Wednesday, July 31, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA AZINDUA UZIO ULIOJENGWA KWA FEDHA ZA WAHISANI KUTOKA MAREKANI KATIKA KITUO CHA WATOTO YATIMA CHA ST. MARTIN DE PORES KATANDALA MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizindua rasmi uzio wa ukuta katika kituo cha kulelea watoto yatima St. Martin De Pores Katandala Mkoani Rukwa leo. Uzio huo ambao ni msaada wa wahisani kutoka Marekani pamoja na upanuzi wa jiko, nyumba ya kufulia nguo (Laundry), ununuzi wa mashine za kufulia nguo za watoto na ujenzi wa nyumba ya ng'ombe umegharimu fedha za kitanzania  shilingi milioni 190. Kushoto ni Baba Askofu Kiharuzi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga.
 
Baba Askofu Kiharuzi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga katikati akibariki tukio hilo. Geti linaloonekana ni sehem ya uzio wa huo uliojengwa kwa fedha za wahisani kutoka Marekani. Katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliendesha harambee fupi ya kuchangia kituo hicho ambapo jumla ya Tsh. 835, 000/ zilipatikana.  


  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akikabidhi zawadi ya batiki kwa Mama Ann Marie English pamoja na wahisani wengine sita kutoka Marekani ambao ni mmoja kati ya wahisani waliofadhili miradi hiyo mbalimbali katika kituo hicho cha St. Martin De Pores.  
 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akikabidhi Hati ya Pongezi kwa Mama Ann Marie English pamoja na wahisani wengine sita kutoka Marekani ambao ni mmoja kati ya wahisani waliofadhili miradi hiyo mbalimbali katika kituo hicho cha St. Martin De Pores.
 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akikabidhi zawadi ya nembo ya bendera ya Taifa kwa Mwenyekiti wa jumuiya ya St. Martin Kids ya Marekani Mama Marry Lynne Cassleman na wahisani wengine sita kama kumbukumbu kwako kwa kufika Mkoani Rukwa.
 
Mwenyekiti wa jumuiya ya St. Martin Kids ya Marekani Mama Marry Lynne Cassleman akizungumza katika hafla hiyo.
 
Ndugu Michael Caraway ambaye ni mmoja ya wahisani hao kutoka Marekani akizungumza katika hafla hiyo. Kulia anaeonekana kichwa kwa nyuma ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya.
 
 Ndugu Michael Caraway kulia aliomba kupiga picha ya kumbukumbu na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
 
Picha ya pamoja

Friday, July 26, 2013

PICHA ZA MATUKIO YA RAIS KIKWETE AKIWA ZIARANI MULEBA

Rais Kikwete akivikwa skafu na skauti baada ya kuwasili Muleba.


Vikundi vya ngoma vikitumbuiza wageni
 

Mwananchi mwingine akitwishwa maji


Ngoma ya utamaduni ikimlaki Rais Kikwete alipowasili katika mkutano wa hadhara
 

Rais Kikwete akisalimia wananchi


Rais Kikwete akijiunga na waumini wa Muleba kusali swala ya Magharibi kabla ya kufuturu


Dua ikiombwa baada ya futari
Kwa matukio zaidi BOFYA HAPA 

UKIWA ZIARANI MKOANI RUKWA MWENGE WA UHURU ULIMULIKA MIRADI MBALIMBALI YA MAENDELEO YENYE THAMANI ZAIDI YA TSH. BIL 1.3 WILAYANI KALAMBO

afya matai
Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2013 Juma Ali Simai akizindua nyumba ya mganga katika kituo cha afya cha Matai wilaya ya Kalambo wakati mwenge wa uhuru ukiwa ziarani Mkoani Rukwa hivi karibuni. Kwa ujumla mwenge wa Uhuru ulitembelea miradi 23 ya maendeleo na miradi 28 ya vikundi Mkoani Rukwa vyenye thamani ya fedha za kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 3.4 ikiwa ni mchango wa Serikali kuu, Halmashauri, Wananchi na Wadau wengine wa maendeleo. 
 
bodaboda
Mwenge wa Uhuru pia uliwamulika vijana wa kikundi cha usafirishaji abiria kwa kutumia pikipiki maarufu bodaboda cha mjini Matai makao makuu ya wilaya ya Kalambo kwa kiongozi wa mwenge kuwakabidhi zawadi mbalimbali ikiwepo "reflactors" na fedha za kutunisha mfuko wao kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Kalambo.
 
hati za kimila
Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2013 Juma Ali Simai akimkabidhi hati ya kimila ya kumiliki ardhi mmoja wa wakazi takribani 179 wa kijiji cha Katuka wilaya ya Kalambo hivi karibuni mwenge wa uhuru ulipokuwa ziarani Mkoani Rukwa. Katikati ni Mkuu wa Wilaya hiyo Moshi Chang'a.
 
mzinga
Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2013 Juma Ali Simai akitundika mzinga katika mradi wa ufugaji nyuki kwenye msitu wa kiijiji cha Katuka wilaya ya Kalambo hivi karibuni mwenge wa uhuru ulipokuwa ziarani Mkoani Rukwa.
 
…………………………………………………….
NA RAMADHANI JUMA
AFISA HABARI KALAMBO
Halmashauri ya wilaya Kalambo mkoa wa Rukwa imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.9 katika miradi 13 ya maendeleo iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu uliomaliza mbio zake Mkoani Rukwa hivi karibuni.
Baadhi ya miradi hiyo inajumuisha matengenezo ya barabara ya Kaluko-Ngoma-Kamawe yenye urefu wa kilometa 12, mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika kijiji cha Singiwe, ujenzi wa nyumba ya mganga katika kituo cha Afya cha Matai, ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari ya Kanyele iliyopo kata ya Sopa.
Vilevile, miradi hiyo inajumuisha vikundi vya wajasiriamali, ikiwemo kikundi cha vijana wapanda pikipiki maarufu kama bodaboda katika kijiji cha Santamaria mjini Matai, na kikundi cha vijana mafundi seremala wa Tuinuane pia cha mjini Matai.

Tuesday, July 23, 2013

MWENGE WA UHURU WAMALIZA ZIARA YAKE MKOANI RUKWA, WAPAA ANGANI KWA NDEGE KUENDELEZA MBIO ZAKE MKOANI TABORA

Mwenge huo wa Uhuru umetembelea miradi 23 ya maendeleo na miradi 28 ya vikundi Mkoani Rukwa vyenye thamani ya fedha za kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 3.4 ikiwa ni mchango wa Serikali kuu, Halmashauri, Wananchi na Wadau wengine wa maendeleo.
 
Ndege ndogo ya Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) ikipaa angani katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga leo tarehe 23 Julai 2013 ikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya, wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa sita pamoja na Mwenge wa Uhuru utakaoenda kukabidhiwa Mkoani Tabora na Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa. Wakimbiza mwenge hao ni Ndugu Juma Ali Simai (Kiongozi), Zamda A. John, Christopher Emmanuel, Seperatus Lubinga, Zuwena Abdallah na Mgeni S. Mgeni.
 
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya Mwenge wa Uhuru mara baada ya kukamilisha ratiba yake katika Wilaya hiyo na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla. Mkuu huyo wa Mkoa atasafiri kwa ndege kuukabidhi Mwenge huo Mkoani Tabora.
 
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akitoa hotuba ya kuwaaga wakimbiza mwenge kitaifa na Mwenge wa Uhuru muda mfupi kabla ya kusafiri na Mwenge huo kwa ajili ya kuukabidhi Mkoani Tabora mapema leo tarehe 23 Julai 2013. Katika hotuba yake hiyo aliwapongeza wakimbiza Mwenge wote na wananchi Mkoani Rukwa kwa kufanikisha zoezi hilo kikamilifu na kuwapa vyeti vya pongezi wakimbiza Mwenge hao wa kitaifa.
 
 Picha ya pamoja kati ya kikundi cha matarumbeta kilichokuwa mstari wa mbele katika kutumbuiza kwenye ziara ya Mwenge Mkoani Rukwa na baadhi ya wakimbiza Mwenge kitaifa na mratibu wa Mwenge Mkoa wa Rukwa Ndugu Abubakari Serungwe wa kwanza kulia (mbele).
 
 Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Ndugu Juma Ali Simai akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga katika Stendi kuu ya mabasi Mjini Sumbawanga tarehe 22 Julai 2013. Kulia ni Diwani wa kata ya katandala Ndugu Kisabwite na Mbunge Jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hillal.
 
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Hassan Kmanta akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a Mwenge wa Uhuru mara baada ya kumaliza mbio zake Wilayani humo tarehe 20 Julai 2013.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo machachari katika mbio za mwenge wa Uhuru Moshi Chang'a akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka Mwenge wa Uhuru mara baada ya kumaliza mbio zake Wilayani Kalambo tarehe 21 Julai 2013.
 
 Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methwew Sedoyyeka akipokea mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a tarehe 21 Julai 2013 na kuahidi kuukimbiza katika wilaya yake kwa amani, nguvu na uadilifu mkubwa.
 
 Baadhi ya raia wa kigeni nao waliomba kupiga picha na Mwenge wetu wa Uhuru.

Wananchi na wanafunzi walihamasika vya kutosha na Mwenge wa Uhuru kiasi cha wengine kupanda juu ya miti ili waweze kupata taswira yake mwanana.
 
 Wanafunzi na wananchi wakiwa juu ya miti kushuhudia Mwenge wa Uhuru na ujumbe wake.
 
  Kwa wengine kuuona Mwenge wa Uhuru vizuri haikuwa kazi rahisi walilazimika hata kuhatarisha maisha yao.
 
 Picha ya pamoja kati ya mratibu wa Mwenge Mkoani Rukwa ndugu Abubakar Serungwe na baadhi ya wakimbiza mwenge kitaifa pamoja na katibu wa CCM Sumbawanga Mjini Mama Silaf Maufi.

Friday, July 19, 2013

MWENGE WA UHURU WALAKIWA KWA SHANGWE MKOANI RUKWA UKITOKEA MKOA WA KATAVI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya na viongozi wengine pamoja na watumishi wa serikali ya Mkoa huo wakishangilia mapokezi ya mwenge wa uhuru uliowasili Mkoani Rukwa mapema leo tarehe 19 Julai 2013, ukitokea Mkoani Katavi.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima na viongozi wengine pamoja na watumishi wa serikali ya Mkoa huo wakishangilia mapokezi ya mwenge wa uhuru uliowasili Mkoani Rukwa mapema leo tarehe 19 Julai 2013, ukitokea Mkoani Katavi.
 
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Rajab Mtumwa Rutengwe akimkabidhi mwenge wa uhuru Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya mapema leo tarehe 19 Julai 2013, baada ya mwenge huo kumaliza ziara yake Mkoani Katavi na kuanza ziara ya siku nne Mkoani Rukwa.
 
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Ndugu Juma Ali Simai akizindua mradi wa maji katika kijiji cha Challa B leo tarehe 19 Julai 2013. Mwenge wa Uhuru umeanza ziara yake ya siku nne Mkoani Rukwa kwa kuanzia na Wilaya ya Nkasi na kuendelea Kalambo na Sumbawanga.
 
Baadhi ya watumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa wakifurahia mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.

Thursday, July 11, 2013

MAKALA MAALUM.....NA MWANDISHI WETU....MHANDISI STELLA MANYANYA ATHIBITISHA UWEZO WAKE WA UONGOZI MKOANI RUKWA

Na, Stephano Mango
SIKU za hivi karibuni nimebahatika kufuatilia mambo mawili huko Mkoani Rukwa ambayo leo nakusudia kuwajuza wasomaji wa andiko la Ukanda wa Uranium popote pale mlipo kwani naamini bila kueleza nitakuwa sijawatendekea haki wasomaji na wapenzi wa Viongozi ambao wanafanya vyema kwenye Serikali hii ya awamu ya nne.

 
Mambo hayo ni uandikaji wa kitabu cha Sumbawanga Ng’ara na uanzishaji wa Makumbusho ya Mkoa wa Rukwa iliyopo ndani ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye kwa sasa ni Mhandisi Stella Martin Manyanya(MB).

 
Nimebahatika kutembelea Mkoa huo na kuona Makumbusho hayo pamoja na kukisoma kitabu hicho kizuri cha Sumbawanga Ng’ara ambacho kimeandikwa na Mkuu wa Mkoa huo.

Licha ya mambo mazuri mengi ambayo yanapaswa kuelezwa kwa wananchi ili waweze kubadili mwenendo wao katika uendeshaji wa jamii zinazotuzunguka , leo mie nakusudia kueleza haya mawili ya kuhifadhi mazingira na kumbukumbu za maeneo yetu.
 
Viongozi wengi nchini wanapenda kufanya vitu vya muda mfupi ambavyo vina maslahi kwao na havionekani kwenye jamii pana wala havishikiki na kusababisha kutokikidhi dhana ya Uongozi kwa maslahi ya Umma.
 
Naamini kuwa sifa za kiongozi bora ni miongoni na kuwa kiongozi wa vitendo na sio madaraka, kuwa na uwezo wa kushawishi watu ili kufanikisha jambo bora kwa manufaa ya watu na kuleta matokeo yanayotarajiwa

 
Uongozi ni mchakato wa kujua njia, kuonyesha njia, kutembea katika njia hiyo ili kufikia lengo kusudiwa mahali na wakati husika, uongozi ni kipaji na taaluma, ingawa wahenga wanasema kuwa “Kiongozi mzuri ni yule asiyependa kuwa kiongozi , lakini kutokana na uzembe wa viongozi waliopo, anashawishika na kuamua kuwa kiongozi”

 
Licha ya kuwa uongozi ni utumishi lakini sio ubwana na pia uongozi ni vitendo na sio madaraka, hivyo uongozi unahitaji nia thabiti na moyo wa kujitolea kwa kutumia taaluma na kipaji ulichonacho

 
Na katika maisha ya binadamu miongoni mwa mambo muhimu ni utamaduni na mazingira ambayo yanamzunguka katika kuimarisha uhai wake, na ndio maana mie leo nakusudia kuzungumzia kitabu cha Sumbawanga Ng’ara na uanzishaji wa Makumbusho katika Mkoa wa Rukwa

 
Leo nakusudia kumpa ushindi wa kiuongozi Mhandisi Stella Martin Manyanya kuwa ni kiongozi ambaye ameweza kukidhi malengo ya yeye kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza Mwanamke Mkoani Rukwa na hasa kwa mambo ambaye ameyafanya katika mkoa huo katika Nyanja zote

 
Ni mengi mno aliyoyafanya lakini kama nilivyosema kuwa kwa leo nayazungumzia hayo mawili na nikipata muda mwingine nitayazungumzia mengine ambayo nayo yanafaida kwa wananchi na mustakabali wan chi yetu

 
Mhandisi Manyanya amethubutu kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa kwanza kuandika kitabu cha mazingira katika eneo lake na pia amekuwa wa kwanza kuanzisha Makumbusho katika Mkoa wake tangu wakuu wa mikoa wapya katika awamu zote mbili za Uongozi wa Rais Jakaya Kikwete walipoteuliwa

 
Katika hali ya kumpongeza Mkuu huyo Manyanya mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya mpya ya Nyasa katika Kata ya Kihagara nayazungumzia mambo hayo mawili aliyoyaasisi katika Mkoa wa Rukwa toka alipoteuliwa mwaka 2011 ambayo matokeo yake tumeyaona

 
Kitendo chake cha kuandika kitabu cha Sumbawanga Ng’ara kimefufua na kuanzisha moyo mpya wa uhifadhi mazingira kwa wadau mbalimba , pamoja na kupendesha mji kwani ukienda katika mitaa ya Sumbawanga usiku imekuwa kama mchana. Hii ni kutokana na ushirikishwajiu wa wadau mbalimbali katika uhifadhi wa mazingira kama vile Vodacom, Tigo, na wengine

 
Katika mambo yalioredheshwa kwenye cha Sumbawanga Ngara kwani uchafuzi uliopo unaoendana na kusambaa kwa taka ngumu umeleta athari kubwa kwa viumbe hai ikiwemo binadamu, wanyama wanyonyeshao na wasionyonyesha, wadudu ambao wengine ni muhimu katika maendeleo chanya ya ardhi,

 
Kuongezeka kwa mmomonyoko wa ardhi unaosababisha vina vya maji kupungua katika maziwa kama Rukwa na Tanganyika na kukauka kwa baadhi ya mito , Utiririshaji wa maji taka yenye viashiria vya sumu au sumu kamili vinavyotokana na mabaki ya bidhaa za viwandani zimekuwa na athari kwa viumbe hai waishio nchi kavu na majini na kusababisha kupungua kwa wanyama na baadhi ya aina za samaki, na wengine kubadilisha hata ladha yao ya asili.

 
Kwa ujumla wake uharibifu huo umechangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabia nchi hususan, hali ya hewa katika baadhi ya maeneo, na hivyo kubadili uzuri wa asili na kupoteza baadhi ya vivutio.

 
Mfano ni kuhama kwa wanyama na ndege katika maeneo yao ya asili, kukauka kwa maporomoko ya maji na kadhalika.Uharibifu unaoendana na taka umesababisha miji ya maeneo ya Mkoa huo kuwa michafu na isiyovutia, milipuko ya magonjwa kama kuhara na kipindupindu, magonjwa ya ngozi kama upele, kudumaa kwaafya, kimsingi watu kuwa na afya hafifu na vifo. Matumizi ya dawa yamekuwa ya kiongezeka, gharama kubwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya, kushuka kwa kipato kutokana na kupoteza nguvu kazi, au kuwa na nguvu kazi hafifu na kwa ujumla wake kuongezeka kwa umaskini uliokithiri hasa katika miji

 
Kitabu hicho ambacho kimezinduliwa na Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda (Mb kinatoa mwongozo wa kufanikisha Mpango wa Sumbawanga Ng’ara kwa faida ya watanzania wote nchini
 

 
Ni muhimu kukisoma na kukielewa kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijacho kwani malengo yake ni kuona kuwa jamii ina ishi katika mazingira safi na salama , kwani hakuna maisha katika mazingira machafu na yenye viashiria vya hatari katika pumzi ya binadamu, leo ukifika Rukwa unakutana na mabadiliko mengi katika uhifadhi wa mazingira

 
Jambo jingine ambalo nimekusudia kulisema leo ni juhudi za Manyanya kuanzisha makumbusho katika Mkoa wa Rukwa Kwani Makumbusho ni sehemu ambayo watu wanaweza kujifunza namna ya uhifadhi bora wa mazingira kwa kuangalia watu wa kale walivyoweza kunufaika na mazingira yaliyowazunguka na mali asili zilizokuwepo kwa kupata dawa za miti shamba,chakula na vitoweo
 
Kupitia Makumbusho wananchi wanaweza kujifunza wajibu wao kwa nchi yao na jamii nzima inayowazunguka kwa kuangalia Mashujaa wa kale waliojitoa kwa moyo kupigana kwa ajili ya uhuru wa nchi,ulinzi na usalama wa mali zao
 
Uwepo wa Makumbusho ni jambo la kujivunia kwani yanaweza kutumika kujenga amani katika jamii ya watu wanaoishi kama ndugu na marafiki kwa kuangalia maisha ya watu wa kale walivyoishi kwa kushirikiana katika mambo yaliyokuwa yanawahusu wao na jamaa zao
Pia ni sehemu ambayo huwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali wanaokuja kuzitembelea na kujifunza historia na tamaduni zetu hivyo kuifanya dunia kuwa mahali padogo kwani vitu wanavyojifunza hupelekwa nchi za mbali na kujulikana kwa watu wa mataifa mbalimbali
Nakufanya kuwa kiungo cha mabadiliko na maendeleo ya Taifa kwani kupitia Makumbusho watu wanaweza kujifunza umuhimu wa mabadiliko na umuhimu wa kila mmoja kujiletea maendeleo kwa kuangalia namna mwanadamu alivyopitia hatua mbalimbali za mabadiliko mpaka kufikia hatua tuliyopo hivi sasa
Kukuza amani na kuchangia kwa ufanisi zaidi katika kujenga amani Dunia, Makumbusho yanaweza kuandaa midahalo, kuonesha filamu, jitihada za utafiti, matembezi, mikutano ya amani na maonyesho ya utalii
Ni sehemu ambayo huvuta watalii,hukuza sayansi,hushangaza/kustaajabisha,kuelimisha,kuburudisha na hutia chachu ya uwajibikaji kwani ndani yake yana kumbukumbu zilizohifadhiwa hivyo makumbusho ni historia inayoishi
Uwepo wa Makumbusho ni wasaa wa kutafakari sisi wenyewe maisha yetu hivyo tunapaswa kuweka juhudi za kutunza makumbusho zilizopo na zinazoendelewa kujengwa
Suala la kutunza Makumbusho ni tete kulibinafsisha kwani linabeba utamaduni na utambulisho wa Taifa au jamii husika, hivyo zinawezwa kutunzwa na mtu binafsi kwa maendeleo yake, taasisi au Taifa lakini kuwepo kwenye taasisi ya umma ni kufanya uhai uendelee kuwepo
Mchango wa Tanzania kwenye tamaduni za nchi za Ulaya ni mdogo mno na hajulikani vyema, japo tumeshuhudia watu wa mataifa mbalimbali wamekuja kujifunza tamaduni, ingawa kila siku tunaendelea kutothamini utamaduni wetu kwa kuendelea kuiga tamaduni za nje bila sababu za msingi
Utamaduni wa jamii za Watanzania unastahili kukuzwa,kutangazwa na kusimamia ili nasi tuweze kuchangia utamaduni wetu kwenye mataifa mengine na ustaarabu wa ulimwengu, hivyo utambulisho binafsi na wa pamoja, kati ya kumbukumbu na historia
Makumbusho ni benki ya kumbukumbu licha ya kuwa ni sehemu ya kuelimishana na kuburudisha, pia makumbusho ni kumbukumbu ya fikra, kazi,maisha,mtazamo wa matukio ya watu mbalimbali, Viongozi na wananchi wengi leo, kuna kila kila sababu ya wananchi kutembelea na kuikuza Makumbusho yao kwa maslahi ya vijazi vilivyopo na vijavyo
Leo wakazi wengi wa Rukwa wanatembelea Makumbusho hayo kwa kasi kwani yamekuwa ya kwanza kuanzishwa katika mkoa huo licha ya kuwa ni Makumbusho ya kipekee katika mikoa yote nchini
Nimalizie makala yangu kwa kusema tunawajibika kuwaiga na kuwaenzi viongozi wenye nia ya dhati ya kusukuma guruduma la maisha ya jamii mbele, wakiwa hai au wakitangulia mbele ya mwenyezi Mungu
Mtazamo wangu na wako ndio unaotengeneza uhai wa Makumbusho na mazingira ya taifa letu, hivyo tuamue kuwa chombo cha mabadiliko kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha umuhimu wa utamaduni, mazingira na makumbusho kwani utambulisho una uwezo mkubwa wa kuakisi maendeleo kusudiwa
Kama Mhandisi Stella Manyanya alivyomnukuu Mwandishi wa Marekani Hellen Keller alisema kwamba, “Peke yetu tunafanya machache, pamoja tunafanya mengi.” Tukijitoa sote kufanya kazi kwa bidii, ufahamu na maarifa hata yale yanayoonekana hayawezekani yatawezekana na hata yale yanayoonekana magumu yatakuwa mepesi
Maandishi haya yatuongezee nguvu ya kuanza safari yetu ya kuhakikisha kuwa Sumbawanga ina Ng’ara na Halmashauri nyingine za Rukwa zifuate na maeneo mengine nchini nayo yanapaswa kuiga kwa nguvu kubwa
Hakika siwezi kukuzuia kusoma maandishi yenye tija kwako, kwa maana ya kuwa siwezi kuzuia sikio lako kusikia lakini naweza kuzuia mdomo wako usiseme, nami kwa uhakika naweza kuzuia mkono wangu usiandike zaidi lakini siwezi kukuzuia wewe kusoma uthubutu wa kiuongozi wa Mhandisi Manyanya kwani ameonyesha njia na wengine wanapaswa kujipanga na kuonyesha uongozi tarajiwa kwa faida ya wananchi wanaowaongoza na Taifa kiujumla, na hakika uongozi hauna jinsi
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana, 0715-335051

Wednesday, July 10, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA MHANDISI STELLA MANYANYA AANZISHA MKAKATI KABAMBE WA KUIMARISHA NA KUFUNGUA MAENEO YA KIHISTORIA NA UTALII MKOANI RUKWA

090
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya (Mb) akiwaongoza wakazi wa kijiji cha Kapozwa Kata ya Kisumba wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa kulima barabara yenye urefu wa kilometa mbili kutoka kijijini hapo kuelekea kwenye maporomoko ya mto Kalambo ikiwa ni juhudi za Mkoa kuweka mazingira rafiki ya kukuza utalii wa eneo hilo la kihistoria. Kalambo Falls ambayo ni maporomoko makubwa ya maji ya asili yanayochukua nafasi ya pili kwa ukubwa barani Africa yakiwa na urefu wa mita 235 yanapatikana Mkoani Rukwa mpakani na nchi jirani ya Zambia na ni miongoni mwa vivutio vya asili nchini Tanzania na barani mwa Afrika.
 
084
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya (Mb) akizungumza na akina mama wakazi wa kijiji cha Kapozwa Kata ya Kisumba wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa waliojitokeza kumuunga mkono katika harambee ya kazi ya kulima barabara yenye urefu wa kilometa mbili kutoka kijijini hapo kuelekea kwenye maporomoko ya mto Kalambo ikiwa ni juhudi za Mkoa kuweka mazingira rafiki ya kukuza utalii wa eneo hilo la kihistoria.

091
Katibu wa Mkuu, Bwana Frank Mateni akiwa na wakazi wa kijiji cha Kapozwa Kata ya Kisumba wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa kulima barabara yenye urefu wa kilometa mbili kutoka kijijini hapo kuelekea kwenye maporomoko ya mto Kalambo ikiwa ni juhudi za Mkoa kuweka mazingira rafiki ya kukuza utalii wa eneo hilo la kihistoria.

087
Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya Kalambo John Maholani akitoa maelekezo kwa vijana wa kijiji cha Kapozwa Kata ya Kisumba wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa kulima barabara yenye urefu wa kilometa mbili kutoka kijijini hapo kuelekea kwenye maporomoko ya mto Kalambo ikiwa ni juhudi za Mkoa kuweka mazingira rafiki ya kukuza utalii wa eneo hilo la kihistoria. (Picha zote na Ramadhan Juma - DED Kalambo)

MSANII MRISHO MPOTO MAARUFU KWA JINA LA MJOMBA ATEMBELEA MAPOROMOKO YA MTO KALAMBO YALIYOPO KATIKA KIJIJI CHA KAPOZWA KATA YA KISUMBA WILAYANI KALAMBO MKOA WA RUKWA.

052
Mjomba, Mrisho Mpoto akiwa amepigwa na butwaa mara baada ya kuona maajabu ya maporomoko ya mto Kalambo. Alisema hakutegemea kama Tanzania ina maeneo ya kiutalii na ya ajabu ya kuvutia kama maporomoko ya mto huo ambayo ni ya pili kwa ukubwa barani Afrika. Mto Kalambo ndio mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Zambia. (Na Ramadhan Juma - DED Kalambo)