Friday, November 29, 2013

KAIMU KATIBU TAWALA MKOA WA RUKWA ALBINUS MUGONYA AFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA SHIRIKA LA WATER REED PROGRAM LINALOFADHILI MIRADI YA KUPAMBANA NA UKIMWI KANDA YA NYANDA ZA JUU - RUKWA

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa ambae ni Katibu Tawala Msaidizi Kitengo cha Serikali za Mitaa akifungua kikao cha wadau wa shirika la Water Reed Program linalofadhili miradi ya kupambana na ukimwi kanda ya nyanda za Mkoani Rukwa. Katika hotuba yake hiyo aliitaka jamii yote kushirikiana ikiwemo Serikali na asasi binafsi katika mapambano dhidi ya Ukimwi ili kuokoa nguvu kazi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla. 
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Rukwa Dkt. Hansi Ulaya akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema Mkoa wa Rukwa kwa sasa umepanda kimaambukizi hadi kufikia asilimia 6.2 % ukiwa ni Mkoa wa saba kimaambukizi kitaifa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Ndugu  Ferbert Sebastian Ngaponda akichangia katika kikao hicho.
Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho ambao wametoka katika Halmashauri zote pamoja na taasisi zisizo za kiserikali ndani ya Mkoa wa Rukwa.


Thursday, November 21, 2013

MAJARIBIO YA AWALI YA MATUMIZI YA "VIDEO CONFERENCE" YAFANYIKA KWA KUZIKUTANISHA OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA OFISI ZA MAKATIBU TAWALA NA WAKURUGENZI WA MAMLAKA YA SERIKALI ZA MITAA MIKOA YA RUKWA, LINDI, MARA, RUVUMA NA SHINYANGA

Pichani wajumbe mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa, Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo, Nkasi na Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia Mkutano wa kwanza wa majaribio ya huduma ya Video Conference leo katika ukumbi wa "Video Conference" uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Anayeonekana kwenye Luninga akiwasilisha mada ni Naibu Katibu Mkuu Utumishi Ndugu Hab Mkwizu ambao ndio walioandaa mkutano huo uliojadili mada mbalimbali.
 
........................................................
Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikoa iliyowezeshwa kuwa na Miundombinu ya huduma ya "Video Conference" ambao unaratibiwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Huduma hii muhimu itasaidia sana katika kurahisisha mawasiliano Serikalini na hivyo kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji huduma kwa wananchi.
 
Katika majaribio ya awali Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetoa mada mbalimbali kupitia mfumo huo kwa Makatibu Tawala pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mikoa ya Rukwa, Mara, Lindi, Ruvuma na Shinyanga.
 
Miongoni mwa mada hizo zilizowasilishwa zikifuatiwa na majadiliano ni Utekelezaji wa Mfumo wa "OPRAS" katika Utumishi wa Umma, Mwenendo wa utekelezaji wa masuala Anuai za jamii katika Utumishi wa Umma, Usimamizi na uzingatiaji wa Maadili ya Utumishi wa Umma na Mafanikio na Changamoto za utekelezaji wa Mfumo wa Taarifa za kiutumishi na Mishahara Serikalini.
 
Zoezi hili la majaribio limefanikiwa japo kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo kukatika kwa mawasiliano yanayounganisha picha na sauti sababu kubwa ikiwa ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kukosa huduma za Mkongo wa Taifa unaoratibiwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayanisi na Teknolojia.
 
Changamoto nyingine ni baadhi ya picha kuwa na muonekano hafifu, ambayo kwa mujibu wa Mchambuzi wa Mifumo ya Komputa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Ndugu Emmanuel Mwandiga inasababishwa pia na kasi ya huduma za mtandao kuwa chini pamoja na masafa ya mawasiliano kuwa hafifu.
 
Changamoto hizo zikifanyiwa kazi na Wizara husika ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ni wazi kuwa mfumo huo utakua njia sahihi zaidi na kisasa inayokwenda na wakati katika kurahisisha na kuboresha mawasiliano Serikali.
Wajumbe wakifuatilia mada kwa makini kupitia Luninga kubwa iliyopo mbele yao (Video Conferencing) Mambo yalikuwa yanakwenda "LIVE" ikiunganishwa Mikoa ya Rukwa, Lindi, Mara, Ruvuma, Shinyanga na Dar es Salaam ilipo Wizara ya UTUMISHI.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (wapili kushoto) nae alikuwepo kushuhudia Mkutano huo wa majaribio ambapo alipewa dakika kumi kuchangia juu ya mfumo huo ambapo alisema Serikali itaokoa fedha nyingi kuliko ilivyokuwa hapo awali ambapo wajumbe kutoka Mikoa mbalimbali walikuwa wakilazimika kusafiri kwa magari ya ofisi kuhudhuria vikao nje ya mikoa na maeneo yao ya kazi kwa gharama kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (kushoto) na Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima wakifuatilia moja ya mada iliyokuwa ikiwasilishwa kupitia mfumo huo mpya wa "Video Conferencing".
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Ndugu William Shimwela akichangia moja ya mada katika mkutano huo. Kulia ni Muhasibu Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ndugu Sosthenes Mutarubukwa.
Wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali katika Mkutano huo.
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Ndugu Samson Mashalla akichangia moja ya mada katika mkutano huo. 
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada katika Mkutano huo.


Tuesday, November 19, 2013

WEZI WA MAFUTA KWENYE MALORI YA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI WAFUMANIWA NA MSAFARA WA MKUU WA MKOA WA RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwafokea wafanyakazi wawili wa kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China baada ya kufumwa na msafara wake wakiiba mafuta ya Diesel kwenye tanki la lori la la kumwagilia maji (Boza) la kampuni hiyo tarehe 19 Novemba 2013 Katika kijiji cha Ntendo Manispaa ya Sumbawanga. Mkuu huyo wa Mkoa alikemea tabia hiyo ya wafanyakazi wezi na kusema umekua ni ugonjwa wa mda mrefu unaozorotesha kukamilika kwa ujenzi wa barabara za lami zinazoendelea kujengwa Mkoani Rukwa.
 
Wafanyakazi hao waliokamatwa ni dereva William Ebron (kulia pichani)
na kibarua Isaya Godwin  ambao walifumwa majira ya saa nne asubuhi wakinyonya mafuta kwenye tanki la Lori hilo lenye namba za usajili T-518 BDV mali ya kampuni hiyo kwa kutumia mpira wa kupitishia maji na kumuwekea mteja kwenye dumu la lita tano, hata hivyo mteja huyo alifanikiwa kukimbia. Baada ya kuhojiwa walidai kuwa mteja wao huyo angelipia lita hizo tano kwa Tsh. 3500/= bei ambayo kihalali haiwezi kununua japo lita mbili za mafuta hayo katika soko. 
 
 Msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ulikua ukielekea katika kata ya Mtowisa kwa ajili ya shughuli za kuhamasisha maendeleo ambapo ulikumbana na mkasa huo njiani katika Kijiji cha Ntendo. Barabara ya Sumbawanga - Namayere inajenga kwa kiwango cha lami na mkandarasi Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd. kutoka Tanzania kwa gharama ya Sh. bilioni 78.8 ambazo ni fedha za ndani.
 
Watuhumiwa William Ebron (kulia) na kibarua Isaya Godwin (kushoto) muda mfupi baada ya fumanizi wakiwa hawana cha kujitetea.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwakabidhi wezi hao kwa vyombo vya usalama ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Watuhumiwa wakiwa mikononi mwa Polisi.
Mashuhuda wa tukio hilo.
Baada ya kuanza ziara yake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akimuapisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Adam Misana (wapili kulia) na baadhi ya watendaji wa Kata ya Mtowisa na Kijiji cha Muze juu ya utekelezaji wa maazimio na makubaliano waliowekeana. Maazimio hayo ni pamoja na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shuguli za maendeleo ya vijana, kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wakulima na wafugaji katika kila kijiji kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji, kuwekeana utaratibu maalum wa idadi ya mifugo inayotakiwa kufugwa kulingana na ukubwa wa maeneo husika, uhifadhi wa mazingira hususani ujenzi wa vyoo kuepukana na maradhi ya milipuko pamoja na maagizo mengine mbalimbali yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa. 
Katika ziara yake hiyo alifanya mikutano minne ikiwepo miwili ya nje na miwili ya ndani ambapo maagizo mbalimbali kwa ngazi ya Wilaya, Halmashauri na vijiji yalitolewa kwa watendaji husika.

Sunday, November 17, 2013

MKUU WA MKOA WA RUKWA AMTEMBELEA MAMA MARIANNE MJERUMANI ALIYEHAMIA TANZANIA NA KUJITOLEA KULEA WATOTO YATIMA 12 NA KUISHI NAO KAMA FAMILIA MOJA MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiteta jambo na Mama Marianne Lwanetzki  raia wa Ujerumani alipomtembelea nyumbani kwake jana kujionea maisha ya mama huyo ambae kwa sasa anaishi Mkoani Rukwa katika nyumba yake inayoitwa 'Kinder House" na watoto yatima 12 ambao aliamua kuwachukua kutoka katika mazingira magumu na kuishi nao kama watoto wake huku akiwapatia huduma mbalimbali za chakula, malazi, elimu na tiba. Watoto hao yatima wapo wanaume sita na wanawake ni sita.
 
Katika historia yake fupi Mama huyo alifika Mkoani Rukwa kwa shughuli za kitalii na ndipo alipomuona mtoto mmoja katika moja ya kituo cha kulelea mayatima akiwa na hali mbaya ya kiafya huku akiwa mgojwa sana, Aliamua kumchukua mtoto huyo na kuishi nae hadi akapona ndipo aliposhawishika na kuamua kuhamia Tanzania na kuchukua watoto wengine yatima hadi kufikia 12 ambao kwasasa amesema wanatosha kulingana na uwezo alionao.
 
 Aliongeza kuwa katika kuwalea watoto hao anatumia uwezo wake yeye binafsi pamoja na misaada  mbalimbali kutoa kwa ndugu, jamaa na marafiki wa nchini kwake Ujerumani.
Mtoto Kastory Mabruki ambaye ametajwa kuwa na sifa mbalimbali ikiwemo Uongozaji wa kwaya kama inavyoonekana pichani na hata uongozaji wa midahalo"debate" mbalimbali shuleni kwao zikiwemo za wanafunzi wa madarasa ya juu zaidi ya lile analosoma na kuzimudu vizuri. Katika watoto hao 12 kila mmoja anaonekana kuwa na kipaji cha aina yake ambapo Mama yao Mlezi anajitahidi kuviendeleza na kuvipa nafasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongea kumpongeza Mama Marianne kwa juhudi alizozichukua ambapo ameguswa sana na mpango huo wa mtu binafsi kulea watoto kama familia moja tofauti na sehemu nyingine nyingi ambazo taasisi ndizo zinazojishughulisha na vituo vya kulelea mayatima. Mkuu huyo wa Mkoa amewaasa watanzania wenye uwezo kuiga mfano huo kusaidia jamii kuondokana na kero za watoto wa mitaani.
Picha Ndani: Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (katikati mbele waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mama Marianne Lwanetzki (wapili kushoto mbele waliokaa) raia wa Ujerumani na watoto yatima 12 alioamua kuwachukua na kuwalea kama watoto wake wakitokea katika mazingira magumu na ambao anaishi nao katika nyumba yake anayoiita "Kinder House" iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa. Mama huyo anawapatia watoto hao mahitaji yao yote ikiwemo chakula, malazi na elimu. Kulia ni Katibu wa Mhe. Manyanya Frank Mateni. 
 Picha Nje: Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (watatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mama Marianne Lwanetzki (watatu kulia) raia wa Ujerumani na watoto yatima 12 alioamua kuwachukua na kuwalea kama watoto wake wakitokea katika mazingira magumu na ambao anaishi nao katika nyumba yake anayoiita "Kinder House" iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa. Mama huyo anawapatia watoto hao mahitaji yao yote ikiwemo chakula, malazi na elimu. Wapili kulia ni Hamza Temba - Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa.
Handshaking.
Nyumba hii inajulikana kama "KINDER HOUSE" ambapo kwa mujibu wa Mama mwenye nyumba hii Marianne Lwanetzki ambae ni raia wa Ujerumani alisema neno "kinder" kijerumani lina maana ya watoto. Mama Marianne amesema nyumba hiyo ambayo ni kubwa ikiwa na eneo la kutosha ameshaiandikia kisheria na kwamba ni urithi kwa watoto hao 12 anaowalea hata kama hatokuwepo tena duniani basi hapo ndipo nyumbani kwao.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akiagana na familia ya Mama Marianne Lwanetzki yenye watoto yatima 12 pamoja na wafanyakazi wake wanaomsaidia kwenye shughuli za malezi.

Saturday, November 16, 2013

KAZI MAALUM - USHIRIKIANO KAZINI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injnia Stella Manyanya, Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Chima watatu kushoto na baadhi ya wakuu wa idara na wataalam wakipinda mgongo kuandaa wazo la mpango maalum wa kuendeleza ujenzi wa Reli ya TAZARA kutoka Tunduma Mkoani Mbeya hadi Kasanga Mkoani Rukwa pamoja na vituo vitatu vya kibishara vya Kabwe, Kipili na Kasanga kuweza kuunganisha fursa na huduma za kibiashara kwa nchi za Tanzania Zambia, Burundi na Congo DR. Lengo kuu la mpango huo likiwa na ndoto za kuunganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantic kupitia Ziwa Tanganyika. 
Utendaji kazi wa namna hii unatoa picha ya ushirikiano mkubwa wa kikazi uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambapo viongozi wa juu hushirikiana na viongozi wa chini katika kusukuma guruduma la maendeleo ya Mkoa na taifa kwa ujumla bila kujali cheo, hadhi, umri, dini, rangi au kabila. Udumu ushirikiano huu...USHIRIKIANO HOYEEEEEEE!!!!!!!!

MAMA TUNU PINDA ATOA MSAADA WA VIATU PEA SITINI KWA WATOTO YATIMA WA KITUO CHA KATANDALA (MARTIN DE PORES) SUMBAWANGA MKOANI RUKWA

Katibu wa Waziri Mkuu Jimbo Ndugu Charles Kanyanda akimkabidhi Sister Scholastica Mwembezi wa Masista Maria Mtakatifu Malkia wa Afika ambao ni wamiliki wa kituo cha kulea mayatima cha Katandala Mkoani Rukwa viatu pea sitini zilizotolewa na Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda ikiwa ni ahadi aliyoitoa alipotembelea kituo hicho mapema mwaka huu. Aidha Sister Mwembezi amemuomba Katibu Kanyanda kumfikishia salamu za shukrani Mama Pinda ikiwa ni pamoja kumkumbusha ahadi ya gari aliyoitoa kwa kituo hicho.  
 Ndugu Charles Kanyanda akimvisha viatu mmoja ya watoto yatima katika kituo hicho baada ya kukabidhi zawadi hizo kutoka kwa Mama Tunu Pinda. Mzee Kanyanda amewataka wadau mbalimbali kuonyesha moyo wa upendo katika kusaidia mahitaji mbalimbali kwa watoto na kituo hicho.
Katibu wa Waziri Mkuu Jimbo Ndugu Charles Kanyanda akiimba moja ya wimbo na watoto wa kituo cha kulea mayatima cha Katandala.

Thursday, November 14, 2013

COSTECH YATOA FEDHA KIANZIO (SEED FUND) TSH. MILIONI 8 KWA KONGANO LA UMOJA WA WAFUGAJI WILAYANI NKASI MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injnia Stella Manyanya akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni nane (8) Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa Ndugu Pancras Maliyatabu kama fedha ya kianzio kwa Kongano la umoja wa wafugaji hao zilizotolewa na Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini (COSTECH) kwa lengo kuendeleza ufugaji wa kisasa usioathiri mazingira na kumnufaisha mfugaji kiuchumi. Kulia ni Ndugu Festo Maro Afsa Utafiti Mkuu wa COSTECH na kushoto ni Katibu wa Umoja wa Wafugaji hao Ndugu Jisena Biliya.
Viongozi wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi wakionyesha hundi yenye thamani ya shilingi milioni nane waliyopewa na COSTECH kama "Seed Fund" kwa ajili kuendeleza kongano la wafugaji Wilayani humo. Kulia wanaoshuhudia ni Ndugu Festo Maro Afsa Utafiti Mkuu wa COSTECH na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na Wanakongano wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi (hawako pichani) katika Mkutano uliofanyika Kalambo Ranch  Wilayani humo tarehe 14 Novemba 2013. Mkuu huyo Mkoa aliwataka wafugaji kufuga kisasa bila kuathiri mazingira kwa kufuga mifugo michache inayoendana na maeneo husika, aliwataka pia wafugaji kuwaendeleza watoto wao kielimu tofauti na ilivyo hivi sasa amabao wengi wao hufanyishwa kazi za uchungaji wa mifugo. Katika hotuba yake fupi alitoa agizo kwa halmashauri zote Mkoani Rukwa kuweka kipaombele katika kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima katika kila kijiji na kujiwekea mkakati wa idadi ya mifugo itakayofugwa kulingana na ukubwa wa eneo la malisho.
Ndugu Festo Maro Afsa Utafiti Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Nchini COSTECH akizungumza na wanakongano wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa jana tarehe 14 Novemba 2013. Katika maelezo yake alisema kuwa sio kila Kongano hupewa fedha za kianzio bali hushindanishwa na kwamba Kongano la Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi likiwa na wanachama 167 limeibuka washindi kwa kuwa na mipango thabiti ya kuendeleza shughuli zao za ufugaji kisasa kwa kuwainua kiuchumi, kielimu, kiafya na kubwa zaidi bila kuathiri mazingira. Alisema Lengo la COSTECH kutoa misaada kama hiyo ni kuwawezesha wadau wafanye shughuli zao kisayansi zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aweze kuzungumza na Wanakongano wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani humo ambao yeye ndie muasisi wa umoja huo. Katika neno lake la awali alimtaarifu Mkuu huyo wa Mkoa kuwa Umoja huo ulianzishwa mwaka jana 2012 tarehe 29 Agosti na kusajiliwa rasmi tarehe 30 Agosti 2013 ukiwa na wanachama 167 na lengo kuu likiwa ufugaji bora wa kisasa usioathiri mazingira na utakaomnufaisha mfugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Wilayani Nkasi Ndugu Pancras Maliyatabu Cheti rasmi cha usajili wa umoja huo uliosajiliwa rasmi tarehe 30 Agosti 2013. Katikati anaeshuhudia ni Katibu wa umoja huo ndugu Jisena Biliya.
Picha ya pamoja.

Wednesday, November 13, 2013

MAKAMU MWENYEKITI WA CCM TAIFA NDUGU PHILIP MANGULA AMALIZA ZIARA YAKE YA KICHAMA MKOANI RUKWA


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Hiporatus Matete wapili kushoto kwa niaba ya viongozi wa chama na Serikali Mkoa wa Rukwa akimuombea dua Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Philip Mangula wakwanza kushoto aweze kusafiri salama kuelekea Mkoani Mbeya katika maagano yaliyofanyika Mpakani mwa Mkoa wa Rukwa na Mbeya tarehe 13 Novemba 2013. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya.
 

Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Philip Mangula akionyesha mchoro wa asili wa Twiga aliopewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya wa pili kushoto katika hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Mkuu huyo wa Mkoa tarehe 12 Novemba 2013 kama ishara ya kulinda na kuzipenda maliasili za taifa na kuendeleza vita dhidi ya ujangili nchini. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Hiporatus Matete na wa kwanza kulia ni Katibu wa CCM Mkoa huo Bi. Rahel Ndengeleke.
 
Mhe. Mangula amesema amejifunza mengi Mkoani Rukwa ikiwemo mipango mbalimbali ya maendeleo ya Chama na Serikali, alipendezewa na maendeleo aliyoyaona sasa Mkoani Rukwa tofauti na miaka 10 iliyopita alipofika Mkoani hapo kwa mara ya mwisho. Alifurahishwa na Mpango wa Serikali ya Mkoa wa Rukwa wa ONYARU; Ondoa nyasi Rukwa ambao umehamasisha wananchi wengi kuondoa nyasi na kuezeka bati katika nyumba zao.
 

Baadhi ya viongozi wa chama (CCM) na Serikali Mkoani Rukwa wakiwa katika hafla ya chakula cha jioni cha kuagana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Philip Mangula katika Hoteli ya Holland Mjini Sumbawanga tarehe 12 Novemba 2013.
 
Baadhi ya viongozi wa chama (CCM) na Serikali Mkoani Rukwa wakiwa katika hafla ya chakula cha jioni cha kuagana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Philip Mangula katika Hoteli ya Holland Mjini Sumbawanga tarehe 12 Novemba 2013.
 
Gari anayoitumia Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Philip Mangula ikitembea katika barabara ya Lami kutoka Sumbawanga kwenda Jijini Mbeya. Sehemu kubwa ya Barabara hiyo kwa sasa imeshakalika hususani miradi miwili ya Tunduma - Ikana na Ikana - Laela, mradi mmoja wa Laela-Sumbawanga unaojengwa na Mkandarasi Aasleaff Bam International ambao ulikua unasusua sasa unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha. Maendeleo haya ya barabara na mengine mengi aliyoyaona yalikua kivutio kikubwa kwa Mhe. Mangula ambae alitoa ushuhuda kwamba tangu afike Mkoani Rukwa mara ya mwisho mwaka 2003 na sasa hali ni tofauti kabisa na kwamba kwa kipindi hicho cha Miaka 10 ameioana Rukwa Mpya.

Tuesday, November 12, 2013

MAKAMU MWENYEKITI WA CCM NDUGU PHILIP MANGULA ZIARANI MKOANI RUKWA

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Ndugu Philip Mangula akifurahia jambo na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Alhaj Salum Mohammed Chima mara baada ya kuwasili Mkoani Rukwa akitokea Katavi kwa ziara ya kichama hivi karibuni. Mheshimiwa Mangula atamaliza ziara yake leo tarehe 12 Novemba 2013 Mkoani Rukwa ambapo amefanya mikutano mbalimbali ya nje na ya ndani pamoja na kukagua miradi mbalimbali inayoendeshwa na Chama cha Mapinduzi na Serikali.
 

Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta alipowasili Wilayani hapo hivi karibuni kwa ziara ya kichama ya siku nne Mkoani Rukwa.
 
Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula akipeana mikono na Mbunge wa Nkasi Kusini Ali Kessy maarufu kama Ali Mabodi katika ziara yake Wilayani Nkasi hivi karibuni.
 
Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa watatu kushoto, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Hiporatus Matete wa pili kushoto na Katibu wa CCM Mkoa wa rukwa wakifurahia mapokezi ya wananchi wa kijiji cha Kizi kilichopo Wilayani Nkasi waliokuwa wakimlaki Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Ndugu Philip Mangula kwa ujio wake Mkoani Rukwa.
 
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Rajab Mtumwa Rutengwe wa pili kushoto na msafara wa viongozi wa Chama Tawala kutoka Mkoa wa Katavi wakiondoka katika viwanja vya Kizi baada ya kumuaga na kumkabidhi Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula kwa viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya ziara ya kichama Mkoani humo.

Friday, November 8, 2013

SOMA NA TAZAMA KWA MAKINI VIDEO YA HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ALIYOITOA BUNGENI KUHUSU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, 7 NOVEMBA, 2013, DODOMARAIS KIKWETE ALIHUTUBIA BUNGE DODOMA, ASEMA TANZANIA HAINA MPANGO WA KUJITOA KWENYE JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

D92A0027
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma leo jioni(picha na Freddy Maro)
 
D92A0483
 
Na  fUll Shangwe Blog
.........................................................
 
Rais Jakaya Kikwete amesema kwamba Tanzania haina mpango wa kujitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na itaendelea kuwepo kwa kuzingatia matakwa ya mkataba wa EAC na Itifaki zake,licha ya kutoshirikishwa kwa baadhi ya mambo.

 
Aidha Rais Kikwete amesisitiza kuwa Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja na kuongeza kuwa huo sio msimamo wake au Serikali pekee bali ndio Watanzania walio wengi.

 
Kauli hiyo ilitolewa leo Bungeni mjini Dodoma wakati Rais Kikwete alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wa Tanzania juu ya EAC.

 
“Napenda kuwahakikishia waheshimiwa wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!,” Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za EAC na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki .

 
“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake. Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa EAC inaendelea kustawi,” alisema Rais Kikwete.

 
Alisema kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, ilieleza kuwa asilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.

 
Rais Kikwete alisema ni lazima ni kutambua ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa EAC.

 
Alisema Tanzania itaendelea kukumbusha umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa, kama vile kuheshimu matakwa na masharti ya mkataba ulioanzisha EAC, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za jumuiya hiyo .

 
“Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake,” alisisitiza.
Rais Kikwete.

 
Alisema msimamo na mtazamo wa nchi , kuundwa kwa Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho.

 
Akizungumzia kuhusu kumekuwepo na madai Tanzania inachelewesha maendeleo ya jumuiya hiyo alisema hayana ukweli wo wote.

 
Huku akiongeza Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa utengamano, lakini inapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla hazijakamilika. Hivyo alizitaka nchi uanachama kuwa makini katika kila hatua tunayochukua.

 
Alisema kwa msimamo na mtazamo wa nchi , suala la Shirikisho liwe ndiyo hatua ya mwisho.

 
Hata hivyo Rais Kikwete alisema pengine msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji,ndiyo yanayotuletea vikwazo.

 
Hivi karibu viongozi wa nchi tatu wanachama wa EAC yaani Uganda, Rwanda na Kenya walikutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani Juni 24-25 , 2013 mjini Entebbe, Uganda; Agosti 28, 2013 mjini Mombasa, Kenya na Oktoba 28 , 2013 mjini Kigali, Rwanda.