Thursday, April 24, 2014

SAFARI YA HAPA DUNIANI YA ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA KALAMBO MKOANI RUKWA NDUGU MOSHI CHANG'A YAFIKIA TAMATI, AZIKWA NA MAMIA YA WANANCHI KWAO KIHESA MKOANI IRINGA

Baadhi ya Wakuu wa Wilaya nchini na Wananchi wakishiriki kubeba mwili wa Marehemu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa Hayati Moshi Mussa Chang'a kwa ajili ya kwenda kuusalia katika Msikiti wa Mwanchang'a Kihesa na baadae kupelekwa katika makaburi Mtwivila alikozikwa rasmi na mamia ya wananchi walijitokeza katika msiba huo Mkoani Iringa jana. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisalimiana kwa majonzi makubwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda mara baada ya kuwasili Nyumbani kwa Marehemu Moshi Chang'a kwa ajili Mazishi. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Hawa Ghasia aliyeiwakilisha Serikali katika Msiba huo mkubwa.
Sehemu ya meza kuu ikitafakari msiba huo kwa majonzi.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda akisaini kitabu cha maombolezo, Katika salam zake Mhe. Makinda alimuelezea Chang'a kama mtu muhimu sana katika maisha yake ya siasa kwani mnamo mwaka 1995 akiwa Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe alimsaidia sana katika harakati za kisiasa ambazo zimemfikisha hapo alipo hivi leo, Kwa mujibu wa Mama Makinda alisema "...bila ya Chang'a leo hii nisingeitwa Spika....".
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akisoma wasifu wa marehemu ambae ameacha watoto watano; wakiume watatu na wakike wawili na mjukuu mmoja. Katika kumuelezea Ndugu Chang'a Mkuu huyo wa Mkoa alieleza miongoni mwa mambo yatakayomfanya asimsahau chang'a ikiwa ni pamoja na kumuubiri Mungu mara zote katika ziara zake ambapo alitolea mfano kwa kuimba moja ya wimbo aliokuwa akiupenda zaidi wa kumtukuza Mungu wa "KWELI MUNGU WA AJABU" wimbo ambao uligusa hisia za watu na kupelekea kutokwa na machozi ya bila kupenda wakiwepo wanawake na wanaume.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro wakisikitika kwa msiba huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Symthies Pangisa akitoa salam zo Ofisi yake katika msiba huo.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mhe. Iddi Kimanta ambae mpaka Marehemu anakutwa na Umauti ndiye aliyekuwa akikaimu nafasi yake ya Ukuu wa Wilaya ya Kalambo akishirikina na Mhe. Venance Mwamoto Mkuu wa Wilaya ya Kibondo kufunua jeneza la Ndugu Chang'a kwa kuondoa bendera ya taifa kuashiria itifaki za Kiserikali kukamilika tayari kupisha taratibu za kidini za kwenda kumpumzisha Marehemu aliyezikwa kwa taratibu za dini ya Kiislamu.
Mamia ya wananchi  wakielekea katika makaburi ya Mtwivila Mkoani Iringa kwa ajili ya kumpumzisha Ndugu Chang'a.
Safari ya mwisho hapa duniani ya Mhe. Chang'a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo ndio imeishia hapa, wananchi wakishirikiana kuuhifadhi mwili wake katika nyumba yake ya kudumu (kaburi). Kila mmoja ajipime na ajiandae kwa safari hii isiyokwepeka.

Monday, April 21, 2014

TAARIFA RASMI KWA UMMA YA KIFO CHA MKUU WA WILAYA YA KALAMBO MHE. MOSHI CHANG'A, KUZIKWA JUMATANO MKOANI IRINGA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

MKOA WA RUKWA

Anuani ya simu:”REGCOM”                          Simu Na:(025)-2802138/2802144

Fax Na. (025) 2802217

Baruapepe: rasrukwa@yahoo.com


             OFISI YA MKUU WA MKOA,
     S.L.P. 128,
     SUMBAWANGA.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella M. Manyanya (Mb) kwa masikitiko makubwa anapenda kuwajulisha juu msiba mkubwa ulioukumba Mkoa wetu wa Rukwa wa kuondokewa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Moshi Mussa Chang’a (62) aliyefariki jana jioni terehe 20 April, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Shinikizo la Damu na Kisukari.

Mwili wa Marehemu Mhe. Chang’a unategemewa kusafirishwa kesho jioni kutoka Jijini Dar es Saam hadi nyumbani kwao Mkoani Iringa ambapo mazishi yake yatafanyika keshokutwa siku ya Jumatano tarehe 23 April, 2014.

Marehemu Mhe. Chang’a alizaliwa Mkoani Iringa Januari Mwaka 1952 na amewahi kushika nafasi mbalimbali Serikalini na katika Chama cha Mapinduzi (CCM). Katika nafasi ya Ukuu wa Wilaya amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mbeya, Tabora, Mkalama na Kalambo Mkoani Rukwa ambapo mauti yake yamemfika.

Katika Ngazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewahi kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe na Iringa Vijijini na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Iringa.

Marehemu Mhe. Chang’a ameacha watoto watano (5) na Mjukuu Mmoja (1).Watoto wa kiume 3 na Wakike 2.
Kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki, na wote walioguswa na msiba huu mkubwa. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Sisi tulimpenda lakini Mungu kampenda zaidi.

Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi “AAAMIN”


Imetolewa na:

OFISI YA MKUU WA MKOA
RUKWA
Tarehe 21 April, 2014.


Sunday, April 20, 2014

TANZIA: MKUU WA WILAYA YA KALAMBO MKOANI RUKWA MHE. MOSHI MUSSA CHANG'A AFARIKI DUNIA JIONI YA LEO

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo enzi za uhai wake Mhe. Moshi Mussa Chang'a ambae amefariki dunia jioni ya leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugojwa wa shinikizo la damu na Kisukari. Taratibu za mazishi zitatangazwa mapema mara baada ya kikao cha familia. Tunatoa pole kwa wale wote walioguswa na msiba huu. Sisi tulimpenda lakini Mungu kampenda zaidi. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe.

Wednesday, April 16, 2014

KIKUNDI CHA KINAMAMA OFISI YA MKUU WA MKOA RUKWA WATOA MSAADA KWA WANAFUNZI WA SHULE YA WASIOONA YA MALANGALI MJINI SUMBAWANGA

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wasioona Malangali Mwl. Orthor M. Mkangara akitoa maelezo mafupi ya shule hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1998 ambapo mpaka hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 71 wengi wao wakiwa wasioona na baadhi wakiwa ni walemavu wa ngozi "Albinism". Alisema kwa sasa shule hiyo inahitajio kubwa na vifaa vya kufundishia pamoja na usafiri kwa ajili ya kurahisisha shughuli mbalimbali shuleni hapo. Alisema kuwa zipo changamoto nyingi shuleni hapo ambapo wadau mbalimbali wanakaribishwa katika kusaidia kuzitatua. Aliwashukuru kikundi cha kinamama kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa (pichani kushoto) kwa msaada waliotoa na kuomba wadau wengine kuwa na moyo kama huo katika kusaidia watoto wenye ulemavu hapa nchini. 
Katibu wa Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Bi. Joyce Mwanandenje akizungumza kwa niaba ya umoja huo ambapo alisema lengo la ujio wao Shuleni hapo ni kutimiza desturi yao ya kila mwaka ambapo hutembelea makundi ya wahitaji mbalimbali katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani. Katika salam zao shuleni hapo walitoa msaada wa magodoro 20, Sukari, sabubi na zawadi mbalimbali kwa aijili ya wanafunzi. Kikundi hicho cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa kinaundwa na watumishi wanawake kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Hazina Ndogo, Ukaguzi wa Ndani, Chuo Kikuu Huria na Baraza la Nyumba na Ardhi Mkoa.
Baadhi ya wanafunzi shuleni hapo wakiimba wimbo mwanana wa kuwakaribisha kikundi cha kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa walipofika shuleni hapo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Bi. S. Mwasilu akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Msingi Wasioona ya Malangali Mwl. Orthor M. Mkangara msaada wa magodoro na zawadi mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.Mwenyekiti wa Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Bi. S. Mwasilu na Katibu wake Bi. Joyce Mwanandenje wakigawa zawadi za biskuti kwa wanafunzi wasioona wa Shule ya Msingi Malangali katika hafla fupi ya kutoa msaada shuleni hapo.
Sehemu ya Msaada uliotolewa shuleni hapo.
Baadhi ya wanafunzi walemavu shuleni hapo wakiimba wimbo wa kushukuru kwa hisia kubwa.
Msafara wa kikundi cha kinamama wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa wakiingia kuangalia mabweni shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Wasioona Malangali Mwl. Orthor M. Mkangara akitoa maelezo mafupi kwa kikundi hicho cha kinamama walipoingia kukagua mabweni shuleni hapo, Mwalimu huyo alishukuru kwa msaada walioutoa wa magodoro na kusema utasaidia sana kuondoa tatizo la upungufu wa magodoro uliokuwepo.
Hakika msafa huu wa kikundi cha kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ulikua na mengi ya kujifunza shuleni hapo. Uandishi na namna ya kusoma kwa watu wasioona ni tofauti kabisa na uandishi wa kawaida. Hutumia kifaa maalum kuandikia, kalamu maalum na karatasi maalum, hali kadhalika usomaji wa maandishi hayo huwa ni wa kupapasa.
Wanafunzi wasioona hutumia kifaa maalum kwa ajili kuandikia maandishi yenye nundu ambayo husomeka kwa njia ya kupapasa. Kalamu ya kuandikia huwa na ncha kali kama sindano ya fundi viatu. Karatasi za kuandikia huwa ngumu kuweza kutoa vinundu ambavyo husomeka kwa kupapaswa.
Mwanafunzi S. Ngajiro ambae alikuwa haoni kabisa alipojiunga shuleni hapo na kubahatika kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam na kufanikiwa kuona akitumia mashine maalum ya kuandikia ("Tyre Writter") kwa ajili wanafunzi wasioona shuleni hapo. Mashine hiyo maalum kwa ajili ya watu wasioona ina vitufe sita tu vya kuandikia ambavyo hutumika kutengeneza Alfabeti zote katika uandishi  wa lugha kwa kutumia ujuzi wa hali ya juu.
Moja ya darasa dogo kabisa shuleni hapo ambalo huchukua wanafunzi wasiozidi tisa.
Kikundi cha Kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa wakiangalia bustani ya mbogamboga  ambayo ina hudumiwa na wanafunzi  shuleni hapo.
Picha ya Pamoja kati ya uongozi wa shule ya wasioona Malangali, kikundi cha kinamama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo.

Tuesday, April 15, 2014

WATUMISHI OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA WAPIGWA MSASA JUU YA ELIMU YA UKIMWI MAHALA PA KAZI

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akifungua mafunzo ya Ukimwi mahali pa kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mwishoni mwa juma, Semina hiyo iliyoandaliwa na Katibu Tawala Mkoa kupitia idara ya maendeleo ya jamii Mkoa kwa watumishi hao ilikua na lengo la kuelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali yanayohusu janga la Ukimwi na umuhimu wa Tohara kwa wanaume katika kujikinga na janga hilo. Katika hotuba yake Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa hakusita kuonyesha hisia zake kali kwa watumishi watakaohusika katika rushwa za ngono na kusema kuwa watachukuliwa hatua kali bila ya utetezi wowote kutoka kwake.
Mratibu wa TACAIDS Mkoa wa Rukwa Ndugu Daniel Mwaiteleke akitoa mada juu ya uelewa wa jumla kuhusu gonjwa la UKIMWI kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa RDC Mjini Sumbawanga.
Muwezeshaji wa mada ya magonjwa ya zinaa STD na STI Dkt. Lunyelele akiwasilisha mada yake kwa umahiri mkubwa bila ya kutafunatafuna maneno
Dkt. Lunyelele akiwa anatoa mafunzo hayo.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia mafunzo hayo.
Mjumbe katika Semina hiyo Ndugu Frank Mateny akichangia moja ya mada katika mafunzo hayo. 
Mdau Mussa Mwangoka na Paul Ngany'anyuka ndani ya Semina hiyo.
Dena na Richard Ndambala nao walikuwepo.

Monday, April 7, 2014

MKUU WA MKOA WA RUKWA ASHIRIKIANA NA UVCCM KATIKA MBIO ZA UZALENDO TANZANIA KUADHIMISHA MIAKA 50 YA MUUNGANO WA TANZANIA BARA NA TANZANIA ZANZIBAR MKOANI RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akipokea msafara wa pikipiki wa vijana wa CCM (UVCCM) ambao wanaendesha mbio za Uzalendo Tanzania zikiwa na lengo la kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar jana tarehe 07-04-2014. Mbio hizo za kitaifa zinahusisha msafara wa pikipiki tano zinazoongozwa na viongozi watatu wa UVCCM ambao wanakuwa kwenye gari, aidha zinashirikisha wadau mbalimbali wa UVCCM katika kuzifanikisha. Mbio hizo  zinahimiza vijana kudumisha muungano, kuweka utaifa mbele na kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao. Mbio hizo zitakuwa Mkoani Rukwa tarehe 07 na 08 April 2014 na kuelekea Mkoani Mbeya. 
Ujumbe wa mbio hizo za Uzalendo Tanzania ambazo zinaendeshwa na UVCCM.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (kati) akiendesha duwa rasmi ya kuwaombea viongozi waasisi wa Muungano ambao wametangulia mbele za haki kama wanavyonekana kwenye picha Hayati Mwalim Julius K. Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume muda mfupi baada ya kupokea msafara wa mbio hizi ofisini kwake jana tarehe 07-04-2014.
Msafara wa Mbio za Uzalendo Tanzania ukiondoka katika Ofisi ya Mkuu ya Mkoa wa Rukwa mara baada ya kupata baraka za kiongozi huyo na kusaini kitabu tayari kwa zoezi la mbio hizo katika Manispaa ya Sumbawanga na baadae kuelekea katika Mji Mdogo wa Laela.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiondoka na pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na Katibu wa UVCCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Philipo Elieza ambapo alishiriki mbio hizo hadi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya uwanja wa Nelson Mandela katikati ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiongoza mbio hizo na vijana wa UVCCM kuelekea kwenye mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (Mb) akizungumza katika Mkutano wa hadhara ambapo alisema tunu ya muungano ni lazma ilindwe na kila moja wetu na kuwa sio jambo la hiari. Aliongeza kuwa madai ya uwepo wa Serikali tatu ni hatua za kuhatarisha Muungano uliopo wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar hivyo hakuna budi kuimarisha Muungano wa Serikali mbili kwa maslahi watanzania wote. Aliuotelea mfano muungano wa Serikali tatu kuwa hauna tofauti na kuchukua kisu na kugawana mtoto ambapo kila mzazi atachukua kipande ambacho sio mtoto kamili.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Katibu wa UVCCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Philipo Elieza cheti cha pongezi kwa ushiriki wa Mbio za Uzalendo Tanzania na kingine kwa UVCCM Mkoa na Taifa kwa kuandaa na kufanikisha mbio hizo. Mkuu huyo wa Mkoa aliandaa vyeti vya pongezi kwa washiriki wote wa mbio hizo.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Godwin Mzurikwao akitoa salam za vijana wa CCM katika mkutano huo wa hadhara ambapo alisisitiza juu ya vijana kutumia fursa zilizopo katika kujiendeleza kiuchumi na kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Kulia ni Katibu Muenezi wa CCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Clemence Bakuli.

Saturday, April 5, 2014

CIDA NA PLAN INTERNATIONAL KUPITIA MRADI WA WAZAZI NA MWANA (THE MnW PROJECT) LATOA MSAADA WA VIFAA TIBA KUSAIDIA HUDUMA YA DHARURA KWA MAMA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA MKOANI RUKWA

Afisa Tawala wa Mradi wa Wazazi na Mwana (MnW) Bwana Mashauri Ndebile akimuonyesha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mhe. Iddi Kimanta shehena ya vifaa vya msingi kwa ajili ya kutoa huduma za dharura kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga Mkoani Rukwa. Vifaa hivyo mbalimbali vyenye thamani ya Tsh. Milioni 912 vimetolewa kwa Mikoa miwili ya Rukwa na Mwanza, ambapo kwa Mkoa wa Rukwa Mhe. Kimanta amevipokea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa huo Injinia Stella Manyanya. Jumla ya Zahanati 172 zitapatiwa vifaa hivyo ambapo kwa Mkoa wa Rukwa ni zahanati 114 kwa Halmashauri za Nkasi na Sumabwawanga Vijijini na Mwanza ni zahanati 64. Vifaa hivyo vimetolewa kwa ushirikiano wa mashirika ya Plan International, Jhpiego na Africare.
Dokta Neema Mamboleo mshauri wa Mradi wa Wazazi na Mwana akimuonyesha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta kitanda maalum kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga waliozaliwa kabla ya muda kutimia na kuwa na matatizo ikiwa ni sehemu ya vifaa hivyo vilivyotolewa na mradi huo. Msaada huo ni sehemu ya misaada mbalimbali ya mashirikia hayo Mkoani Rukwa ambapo hivi karibuni walitoa msaada wa "Ambulance" mbili na kujenga vyumba vya upasuaji kwa Halmashauri za Nkasi na Sumbawanga Vijijini.
Dokta Neema Mamboleo mshauri wa Mradi wa Wazazi na Mwana akimuonyesha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta kitanda maalum kwa ajili ya kusaidia kinamama wajawazito wakati wa kujifungua.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mhe. Iddi Hassan Kimanta kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Ndugu Kimulika Galikunga orodha ya mgao wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya Halmashauri hiyo. 
Wadau na wafanyakazi wa Africare Mkoani Rukwa wakiwa katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano. Kulia ni Ndugu Gasper Materu Mratibu wa Africare Mkoa wa Rukwa.
Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo.
Picha ya pamoja.