Wednesday, August 29, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AONANA NA UONGOZI WA TBL UNAOTAKA KUWEKEZA KWENYE ZAO LA SHAIRI MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na uongozi wa  Kiwanda cha Bia cha Tanzania (TBL) uliomtembelea ofisini kwake leo ukiwa na lengo la kuwekeza kwenye kilimo cha shairi ambayo ni malighafi muhimu katika kiwanda hicho cha kutengeneza bia nchini. Mkoa wa Rukwa una ardhi yenye rutuba kustawisha mazao mbalimbali ya kilimo ikiwemo mchele, mahindi, maharagwe, ngano, alizeti, mtama, ulezi n.k. Katika kuwekeza kwao wataanza kwa kushirikiana na wakulima wadogowadogo ambao wapo Mkoani Rukwa kwa kuwawezesha zana bora za kilimo hicho pamoja na pembejeo ambapo pia watamiliki mashamba yao wenyewe kwa ajili ya kilimo hicho.
 
Ndugu Gerry Van Den Houten ambaye ni Mkurugenzi wa Usambazaji wa Sabmiller ya South Africa ambayo ina mashirikiano na TBL akielezea lengo na faida za uwekezaji huo ambao licha faida kubwa itakayopatikana pia itatoa ajira kwa vijana wengi Mkoani Rukwa pamoja na kuhamasisha kilimo cha zao hilo. Kulia kwake ni Bennie Basson ambaye ni Menenja wa Shairi wa kiwanda hicho cha bia cha Tanzania (TBL). 
 
Timu ya Uongozi wa TBL ambayo pia ilikuwa imeongozana na baadhi ya wakulima wadogowadogo wa shairi Mkoani Rukwa wakiwa Ofsini kwa Mkuu wa Mkoa huo kwenye mazungumzo juu ya uwekezaji huo.
 

Picha ya Pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, baadhi ya viongozi wa Mkoa na Viongozi wa TBL uliombatana na baadhi ya wakulima wadogowadogo wa shairi Mkoani Rukwa.

TANESCO YAAHIDI KUSAIDIA UPATIKANAJI WA UMEME SOKO LA SAMAKI LA KASANGA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi Uwekezaji wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO Maneno Katyega Ofsini kwake jana alipotembelea Mkoani Rukwa kwa ajili ya kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo alitembelea Soko la Samaki la Kasanga pamoja na kujionea maendeleo ya mradi wa umeme kwenda Wilaya ya Nkasi. 
 
Hakika ziara ya Mkurugenzi huyo Msaidizi imekuwa ya mafanikio makubwa kwani baada ya kutembelea Soko kubwa la Samaki la Kasanga na kujionea umuhimu uliopo wa nishati ya umeme katika kuendesaha soko hilo ameahidi kupitia Shirika lake kuwa soko hilo litapatiwa Jenereta kubwa mbili kila moja ikiwa na uwezo wa 50KV. Alisema kuwa Umeme utakaozalishwa kutokana na Jenereta hizo utaweza pia kuhudumia Vijiji vya jirani vinavyolizunguka Soko hilo.
 
Jitihada za kulipatia Soko hilo umeme zimekuwa zikipewa msukumo mkubwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ambae amekuwa akilifuatilia kwa karibu ambapo amefanikiwa kumpeleka kiongozi huyo wa Tanesco hadi eneo la mradi huo ikiwa ni katika jitihada zake za kutekeleza agizo la Mhe. Makamu wa Rais alipofanya ziara yake Mkoani Rukwa na kutoa agizo kwa uongozi wa Mkoa ushirikiane na Tanesco kuhakikisha Soko hilo linapatiwa umeme.
 
Akiwa Mkoani hapa Kiongozi huyo wa Tanesco alikuta baadhi ya mapungufu katika utekelezaji wa mradi utakaopeleka umeme Wilayani Nkasi ambapo walishauriana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambapo walikubaliana litafutwe suluhu la changamoto hizo badala ya kulaumiana ili kukamilisha mradi huo muhimu kwa Wilaya ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla.
 
Mazungumzo yakiendelea Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Kutoka kulia ni Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Rukwa Emmanuel Kachewa, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a, Mrs. Katyega,  Mkurugenzi Mkuu Msaidizi Uwekezaji wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO Maneno Katyega, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya, Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima na Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Florence Mtepa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi Uwekezaji wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO Maneno Katyega (Kushoto) na Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Rukwa Emmanuel Kachewa walipotembelea Soko la Samaki la Kasanga jana.
 
Soko la Samaki la Kasanga.

Monday, August 27, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA NA FAMILIA YAKE WAHESABIWA KWENYE SENSA YA WATU NA MAKAZIMkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akijibu maswali ya Msimamizi wa Sensa aliyemuwakilisha karani bwana Hamad tarehe 26, Agosti 2012 ambapo amejumuika na wakazi wa Mkoa wa Rukwa katika zoezi hilo linaloendelea nchi nzima.
 
Miongoni mwa wanafamilia wa Mkuuu huyo wa Mkoa wakijibu maswali ya Sensa. Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Wananchi wote kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo ambalo ni muhimu kwa mipango ya Serikali na Maendeleo ya wananchi wote. Alisema yeyote atayekwamisha zoezi hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.

TAARIFA ALIYOITOA MKUU WA RUKWA JUU MAENDELEO YA MAANDALIZI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI MKOANI RUKWA TAREHE 25 AGOSTI 2012

1.0.       UTANGULIZI:
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya watu na makazi nchi nzima ifikapo tarehe 26/8/2012, ambapo maandalizi ya zoezi hili yapo katika hatua mbali mbali, ikiwemo: Kutenga maeneo madogo madogo (EA) ya  kuhesabia watu, mafunzo ngazi ya Taifa (TOT) mafunzo ya ngazi ya Mkoa, mafunzo ngazi ya Tarafa, nyaraka mbali mbali za Sensa pamoja na fedha kwa ajili ya kuendesha zoezi la Sensa.
2.0.       HALI YA MAANDZLIZI KWA  MKOA WA RUKWA
2.1.       Maeneo madogo madogo ya kuhesabia watu (EA)
Jumla ya maeneo madogo madogo 2986 kwa mkoa mzima wa Rukwa yametengwa kwa mchanganuo ufuatao:  Nkasi 855, Manispaa ya Sumbawanga 710, Halmashauri ya Sumbawanga 800 na Kalambo 621.
2.2.       Mafunzo:
Kama sehemu ya maandalizi ya Sensa mkoa umeendesha mafunzo ngazi ya mkoa kuanzia tarehe 17/07/2012 hadi tarehe 28/07/2012, ambapo waliofunzwa ngazi hii ya mkoa  walikwenda kuwafunza wasimamizi na makarani ngazi ya tarafa, mafunzo haya yalihusisha makundi yafuatayo:
1.                  Maafisa Elimu Kata zote 64 za  mkoa wa Rukwa
2.                  Maafisa maendeleo ya jamii, Halmashauri zote
3.                  Maafisa Afya toka kila Halmashauri
4.                  Maafisa ardhi toka  kila Halmashauri
5.                  Maafisa Kilimo toka kila Halmashauri
6.                  Maafisa Elimu toka kila Halmashauri
7.                  Maafisa toka Wizara ya Mambo ya ndani
8.                  Maafisa toka Ofsi ya Mkuu wa Mkoa
9.                  Wawakilishi wa walemavu.
Baada ya kukamilika mafunzo  ngazi ya Mkoa yalifuatia mafunzo mengine ngazi ya Tarafa kuanzia tarehe 09/8/2012 hadi 19/8/2012 ,ambapo katika ngazi hii makarani na  wasimamizi wa Sensa waliweza  kufunzwa  namna ya kwenda kukusanya taarifa hizi za sensa kwenye maeneo yaliyopangiwa.  Makarani/wasimamizi walipatikana kupitia taratibu zote  zilizoelekezwa na Serikali, ambapo walimu na watu wengine  wasio walimu waliweza kupata nafasi za kuwa  makarani wa Sensa.
3.0.       VIFAA NA NYARAKA ZINGINE ZA SENSA
Vifaa na nyaraka zingine za Sensa toka Kituo cha Vifaa kilichopoo Kibaha – Pwani zililetwa mikoani kwetu japo baadhi ya vifaa vililetwa kwa kuchelewa katika hatua ya mafunzo. 
4.0.       FEDHA:
Fedha kwa ajili ya mafunzo ngazi zote mbili (2) Mkoa na Wilaya/Tarafa pamoja na mafunzo ya  madiwani zililetwa kupitia Hazina ndogo Rukwa na kuzigawa kwenye Halmashauri husika kwa kuzingatia mgawanyo wa bajeti.
5.0  IDADI YA MAKARANI NA WASIMAMIZI WA SENSA - RUKWA:
 
WILAYA
MAKARANI
WASIMAMIZI
JUMLA
Manisspaa SBA
986
86
1,072
Sumbawanga
1030
95
1,125
Kalambo
804
80
884
Nkasi
1109
100
1209
3929
361
4290
 
6.0 CHANGAMOTO:
Katika hatua zote mbili za mafunzo (Mkoa na Tarafa) kumejitokeza  changamoto kadhaa kama ifuatavyo:-
1.                  Kuchelewa kupata fedha za kujikimu na mambo mengine siku za  mwanzo za mafunzo katika hatua zote mbili za (Mkoa na Tarafa)
2.                  Baadhi ya vifaa vya mafunzo kuchelewa kuletwa mkoani ikiwemo Ramani  na bags za kutunzia vifaa na nyaraka zingine.
3.                  Upungufu wa  vyumba vya kulala  (ngazi ya Tarafa) na hivyo wengine kulazimika kulala madarasani
4.                  Kutopata maeneo ya kuaminika (usalama wa chakula) kwenye baadhi ya maeneo/vituo vya mafunzo ngazi ya tarafa.
5.                  Upungufu wa madawati kwenye baadhi ya vituo  vya kufundishia (ngazi ya Tarafa).
6.                  Halmashauri zetu kutokuwa na fedha za kutosha kukabiliana  na maagizo  toka HQ Dar es Salaam ya kugharamia/kuwapa  fedha za kuendesha zoezi la Sensa.
7.                  Uhaba wa magari mkoani/wilayani.
8.                  Baadhi ya vifaa kutoletwa kabisa (refrectors, t-shirts  n.k.)
9.                  Baadhi ya watu/vikundi vya watu kuhamasisha watu wasihesabiwe, hata hivyo, jitihada za makusudi zinaendelea kuchuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa ki-dini na wadau wengine  wa serikali kudhibiti/kupunguza hali hiyo.
Hali ilivyo hadi sasa:
Mkoa upo tayari kufanya Sensa ya watu na makazi kwani maandalizi yote muhimu yamekwishakamilika, ikiwemo fedha, na nyaraka mbalimbali za sensa. Aidha vifaa vyote muhimu kama vile vikokotozi (calculators, vitambulisho, begi maalum (special bags) vimeshapatikana toka jana terehe 24/08/2012 usiku,   isipokuwa “unirform” yaani T-shirts na Recfectors. Hata hivyo kwa kuwa vitambulisho vipo upungufu huo hautaathiri zoezi hili.
 7.0 HITIMISHO
Ofisi ya mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa inapenda kuwashukuru Wadau wote kwa hatua za awali za zoezi la sensa katika uhamasishaji na elimu wakiwemo Katibu Tawala wa mkoa, waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wote, Viongozi wa Halmashauri zote, vyombo vya Ulinzi na Usalama, Mashehe na Maaskofu na Wachungaji, Watumishi, wanasiasa, Waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa pamoja na  Wananchi wote kwa ujumla. Napenda kusisitiza kuwa watu wote wajitokeze kuhesabiwa hapo kesho tarehe 26/8/2012, kwani sensa ni kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Mkoa wa Rukwa umejipanga kuhakikisha kunakuwa na hali ya amani na utulivu kwa kipindi chote cha zoezi hili, hivyo unawaonya wale wote wenye nia ya kuvuruga zoezi hili, kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa”
Eng. Stella Martin Manyanya (MB)
MKUU WA MKOA WA RUKWA

Wednesday, August 22, 2012

CCM KUKATA RUFAA DHIDI YA HUKUMU YA KESI YA UCHAGUZI IGUNGA

NA FULL SHANGWE BLOG
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakikuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, dhidi ya Mbunge wa jimbo la Igunga, Peter Dalally Kafumu.Taarifa iliyolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye mchana leo, imeseme kufuatia kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Mary Shangali, kitakata rufani.

“Chama Cha Mapinduzi kimetafakari hukumu ya kesi ya uchaguzi iliyotolewa jana Agosti 21, 2012 na Mahakama Kuu kanda ya Tabora. Kimejiridhisha na kufanya uamuzi wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kesi ya uchaguzi, dhidi ya Mbunge wa jimbo la Igunga mkoani Tabora Dokta Dalaly Peter Kafumu.Kusudio hilo linatokana na kutorishwa na hukumu hiyo”. imesema taarifa hiyo.

Jana Jaji Mary Shangali katika hukumu yake, alisema ametengua ushindi wa Dk. Kafumu baada ya kurishishwa na madai saba kati ya 17 yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo na Mlalamilikaji, aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chadema, Joseph Kashindye.

Dk. Kafumu wa CCM alitangazwa kushinda kiti na Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga, katika uchaguzi mdogo uliofanyika, Septemba mwaka jana, baada ya kujiuzulu aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Rostam Aziz.

MHE. RAIS KIKWETE AKAGUA GHALA LAKE LA MAHINDI KIJIJINI KWAKE MSOGA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiwa na mjukuu wao Aziza Ridhiwani (3) katika ghala ya mahindi yaliyovunwa kwenye shamba lao kijijini Msoga, nje kidogo ya mji mdogo wa Chalinze, Mkoa wa Pwani. Rais Kikwete ni mkulima na mfugaji kijijini hapo na ameonesha kufurahishwa sana na mavuno makubwa ya mahindi shambani kwake. Hii katika kutekeleza kwa vitendo sera ya Serikali ya kuendeleza kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya sekta ya kilimo katika Tanzania.
PICHA NA IKULU

Saturday, August 18, 2012

MKUU WA MKOA WA RUKWA AONANA NA BALOZI WA KENYA NCHINI OFSINI KWAKE LEO, ATEMBELEA MAJERUHI ZAIDI YA 30 WALIONUSURIKA KWENYE AJALI YA FUSO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso ofsini kwake leo alipotembelewa na balozi huyo ambaye yupo Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha uhusiano kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kuangalia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Mikoa ya nyanda za juu kusini. Balozi huyo anategemea kwenda Mkoa jirani wa Katavi ambapo pamoja na shughuli nyingine ataembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi. Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa amemuhakikishia balozi huyo uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji Mkoani Rukwa ikiwemo Kilimo, Utalii, Uvuvi, Elimu na Biashara. Alimueleza kuwa kazi kubwa inayoendelea hivi sasa ni utengaji maeneo maalum ya uwekezaji.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mutinda Mutiso akielezea lengo la ujio wake Mkoani Rukwa mbele ya Mkuu wa Mkoa huo na viongozi wengine wa Serikali ya Mkoa mapema leo ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo. Aliiomba pia Serikali ya Tanzania kujenga urafiki na wageni ili kuimarisha mahusiano mazuri amabayo yamekwishajengeka kati ya nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya. Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alimsihi balozi huyo na nchi yake ya Kenya kusaidiana na Tanzania kudumisha amani iliyopo ili Afrika ya Mashariki pawe pahala salama pa kuishi na kufanya maendeleo ikiwemo uwekezaji ambao hauwezi kustawi pasipokuwa na amani.

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima hapo kabla akimtambulisha balozi wa Kenya kwa viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Rukwa Ofsini kwake alipoenda kumsalimia kabla ya kuonana na Mkuu wa Mkoa huo.

Mazungumzo yakiendelea ofsini kwa Mkuu wa Mkoa.

Kutoka kulia ni Afisa Mkuu wa Jeshi la Usalama Barabarani Mkoani Rukwa, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Samson Mashalla, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa (RPC) Jakob Maruanda na Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Francis Kilawe wakiwa kwenye meza ya mazungumzo na Balozi huyo wa Kenya.

Majadiliano yakiwa yanaendelea kwenye meza ya mazungumzo.

Mmoja wa majeruhi wa ajali ya Fuso iliyotokea Wilayani Nkansi jana Mkoani Rukwa akiwa amelazwa katika Hospitali kuu ya Mkoa wa huo huku akiendelea kupatiwa matibabu. Watu saba walifariki papo hapo katika ajali hiyo iliyohusisha Fuso iliyokuwa imebeba mizigo na abiria ambapo majeruhi walikuwa 37, Mpaka sasa jumla ya abiria waliofariki ni 10 na wengine bado wapo hospitalini hapo wakiendelea kupata matibabu na wengine walisharuhusiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimpa pole mmoja wa majeruhi walionusurika kwenye ajali hiyo mbaya kati ya ajali zilizowahi kutokea Mkoani Rukwa. Mkuu huyo wa Mkoa alisikitishwa na ajali hiyo iliyomfanya apige marufuku ujazaji wa abiria kupita kiasi kwenye magari ya mizigo.

Agnes ni mmoja wa majeruhi walionusurika katika ajali hiyo akiwa na watoto wake wawili wadogo wanaonekana pichani na mumewe ambaye alisharuhusiwa baada ya kupata nafuu.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika akitoa maelezo ya majeruhi kwa Mkuu wa Mkoa huo alipotembelea kuwaona kufuatia ajali mbaya iliyotokea jana na kusababisha vifo vya watu 10 na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akitoa agizo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa huo Jakob Maruanda mbele ya waandishi wa habari na viongozi wengine wa Mkoa huo akiwemo Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima, agizo ambalo limepiga marufuku ujazaji wa abiria kupita kiasi kwenye magari ya mizigo. Alimueleza kuwa yeyote atakayekutwa amejaza abiria na mizigo kupita kiasi kwenye malori ya mizigo achukuliwe hatua kali za kisheria kudhibiti ajali za namna hiyo kutokea.

RAIS KIKWETE AKUTANA NA RAIS WA MALAWI JOYCE BANDA MJINI MAPUTO NCHINI MSUMBIJI KUZUNGUMZIA SULUHU YA MPAKA WA NCHI HIZO MBILI

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Malawi Mhe.Joyce Banda mjini Maputo Msumbiji walipokutana leo asubuhi kuzungumzia kutafuta suluhu katika mgogoro wa mpaka kati nchi hizo uliopo kwenye ziwa Nyasa.Wakati wa mazungumzo hayo Marais hao wawili wameelezea nia ya nchi zao kufikia suluhu kwa njia za kidiplomasia kupititia kamati maalumu iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo.
 
Rais wa Malawi Mhe.Joyce Banda akisalimiana na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete mapema leo asubuhi mjini Maputo Msumbiji,walipokutana kuzungumzia kutafuta suluhu katika mgogoro wa mpaka kati nchi hizo uliopo kwenye ziwa Nyasa.Wakati wa mazungumzo hayo Marais hao wawili wameelezea nia ya nchi zao kufikia suluhu kwa njia za kidiplomasia kupititia kamati maalumu iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo.
 
Marais wakizungumza kwa furaha kabisa.
 
Rais Dkt.Jakaya Kikwete akifafanua jambo mbele ya Wanahabari mapema leo asubuhi mjini Msumbiji,ambapo Rais Kikwete amekutana na Rais wa Malawi Mhe.Joyce Banda kuzungumzia kutafuta suluhu katika mgogoro wa mpaka kati nchi hizo uliopo kwenye ziwa Nyasa.Wakati wa mazungumzo hayo Marais hao wawili wameelezea nia ya nchi zao kufikia suluhu kwa njia za kidiplomasia kupititia kamati maalumu iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo.
 
Rais wa Malawi Mhe.Joyce Banda(Kulia) akiteta jambo na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete mapema leo asubuhi mjini Maputo Msumbiji,wa kwanza kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe.Picha na Freddy Maro-IKULU

Wednesday, August 15, 2012

UJENZI WA BARABARA ZA LAMI TUNDUMA-SUMBAWANGA, SUMBAWANGA-MATAI, NA SUMBAWANGA-NKANSI-KATAVI WAENDELEA NA KUTOA MATUMAINI MAPYA YA MAENDELEO KWA WAKAZI WA MIKOA HII

Moja ya barabara kutoka Laela-Sumbawanga inayoendelea kufunikwa kwa lami.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya AasleffBam International inayojenga barabara ya Laela-Sumbawanga wakiwa wanavuta pumzi wakati wakifanya kazi ya kuweka lami katika barabara hiyo.

Ujenzi ukiendelea katika moja ya daraja kwenye barabara hizo