Friday, October 17, 2014

TANGAZO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya anapenda kuwatangazia na kuwakaribisha wananchi wote katika Kongamano la Uwekezaji la Ukanda wa Ziwa Tanganyika – Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi litakalofanyika Mkoani Rukwa kuanzia tarehe 26, Oktoba hadi 01, Novemba 2014.

Lengo kuu la Kongamano hili ni kunadi fursa nyingi za uwekezaji ambazo bado hazijawekezwa ipasavyo Mkoani Rukwa na katika ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Mkoani Rukwa fursa hizi zipo katika Sekta za Viwanda, Madini, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Afya, Elimu, Utamaduni, Michezo, Usafiri na Usafirishaji katika maeneo ya Barabara, Anga na Majini katika Ziwa Rukwa na Tanganyika; ikiwa ni pamoja na vivutio vingi vya kihistoria vinavyohitaji kuhifadhiwa na kuendelezwa. Mkoa wetu pia una vivutio kadhaa vya Kitalii ambavyo havijaendelezwa yakiwemo Maporomoko ya Kalambo, samaki wa mapambo “ornamental fish”, Mbuga ya Lwafi, pamoja na mabwawa ya asili ya Kwela na Sundu.

Kwa upande wa Mkoa wa Rukwa Kongamano hili litakuwa la kipekee ikilinganishwa na Makongamano yaliyotangulia kwa sababu litafanyika sanjari na mambo yafuatayo:-

a)                 Kufanya tathmini ya shughuli za Uwekezaji Kikanda na Kimkoa na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizojitokeza,

b)                 Kufanya tathimini ya Mafanikio ya miaka 40 ya kuanzishwa kwa Mkoa wa Rukwa (1974 - 2014),

c)                 Kutangaza fursa za uwekezaji za Mkoa wa Rukwa katika kipindi hiki,

d)                Kuzindua Wilaya Mpya ya Kalambo, pamoja na fursa za Uwekezaji wa Ndani na Nje za Wilaya hii,

e)                 Kufanya uzinduzi wa miradi mbalimbali ya Wawekezaji walioanza kuwekeza Mkoani Rukwa,

f)                  Kutathimini ubora wa wawekezaji waliojitokeza hadi sasa na kutoa tuzo kwa Wawekezaji bora

g)                 Maonyesho ya SIDO ya  wajasiriamali wa Kanda ya nyanda za juu Kusini inayojumuisha Mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa, Katavi na Njombe.

h)                Kutumia fursa hii kuwaalika Wajasiriamali wa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, kutumia fursa zilizopo za kuwekeza katika Mkoa wa Rukwa ikiwemo Wilaya mpya ya Kalambo.

i)                   Kutangaza fursa za biashara za Kimataifa. Kutokana na mazingira ya mahali Mkoa ulipo kijiografia na Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa ujumla, ipo fursa kubwa ya kufanya biashara za kimataifa kati ya Tanzania (Kupitia Mkoa wa Rukwa), Kongo, Burundi na Zambia. Nchi yetu iko katika mchakato wa kuipanua bandari ya Kasanga ambayo itatumiwa na Nchi za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Burundi katika kusafirisha mizigo na abiria.


Wananchi wote mnakaribishwa kushiriki na kujifunza mengi katika Kongamano hili.