Wednesday, October 30, 2013

BALOZI WA TANZANIA NCHINI DRC ANTHONY CHECHE AONANA NA UONGOZI WA MKOA WA RUKWA KUJADILI MAHUSIANO YA NCHI HIZO MBILI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongoza kikao kati ya balozi wa Tanzania nchini Congo DRC Balozi Anthony Cheche aliyefika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kimahusiano kati ya nchi hizo mbili. Mkuu huyo wa Mkoa alimuomba balozi Cheche kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana Mkoani Rukwa pamoja na kuunganisha nguvu ya nchi hizi mbili katika kuwekeza kwenye usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika. Akizungumzia kuhusu wahamiaji haramu amesema ni bora kujenga ushirikiano mzuri wa kibiashara kwa nchi zote mbili ambapo taratibu maalum zitafuatwa kwa wananchi na wafanyabiashara kuingia na kutoka. 
 
Balozi Anthony Cheche anayoiwakilisha Tanzania nchini DRC akizungumza Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa leo alipoonana na uongozi wa Mkoa kwa lengo la kujitambulisha na kujadili mambo kadhaa ya mahusiano kati ya Tanzania na Congo DRC. Ameiomba Serikali ya Tanzania kuangalia upya vizuizi vya njiani kwa wafanyabiashara wa nje ikiwemo DRC hususani uwepo wa mizani nyingi barabarani na badala yake ziwepo chache na ziwe mbali kidogo na barabara kuepusha usumbufu kwa wasafiri wengine na wafanyabiashara.
 
Balozi Anthony Cheche akizungumza katika kikao hicho.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimuonyesha Balozi cheche toleo maalum katika gazeti la Daily News linaloelezea fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana Mkoani Rukwa kwa ajili ya kuzinadi kwa wawekezaji nchini Congo DRC.
 
Baadhi ya wakuu wa idara katika Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa wakiteta jambo katika kikao hicho, Kulia ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Ndugu Samson Mashalla, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Mipango Ndugu David Kilonzo na Kaimu Katibu Tawala Idar a ya Uchumi na Uwezeshaji Ndugu Respitch Maengo.
 
Picha ya pamoja.
 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiagana na Balozi Anthony Cheche baada kuonana na uongozi wa Mkoa huo mapema leo katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

MKUU WA MKOA WA RUKWA NA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU (TFS) WATEMBELEA HIFADHI NA MAPOROMOKO YA LUANJI NA KALAMBO FALLS MKOANI RUKWA

Maporomoko ya asili ya Luanji (Luanji Falls) yaliyopo Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS) wakizungumza na wanakijiji wa Kapozwa Wilayani Kalambo juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira yanayowazunguka ukiwemo msitu wa Kalambo na Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls) yenye urefu wa mita 225.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS) wakizungumza na wanakijiji wa Kapozwa Wilayani Kalambo juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira yanayowazunguka ukiwemo msitu wa Kalambo na Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls) yenye urefu wa mita 225.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a akionyesha kwa kidole msitu wa hifadhi wa Luanji yanapopatikana maporomoko ya asili ya mto luanji (Luanji Falls). Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wengine ni Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania walipotembelea hifadhi hiyo kwa ajili kuiendeleza.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akionyeshwa kushangazwa na staili ya nywele ya mmoja ya watoto wa kijiji cha Kapozwa Wilayani Kalambo alipofika katika kijiji hicho na Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania kwa ajili ya kuona hifadhi ya Msitu wa Kalambo na maporomoko ya mto Kalambo (Kalambo Falls).
 
Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls)
 
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stella Manyanya katikati waliokaa, Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Salum Chima kushoto waliokaa, watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa na Wakala wa Hifadhi ya Misitu Tanzania (TFS) ofisini kwa Mkuu huyo wa Mkoa.

MHE. NJOOLAY AKIAPISHWA IKULU KUITUMIKIA TANZANIA NCHINI NIGERIA

Aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Daniel Ole Njoolay akila kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nafasi ya ubalozi nchini Nigeria. (Picha na DailyNews)

Monday, October 28, 2013

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI PROF. SOSPETER MUHONGO AZINDUA RASMI MRADI WA UMEME WA SUMBAWANGA - NAMANYERE LEO

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo katikati akishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya kulia kwake, Mbunge wa Nkasi Kusini Ally Kessy kushoto kwake na wazee wawili kulia na kushoto wakiwawakilisha wananchi wa Namanyere (Wilaya ya Nkasi) katika uzinduzi rami wa mradi wa umeme kutoka Sumbawanga hadi Namanyere Wilayani Nkasi leo tarehe 28, Oktoba 2013. Mradi huo uliogharamiwa na Serikali ya Tanzania na kukamilika hivi karibuni una gharama ya Tsh. Bilioni 4.3 na umepitia jumla ya vijiji kumi na mbili vya njiani kabla ya kutua katika Mji huo wa Namanyere uliopo Wialayani Nkasi Mkoani Rukwa. Tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961 na tangu kuundwa kwa Mkoa wa Rukwa mwaka 1974 Wilaya hiyo haikuwa na umeme jambo ambalo limepokelewa kwa shangwe na wananchi wa Wilaya hiyo.  
 

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo na washirika wake katika uzinduzi huo wakibofya kitufe maalum kama ishara ya kuwasha umeme katika Mji wa Namanyere leo tarehe 28, Oktoba 2013 baada ya Wilaya hiyo kukosa huduma hiyo katika kipindi chote cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania. Katika uzinduzi huo Prof. Muhongo amesema Mkoa wa Rukwa umetengewa zaidi ya Tsh. bilioni 30 kwa ajili ya umeme vijijini kupitia REA, Wakala wa Umeme Vijijini ambapo jumla ya vijiji 66 katika kipindi cha miezi 20 ijayo kuanzia Novemba mwaka huu 2013 vitanufaika na mradi huo.
 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima kuwasalimia wananchi wa Kirando katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo Mkoani Rukwa. Katika ziara yake hiyo anatembelea miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi. 
 

Meneja Mahusiano wa Shirika la Umeme nchini TANESCO Bi. Badra Masoud akisherehesha baadhi ya mambo katika hafla fupi ya uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Namanyere Wilayani Nkasi leo tarehe 28, Oktoba 2013.
 

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo akiongea na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Rukwa na Wilaya ya Nkasi leo tarehe 28, Oktoba 2013 juu ya upatikanaji wa umeme katika bandari mpya inayoendelea kujengwa ya Kipili Wilayani humo. Alisema kupitia REA, Wakala wa umeme vijijini kuanzia mwezi Desemba miradi mbalimbali itaanza kufanya kazi kuweza kufikisha umeme katika maeneo tofauti Mkoani Rukwa ikiwemo bandari hiyo ya Kipili.
 


Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo akiwa ameshikilia kinyago cha mfano wa mtoto na mmoja ya wanakikundi cha ngoma za asili cha Kanondo cha Mkoani Rukwa baada ya kufurahishwa na uchezaji wa ngoma ya kikundi hicho inayoelezea malezi bora kwa watoto. 
 
Waziri Muhongo katika mikutano yake na wananchi hakusita kuwainua Mameneja wa Tanesco kuelezea juu ya miradi mbalimbali ya umeme Mkoani Rukwa. Kulia ni Meneja wa Tanesco Kanda ya Nyanda za Juu Magharibi Bi. Salome Nkondola na katikati ni Meneja wa Tanesco Mikoa ya Rukwa na Katavi.
 
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo na baadhi ya viongozi wa chama na Serikali wa Mkoa wa Rukwa.

Thursday, October 24, 2013

SERIKALI YASAINI MIKATABA MINGINE SABA YENYE THAMANI YA DOLA ZA KIMAREKANI BILIONI 1.7

IMG_0222
Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akifungua mkutano wa Biashara kati ya Tanzani na China kwenye Hoteli ya Dong Fang mjini Guangzhou akiwa katika ziara ya kikazi nhcini China Oktoba 24,2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
..............................................................................
 
SERIKALI ya Tanzania leo imeingia mikataba saba na makampuni sita ya Kichina yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 (Sh. trilioni 2.72) ambazo zitawekezwa kwenye ujenzi wa miradi ya umeme na nyumba za makazi na biashara.
Makubaliano ya uwekezaji huo mkubwa yameshuhudiwa leo (Alhamisi, Oktoba 24, 2013) na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mawaziri wengine wa Serikali baada ya kusainiwa kwa mikataba saba ya uwekezaji katika sekta hizo muhimu kwa uchumi wa nchi.
 
Utiaji saini huo ulifanywa mara baada ya Waziri Mkuu kufungua Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na China (Tanzania China Business Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya Dong Fang, jijini Guangzhou jimboni Guangdong, China. Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Baraza la Biashara la China Afrika (China Africa Business Council-CABC) linashirikisha wafanyabiashara wa China na Tanzania.
 
Mikataba iliyosainiwa leo ni kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na Kampuni ya Tabiau Electric Apparatus Stock Co Ltd (TBEA) ambao ni kwa ajili ya ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkubwa wa 400kV katika Gridi ya Taifa inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini Mashariki hadi Arusha.
 
Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Bw. Felchesmi Mramba ndiye aliyesaini mkataba huo wenye thamani ya dola za marekani milioni 692.7. Bw. Mramba pia alisaini mkataba mwingine na kampuni ya Shanghai Electric Power ambayo ndio itajenga mtambo wa Kinyerezi III.
 
Mkataba mwingine uliotiwa saini na Mramba ni kati ya Tanesco na kampuni ya China Gezhouba Group Corporation (CGGC) ambao wamekubali kuendeleza mradi wa umeme unaotokana na nguvu ya maji wa Rumakali ambao uko katika mikoa ya nyanda za juu kusini. Miradi hiyo miwili bado iko kwenye ngazi ya upembuzi yakinifu hivyo gharama zake bado hazijajulikana.
 
Kampuni ya Mkonge Energy Systems Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Tanzania, Bw. Salum Shamte ilitiliana saini mkataba na kampuni ya Sino Hyro Resources Ltd kwa ajili ya kuendeleza umeme wa nguvu za maji wa Masigira. Mradi huo unagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 136.
 
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Nehemia Mchechu aliweka saini mkataba baina ya NHC na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) kwa ajili ya kuliwezesha kifedha shirika hilo liweze kujenga nyumba mbalimbali za makazi na biashara nchini. Mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 500.
 
Bw. Mchechu pia aliwekeana saini mkataba mwingine na kampuni ya Poly Technologies (POLY) wa kuwa na uhusiano kifedha na kiufundi kati ya kampuni hizo ya kichina na NHC kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi na biashara huko Masaki wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Gharama za mradi huo ni dola za Marekani milioni 200.
 
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo (NDC) Bw. Gideon Nassari kwa niaba ya shirika lake aliingia mkataba na kampuni ya China ya Dalian International Economic & Technical Gooperation Group (CDIG) na Kampuni ya Hydro China Kunming Engineering Corporation kwa ajili ya kujenga kituo cha utafiti na mafunzo ya nishati mbadala. Mradi huo una thamani ya dola za Marekani milioni 136.
 
Mramba na Mchechu kwa nyakati tofauti walisema kwamba utekelezaji wa miradi hiyo utaanza wakati wowote kwani mambo mengi walishayakamilisha kwenye mazungumzo.
 
Wakati utambulisho, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bibi Julieth Kairuki alisema jumla ya Makampuni na Taasisi 46 zinazowekeza na kufanya biashara Tanzania zinashiriki katika Kongamano hilo ambapo kwa upande wa China, CABC wameandikisha makampuni 44 yatakayoshiriki kwenye kongamano. Katika Kongamano hilo, TIC imewasilisha mada ya mazingira ya uwekezaji Tanzania na Bodi ya Utalii na Shirika la nyumba la Taifa wamewasilisha mada zinazohusu uwekezaji kwenye sekta ya Nyumba na fursa za utalii nchini Tanzania.
 
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya nane ya ziara yake ya kikazi kwa mwaliko wa Serikali ya China bado anaendelea na mikutano mbalimbali na leo usiku atazungumza na Watanzania waishio Guangzhou.
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 24, 2013

Tuesday, October 22, 2013

MKUTANO WA WADAU WA UTEPE MWEUPE (WHITE RIBBON ALLIANCE ) WA UZAZI SALAMA TANZANIA WAENDELEA MKOANI RUKWA

Mratibu wa taifa wa utepe mweupe wa Uzazi salama Tanzania Dkt. Rose Mlay akiwasilisha mada iitwayo "Wajibika Mama Aishi" katika Mkutano na viongozi wa idara ya afya pamoja na wadau wa Sekta hiyo Mkoani Rukwa katika ukumbi wa RDC tarehe 21 Oktoba 2013 kujadili matumizi bora ya bajeti zilizowekwa na kuzipa kipaombele katika kusaidia uhai wa mama wajawazito katika vituo vya afya Mkoani Rukwa. Akielezea lengo la taasisi hiyo ya "White Ribbon" alisema ni kuimbusha Serikali ya Tanzania kutekeleza ahadi yake ya kuwa na asilimia hamsini ya vituo vya afya Mkoani Rukwa vitakavyotoa huduma kamili za dharura za uzazi zikiwa ni pamoja na upasuaji kumtoa mtoto na kutoa damu salama zinapohitajika ifikapo 2015.
 
Mganga Mkuu Hospitali kuu ya Mkoa wa Rukwa Dkt. John Gurisha akitoa maelezo mafupi juu ya huduma za kinamama wajawazito Mkoani Rukwa katika Mkutano huo. Alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili sekta ya afya Mkoani Rukwa ni uhaba wa watumishi katika sekta ya afya, uhaba wa magari ya wagonjwa kuweza kuwasaidia wananchi waliombali na huduma za afya pamoja na Vituo vingi vya afya na zahanati kutokuwa na vyumba vya upasuaji hususani katika maeneo ya mwambao na maeneo mengine ya pembezoni. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima na Kushoto ni Mratibu wa taifa wa utepe mweupe wa Uzazi salama Tanzania Dkt. Rose Mlay.

Baadhi ya watumishi wa idara ya afya Mkoani Rukwa na wadau wengine wa sekta hiyo wakisikiliza uwasilishwaji wa mada mbalimbali katika Mkutano huo. Shirika la Utepe Mweupe  Tanzania "White Ribbon Alliance for Safe Motherhood in Taznania(WRATZ)" linaendeleza kampeni yake ya miaka mitatu iitwayo "Wajibika Mama Aishi" (Be Accountable sa Mama can Survive Childbirth) kwa kuendesha mikutano na Semina mbalimbali kwa wadau wa afya katika ngazi ya Serikali na kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini; Lengo kuu likiwa kuikumbusha Serikali juu ya utekelzaji wa ahadi yake ya kuboresha huduma kamili za dharura za uzazi zikiwa ni pamoja na upasuaji kumtoa mtoto na kutoa damu salama zinapohitajika ifikapo 2015. Ahadi hiyo kwa kiasi kikubwa inaendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya nne na ifikapo mwaka 2015 itakuwa kipindi cha kuifanyia tathmini.

Friday, October 18, 2013

BARABARA ZA LAMI KUUNGANISHA MIKOA YA MBEYA NA RUKWA MBIONI KUKAMILIKA

 


TAARIFA YA MLIPUKO WA UGONJWA WA UTI WA MGONGO MKOANI RUKWA

Tangu ugonjwa wa Uti wa Mgongo ulipuke Mkoani Rukwa tarehe 9 Septemba 2013 jumla ya wagonjwa 32 wamefariki dunia wakiwemo wanawake 15 na wanaume 17  mpaka kufikia tarehe 17/10/2013.
 
Wagonjwa waliofariki jumla yao ni saba (7) wakiwemo wanawake watatu (3)na wanaume wanne (4), walioruhusiwa ni kumi na saba (17), wanawake  nane (8) na wanaume tisa (9). Waliopo wodini ni waogonjwa nane (8), wanawake watatu (3) na wanaume watano (5).
 
Taarifa hizi zimetolewa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga Dkt. Mussa.
 
Kusoma zaidi bofya Read More Chini kushoto.

Sunday, October 13, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA STELLA MANYANYA AMUWAKILISHA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA KATIKA HARAMBEE YA UJENZI WA KANISA LA MORAVIAN MJINI SUMBAWANGA NA KUCHANGISHA ZAIDI YA TSH. MIL. 58

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kanisa la Moravian Tanzania mjini Sumbawanga akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda aliyemteua kufanya hivyo baada ya yeye kukabiliwa na majumu mengine ya kitaifa. Awali Waziri Mkuu aliafiki mualiko wa Kanisa hilo katika kuongoza harambee hiyo ambayo imefanikiwa kupata zaidi ya Tsh. Milioni  58 zikiwepo fedha taslim zaidi ya shilingi Milioni 47 na nyingine zikiwa ni ahadi. Zimekuwepo pia ahadi za mifuko 30 ya Cement na mlango mmoja mkubwa wa kuingilia kanisani hapo.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stella Manyanya akitoa neno la awali kabla ya zoezi hilo la harambee kuanza ambapo aliwaomba waumini na wageni waliofika katika hafla hiyo kutoa kwa moyo katika kuchangia kazi hiyo ya Mungu. Kwa kuanzia alitoa ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa ambayo ni milioni tano (5) na yeye mwenyewe kuchangia milioni moja. Aliendeleza harambee hiyo kwa kuwachangisha kwanza viongozi wa Serikali alioambatana nao na kuendelea na taratibu zingine kwa mujibu wa ratiba.   
 
Askofu Mkuu Conerad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa akitoa neno katika hafla hiyo ambayo aliwataka waumini wa kanisa hilo kuchapa kazi kwa nguvu na kuepukana na uvivu ambao alisema ni ugonjwa mkubwa kuliko hata gonjwa la ukimwi. Alikemea pia tabia ya watu wengi kuwahusisha watu waliofanikiwa kwa jitihada zao wenyewe na imani za "Freemason" au "Ufisadi".
 
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka akizungumza katika harambee hiyo baada ya kupewa fursa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kutoa mchango wake, aliahidi mchango wa laki tano na mlango mmoja mkubwa wa kuingilia kanisani hapo.
 
Baadhi ya viongozi wa Serikali waliohudhuria katika hafla hiyo, kulia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga William Shimwela ambaye pia ni mwanakamati wa ujenzi katika kanisa hilo, Katikati ni Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hillal na nyuma yake ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Bwana Jakob Mwaruanda.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akiendelea na zoezi la uchangishaji.
 
Baadhi ya waumini wa kanisa la Moravian Sumbawanga wakimfagilia kwa shangwe Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hillal aliyachangia Tsh. Milioni kumi zikiwepo za kwake binafsi Mil. 7 na nyingine Mil. 3 kuchangiwa na wabunge wenzake.

Wednesday, October 9, 2013

MKUTANO WA WADAU WA UTEPE MWEUPE WA UZAZI SALAMA TANZANIA WAFANYIKA MKOANI RUKWA

Mratibu wa taifa wa utepe mweupe wa Uzazi salama Tanzania Mama Rose Mlay akizungumza katika Mkutano wa siku moja kati ya Uongozi wa Mkoa wa Rukwa, viongozi wa dini, wabunge, viongozi wa asasi za kijamii na za kidini na Muungano wa utepe mweupe wa Uzazi wa Salama Tanzania katika ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga tarehe 8 Oktoba 2013. Akielezea malengo ya mkutano huo alisema Serikali ya Tanzania inaheshimu ahadi yake ya kuwa na asilimia hamsini ya vituo vya afya Mkoani Rukwa vitakavyotoa huduma kamili za dharura za uzazi zikiwa ni pamoja na upasuaji kumtoa mtoto na kutoa damu salama zinapohitajika ifikapo 2015. Ktikati ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Ndugu Samson Mashalla.

Vikundi kazi katika kujadili mpango mkakati utakaotumiwa kuendeleza umuhimu wa huduma za uzazi salama katika jamii.
 

Dkt. Lunyelele akichangia moja ya mada katika Mkutano huo.
 
Picha ya pamoja

Chakula cha pamoja.

Tuesday, October 1, 2013

MAALIF SEIF AFUNGA IJITIMAI YA KIMATAIFA MKOANI RUKWA SEPT 30, AWATAKA WAISLAMU KUWA WAMOJA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya kabla ya kuagana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad alimkbidhi zawadi mbalimbali ikiwemo nyama maalum inayotengenezwa na kiwanda cha Saafi kilichopo Sumbawanga Mkoani Rukwa na vitambaa maalum vya kushonea nguo na kanga. 
 

 Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad akisindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga kwa ajili kuanza safari ya kurudi Zanzibar tarehe 30 Septemba 2013.
 
Makamu wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiagana na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu waliohusika na maandalizi ya Ijitimai hiyo Mjini Sumbawanga. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a.
 
....................................................................................................
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa wito kwa waislamu kuungana kwa mambo ya msingi yaliyomo katika dini hiyo na kuacha kutofautia kwa sababu ya madhehebu yao.
 
Amesema kuwa na madhehebu tofauti ni neema katika dini, hivyo hakuna sababu ya kugawanyika kutokana na tofauti ya madhehbu waliyonayo waislamu.
 
Maalim Seif ametoa nasaha hizo wakati akifunga rasmi Ijtimai ya Kimataifa iliyofanyika Mjini Sumbawanga, Mkoani Rukwa. Amesema ni jambo la kushangaza kuona waislamu wanakubaliana katika mambo ya msingi, lakini wanatofautiana na kulumbana kwa mambo madogo ambayo hayana athari ndani ya misingi na mihimili mikuu ya dini.
 
Amefahamisha kuwa iwapo waislamu wataungana na kuwa kitu kimoja, wataweza kuwashinda maadui wa Uislamu ambao siku zote wamekuwa wakishabikia migawanyiko ndani ya dini hiyo, akiwataja baadhi ya maadui hao kuwa ni maradhi ya ukimwi na dawa za kulevya.
 
Kwa upande mwengine amesema wakati waislamu wakijadili juu ya maadili ya dini yao, pia hawana budi kuhimizana katika kukabiliana na maadui wanaoathiri maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na janga la UKIMWI pamoja na matumizi ya dawa za kulevya. Amesema majanga hayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na kuporomoka kwa maadili, na kwamba wanaoathirika zaidi ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
 
Ameongeza kuwa ni wajibu wa masheikh, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kuelimishana juu ya majanga hayo, sambamba na kuachana na makatazo ya Mwenyezi Mungu yakiwemo pia vitendo vya zinaa.
 
Amesema, inaweza kueirejesha jamii katika maadili mema iwapo waislamu watakubali kufuata misingi thabiti na miongozo sahihi iliyomo katika uislamu.
 
Akizungumzia usalama wa nchi amesema wananchi hawana budi kuwa mstari wa mbele kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini ukizingatia hali ya sasa ya ugaidi inayoitikisa dunia na afrika ya mashariki, akitolea mfano tukio la Westgate na kwamba kama limejitokeza Kenya basi hata Tanzania laweza kuja.
 
Naye Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, amewahimiza waislamu waliohudhuria katika Ijtimai hiyo ya siku nne, kuitumia kivitendo elimu waliyoipata juu ya dini yao.
 
Amewahimiza waislamu hao kuwafikishia wengine elimu hiyo, ili nao waweze kuitekeleza dini ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa maamrisho yake na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW).
 
Kwa upande wake, Amiri wa Jumuiya ya Fiysabilillahi Tabligh Markaz Mkoani Rukwa Sheikh Abdallah Abubakar amewashukuru wailamu pamoja na viongozi wa Mkoa huo, kwa mshikamano walioonyesha katika kufanikisha Ijtimai hiyo.
 
Mapema akisoma Risala ya Jumuiya hiyo Amir Ali amesema Jumuiya imepata mafanikio makubwa tangu kuasisiwa kwake na kupatiwa usajili mwaka 1992, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha waislamu katika kutekeleza maamrisho ya Munyezi Mungu na kuacha kabisa makatazo yake, iki kujijengea mustakbali mwema katika maisha ya akhera.
 
Viongozi mbali mbali wa dini na Serikali wameshiriki katika ufungaji wa Ijtimai hiyo akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk.