Thursday, March 29, 2012

MKOA WA RUKWA WAPANIA KUHAKIKISHA WANAFUNZI WOTE WALIOFAULU NA KUCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA WANAKWENDA SHULE IFIKAPO MWEZI APRILI MWAKA HUU

Miongoni mwa madarasa mawili yaliyojengwa kwa fedha za Serikali katika Shule ya Kilimani katika Manispaa ya Sumbawanga ambayo yamekwama baada ya kukosekana michango ya wananchi ambapo ni sera ya Serikali kushirikisha wananchi katika miradi hiyo ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya, Diwani Kata ya Katandala Mhe. Kisabwite na wajumbe wa Kikundi Kazi kitachowajibika kuhamasisha wananchi katika uchangiaji katika Kata ya Majengo na Katandala. 

Mkoa wa Rukwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo umejipanga kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wanakwenda shule kwa kuanza mapambano makali ya kukabiliana na changamoto zinazosababisha tatizo hilo. Hatua hiyo imekuja kutokana na baadhi ya wanafunzi waliofaulu kushindwa kwenda Shule kutokana na upungufu wa vyumba madarasa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Ndugu William Shimwela, jumla ya wanafunzi 678 kati ya wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu Mkoani Rukwa na kuchaguliwa wameshindwa kujiunga na shule walizopangiwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Hali hiyo imeusukuma Mkoa kuona kuna haja kubwa ya kuunganisha nguvu kati ya Serikali ya Mkoa, Halmashauri, Serikali za Mitaa ili kuhamasisha wananchi kuchangia kuondokana na tatizo hilo ambalo kimsingi limetokana na muamko hafifu wa wananchi kuchangia miradi hiyo.   

Miongoni mwa hatua zailizoanza kuchukuliwa ni pamoja na Mkoa kuunda Vikundi Kazi (Clusters) viwili vilivyojigawia maeneo ya kuhamasisha, kimoja kikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Injinia Stella Manyanya na kingine kikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Salum Mohammed Chima ili kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa miradi hiyo na kuweza kuchangia.

Kazi kubwa ya vikundi kazi hivyo ni kuhamasisha wananchi katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujenzi wa vyumba kadhaa vya madarasa ambavyo vimekwama kwenye baadhi ya Shule katika Manispaa ya Sumbawanga baada ya fedha iliyotolewa na Serikali kukosa nguvu na mchango wa wananchi.

Sera kuu ya Serikali ni kutoa fedha kiasi na kuacha sehemu kidogo ya wananchi kuchangia  katika baadhi ya miradi ili kuongeza uwajibikaji wa miradi hiyo kwa wananchi wenyewe. Zimechaguliwa Kata nne za mfano katika Manispaa ya Sumbawanga ambazo ni Majengo. Katandala, Kizwite na Chanji.

Serikali imetoa jumla ya Shilingi milioni 18 kwa Kata mbili za Majengo na Katandala kujenga madarasa manne katika shule ya Kilimani. Mpaka sasa madarasa hayo yameshindwa kukamilika kwa kukosa michango ya wananchi.

Kila darasa moja linategemewa kuchukua wanafunzi 40, hivyo vinahitajika vyumba vya madarasa 16 kuondoa tatizo hilo katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo vitawatosheleza wanafunzi 678 walioshindwa kwenda shule kutokana na uhaba wa vyumba hivyo.  

OFISI YA MKUU WA MKOA RUKWA INAOMBA WANANCHI WOTE WENYE UCHUNGU NA ELIMU KUUNGA MKONO JUHUDI ZILIZOANZISHWA NA SERIKALI KUCHANGIA ILI ZOEZI LA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA UWEZE KUKAMILIKA KWA WAKATI NA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA WAWEZE KWENDA SHULE MARA MOJA. AIDHA OFISI INAPENDA KUWASHUKURU WALE WOTE AMBAO MPAKA SASA WAMECHANGIA. 

  Bwana Elias Bebwa Mkurugenzi Mtendaji wa Seca Contractors akikabidhi shilingi milioni moja kwa Mkuu wa Mkoa Rukwa Injinia Stella Manyanya Ofisini kwake leo kama mchango wake kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Manispaa ya Sumbawanga ikiwa ni jitihada za Serikali ya Mkoa wa Rukwa katika kuhamasisha wananchi na wadau kuchangia katika sekta ya Elimu. Kulia ni Katibu wa Mkuu huyo wa Mkoa Frank Mateny.

BAADHI YA MATUKIO KATIKA UZINDUZI WA SAFARI ZA ANGA ZA KAMPUNI YA AURIC AIR KUTOKA SUMBAWANGA-MBEYA-DAR ES SALAAM TAREHE 25 MACHI 2012 MJINI SUMBAWANGA

Katibu tawala wa mkoa wa Rukwa, Salum Mohammed Chima akijiandaa kushuka katika ndege ya Auric Air wakitokea Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa safari za anga Sumbawanga-Mbeya-Dar es salaam tarehe 25 Machi 2012 katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya akisalimiana wa viongozi mbalimbali wa Serikali muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa mjini Sumbawanga wakati wa uzinduzi wa safari hizo za anga.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa akiimba nyimbo ya kabila la kifipa sambamba na wanakikundi cha Katandala B cha mjini Sumbawanga muda mfupi baada ya kuzindua safari za anga kutoka Dar es salaam hadi Sumbawanga zinazofanywa na ndege ya Auric Air.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya, akizungumza na wananchi wa mji wa Sumbawanga waliojitokeza katika uzinduzi wa safari za anga, pembeni yake ni walimu wawili waliofaulisha vizuri aliyesimama katika ni Morison Kibona wa shule ya Msingi Jangwani na pembeni yake ni Pius Nzwalil wa Sekondari ya Kantalamba. pia walimu hapo walipata ofa ya kusafiri na ndege hiyo kutoka Sumbawanga hadi Mkoani Mbeya.
Ndege ya Auric Air inayofanya safari kati ya Dar es salaam na Sumbawanga ikiwa imetua katika kiwanja cha ndege cha mjini Sumbawanga muda mfupi kabla uzinduzi rasmi wa safari hizo. (Picha kwa hisani ya pembezonikabisa blog)

Tuesday, March 27, 2012

TIPS ON HOW TO BROWSE IN THIS BLOG EFFECTIVELY (FAHAMU NAMNA YA KUTUMIA BLOGU HII KIUFASAHA)


  1. Katika Blogu hii, hakuna picha au taarifa yeyote inayoondolewa baada ya kuonekana ukurasa wa kwanza, bali inahamia ukurasa wa pili au wa tatu na kuendelea kutokana na wingi wa taarifa zinazowekwa humu.
  2. Ukitaka kuhamia kurasa zingine zilizopita ambazo pengine hukuziona, nenda hadi chini kulia kwako bofya "Older Posts" kuona kurasa za nyuma zilizopita ambazo zimehamia kurasa za ndani. Fanya hivyo tena na tena kuona kurasa zote katika Blogu hii.
  3. Ukitaka kurudi mwanzo nenda chini kabisa, katikati bofya "Home" kurudi ukurasa wa mwanzo wa blogu hii.
  4. Ukitaka kutafuta habari kwa jina la mtu, sehemu au kitu nenda kulia utaona kisanduku juu yake kimeandikwa Tafuta/ Search andika unachikitaka hapo alafu bofya Search subiri kwa muda utaona majibu ya ulichokiandika. Mfano ukitaka kupata habari za mpanda andika"mpanda" alafu bofya search.
  5. Kama umevutiwa na habari, picha au kero na maoni yako unaweza kuandika kwa kubofya sehemu iliyoandikwa "comments" ambayo ipo chini ya kila habari (post) chagua annonymus kama hutaki ujulikane au chagua hizo nyingine kama unataka ufahamike.
Kwa yeyote mwenye maoni, ushauri, habari au picha nzuri za kuelimisha na kuhabarisha jamii unaweza kututumia kupitia tembs2001@gmail.com.

MKUTANO WA KITAIFA WA MWAKA WA WAKURUGENZI WAKUU WA WIZARA NA MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI KITENGO CHA UTAWALA NA RASILIMALI WATU MIKOA WAFUNGULIWA JANA MKOANI RUKWA, WAJUMBE WAANDALIWA HAFLA FUPI YA KUWAKARIBISHAMkuu wa mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya, akifungua mkutano wa mwaka wa wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa Wizara na makatibu tawala wasaidizi Utawala na Rasilimali Watu wa Mikoa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa huo (RDC) jana mjini Sumbawanga. 

Kutoka kushoto ni Bi. Elizabeth Nyangumi Naibu Katibu Mkuu Hazina, George Yambesi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya akifuatilia moja ya mada katikamkutano wa mwaka wa wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu na makatibu tawala wasaidizi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa huo (RDC) leo mjini Sumbawanga.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza kwenye hafla fupi (Cocktail Party) iliyoandaliwa jana usiku na Ofisi yake kwa ajili ya kuwakaribisha wageni waliohudhuria kwenye Mkutano huo. Katika Hafla hiyo vitu mbalimbali viliandaliwa ikiwemo vyakula vya asili ambavyo huzalishwa Mkoani Rukwa kama Maboga, Mihogo, Mahindi Mabichi, na Matunda mbalimbali. Pia walikuwepo Samaki aina ya Migebuka ambao wanapatikana kwa wingi kutoka Ziwa Tanganyika, Mchele (Wali) Mzuri ambao wengine wameubandika jina la Mchele wa Kyella wakati unazalishwa Mkoani hapa pamoja na vinywaji kadha wa kadha. Vilele zilikuwepo Nyama Bora kutoka kiwanda cha SAAFI kinachomilikiwa na Mjasiriamali mzawa na Mbunge Mstaafu Ndugu Chrissant Mzindakaya na Ugali kwa unga unaozalishwa na kiwanda cha Energy Milling cha Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa.

Mkuu huyo wa mkoa aliziomba mamlaka zinazohusika ikiwemo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kupitia Katibu wake Mkuu George Yambesi kusaidia kuhakikisha kuwa ile kasumba iliyokuwepo hapo kabla ya kuleta watumishi walioshindikana Mkoani Rukwa inaondolewa kwa kuleta watumishi wenye sifa kwani Rukwa Mpya ni tofauti na ile ya zamani. "Rukwa sasa inaruka katika kila sekta" alisema Injiniia Manyanya.     


 Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum mohammed Chima akizungumza katika hafla hiyo jana, miongoni mwa mambo ya msingi aliyoyasema jana ni pamoja na changamoto kubwa ya uhaba wa watumishi wenye sifa unaoukabili Mkoa wa Rukwa ambapo aliwaomba wakurugenzi wote wa Utawala na Makatibu Wakuu wakiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi, George Yambesi kuhusu kuona haja ya kuleta watumishi zaidi tena wenye Sifa kuweza kukabiliana na tatizo lililopo hususan katika sekta ya afya.

 Kutoka kushoto ni Hiporatus Matete Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, George Yambesi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Chrissant Mzindakaya na wadau wengine waliokuwepo kwenye hafla hiyo.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akigonganisha Glasi ya Whisky na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Salum Chima viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo jana.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akigonganisha Glasi ya Whisky na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Yambesi katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo jana.
 Zoezi la kugonganisha Glasi kama ishara ya kufurahi pamoja likiendelea.

 Burudani ya Ngoma na Twist nayo ilishika nafasi yake katika kutoa burudani kwenye hafla hiyo. Baadhi ya wageni na wenyeji wakijumuika na kikundi cha Ngoma cha Kanondo kucheza Ngoma kama inavyoonekana pichani.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya, Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Salum Chima na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Kanali John Antonyo Mzurikwao wakijumuika kwenye Twist na baadhi ya Wajumbe waliohudhuria kikao hicho.
 Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakiangalia Ngoma ya Kanondo ikitumbuiza.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kisasa cha Nyama cha SAAFI kilichopo katika Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa akionyesha moja ya bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho. Alisisita kuwa kiwanda chake kinatoa nyama bora ambayo ni "HALAL MEAT" iliyochinjwa kwa Ng'ombe kuelekezwa Kibla.

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Yambesi zawadi kwa niaba ya Ofisi yake kwa wajumbe wote kushiriki kikao hicho Mkoani Rukwa.
 Baadhi ya Wajumbe wa kikao hicho wakipokea nyama maalum zilizohifadhiwa kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa zinazozalishwa na kiwanda cha SAAFI.

 

Sunday, March 25, 2012

AURIC AIR YAZINDUA HUDUMA YA SAFARI ZA NDEGE DAR - SUMBAWANGA LEO JIJINI DAR ES SALAAM

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya akipanda kwenye ndege inayomilikiwa na Kampuni ya Auric Air Services Ltd leo katika uwanja wa ndege wa Mwl. J.K. Nyerere Dar es Salaam kama ishara ya kuzindua rasmi huduma ya safari za anga kutoka Dar es Salaam kwenda Sumbawanga Mkoani Rukwa itakayoendeshwa na Kampuni hiyo, huduma hiyo haikuwepo hapo kabla. Kampuni hiyo itakuwa inaendesha safari zake siku ya Jumatano na Jumapili ambapo gharama za safari hiyo kwenda na kurudi itakuwa Dola za Kimarekani 370$ sawa na takriban Tshs 598,000/= kwenda na kurudi. Wanaoshuhudia ni Katibu Mkuu Utumishi GeorgeYambesi, Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hillal, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Huduma za Ndege ya Auric Air Services Ltd Deepesh Gupta na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Salum Mohammed Chima.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya akimkabidhi Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Huduma za Ndege ya Auric Air Services Ltd Deepesh Gupta zawadi ya Ua na Kadi kama pongezi na shukrani kwa kampuni hiyo kwa kuanzisha huduma ya safari za ndege za abiria kutoka Dar es Salaam-Sumbawanga Mkoani Rukwa kupitia Mbeya leo katika uwanja wa ndege wa Mwl. J.K. Nyerere Dar es Salaam. Kampuni hiyo itakuwa inaendesha safari zake siku ya Jumatano na Jumapili ambapo gharama za safari hiyo kwenda na kurudi itakuwa Dola za Kimarekani 370$ sawa na takriban Tshs 598,000/= kwenda na kurudi. Wanaoshuhudia ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Salum Mohammed Chima, Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hillal na Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi.


Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima akipanda ndege ya Kampuni ya Auric Air ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa huduma hiyo kwa safari ya kuelekea Sumbawanga Mkoani Rukwa leo.

 Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini (CCM) Aeshi Hillal alikuwa sehemu ya abiria 13 waliopanda ndege hiyo leo Jijini Dar es Salaam kuelekea Sumbawanga Mkoani Rukwa katika uzinduzi wa huduma hiyo. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa kwa ushirikiano na Mbunge huyo pamoja na wadau wengine ndiyo matunda ya muwekezaji huyo Mkoani Rukwa. 

 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi George Yambesi ambaye pia ni Mwanarukwa akijibu baadhi ya maswali ya waandishi wa habari na kuelezea furaha yake kwa kuanzishwa safari hizo.
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stella Manyanya akiwa na  Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Huduma za Ndege ya Auric Air Services Ltd Deepesh Gupta (kushoto kwake), Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Salum Mohammed Chima (kushoto), Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hillal (kulia) na Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi muda mfupi kabla ya kuondoka katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam leo kuelekea Sumbawanga Mkoani Rukwa katika sherehe za uzinduzi wa huduma hiyo.
Ndege ya Auric Air itakayoendesha huduma za anga za kampuni hiyo ikiwa katika maandalizi ya safari ya leo kutoka Dar es Salaam kwenda Sumbawanga Mkoani Rukwa.

Thursday, March 22, 2012

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAJI, ILEMBA WAPATA HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA.

Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha akimtwisha ndoo ya maji, Rose Simtowe juzi baada ya kuzindua mradi safi katika kijiji cha Ilemba katika wiki ya maji. habari zaidi soma hapo chini.
VIONGOZI wa vijiji na kata wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, wameshauriwa kutumia sheria ndogo ndogo kudhibiti mazingira zilizitungwa na halmashauri ya wilaya hiyo ili kuwadhibiti baadhi ya watu wanaondesha shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji.

Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha alisema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ilemba , muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa maji katika maadhimisho ya wiki ya maji yaliyofanyika katika kijiji cha Ilemba.

Alisema kuwa kero ya maji ambayo inajitokeza hivi sasa katika maeneo mengi ni kutokana na kukithiri kwa uharibifu wa mazingira, ikiwa ni ukataji miti, uchomaji wa misitu hovyo na baadhi ya watu kulima katika vyanzo vya maji na kusababisha vyanzo hivyo kukaukaharibifu wa mazingira ambapo athari zake ni wananchi kukosa maji kwaajili ya matumizi mbalimbali.

Mbunge huyo alisema kuwa sheria hiyo ikitumika ndi suluhisho la kuepukana ukame ambao unajitokeza sasa katika maeneo mengi ambao ni sehemu ya athari kubwa ya mabadiliko tabia nchi yanayojitokeza katika nchi magharibi.

Kwa upande wake, Kaimu Mhandisi wa maji wa Halmashauri ya wilaya, Habibu Salum alisema kuwa mradi huo umegharimu zaidi ya Sh 27 milioni utasaidia kupunguza kero ya maji katika vijiji vipatavyo saba katika kata ya hiyo inayoelezwa kuwa na vijiji 27.
Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha akifungua bomba ya maji safi katika kijiji cha Ilemba juzi ikiwa ni sehemu ya kuzindua mradi wa maji katika wiki ya maji wilayani Sumbawanga mkoni Rukwa. (Picha kwa hisani ya pembezonikabisa blog)

RAIS KIKWETE ATEUA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA SABA NA KUFANYA UHAMISHO WA WENGINE WATATU TAREHE 21 MACHI 2012

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatano, Machi 21, 2012 ameteua  Makatibu Tawala wa Mikoa saba na kufanya uhamisho wa wengine watatu.
Ifuatayo chini ni taarifa kamili iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue ikitangaza uteuzi huo:-
A:        MAKATIBU TAWALA WA MIKOA
(i)                 Dkt. Faisal Hassan Haji ISSA, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa KILIMANJARO. Kabla ya hapo Dkt. Faisal alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Rasilimali Watu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
(ii)              Bibi Mariam Amri MTUNGUJA, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa MBEYA. Kabla ya hapo Bibi Mtunguja alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
(iii)            Bwana Eliya Mtinangi NTANDU, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa MOROGORO. Kabla ya hapo Bwana Ntandu alikuwa Katibu Tawala Msaidizi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,           Dar es Salaam.
(iv)            Bwana Severine Bimbona Marco KAHITWA, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa GEITA. Kabla ya hapo Bwana Kahitwa alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dodoma.
(v)               Eng. Emmanuel N.M. KALOBELO, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa KATAVI. Kabla ya hapo Eng. Kalobelo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasharui ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi.
(vi)            Bwana Hassan Mpapi BENDEYEKO, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa RUVUMA. Kabla ya hapo Bwana Bendeyeko alikuwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro.
(vii)          Dkt. Anselem Herbert Shauri TARIMO, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa SHINYANGA. Kabla ya hapo Dkt. Tarimo alikuwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma.
Uteuzi huu unaanzia tarehe 21 Machi, 2012. Wataapishwa Ikulu, Jumamosi tarehe 24 Machi, 2012 saa nne asubuhi.
B:        UHAMISHO
(i)                 Bibi Mgeni BARUANI – Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro anahamishiwa Mkoa wa NJOMBE.
(ii)              Bibi Mwamvua A. JILUMBI – Katibu Tawala wa Mkoa wa  Shinyanga anahamishiwa Mkoa wa SIMIYU.
(iii)            Bibi Bertha O. SWAI, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya anahamishiwa Mkoa wa PWANI.
Balozi Ombeni Y. Sefue
     KATIBU MKUU KIONGOZI 
IKULU,
DAR ES SALAM. 
21 Machi, 2012

Wednesday, March 21, 2012

RAIS KIKWETE AAPISHA WAKUU WA MIKOA MIPYA YA KATAVI, NJOMBE, SIMIYU NA GEITA LEO IKULU

Rais Kikwete akimwapisha Dkt Rajab Mtumwa Rutengwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha Kapt Asery Msangi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe katika sherehe zilizofanyika leo asubuhi Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais akimwapisha Kapt. Paschal Kulwa Mabiti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Rais Kikwete akimwapisha Mh Magalula Saidi Magalula kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Tuesday, March 20, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AFUNGA MAFUNZO YA WAJASIRIAMALI WA UFUNDI YALIYOENDESHWA NA SIDO MKOANI RUKWA NA KUKABIDHI ZANA ZA KAZI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiendesha mafunzo kwa vitendo kwa wakati akifunga mafunzo ya siku 15 ya mafundi wadogo kutoka vikundi 55 katika Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa yaliyoandaliwa na SIDO kwa ushirikiano na Shirika Lisilo la Kiserikali la Uingireza liitwalo Tools for Self Reliance kupitia Program ya SIDO ya kusaidia Mafundi wadogo wa Vijijini  (Artisans Support Programme) . Katika mafunzo hayo jumla ya washiriki 55 waliwakilisha vikundi vyao kutoka katika fani mbalimbali kama Useremala, Ushonaji, Viatu, Uhunzi, Bomba, Makanika, Baiskeli, Redi/TV, Pikipiki, Upasuaji Magogo, Uchomeleaji vyuma, Ujenzi n.k.

Miongoni mwa mambo waliojifunza wajasiriamali hao ni kuandaa Mpango Kazi, Mahusiano ya Familia na Biashara, Utunzaji wa Kumbukumbu, Upangaji wa Bei, Uzalishaji na Ununuzi, Urasimishaji Biashara, Masoko, Taratibu za Kuanzisha Vikundi na Faida Zake, Fedha, Utambuzi wa Zana na Kazi Kila Fani, Utunzaji wa Zana na Matengenezo ya tahadhari, Ubora wa Karakana, Usalama Kazini, Uzalishaji wa Bidhaa, Ubunifu wa bidhaa Mpya, Kulinda ubora wa bidhaa na Afya N.K

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya alisema kuwa Mjasiriamali ni yule anayebuni mawazo na kuthubutu kubadilisha mawazo hayo kuwa kitu kinachoonekana chenye faida kwake na jamii kwa ujumla. Aidha aliongeza kuwa Mjasiriamali huyo ni lazima awe na uwezo wa kuunganisha rasilimali mbalimbali katika jamii kwa kutumia ubunifu aliokuwa nao pamoja na kuongezea thamani kile alichokibuni ikiwa ni bidhaa au huduma.
Meneja wa Sido Mkoa wa Rukwa Martin Augustino Chang'a akitoa taarifa ya mafunzo hayo kwa Mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Tarafa ya Matai katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga yaliandaliwa na SIDO katika Programu yake ya kusaidia Mafundi wadogo wa Vijijini (Artisans Support Programme) kwa ushirikiano na Shirika Lisilo la Kiserikali la Uingireza liitwalo Tools for Self Reliance. Kwa ushirikiano na Shirika hilo SIDO ilikadhi vifaa mbalimbali vya ufundi kutoka Uingereza vyenye jumla ya Shilingi Millioni 37.5 za Kitanzania. Katika taarifa yake hiyo Ndugu Chang'a hakusita kutoa shukrani zake za dhati kwa Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Rukwa kwa Ushirikiano wake wa hali na mali katika kusaidia shirika hilo na wajasiriamali kwa ujumla. 
  
Ndugu Oswald Fungavyema ambaye ni Mwenyekiti wa Drasa la Mafunzo hayo akitoa maelezo mafupi kwa Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa juu ya vifaaa mbalimbali vilivyotengezwa na wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo. Vifaa hivyo ni pamoja na Nguo, Viatu, Mpira wa Miguu, Tairi la baiskeli n.k  

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiangalia Mpira wa Miguu uliobuniwa na baadhi ya mafundi wajasiriamali wa maafunzo hayo ya SIDO. Mpira huo umetengenezwa kwa ngozi ya Mbuzi na kushonwa kwa  sindano ya mkono kwa ustadi wa hali ya juu. Kwa mujibu wa Mkuuu hyo wa Mkoa vipaji ni vingi katika nchi yetu na kinachohitajika sasa ni uendelezwaji wa vipaji hivyo viweze kuleta tija kwa wabunifu wenyewe na taifa kwa ujumla. Kulia anayeshuhudia ni Meneja wa SIDO Mkoa wa Rukwa Martin Chang'a.

Huu ndio Mpira wa Miguu (Football) pamoja na viatu vilivyotengenezwa na wajasiriamali hao wa SIDO kwa kutumia ngozi ya Mbuzi.
Wahitimu wote 55 wa mafunzo hayo walipewa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo. Hapo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Ndugu Kenan Mwimanzi ambaye ni fundi Serimala Cheti chake cha kuhitimu mafunzo hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akikabidhi Cherehani kwa Zaituni Matofali ambaye ni miongoni mwa washiriki 55 wa mafunzo hayo ambao walipatiwa vifaa mbalimbali vya ufundi na SIDO kwa ushirikiano na Shirika lisilo la Kiserikali kutoka Uingereza liitwalo Tools for Self Reliance. Wa kwanza kushoto Mtaalamu wa Ufundi wa Mafunzo hayo na wa pili Meneja wa Sido Mkoa wa Rukwa Martin Chang'a.

  Hapo Mkuu wa Mkoa akikabidhi Mashine ya Kuchomelea (Welding Mashine) kwa Charles Msangawale muda mfupi kabla ya kufunga mafunzo hayo. Vifaa mbalimbali vilikabidhiwa kwa wajasiriamali hao vikiwa na thamani ya Shilingi Millioni 37.5 Tshs. Mkuu huyo wa Mkoa alisema vifaa hivyo vikitumika vizuri kwa lengo lililokusudiwa basi vitaongeza Ajira na kipato kwa wajasiriamali hao na wengine watakaonufaika kupitia vifaa hivyo.
Washiriki wakiwa katika chumba cha mafunzo wakisikiliza "Lecture" ya muda mfupi iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati wa kufunga mafunzo hayo

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi Sido mkoa wa Rukwa, sambamba na wajasiliamali wapatao 55 walioshiriki mafunzo ya ujasiliamali katika fani tofauti na kufanyika katika mji wa Matai.