIKA ZIARA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA WILAYANI MPANDA HIVI KARIBUNI

Njiani kuelekea Mpanda Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya alikutana na wajasiriamali wadogowadogo wakifanya biashara ya matunda kandokando ya barabara itokayo Sumbawanga kuelekea Mpanda. Aliwaunga mkono wajasiriamali hao kwa kununua bidhaa zao na kuwapa kinamama waliokuwa na watoto zawadi kidogo ya fedha ambazo waligawana na watoto zao.

Hili eneo linaitwa Magamba ambalo lipo wilayani Mpanda ambapo katika msimu huu wa masika maembe mengi yanapatina katika eneo hili, Ndoo moja ya maembe inayoonekana inauzwa shilingi alfu mbili. Ni fursa kubwa kwa wawekezaji kujenga miundombinu katika maeneo haya kwa ajili ya viwanda vya kusindika matunda na kusafirisha bidhaa hiyo.

Katika ziara yake hiyo alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wa Halmashauri ya Mji Mpanda na kujadiliana nao baadhi ya mambo. Aliiagiza Halmashauri ya Mji Mpanda kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato mbali na ilivyokuwa navyo hivi sasa kuweza kuongeza wigo wa kodi za Halmashauri hiyo. Aidha alimuagiza Mkurugenzi wa Mji Mpanda kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye kuajiri katika Halmashauri hiyo. Hiyo ilikuja kutokana na kuwepo kwa wanaume wengi zaidi ya asilimia 90 kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wafanyakazi wa Halmashauri hiyo ya Mji Mpanda.

Alipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari ambapo alizungumzia mambo ya kadha wa kadha likiwepo suala la nafasi za ajira zinazopatikana Mkoani Rukwa na kuwatoa hofu watanzania ambao hupata fursa ya kuja kufanya kazi Rukwa na kuacha kufika kwa visingizio kuwa hakufai kuishi na kwamba ni Mkoa wa pembezoni pamoja na kuuhusisha na mambo ya kishirikina. Alisema kuwa Rukwa ni pahala salama sana kwa makazi na hakuna matatizo yeyote, yote mabaya yanayozungumzwa kuhusu Rukwa hayana ukweli wowote. Alisema "mimi nimekaa Rukwa na nimeona ni jinsi gani wananchi wake walivyo wakarimu na wenye upendo wa hali ya juu"

Alifanya kikao cha kazi na viongozi wote wa Mkoa wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa idara za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Uhamiaji na wakuu wa idara katika Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda. Aliwata viongozi hao kila mmoja kutimiza wajibu wake na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikiano wa karibu miongoni mwao kuleta ufanisi katika shughuli za Serikali kwenye ngazi ya Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Msafara wake ambao ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima, Mkuu wa Wilaya ya MpandaMhe. Dkt. Rajab Rutengwe na wasaidizi wake wengine pamoja na viongozi wa Halmashauri walifanya ziara kwenye Kampuni ya Uyeyushaji na ununuaji wa Shaba kutoka Uturuki ya TPM Mining.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya (MB) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi za TPM Mining. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiwa na mwenyeji wake kiwandani hapo ambae ni Kaimu Meneja wa Uzalishaji Kiwandani aliyejulikana kwa jina moja la Mermet ambae pia ni Raia wa Uturuki.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (MB) alionyeshwa makaa ya mawe yenye jumla ya tani 300 yaliyoagizwa kutoka China kwa ajili ya kuzalishia umeme wa kuendesha mitambo na shughuli za Kampuni hiyo. Aliwapasha wawekezaji hao kuacha kununua makaa hayo nje na badala yake wanunue hapa nchini. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe. 

Alionyeshwa pia vyakula mbalimbali wanavyoagiza wawekezaji hao kutoka nchini kwao Uturuki. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliwataka wanunue vyakula vinavyopatikana hapa nchini.

Baadhi ya vyakula hivyo na vinywaji mbalimbali

Store ya kuhifadhia vifaa na vyakula vya Kampuni hiyo

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiangalia moja ya madini yanayonunuliwa na Kampuni hiyo ya Kituruki Wilayani Mpanda, Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe.

Mkuu wa Mkoa na Msafara wake wakiangalia vyakula vinavyoagizwa na Kampuni hiyo kutoka nje ya nchi (Uturuki)

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya alipewa zawadi ya mapambo na wawekezaji hao, Kampuni ya TPM Mining.