Tuesday, January 31, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AMUWAKILISHA WAZIRI MKUU KWENYE MAHAFALI YA KIDATO CHA SITA SHULE YA SEKONDARI USEVYA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injnia Stella Manyanya akisalimiana na baadhi ya viongozi na maafisa elimu wa Wilaya ya Mpanda na Mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili katika mazingira ya shule ya Sekondari ya Usevya tayari kushiriki mahafali ya Kidato cha Sita kwa niaba ya Waziri Mkuu ambaye hakuweza kuhudhuria kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine muhimu ya kiserikali. Shule ya Sekondari Usevya ipo Wilayani Mpanda Jirani na Kijiji cha Kibaoni ambacho ni Nyumbai kwa Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda. 

Mkuu wa Mkoa akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Shule hiyo. Anayeshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Naomi Nko.

Mkuu wa Mkoa alianza shughuli za mahafali hayo kwa kukagua Kikosi cha Gwaride la shule hiyo ambacho kilikuwa kimejipanga kikakamavu bila ya kutikisa hata kidole.

Vijana wa Shule ya Sekondari Usevya walionekana kuwa na vipaji mbalimbali, hapa ikiwa ni baadhi ya wanafunzi wanaohitimu wakijiandaa kwa namna yake kwa ajili ya kusoma Shairi kwa Mgeni Rasmi.

Risala ya Wanafunzi wanaohitimu ikisomwa kwa Mgeni Rasmi, Kushoto ni Gatus Mgasira na Mussa Hussein.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Naomi Nko alishindwa kuvumilia na kuamua kuinuka kusakata rumba na wanafunzi wanaohitimu.

Risala ya wanafunzi wanaobaki ikisomwa na Mwanafunzi Revocatus Pigangozi.

Baadhi ya wanafunzi waliandaliwa kuonyesha gwaride maalum lililopita mbele ya Mgeni Rasmi, Wanafunzi hawa walioneka kupikwa vizuri kwani walionyesha ukakamavu wa hali ya juu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Usevya Mwl. Makanganya Makalanga akisoma taarifa ya shule yake kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya.
Alisema kuwa Shule yake ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi 80, lakini mwaka 2010 walihitimu wanafunzi 18. Mwaka jana 2011 Shule hiyo ilikuwa ya kwanza kimkoa na ikashika nafasi ya 26 kitaifa hali iliyompa moyo Waziri Mkuu na kutoa zawadi ya 100, 00/= kwa kila mwalimu na 50, 000/= kwa kila mjumbe wa bodi ya shule hiyo.
Mkuu huyo wa shule akikabidhi taarifa yake hiyo kwa Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Lilifuata zoezi la ugawaji wa vyeti kwa wanafunzi wanaohitimu. Hapo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akimkabidhi cheti mmoja ya wahitimu katika Shule hiyo.

Burudani ya Muziki kutoka kwa wanafunzi wanaohitimu ilichukua nafasi yake kuweka mazingira sawiyya.

Ilifika wakati Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kutoa nasaha zake kwa wanafunzi wanaohitimu. Kwanza kabisa aliwaambia wanafunzi hao kuwa alikuwepo mahala hapo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda ambaye hakuweza kuhudhuria mahafali hayo kutokana na kukabiliwa na shughuli nyingine muhimu za kiserikali.
Katika nasaha zake hizo aliwataka Wanafunzi hao kujijengea fikra za kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao na sio kubaki kuitegemea Serikali ambayo ina mambo mengi ya kufanya. "Jitahidini muokoe maisha yenu wenyewe, mnahitaji kulea maisha yenu...Askari namba moja ni wewe kuikoa familia yako" Alisema Injinia Manyanya.
Alizungumzia pia suala la mimba za mashuleni na kusema kuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya elimu mashuleni. Aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwaahidi wale wote watakaopata Division One na Two atahakikisha anawasaidia kupata Shule za kujiendeleza.
Katika nasaha zake hizo aliwataka wanafunzi hao kutopumbazika na kauli za baadhi ya viongozi na wananchi kuwa eti Watanzania ni masikini. Aliwataka kutumia fursa waliyonayo katika kuhakikisha jamii inaondokana na fikra hizo na kujiendeleza zaidi kielimu waweze kuikomboa jamii ya wanarukwa.
Kwa upande mwingine aliwataka wazazi wote Mkoani Rukwa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo ya kuwa na elimu bora. Aliomba ushirikiano kutoka kwa wazazi pamoja na waalimu ili kuiweka Rukwa katika hatua nyingine kielimu. Aliwaasa wazazi kuchangia huduma za elimu ikiwepo chakula mashuleni.
Alisema kuwa Rukwa kama Mikoa mingine inakabiliwa na tatizo la uhaba wa waalimu na kuwataka waalimu wanaopangiwa Rukwa kuondokana na fikra potofu za imani za kishirikina na kwamba Rukwa ni Mkoa salama ambao mambo hayo sasa yamebaki kuwa ni historia.
Kuna wakati aliamua kuinuka na kuiacha meza kuzungumza na wanafunzi kwa ukaribu huku akitumia mifano halisia. Aliwaita baadhi ya watumishi kutoka Ofisi yake akiwepo Katibu wake na Afisa Habari wake pamoja na Afisa Tawala Wilaya ya Mpanda na Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda. Aliwatumia watumishi hao kama mfano wa  mafanikio ya elimu kwa wanafunzi wanaohitimu na kuwaeleza kuwa wana fursa kubwa ya kufikia mafanikio watumishi hao waliyofikia cha msingi ni kujitambua, kujiwekea malengo na kusoma kwa bidii.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ndiye aliyefungua Muziki ikiwa ni ratiba ya mwisho kwenye mahafli hayo. Hapo akionekana na baadhi ya wanafunzi wakivunja mifupa.

Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita 2012 shule ya Sekondari Usevya.

Sunday, January 29, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AWATEMBELEA WAZAZI WA WAZIRI MKUU KIJIJINI KWAO KIBAONI WILAYANI MPANDA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya akisalimiana na Mzee Kayanza Pinda wakati alipowatembelea jana kuwajulia hali. Kushoto ni Mama Kayanza Pinda ambao ni Baba na Mama wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiwa katika picha ya pamoja na Mzee na Bibi Kayanza Pinda ambao ni wazazi wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nyumbani kwao Kibaoni Wilayani Mpanda Mkoani Rukwa. Mkuu wa Mkoa alikuwa Wilayani hapo kumuwakilisha Waziri Mkuu kwenye mahafali ya Kidato cha sita Shule ya Sekondari Usevya.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akitaniana na Mzee Kayanza Pinda alipokuwa anamuaga kuelekea kwenye mahafali ya Shule ya Sekondari Usevya ambapo alienda kumuwakilisha Waziri Mkuu aliyekuwa amealikwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye mahafali hayo. Miongoni mwa utani alioutoa Mzee Pinda ni pamoja na kumuita Mkuu huyo wa Mkoa "Mnyatomato" kumaanisha kuwa ni Mtoto wa Manyanya ambapo nyanya kwa kiingereza ni Tomato. Hahahahaaah!

MKUU WA MKOA WA RUKWA AISHAURI HOSPITALI YA WILAYA YA MPANDA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO KUTATUA MATATIZO MADOGOMADOGO YANAYOIKABILI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda Dkt. Yahya Hussein alipomtembelea Ofsini kwake jana kufuatia malalamiko ya watumishi katika hospitali yake juu ya madai ya mapunjo ya stahili zao ikiwepo malipo ya muda wa ziada, malipo ya nyongeza ya mshahara na usafirishaji wa mizigo.

Ofisini hapo alipokea taarifa ya madeni yaliyokwishahakikiwa  ya watumishi hao ambayo jumla yake ni zaidi ya Milioni 100. Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo alimueleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa kikwazo kikubwa cha kushindwa kulipa madai hayo ni mtiririko mbovu wa OC ambayo inatolewa na Serkali kila mwezi. Alisema kuwa mtiririko wa fedha wanayopewa haiendani na bajeti yao, alisema kuwa kwa mwezi anatakiwa kupewa zaidi ya Milioni 20 ili kuendesha shughuli zao bila kikomo lakini cha kushangaza huweza kupata Milioni 9 na fedha nyingine huchelewa jambo linalokwamisha utendaji kazi hospitalini hapo.

Aliongeza kusema "unaweza kupitisha likizo ya mtumishi katikati ya mwezi kwa mategemeo ya kumlipa stahili zake za likizo ifikapo mwishoni mwa mwezi lakini OC inakuja kidogo na hivyo tunashindwa kutimiza majukumu hayo na mengineyo ya msingi".

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Naomi Nko alisema kuwa upande wa madai ya nyongeza ya mishahara ambayo madai yao ndio makubwa kwa wale watumishi waliopandishwa vyeo, tatizo kubwa lipo wizarani (Utumishi)ambapo kwani taarifa zao zimeshapelekwa na utaratibu wa kuwabadilishia mishahara yao bado halijafanyiwa kazi kikamilifu. Alisema kuwa "Mtumishi huwezi kulipwa malimbikizo kabla ya kupewa mshara mpya jambo ambalo lipo chini ya Wizara husika".

Kufuatia kupokea taarifa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameishauri Hospitali hiyo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwepo kutilia mkazo sera ya kitaifa ya wananchi kuchangia katika huduma ya afya. "Kuna madeni mengine madogomadogo mfano kuna watu wanadai 5000 kwenye taarifa yenu hii, ni wazi mkiwa na vyanzo vyenu wenyewe vya mapato mnaweza kulipa madeni madogomadogo kama haya" alisema Injinia Manyanya. 

Kufuatia migomo ya madaktari nchini Mkuu huyo wa Mkoa aliwaasa madaktari kuwa na moyo wa kizalendo na subira kwa kutoa muda kwa uongozi uliopo serikalini ili uweze kutatua matatizo yao. Kupitita Mganga Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Wilaya aliwashauri Madaktari wote nchini kuona na jinsi gani wataunda timu ya majadiliano ya kitaifa juu ya hatma ya sekta ya afya nchini.

USAFIRI WA MABASI MPANDA-TABORA WASIMAMA KWA MUDA KUFATIA UBOVU WA BARABARA KUTOKANA NA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA

Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchi nzima, usafiri wa barabara kutoka Mpanda kwenda Tabora kwa mabasi umesimama kwa muda kufuatia barabara hiyo inayopita inyonga kuwa katika hali isiyoridhisha sana kwa mabasi  hayo kupita kirashisi. Usafiri wa umma unaotumika kwa sasa ni Treni. Magari madogo na hata malori yanaendelea kutumia barabara hiyo kama "PICKUP" inayoonekana pichani ilivyokutwa na mpigapicha wetu ikisafirisha mizigo na abiria kutoka Mpanda kuelekea Inyonga (Hata hivyo usafiri huo sio salama sana kwa abiria hao).

Magari madogo aina ya LandCruiser na Nissan Patrol kama inavyoonekana pichani sio kikwazo sana kwayo kuweza kutumia barabara hiyo. Hata hivyo mpango wa Serikali ya sasa ni kuunga barabara zote za Mikoa kwa kiwango cha lami mpango ambao umeshaanza kwani barabara ya Tunduma (Mbeya) -Sumbawanga- Mpanda (Rukwa) Makandarasi wapo "Site" na tayari baadhi ya maeneo katika barabara hizo yameshaanza kufunikwa kwa lami. Kwa barabara ya Mpanda- Tabora maboresho yanaendelea kuhakikisha barabara hiyo inapitika kirahisi huku mchakato wa upembuzi yakinifu. ukiendelea kuhakikisha barabara hiyo nayo inajegwa kwa kiwango cha lami.

Thursday, January 26, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA ASHIRIKI MKUTANO WA UJIRANI MWEMA MIKOA YA KANDA YA MAGHARIBI WILAYANI NZEGA LEO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Martin Manyanya (Mb) (wapili kushoto) na Wakuu wa Mikoa ya Tabora Mhe. Fatma Mwasa, Kigoma Kanali Mst. Issa Machibya (kulia) na Shinyanga Mhe. Ally Nassoro Rufunga wakiangalia moja ya mada zilizowasilishwa kwa njia ya projekta katika Mkutano wa Ujirani mwema Mikoa ya Kanda ya Magharibi mwa Tanzania uliofanyika Wilayani Nzega katika Mkoa wa Tabora. Mkutano huo ambao umefanyika leo umelenga kujadili mambo muhimu ya kimaendeleo na changamoto zinazoikabili Mikoa hiyo.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Ijnjinia Stella Manyanya (kushoto) akimkabidhi zawadi ya kinyago maalum Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Fatma Mwassa. Kinyago hicho chenye picha ya watu wawili mume na mke wakiwa wamebeba kuni na kibuyu cha maji pamoja na shoka na jembe kama ishara ya pongezi kwa Mkoa wake kuandaa kikao hicho, Alisema kuwa "kuna usemi usemao mzigo mkubwa mbebeshe mnyamwezi", hiyo ni kutokana na kwamba wakazi wengi wa Mkoa wa Tabora ni Wanyamwezi hivyo akaona amkabidhi zawadi hiyo kama ishara ya Mkoa wake kukubali kubeba mzigo mkubwa wa kuandaa kikao hicho cha ujirani mwema.  

 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Fatma Mwassa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo akionyesha zawadi hiyo kwa wajumbe wa Mkutano huo.

Wednesday, January 25, 2012

VIKUNDI VYA WAKULIMA HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA VYANUFAIKA NA ELIMU YA KILIMO KUPITIA MRADI WA MASHAMBA DARASA

Hili ni miongoni mwa shamba darasa lililopandwa kitaalamu katika kijiji cha Kaoze Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
 
Baadhi ya Maafisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na wakulima wakikagua shamba darasa katika kijiji cha Kaoze wilaya humo juzi.

VIKUNDI vya wakulima katika Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa vimeanza kufaidika na miradi ya kilimo kupitia Mashamba Darasa inayodaiwa kuwaongezea mbinu za kisasa za kilimo bora hali inayotarajiwa kuwaongezea mavuno na kipato ikiwa ni juhudi za kujikwamua kutoka katika lindi la umasikini.

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha CHEMKA kilichopo katika kijiji cha Kaoze kilichopo bonde la ziwa Rukwa walisema wamenufaika sana na elimu ya mradi wa shamba darasauliotekelezwa katika kijiji hicho na kwamba wamekuwa wakipoteza mazao mengi kwa kulima kilimo cha kiasili.
Walisema kuwa, kwa kipindi kirefu wamekuwa wakivuna magunia matatu mpaka matano kwa hekari moja walipokuwa wakilima kilimo cha asili lakini kwa kilimo bora cha kisasa wanategemea kupata magunia 25 mpaka 30 kwa hekari moja hivyo wanategemea kujiongezea kipato na kujikwamua katika umasikini.

Kwa mujibuwa Afisa Kilimo wa wilaya hiyo Shaaban Bahari, Halmashauri hiyo ina jumla ya mashamba Darasa 151 katika vijiji mbalimbali wilayani humo na kwamba hali hiyo inatarajiwa kuwafaidisha wakulima.
“Tunategemea miradu hii itawasaidia wakulima wetu kujiongezea mbinu mbalimbali za kilimo cha kisasa ikiwemo matumizi ya mbolea, kupanda kwa kuzingatia nafasi, pamoja na kutumia mbegu bora” alisema Juma.

Miradi hiyo ya mashamba darasa inatekelezwa na wilaya hiyo katika vijiji na Kata mbalimbali kwa lengo la kuwaongezea ujuzi wakulima wilayani humo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbolea pamoja na mbinu nyingine za kilimo cha kisasa

NA RAMADHANI JUMA-AFISA HABARI HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA

Sunday, January 22, 2012

HABARI KUTOKA MKOA JIRANI WA RUVUMA: RC RUVUMA AWAASA VIJANA WA JKT KUWA WAZALENDO NA NCHI YAO

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu akihutubia wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana 822 katika kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Mlale wilaya ya Songea mkoani Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said  Mwambungu akikagua gwaride lililoandaliwa na wahitimu wa mafunzo ya awali ya kiejshi katika kikosi cha 842 Mlale JKT ambapo alikuwa mgeni rasmi.Jumla ya vijana wapatao 822 wamehitimu mafunzo hayo juzi. Anayemuongoza Mkuu huyo wa Mkoa ni kiongozi wa gwaride hilo Meja Ramadhan.

Wahitimu wakipita mbele ya jukwaa na kutoa heshima kwa mgeni rasmi wakati wa gwaride la kuhitimu mafunzo ya awali ya kijeshi yaliyofanyika juzi katika kikosi cha 842 KJ Mlale JKT.Jumla ya vijana 822 walihitimu mafunzo hayo yaliyofungwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu

Na Revocatus Kassimba- Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa RUVUMA.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu  amewaasa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kuwa wazalendo na wenye kuipenda nchi yao ili waweze kuitumikia iweze kuwa na Maendeleo  endelevu.
Ametoa wito huo juzi wakati akifunga mafunzo awali ya kijeshi  yaliyojulikana kama Oparesheni  Miaka 50 ya Uhuru yalitolewa katika kikosi cha jeshi 842 Mlale JKT  kilichopo Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma.
Mwambungu amewapongeza Vijana hao kwa kuonyesha moyo wa kizalendo tangu wajiunge na mafunzo hayo mwaka jana Julai ambapo wamejifunza mambo mengi yakiwepo stadi za kazi na mafunzo ya awali ya kijeshi.

Thursday, January 19, 2012

FAHAMU ENEO LILILOTENGWA TANGU MWAKA 1984 KWA AJILI YA KUJENGWA UWANJA WA NDEGE KATIKA MJI WA SUMBAWANGA, KUNA HAJA YA ENEO HILI SASA KUENDELEZWA?

Hili ni eneo la Kisumba takribani Kilomita 23 nje kidogo ya Mji wa Sumbawanga. Eneo hili lipo ndani ya Manispaa ya Sumbawanga. Eneo hili lilitengwa tangu mwaka 1984 enzi za Utawala wa Mhe. Maj. Gen. T. Kiwelu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wa awamu ya tatu tangu Mkoa huo uanzishwe mwaka 1974.

Kutokana na kuwepo kwa fedha kwa ajili ya kuboresha uwanja mdogo wa ndege wa sasa ambao upo katikati ya Mji wa Sumbawanga, Uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Martin Manyanya umeona kuna haja kubwa ya fedha hizo kuhamishiwa katika eneo hili la kudumu ambalo ni kubwa kutosha kujenga uwanja mkubwa wa kimataifa.

Haja hiyo imekuja kutokana na sababu kuu mbalimbali moja ikiwa ni udogo wa eneo la uwanja wa sasa hali itakayopelekea Mkoa kuwa na uwanja mdogo usiokidhi mahitaji yote ya usafiri wa anga. Hata hivyo kutakuwepo na haja ya kupanua uwanja huo kama ukifanyiwa maboresho jambo litakalosababisha migogoro na wananchi litakapokuja suala la kuhamishwa wananchi hao.

Tatu kutakuwepo na ulazima wa kuwafidia wananchi watakaohamishwa jambo litakaloigharimu Serikali wakati kuna eneo hilo kubwa ambalo lipo wazi kuweza kujengwa uwanja mkubwa zaidi hata kama ujenzi wake utachukua muda mrefu. "Ni bora nguvu ya kuboresha uwanja huo mdogo ipelekwe kujenga uwanja mkubwa ambao utakuwa ni wa kudumu katika eneo la Kisumba ambalo lilishatengwa kwa ajili hiyo hata kama ujenzi huo utachukua miaka mitatu, faida yake itakuwa kubwa" alisema Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya.

Sababu nyingine ni kuwa, baadhi ya marobani wamekuwa wakisikika wakisema uwanja wa ndege wa Sumbawanga ni kipimo tosha kwa robani mzuri kutokana na ugumu wake wakati wa kutua na kupaa. Aidha wataalam nao wanasema kuwa uwanja wa ndege ukiwa katikati ya Mji ni tatizo kwani barabara za magari humchanganya robani na barabara za mapitio ya ndege jambo linaloweza kusababisha ajali mda wowote.

Uwanja mdogo wa ndege wa Sumbawanga umezungukwa na makazi ya wananchi jambo ambalo sio salama kwa wananchi husika pamoja na uwanja pia. Hivyo kuna haja kubwa ya nguvu hiyo ya kukarabati uwanja huu kupelekwa katika eneo lililotengwa kuepusha migogoro na wananchi.

Eneo hili la Kisumba lipo katika barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami inayoelekea Matai- Kasanga. Uwepo wa barabara hii itakuwa ni kiunganishi kizuri cha uwanja huo utakaojengwa na Mji wa Sumbawanga na Wilaya mpya ya Kalambo ambapo uwanja huo utakuwa katikati ya Wilaya hizo mbili.

Hata hivyo katika ziara ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alikuta sehemu kubwa ya eneo hilo ikiwa wazi na sehemu ndogo ikiwa imevamiwa na wananchi ambao wamelima na baadhi yao kujenga vijumba vya muda. Mkuu huyo wa Mkoa alitumia fursa hiyo kumuagiza Mkuu wa Kitengo cha Miundombinu Mkoa kupima eneo hilo. Aidha alimuagiza Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisumba Ndugu Nestori Kakwaya ashirikiane na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga katika kuzungumza na wananchi wa eneo hilo wafaham dhima ya Serikali juu ya eneo hilo na kwa wale ambao wameshahodhi maeneo waweze kuayaachia mara moja. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Antonyo Mzurikwao (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisumba Bw. Nestori Kakwaya kuhusu uwanja huo.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Meneja wa Tanroad Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala Msaidizi Kitengo cha Miundombinu, Naibu Meya Manispaa ya Sumbawanga na Afisa Habari Mkoa wa Rukwa walipotembelea eneo hili la Kisumba.

Uwanja Mdogo wa Ndege wa Sumbawanga. Hapo akionekana Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Joyce Mgana akimkaribisha Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Lazaro Nyarandu alipokuja kufungua maonesho ya Sido Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika uwanja wa Nelson Mandela mwishoni mwa mwaka jana.

Tuesday, January 17, 2012

MKUU WA MKOA RUKWA ATEMBELEA MKANDARASI AASLEFF BAM INTERNATIONAL ANAYEJENGA BARABARA YA LAELA-SUMBAWANGA KWA KIWANGO CHA LAMI, ATANGAZA VITA NA WEZI WA MAFUTA NA VIFAA VYA UJENZI VYA MKANDARASI HUYO


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Martin Manyanya akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika kambi ya mkandarasi Aasleff Bam International ya Uholanzi iliyopo Kyanda katika Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga.
Tayari kwa ajili ya kwenda kutembelea eneo la kazi, inabidi kuvaa vifaa maalum ili mtu uweze kuonekana kirahisi pamoja na kofia kwa sababu za kiusalama, kama ilivyo kaulimbiu ya kampuni hiyo kuwa ni "Usalama Kwanza". Mkuu huyo wa Mkoa pamoja na timu yake aliyoongozana nayo ambayo ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala wa Mkoa Msaidizi Idara ya Miundombinu, Afisa Habari Mkoa na Katibu wake walipewa vifaa hivyo kwa ajili ya kwenda "Site" kujionea shughuli za Kampuni hiyo.

Eneo hili ambalo lipo nje kidogo na kambi ya Mkandarasi huyo linatumika kwa ajili ya uchimbaji, upasuaji, na hatimaye utengenezaji wa kokoto kwa ajili ya kuweka lami katika barabara anayojenga mkandarasi huyo. Aasleff Bam International inajenga barabara ya Laela- Sumbawanga (95.31 Km) kwa kiwango cha lami. Barabara ya Tunduma- Laela- Sumbawanga kufikia kiwango cha lami imegawanywa sehem kuu tatu ikiwemo Tunduma- Ikana (63.7 Km), Ikana- Laela (64.2 Km ) na Laela- Sumbawanga (95.31 Km ). 

Msafara wa Mkuu wa Mkoa ukipokea maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa Aasleff Bam kuhusu ujenzi wa barabara unaoendelea. 
Barabara hii inaendelea kujengwa na mpaka sasa kipande hiki cha Laela- Sumbawanga kinachojengwa na Aasleff Bam Internatinal kimeshakamilika kwa takriban aslimia 25% na tayari kuna kilomita 10 za majaribio zimeshawekwa lami. Kandarasi huyo pamoja na wengine waliopo Mkoani Rukwa wanatakiwa kukabidhi barabara zote mwanzoni mwa mwaka 2013.

Kutoka muda uliopangwa Mkandarasi huyu ameomba kuongezewa muda wa miezi minne kutokana na sababu kuu tatu, moja ikiwa ni kuchelewa kufika kwa vifaa vya ujenzi walivyoagiza kutoka nje ya nchi, kucheleweshwa vifaa hivyo bandarini kwani vilichukua muda wa miezi minne, na ukubwa wa kazi iliyopo kuwa chini ya makisio yao hivyo kuchukua muda mwingi wa majadiliano namna ya kukamilisha kazi kubwa kwa gharama za makisio madogo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na wakandarasi wa Kampuni ya Aasleff Bam International ya Uholanzi inayojenga barabara ya Laela - Sumbawanga kwa kiwango cha lami katika Mkoa huo. Mkuu huyo wa Mkoa alilazimika kufanya ziara kujionea hali ya ujenzi inavyoendelea pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa Kampuni hiyo. Kulia ni Mashine aina ya mixer inayochanganya udongo na cement na kunyoosha barabara kabla ya kokoto ngumu na lami kuwekwa. 
 

Injinia Manyanya akishikana mikono na mmoja wa makandarasi wa Aasleff Bam mara baada ya kupewa maelezo juu ya mashine inayoonekana nyuma yao ya kuchanganya udongo na cement. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Antonyo Mzurikwao na Kushoto ni Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa Kabaka Florian Mwombeki.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wazawa wa kampuni ya Aasleff Bam International ya Uholanzi inayojenga barabara ya Laela - Sumbawanga kwa kiwango cha lami. Aliomba kuzungumza na wafanyakazi hao kutokana na kulaumiwa kuiibia kampuni hiyo vifaa ikiwepo mafuta ya diesel zaidi ya lita 30,000, tani 40 za simenti , na nondo zaidi ya tani 300. 

Mkuu huyo wa Mkoa aliwaasa wafanyakazi hao kuwa na moyo wa kizalendo kwa kuona kuwa kazi anayofanya kandarasi huyo italeta manufaa kwao. Alitangaza vita na yeyote yule atakayethibitika kuhusika na wizi katika kampuni hiyo pamoja na kampuni zingine zinazofanya kazi hiyo ya ujenzi Mkoani Rukwa. Alisema kuwa ni aibu kuona wizi wa namna hiyo kwani kazi anayofanya kandarasi huyo ni kwa manufaa ya watanzania wenyewe.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Msafara wake walipata chakula cha mchana katika kambi ya Mkandarasi huyo