Tuesday, March 31, 2015

TUME YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA (TCRA) KUZIMA MFUMO WA ANALOJIA LEO MACHI 31, SUMBAWANGA TELEVISION (STV) KUTOONEKANA TENA KUPITIA ANTENNA

Uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ya mfumo wa analojia kwa awamu ya kwanza ulianza kutekelezwa nchini tarehe 31/12/2012 saa sita kamili usiku katika jiji la Dar es Salaam kwa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Uzimaji ulindelea hadi mwisho wa mwezi wa nne 2013 katika miji ya Dodoma, Tanga, Mwanza, Moshi, Arusha na Mbeya. Uzimaji huu ulikuwa ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya uzimaji mitambo ya analojia kulingana na ratiba iliyotolewa na Serikali mnamo mwezi Desemba 2012 kuhusu mji saba tajwa hapo juu.
Baada ya kukamilisha utekelezaji wa awamu ya kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikamisheni kwa wataalam wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya tathmini ya mchakato mzima wa uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa kidijiti pamoja na uzimaji wa mitambo hiyo kwenye miji saba tajwa hapo juu kabla ya kuanza awamu ya pili.
Matokeo ya tathmini hii yameonyesha wananchi wameupokea vyema mfumo wa utangazaji wa kidijiti na hivyo kupelekea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Serikali kuridhia kufanyika kwa awamu ya pili ya uzimaji mitambo ya analojia.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Serikali mnamo mwezi February, 2014, Awamu ya Pili ya uzimaji wa mitambo ya analojia ulianza kwenye miji ya Singida na Tabora mwishoni mwezi wa tatu wa tarehe 31 Machi, 2014 wakati ambapo miji mingine mitatu ilifata katika zoezi la uzimaji wa mitambo ya analojia ambayo ni Musoma, Bukoba, na Morogoro. Miji ya Kahama na Songea ilihusika katika uzinduzi wa mitambo ya dijitali ikizingatiwa kuwa miji hiyo haikuwa na matangazo ya televisheini ya mfumo wa analogia.
Maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia ya utangazaji wa televisheni kwa Mji wa Sumbawanga yamekamilika kwa kuwashirikisha wadau wa sekta ya utangazaji. Mitambo itazimwa saa sita kamili usiku wa tarehe 31 Machi, 2015. Vigezo vinavyotumika kuzima mitambo ya analojia ni pamoja na kuwepo utangazaji wa mfumo wa analojia pamoja na kidijiti kwenye eneo husika, upatikanaji ving’amuzi na uwepo wa chaneli tano za kitaifa kwenye mfumo wa kidijiti.
Elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali kuhusu kuhamia katika teknolojia ya mfumo wa utangazaji wa dijitali imekuwa ikitolewa kwa kiwango cha kuridhisha. Matangazo ya dijitali yanawafikia watu asilimia zaidi ya 20% kati ya watu asilimia 24% waliokuwa wanapata matangazo ya televisheni ya analojia.
Kama ilivyoelezwa tangu awali, utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia utakuwa kwa maeneo yenye matangazo ya dijitali tu. Maeneo ambayo hayana miundombinu ya dijitali hayatazimwa kwa sasa hadi yapate dijitali.
Mabadiliko haya hayahusu matangazo kwa njia ya utangazaji wa satelaiti, waya (cable) na redio. Tunawataka wananchi wa Mji wa Sumbawanga wasizitupe TV zao za analojia bali wanunue ving’amuzi ili kupata matangazo ya dijitali.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeagiza watoa huduma za kusambaza ving’amuzi walioko Sumbawanga kuhakikisha kuwa kunakuwa na ving’amuzi vya kutosha. Tumefanya ukaguzi katika mji wa Sumbawanga na tumehakikisha viko ving’amuzi vya kutosha na tumehakikishiwa kuwa vingine viko njiani kuja mjini Sumbawanga
Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni wa mfumo wa analojia hapa ili kufanikisha zoezi hili.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Machi, 2015 – Sumbawanga

Friday, March 27, 2015

MHE. LUKUVI AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA NYUMBA MPYA ZA MAKAZI ZA NHC MJINI SUMBAWANGA, APOKEA MALALAMIKO MBALIMBALI YA MIGOGORO YA ARDHI KUTOKA KWA WANANCHI WA MKOA WA RUKWA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi wa tatu kulia na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya wa kwanza kushoto wakikagua mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za makazi zinazojengwa na Shirikia la Nyumba la Taifa (NHC) katikati ya Manispaa ya Sumbawanga tarehe 26/03/2015. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Ndugu Nehemia Mchechu nyumba hizo ambazo ni za ghorofa moja zitauzwa baada ya kukamilika ujenzi wake kwa njia ya fedha taslimu na njia ya Mikopo ya benki. 
Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi katikati akiweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa Mjini Sumbawanga kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama na Serikali Mkoani Rukwa tarehe 26/03/2015.
Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi kushoto akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Ndugu Nehemia Mchechu katika hafla fupi ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa nyumba za makazi za shirika hilo Mjini Sumbawanga.
Michoro ya mradi huo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na wananchi (hawapo pichani) wenye malalamiko mbalimbali yanayohusu migogoro ya ardhi Mkoani Rukwa katika ukumbi wa RDC Mjini Sumbawanga tarehe 26/03/2015. Mhe. Lukuvi aliwatangazia wananchi wenye malalamiko sugu wamuandikie wakiambatisha na vielelezo husika na kuviwasilisha kwake ili aweze kuvifanyia kazi, alisema kuwa "..ni muda sasa wa kuponya mioyo ya watu ambao wamezulumika kwa muda mrefu..." Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya. 
Mzee Julius Nkana Mkazi wa Sumbawanga akiwasilisha malalamiko yake ya mdomo na maandishi kuhusu mgogoro wa ardhi kwa Mhe. William Lukuvi. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya Migogoro takribani yote iliyowasilishwa ilionekana kuibuka kutokana na maeneo mengi yasiyo rasmi ambayo hayajapimwa na kupewa umiliki unaotambulika kisheria. Aliongeza kuwa ipo haja kubwa ya Serikali na mamlaka husika kuimarisha eneo la upimaji wa maeneo na kutoa umiliki wa ardhi kuazia viwanja vya makazi na mashamba kuepusha migogoro ya kuzulumiana ardhi ambayo imekua ikiua  kwa kasi siku hadi siku.
Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi kulia akipokea malalamiko ya maandishi ya migogoro ya ardhi kutoka kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa waliopanga mstari katika ukumbi wa RDC.
Zoezi hilo liliambatana na mahojiano mbalimbali ambapo kwa wale wenye malalamiko ambayo kesi zake zipo mahakamani na hazijatolewa uamuzi walishauriwa kuendelea na kesi zao mpaka zitakapomalizika, Ama kwa wale ambao kesi zao zinatatulika zitafanyiwa kazi na Wizara ya ardhi ambapo Waziri husika Mhe. William Lukuvi aliahidi kujibu barua zao za malalamiko, Malalamiko hayo pia yatafanyiwa kazi na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi nyanda za juu kusini, Ofisi ya baraza la ardhi Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimuhoji diwani wa Kata ya Kizwite Ndugu Mavazi (kushoto) kuhusu malalamiko ya muwekezaji Ndugu Azizi Tawaqal (wa pili kushoto) kuhusu madai kuwa wananchi wanamtumia katika kuuza mashamba yaliyonunuliwa na ndungu Aziz Tawaqal licha ya kuwa walishalipwa fidia. Kesi hiyo bado ipo mahakamani na Mhe. Waziri amemuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Sumbawanga (OCD) kusimamia sheria kuhakikisha maeneo hayo hayauzwi na hakuna shughuli yeyote inayoendelea mpaka kesi iliyopo mahakamani ikamilike na kutoa uamuzi.    

Wednesday, March 25, 2015

WAZIRI WA ARDHI MHE. WILLIAM LUKUVI AWASILI MKOANI RUKWA LEO, AAHIDI KUPATIKANA SULUHU YA MGOGORO WA ARDHI WA MUDA MREFU WA SHAMBA LA MALONJE

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwasili katika uwanja wa ndege wa Mjini Sumbawanga leo tarehe 25/03/2013 kwa ajili ya ziara ya siku mbili Mkoani Rukwa moja ikiwa kufuatilia migogoro sugu ya ardhi ukiwemo wa shamba la Skaungu ambapo ameonana na wananchi na viongozi wa vijiji kumi vinavyolizunguka shamba hilo ambalo lina mgogoro wa muda mrefu kati ya Mmiliki Ephata Ministry na wananchi hao. Lengo la pili la ziara yake ni kuweka jiwe la msingi katika nyumba za makazi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katikati ya Mji wa Sumbawanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya (kulia) akimtambulisha Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi kwa viongozi wa Serikali na Chama Mkoa wa Rukwa muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Sumbawanga.
Katika msafara wake Mhe. Waziri aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini Mhe. Aeshi Hillal (Pichani na Mdau Juddy Ngonyani wa Channel Ten), Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe. Ignas Malocha na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng. Stella Manyanya. 
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akizungumza na viongozi wa Vijiji kumi vya kata za Mollo na Msandamuungano vinavyozunguka sahamba la Skaungu lenye Mgogoro wa muda mrefu kati ya muwekezaji Ephata Ministry na wananchi wa vijiji hivyo. Mhe. Waziri amesema lengo la kufika kwake Mkoani Rukwa ni kuona maeneo ya mgogoro huo pamoja na kuwasikiliza wananchi na baadae kuonana na muwekezaji huyo kabla ya Serikali kufanya uamuzi wa hatma ya shamba hilo ambalo linadaiwa na wananchi kumega maeneo ya vijiji na hivyo kukosa maeneo ya kulima kutokana na ongezeko la watu. Alieleza kuwa taarifa zote kuhusu shamba hilo zimeshaifikia ofisi yake na kilichobaki ni kutoa uamuzi wa Serikali wa kumaliza Mgogogoro huo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi alipofika katika Kijiji cha Skaungu kuongea na wananchi alipokelewa na mabango yenye ujumbe mbalimbali unaolenga kuiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa ardhi yao ambayo ipo ndani ya shamba la Muwekezaji Ephata Ministry. Mhe. Lukuvi amewatoa hofu wananchi hao kuwa mgogoro huo utapata ufumbuzi kabla ya Serikali ya awamu ya nne haijamaliza muda wake.
 Ujumbe mwingine uliokuwa kwenye mabango hayo.
Ujumbe mwingine ukinyesha kuwa toka Kijiji hicho kianzishwe mwaka 2008 na kupewa hati wananchi hao wamekuwa hawana haki na sehemu ya ardhi yao ambayo ipo ndani ya shamba la Muwekezaji huyo. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Skaungu muda mfupi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi kuzungumzia lengo la ziara yake katika Kijiji hicho, alisema ni muda sasa kumaliza mgogoro huo.  

 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (kulia) akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Skaungu leo tarehe 25/03/2015. Alisema kuwa mgogoro huo unawanyima usingizi viongozi wa Serikali na imefika wakati sasa kuumaliza. Aliongeza kuwa iwapo Serikali itaamua sehemu ya shamba hilo irudi kwa wananchi basi halitagawiwa kiholela na badala yake utatumika utaratibu maalum kwa kushirikisha Halmashauri na Serikali ya Kijiji kwa kuanza kuwatambua wale wenye hitajio kubwa la ardhi na baadae kuwaangalia wananchi wengine wenye haki ya kupatiwa maeneo hayo.
 Wadau wa Habari Mkoa wa Rukwa wakitoka kuchukua matukio katika Kijiji cha Skaungu, Kutoka kulia ni Juddy Ngonyani (Channel Ten), Nswima Errrrrnest (TBC), Joshua Joel (ITV), Peti Siame (Habari Leo/Daily News), Gurian Adolph Ndingala FM na Mussa Mwangoka (Mwananchi).
 Bi. Anna Msafiri Mwananchi wa Kijiji cha Mawenzusi akitoa kero yake kwa Mhe. Waziri wa Ardhi.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mawenzusi ambao pia walipata fursa ya kupaza sauti zao kwa Waziri wa Ardhi Mhe. William Lukuvi.

Monday, March 23, 2015

MKUU WA WILAYA YA KALAMBO AMUWAKILISHA MKUU WA MKOA WA RUKWA KATIKA KILELE CHA WIKI YA MAJI MKOANI RUKWA KATIKA KIJIJI CHA KINAMBO NA KUZINDUA MRADI WA MAJI KATIKA KIJIJI HICHO

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Willman Kapenjama akikagua chanzo cha Maji katika Kijiji cha Kinambo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji Mkoani Rukwa tarehe 22/03/2015 . Mkuu huyo wa Wilaya alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya ambaye yupo nje ya Mkoa huo kikazi. Chanzo hicho cha Maji kinatumiwa na vijiji vitatu vya Kinambo, Lianza na Maenje ambapo jumla ya vituo 23 vya kuchotea maji vimejengwa katika vijiji hivyo ambavyo vitahudumia zaidi ya kaya 5,304. Mradi huo ambao ni sehemu ya miradi ya maendeleo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) umekamilika ndani ya wakati (Miezi 6 ya Mradi) na umegharimu zaidi ya fedha za kitanzania Milioni 300. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni "Tekeleza sasa kwa Matokeo makubwa"
Washiriki mbalimbali wa Kilele hicho cha Wiki ya Maji walifika kujionea chanzo hicho cha maji ambacho ni cha asili na hakitumii pampu kusukuma maji kutokana na kuwepo eneo la milimani.
 Mhe. Kapenjama akizindua mradi huo wa Maji.
Mradi huo wa Maji ni pamoja na tanki la kuhifadhia Maji lenye ujazo wa lita laki moja.
 Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Willman Kapenjama akihakikisha uwepo wa maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji katika kijiji cha Kanambo.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bi. Emmy George akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Willman Kapenjama kuzungumza na wananchi wa Vijiji vya Kinambo, Lianza na Maenje. Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kuithamini Serikali iliyopo madarakani kwa mchango mkubwa wa kupeleka huduma mbalimbali kwa wananchi wake, hata hivyo aliwaomba kuwa mstari wa mbele katika kutunza mradi huo pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji.
 Kikundi cha Ngoma za asili cha Wasukuma kikitumbuiza katika Maadhimisho hayo.
Mcheza ngoma akitumbuiza kwa staili ya aina yake akiwa ameshikilia pipa kwa mdomo huku akicheza ngoma ya asili ya kikundi cha Kinambo. 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Mhe. Hyporatus Matete akitoa salam za chama katika maadhimisho hayo. Alisema kuwa kazi ya Chama hicho ni kuisimamia Serikali iliyopo madarakani jambo ambalo limekuwa na matunda makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo kwa kiasi kikubwa imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa ambapo ni pamoja na miradi mbalimbali yenye kutoa huduma kwa wananchi.
 Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Clemence Bakuli akitoa salam za Chama katika Maadhimisho hayo.
 Ndugu Shaban Suleiman Mhandisi wa Maji Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa akisoma risala ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maji Mkoani humo.

Friday, March 20, 2015

WAFANYABIASHARA MANISPAA YA SUMBAWANGA WALALAMIKIA KODI MBALIMBALI SERIKALINI, MKUU WA MKOA WA RUKWA ENG. STELLA MANYANYA AWATAKA KUWA WAZALENDO KULIPA KODI KWA HIARI KUJENGA NCHI YAO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akisikiliza risala ya umoja wa wafanyabiashara wa Manispaa ya Sumbawanga iliyokuwa ikisomwa kwake na Mwenyekiti wa umoja huo Ndugu Willington Kiziba Ndyetabura (Kulia). Katika risala hiyo yalikuwepo malalamiko mbalimbali ikiwemo ya matumizi ya mashine za EFD ambapo ni pamoja na gharama kubwa za mataengenezo, Ada ya ukaguzi wa majanga ya moto(Fire), Kupanda mara mbili kwa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wadogo na Ulinzi na Usalama kwa wafanyabiashara. Wafanyabiashara hao walihoji n ivigezo gani vilivyotumika kupandishwa kwa kodi hiyo. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akizungumza na umoja wa wafanyabiashara wa Manispaa ya Sumbawanga tarehe 19/03/2015 katika mkutano wa pamoja wa kusikiliza kero zao mbalimbali uliofanyika katika ukumbi wa Upendo View katikati ya Mji wa Sumbawanga. Wafanyabiashara hao waliomba kuonana na Mkuu huyo wa Mkoa ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka wafanyabiashara hao kuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya Mkoa na taifa kwa ujumla.

 Katika kujibu kero zao mbalimbali alisema kuwa, zile kero ambazo haziwezi kutatuliwa mpaka yafanyike mabadiliko ya sheria atayachukua na kuyafikisha sehemu husika na pindi marekebisho yatakapohitajika yatafanyiwa kazi, aliwataka pia wafanyabishara hao watii sheria mbalimbali za kodi ikiwemo kuchangia ada ya ukaguzi wa majanga ya moto ili kuimarisha jeshi la zimamoto ambalo linahitaji maboresho makubwa kwa usalama wa wananchi na malizao.

Kuhusu hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Rukwa alisema kwa sasa hali ni shwari ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo hivi karibuni wahalifu mbalimbali waliokuwa wakisumbua wamekamatwa. Aliwataka wafanyabiashara hao kuwa walinzi namba moja wa amani katika Mkoa wa Rukwa kwa kutoa taarifa zozote zenye dalili za uhalifu au za watu wanaowatilia mashaka. 
Sehemu ya wafanyabiashara wa Mjini Sumbawanga wakifuatilia moja ya mada katika Mkutano huo.
 Washiriki wa Mkutano huo ambao ni wafanyabiashara wa mjini Sumbawanga.
 Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Rukwa Ndugu John Ernest Palingo akijibu baadhi ya hoja kutoka kwa wafanyabiashara hao. Ndugu Palingo alisema Mashine za EFD zina manufaa makubwa kwa mfanyabiashara kwani pamoja na kutunza kumbukumbu za kibishara pia husaidia makisio sahihi ya kodi kwa mfanyabishara kuepusha makadirio ya juu ambayo hupelekea kumnyonya mfanyabiashara.  
 Sehemu ya wafanyabiashara waliohudhuria katika mkutano huo.
Mmoja ya wafanyabishara akiuliza swali katika mkutano huo.

Thursday, March 19, 2015

MKUU WA MKOA WA RUKWA ENG. STELLA MANYANYA AKAGUA UJENZI WA MRADI WA MAJI SAFI NA MAJI TAKA SUMBAWANGA MJINI

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akipata maelezo ya mradi wa Maji Taka katika Manispaa ya Sumbawanga kutoka kwa Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Sumbawanga (SUWASA) Ndugu Zakaria Ngunda alipofika kutembelea mradi huo tarehe 19/03/2015. Ujenzi wa mradi wa Maji Taka umeshakamilika na kinachosubiriwa hivi sasa ni magari matatu kwa ajili ya kuzolea taka za vyooni zitakazomwagwa katika mtambo huo  ili uanze kufanya kazi. Miradi yote mikubwa ya Maji Safi na Maji Taka Mjini Sumbawanga inagharimu zaidi ya fedha za Kitanzania shilingi bilioni 30.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akizungumza na Wakandarasi wanaojenga mradi Maji Safi na Maji Taka Mjini Sumbawanga ambao ni Techno Fab na Mkandarasi mshauri GKW ambapo amewataka kuongeza kasi kumaliza mradi huo ambao upo nyuma ya wakati. Amemuagiza Mkandarasi anaejenga kukamilisha ujenzi huo kwa kipindi cha miezi miwili ijayo licha ya kuomba kuongezewa muda wa miezi sita ili aweze kukamilisha kazi hiyo. 

Alisema kuwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ni lazima uende na wakati kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati na hivyo kupisha malalamiko ya wananchi kwa Serikali yao. Kwa upande mwingine ameuagiza uongozi wa Maji Safi na Maji Taka Mjini Sumbawanga kumfikishia taarifa za Mkandarasi Herken Builders Ltd aliyojenga mradi wa maji wa visima nane na "pumps" ambazo hazifanyi kazi aweze kumchukulia hatua stakihi ikiwepo kumuandikia barua kuwa hastahiki kufanya kazi katika Mkoa wake wa Rukwa. 
 Mradi wa Bwawa la kuchujia Maji Taka Mjini Sumbawanga ukiwa umekamilika. 
 Sehemu ya Bwawa hilo.
 Sehemu ya Mradi wa Maji Safi ambao ni Chujio la kuchuja Maji Safi kabla ya kwenda kwa walaji.
 Sehemu ya Mradi wa Maji Safi.
Picha nyuma ni sehemu pia ya ujenzi wa mradi mkubwa wa Maji Safi unaoendelea katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.

Friday, March 13, 2015

SHIRIKISHO LA MICHEZO YA WIZARA NA IDARA ZA SERIKALI (SHIMIWI) MKOANI RUKWA LAPATA VIONGOZI WAPYA LEO

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akizungumza muda mfupi kabla ya wagombea wa nafasi mbalimbali wa SHIMIWI Mkoani Rukwa kuanza kunadi sera zao leo tarehe 13/03/2015. Katika salam zake ameahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa SHIMIWI utakaochaguliwa ili kusukuma gurudumu la maendeleo ya michezo Mkoani Rukwa.
Msimamizi wa Uchaguzi Ndugu Erasmus Rugarabamu ambae pia ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa  akitoa maelekezo na taratibu mbalimbali za uchaguzi huo wa kuwachagua viongozi wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Mkoani Rukwa leo tarehe 13/03/2015
Sehemu ya washiriki wa uchaguzi huo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Ndugu David Mlongo akitoa baadhi ya maelekezo kwa washiriki.
Mwenyekiti mpya wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Mkoani Rukwa Ndugu Godfrey Haule akinadi sera zake muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji wa kura kuanza. Mwenyekiti huyo ameshinda kwa jumla ya kura 47 kati ya kura 95 zilizopigwa.
Makamu Mwenyekiti mpya wa SHIMIWI Mkoani Rukwa Ndugu Furahi Kisogole akinadi sera zake muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji wa kura. Mgombea huyu ameshinda kwa jumla ya kura 75 kati ya kura 95 zilizopigwa.
Katibu mpya wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Mkoani Rukwa Ndugu Lusungu Nyagawa akinadi sera zake muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji wa kura kuanza. Mgombea huyu ameshinda kwa jumla ya kura 39 kati ya kura 95 zilizopigwa.
Katibu Msaidizi mpya wa SHIMIWI Mkoani Rukwa Bi. Asha Kanondo Ally akinadi sera zake muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji wa kura. Mgombea huyu ameshinda kwa jumla ya kura 54 kati ya kura 95 zilizopigwa.
Katika nafasi pekee ilyokuwa na mgombea mmoja ni ile ya Mwekahazina ambayo Ndugu Dotto Leonard pichani akinadi sera zake kabla ya uchaguzi ameshinda kwa kura za ndio 89 dhidi ya kura 16 za hapana  kati ya kura 95 zilizopigwa.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa SHIMIWI Ndugu Leonard Mihayo Kariba akinadi sera zake muda mfupi kabla ya zoezi la upigaji wa kura. Mjumbe huyu alishinda kwa jumla ya kura 47 katika kura 95 zilizopigwa.
 Upigaji wa kura.
 Zoezi la upigaji kura. 
Zoezi la uhesabuji wa kura likiendelea.