Tuesday, March 12, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA AONANA NA UMOJA WA WAFUGAJI WILAYANI NKASI, AWATAKA KUZINGATIA ELIMU NA UFUGAJI WA KISASA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na umoja wa makundi ya wafugaji wa Wilayani Nkasi tarehe 10.03.2013 waliounda umoja wao kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo Iddi Kimanta kwa lengo la kuboresha maisha ya wafugaji na ufugaji Wilayani humo na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla. Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wafugaji hao kutambuana ili kurasimisha kazi yao pamoja na kuirahisishia Serikali katika kudhibiti uhamiaji holela wa mifugo Mkoani Rukwa. Aliwataka pia kusomesha watoto wao badala ya kuwatumia katika shughuli zao za uchungaji wa mifugo kama ilivyo hivi sasa.
 
Mwenyekiti wa umoja huo akizungumzia mikakati waliyojiwekea katika kuimarisha ufugaji wa kisasa wenye tija na masoko ya uhakika Wilayani Nkasi.  Umoja huo utakuwa na lengo kusaidia kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kuelimishana na kuwekeana mikakati juu ya ufugaji wa ng'ombe wachache wenye tija, malisho bora, masoko, madawa na majosho, kudhibiti wafugaji wengine wasiotii sheria na kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha na kuendeleza ufugaji wa kisasa nchini.
 
Baadhi ya wafugaji wakiwa kwenye Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Community Centre Mjini Namanyere tarehe 10.03.2013. Jumla ya wafugaji 150 walitegemewa kushiriki katika kikao hicho. Hata hivyo idadi hiyo haikutimia.
 
Baadhi ya wa wafugaji na viongozi wa Wilaya ya Nkasi walioshiriki kikao hicho.
 
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema nia ya Serikali yake ni kushirikiana na umoja huo kuhakikisha Wilaya yake inajiimarisha zaidi katika ufugaji wa kisasa na kuendeleza umoja huo ambao una mipango ya kujenga ofisi kubwa na shule ya bweni kwa ajili ya watoto wa wafugaji. Hakusita kuweka wazi kuwa  Serikali yake ya Wilaya haitowavumilia wafugaji waliovamia maeneo ya hifadhi (Game Reserves) na kwamba wanatakiwa waondoke mara moja kabla Serikali haijaanza msako wa kuwaondoa ambao unategemewa kuanza muda sio mrefu.
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Ali Kessi akizungumza ambapo alisistizia kuhusu ufugaji wa kisasa wa kupunguza mifugo kwa kufuga mifugo wachache wenye tija pamoja na kupambana na wahamiaji haramu wa mifugo.
 
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini Deosderius Mipata akizungumza katika kikao hicho ambapo alisemea uhifadhi wa mazingira ikiwepo utunzaji wa hifadhi ya akiba ya Lwafi Game Reserve ambayo imeshaanza kuvamiwa na wakulima na wafugaji.
 
Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kwela na Mwanasiasa nguli nchini Ndugu Chrissant Majiyatanga Mzindakaya akishukuru kwa niaba ya wafugaji wenzake wa Wilaya ya Nkasi katika kikao hicho. Ndugu Mzindakaya ambaye pia ni Mmiliki wa kiwanda kikubwa cha nyama Afrika ya Mashariki alielezea fursa kubwa ya masoko ambayo ipo kwa ajili ya wafugaji hao na kusisiktiza juu ya ufugaji bora kufaidi soko hilo. 

Bwana Amidi Baraka Magasha Mfugaji wa Kitalu namba 55/15 Kalambo Ranch akiwasilisha hoja yake katika kikao hicho ambapo aliiomba Serikali kushirikiana kwa karibu na wafugaji kwa ustawi wa sekta hiyo, Aliiomba Serikali na wafugaji wenzake kuweka kipaombele kwenye uhifadhi wa mazingira hususani moto.

Monday, March 11, 2013

ZIARA YA MKUU WA MKOA WA RUKWA WILAYANI NKASI PAMOJA NA SHEREHE ZA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Godfrey Mwanansao Afisa Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi akitoa maelezo ya ubunifu wa kinyago kinachoonyesha baadhi ya michezo kwa kinamama kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akikagua mabanda ya wadau wa siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa Wilayani Nkasi tarehe 08.03.2013. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Iddi Kimanta.
 
Meneja wa PSI Mkoani Rukwa Issa Ismail akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya juu kazi za shirika hilo Mkoani Rukwa na katika maonyesho hayo. Kulia kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta, Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Ramadhan Juma, Mbunge wa Nkasi Kaskazini CCM Ali Kesi na Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa Jakob Mwaruanda.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Samson Mashalla akijionea baadhi ya bidhaa zilizokuwa zikionyeshwa na kuuzwa katika mabanda hayo.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na wananchi katika viwanja vya sabasaba Mjini Namanyere katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwishoni mwa juma.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na wananchi Wilayani Nkasi katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yaliyofanyika Wilayani humo kimkoa tarehe 08.03.2013. Aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kujikwamua kiuchumi kwa kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali na kujiunga kwenye vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo, aliwataka pia kuzingatia uzazi wa mpango katika kujiletea maendeleo yao wenyewe.
 
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nkasi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kimkoa katika Wilayani humo.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na wananchi wa Kata ya Wampembe kujibu kero zao alipotembelea kata hiyo tarehe 09.03.2013. Moja ya kero kubwa za wananchi wa kata hiyo wapatao alfu kumi na tisa (19,000) ni ukosefu wa huduma muhimu ya mawasiliano ya simu za aina zote, umeme, barabara, na Zahanati katika vijiji viwili vya kata hiyo.
 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akiangalia daraja la muda lililoharibika katika kijiji cha Ng'unde Kata ya Wampembe Wilayani Nkasi tarehe 10.03.2013 alipotembelea Kata hiyo kuzungumza na wananchi kujua kero zao. Alimuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Nkasi kwa kushirikiana na wananchi kujenga daraja hilo katika kiwango kinachostahiki.  

Tuesday, March 5, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA AKAGUA MIRADI YA USIMAMIZI WA ZIWA TANGANYIKA (PRODAP) KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akiwa na msafara wake wakikagua ujenzi unaoendelea wa daharia (bweni) katika shule ya sekondari Kasanga. Mradi huo ni sehemu ya miradi inayofadhiliwa na mradi wa usimazi wa ziwa Tanganyika uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pamoja na miradi mingine ya ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Muzi na ujenzi wa wadi ya kujifungulia kinamama kijiji cha Samazi. Miradi yote hiyo itawanufaisha wakazi wa mwambao wa ziwa Tanganyika na inagharimu zaidi ya shilingi milioni 150.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Samazi mwambao na ziwa Tanganika alipofika kukagua ujenzi wa wadi ya kujifungulia kinamama katika kijiji hicho. Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuwafuatilia kwa karibu wahandisi wanaojenga miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati. Aliwaasa pia wananchi kuzingatia uzazi wa mpango katika kuboresha maisha yao pamoja na kuwaendelezea watoto wao kielimu tofauti na hali ilivyo hivi sasa ambapo muamko wa elimu Mkoani Rukwa upo chini. Aliwataka pia kuboresha hali ya ulinzi katika maeneo yao ya mipakani kwa kutokuwakaribisha wageni bila kuwa na taarifa zao za kutosha.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na msafara wake wakikagua ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya Msingi Muzi yaliyowekwa jiwe la msingi na Naibu Waziri wa TAMISEMI Aggrey Mwanri ambayo mpaka kukamilika kwake yatagharimu zaidi ya shilingi Milioni 50. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Muzi iliyopo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika Mkoani Rukwa baada ya kukagua ujenzi unaoendelea wa madara yanayofadhiliwa na mradi wa usimamizi wa ziwa Tanganyika mradi ambao upo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira. Aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wale watakaofaulu vizuri na kukosa uwezo wa kujiendeleza.
 
Sehemu ya fukwe ya Ziwa Tanganyika katika kijiji cha Samazi Mkoani Rukwa ambapo mradi wa usimamizi wa ziwa Tanganyika unatekeleza mradi wa ujenzi wa wadi ya kinamama kwa ajili ya kujifungulia katika Zahanati ya kijiji hicho.