Friday, April 24, 2015

MFUKO WA CHANGAMOTO ZA MILLENIA (MCAT) YAKABIDHIN RASMI KAMBI YA KIANDA ILIYOPO MKOANI RUKWA KWA CHUO KIKUU CHA SAYANSI NA TEKNOLOJIA MBEYA (MUST)

Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Account - MCAT) Eng. Salum Sasilo (kulia) akimkabidhi funguo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya - MUST Prof. Joseph Msambichaka kama ishara ya makabidhiano rasmi ya kambi ya Kianda iliyokuwa ikitumiwa na Mkandarasi Aasleaf Bam International katika ujenzi wa barabara ya lami kuunganisha Mikoa ya Rukwa na Mbeya katika mradi wa Laela - Sumbawanga wenye jumla ya Kilomita 95. Chuo hicho Kikuu cha MUST kimedhamiria kubadilisha kambi hiyo yenye jumla ya ekari 118 na majengo ya kudumu zaidi ya 18 kuwa moja ya Kampasi zake itakayobobea katika sekta ya uhandisi ujenzi hususani ujenzi wa barabara.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya akitoa salamu zake katika hafla hiyo ambapo ameitaka taasisi ya MUST kuhakikisha kuwa inatunza miundombinu waliyokabidhiwa na kuiendeleza kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu nchini kwa vizazi vilivyopo na vijavyo. Aliongeza kuwa dhamira ya Serikale yake ya Mkoa ilikua ni kuona kambi hiyo inakabidhiwa kwa moja ya taasisi kubwa za elimu nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaamn na taasisi zingine ili kuinua sekta ya elimu nchini lakini imekuwa bahati kwa chuo cha MUST kupata nafasi hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya chuo chao na elimu kwa ujumla. Amekiomba Chuo hicho kuona uwezekano wa kuipa Kampasi hiyo ya Kianda jina la Rukwa kwa ajili heshma ya maeneo hayo ambayo yapo Mkoani Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga. 
Meza kuu.
 Miongoni mwa nyumba ndogo ndogo za makazi ambazo zipo ndani ya kambi hiyo.
Sehemu ya washiriki katika hafla hiyo ya makabidhiano kutoka Mkoani Rukwa na Mbeya.
 Picha ya pamoja.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya katikati akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya - MUST Prof. Joseph Msambichaka kulia na Meneja Mradi wa Kampuni ya Aasleaf Bam International iliyojenga barabara ya Lami ya Laela - Sumbawanga Ndugu Russel Rourke muda mfupi baada ya zoezi la makabidhiano ya kambi hiyo ya Kianda.

Thursday, April 16, 2015

EWURA YAENDESHA SEMINA KWA WAFANYABIASHARA WA MAFUTA MIKOA YA RUKWA NA KATAVI MJINI SUMBAWANGA

Meneja Ufundi Idara ya Petroli EWURA Ndugu Gerald Maganga akiwasilisha moja ya mada katika Semina kwa Wafanyabiashara wa Mafuta Mikoa ya Rukwa na Katavi katika ukumbi wa Moravian Centre Mjini Sumbawanga tarehe 15 April 2015. Kushoto ni Afisa Uhusiano EWURA Ndugu Wilfred Edwin. Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika Semina hiyo ni Udhibiti na Kanuni za Ukokotoaji wa bei za Mafuta, Ubora wa Miundimbinu, Usalama na Utunzaji wa Mazingira katika Sekta ya Mafuta ya Petroli, Faida za kutumia Mafuta yenye kiwango kidogo cha Sulphur na Sheria na Kanuni katika udhibiti wa Sekta ya Petroli nchini.
Afisa Biashara Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ndugu Paul Nganyanyuka akichangia moja ya mada katika Semina hiyo ya EWURA na wafanyabiashara ya mafuta Mikoa ya Rukwa na Katavi iliyofanyika katika Ukumbi wa Moravian Centre mjini Sumbawanga tarehe 15/04/2015.
 Sehemu ya wajumbe katika Semina hiyo ambao ni wafanyabishara wa vituo vya mafuta Rukwa na Katavi, Mtoa huduma Serikalini GPSA na Maafisa Biashara kutoka Mikoa ya Rukwa na Katavi.

Monday, April 13, 2015

NAMNA YA KUOKOA NYUMBA ISIUZWE KWA KUSHINDWA KULIPA MKOPO.

Image result for MAHAKAMA

NA  BASHIR  YAKUB-

Wakopaji  nao  wana  haki  zao.  Yapo  mambo  ya  msingi  ambayo  wanapaswa  kuyajua    ili  yawalinde  iwapo  mambo  yamewaendea    vibaya.  Ukweli  ni  kuwa    ni  busara  unapokopa  kulipa deni    lakini    iwapo sababu   za  kibinadamu  zimejitokeza  ambazo  ziko  nje  ya uwezo  wa mkopaji  na  ambazo  kwa  namna  yoyote  hawezi  kuzizuia  basi   ni  vema  mkopaji  awe  na  njia ya  kujiokoa  yeye  pamoja  na  mali  yake.

 Uwepo  wa  sababu  za  kibinadamu  zinazoweza  kumzuia  mtu  kulipa  deni  ndizo    zilizopelekea  kuwapo  baadhi ya  mambo  katika  sheria ambayo    humlinda  mkopaji  pamoja  na  mali yake   ikiwa  ameshindwa  kulipa  mkopo  au  amechelewa  kwa  mujibu  wa  makubaliano.  Si  kweli kuamini  kuwa  mtoa  mkopo   ndiye  mwenye  ulinzi  wa  sheria  peke  yake,   hapana  hata  mkopaji  naye  anao  ulinzi  wa  sheria  ikiwa  mambo  yatamwendea  vibaya  kama  tutakavyoona.  Kwanza  tuangalie  sababu   za  kibinadamu  ambazo  zinaweza  kumfanya  mkopaji  ashindwe  kulipa   deni  kwa  wakati.

1.SABABU  ZINAZOWEZA  KUMFANYA  MKOPAJI  ASHINDWE   KULIPA  DENI.

 ( A )  MATENDO  YA  MUNGU ( Acts  of  God ).

Matendo  ya  mungu  hujumuisha  magonjwa/ugonjwa  ambao   huweza  kumsababisha  mtu  ashindwe  kabisa    kuendelea  na  biashara  kwa  namna  yoyote  ile. Mtu  hawezi  kuwa  amelazwa   na  hajitambui au  anajitambua  lakini  ugonjwa  wake  ni  mkubwa ( serious)  halafu  ukategemea  afanye  biashara  na  arejeshe  deni  kwa  wakati.  

Ni  jambo  ambalo    haliingii  akilini. Ugonjwa  ni  matendo  kati  matendo  ambayo   husababishwa  na  mungu  na   yako  juu ya uwezo  wa mwanadamu  yeyote.  Zaidi,  matendo  ya  mungu  hujumuisha    vitu  kama  mafuriko,  matetemeko  ya  ardhi,  ukame,  vimbunga,  na  kila  kitu  ambacho  hakiwezi  kusababishwa  na  mwanadamu.  Ni  vigumu  mkopaji  kurejesha  deni  iwapo  moja  ya matendo  haya  yameikumba   biashara  yake.

(  B  )   AJALI   ISIYOZUILIKA  (  innevitable  accident) .

Ajali  ni  ajali  suala  la   msingi  ni  kuwa  ajali  isiwe  imesabaabishwa  kwa makusudi  na  mkopaji  ili  akwepe  kurejesha  deni.  Kwa  mfano  juzi  tumeshuhudia  ajali ya  basi  lililoangukiwa  na  lori    njia  ya  mbeya.  Mle  ndani  walikuwamo  watu    wana biashara  zao  ambazo  zimetokana    na  mkopo  na  nyingi  zimepotea  kabisa. Katika  mazingira  yanayotambulika  kama  hayo    hakuna  namna  ambavyo  unaweza  kulazimisha  kuuza  nyumba/kiwanja  cha  mtu   eti  kwakuwa  amechelewa  kulipa  ilihali  kilichomchelewesha  kinajulikana. 

Hiyo  ni  ajali  isiyozuilika    na  lazima  watoa  mkopo  waizingatie.  Pia  tulishuhudia  ajali    za  meli  kule  Zanzibar ambazo  lazima  ndani  yake   walikuwamo  wafanybiashara   wakiwa  na  biashara   za  fedha  za  mikopo. Itakuwa  sio  sawa  kuharakia   kuuza   dhamana  ya  mfanyabiashara  kama  huyu    wakati  sababu   iliyomchelewesha  kurejesha  ikiwa  wazi.  
Vita  ndani  ya  nchi  pia  huingia  katika  ajali  isiyozuilika   na  ni  sababu  ya  msingi  ya  kuzingatia    iwapo  mkopaji  ameshindwa  kurejesha  mkopo.

( C )  SABABU  ZA   KIDOLA/KIUTAWALA.  (Executive  Authority ).

Kwa  mfano  mkopaji  ameweka   biashara  yake  mahali  fulani  halafu  serikali   ikaja  na  sera  ya  kumuondoa  eneo  lile   kwa  lengo  la  kuweka  mradi  fulani  kwa  ajili  ya  taifa,  au  serikali  imebadili    utaratibu  wa  fedha    ghafla  kwa  kuongeza  viwango  vya  riba  tofauti  na   vile  alivyokopea  mkopaji  au mabadiliko  yoyote  ya   kisera  ambayo  moja  kwa  moja  yanaathiri  kwa  kiwango  kikubwa    biashara    na  mkopo  wa  mkopaji.  Sababu  hii  itakuwa  nje  ya  uwezo  wa  mkopaji  na  yafaa  izingatiwe  kabla  ya  kuchukua  hatua  yoyote  ya  kuuza  mali  yake.

( D ) SABABU  ZITOKANAZO  NA  SHERIA/MAHAKAMA (  statutory/judicial  acts).

Yawezekana  mtu  amechukua  mkopo  lakini  wakati  akiendelea  na  biashara  amehukumiwa  kifungo  au  hajahukumiwa  lakini  yupo  rumande  na  hana  dhamana.  Mtu  huyu  ni  vigumu  kurejesha  mkopo.  Au   mtu  amefungua  biashara   lakini  kuna  matatizo  ya  kisheria yamejitokeza  na  mahakama  imetoa  amri  ya  kumzuia  kuendelea  na  biashara  au  amri  ya  kulifungia  eneo  lake  la  biashara. Pia   mtu kama  huyu  hututarajii  arejeshe  mkopo  kwa  wakati  kwa  sababu  zilizo  nje  ya  uwezo  wake.

2.NAMNA  YA  KUOKOA  NYUMBA/KIWANJA  KISIUZWE  KWA  KUSHINDWA/KUCHELEWA  KULIPA  MKOPO.

Ikiwa  zipo  sababu za  msingi  za  kushindwa/kuchelewa  kulipa  mkopo  kama  nilizotaja  hapo  juu   basi   waweza  kuzuia  nyumba/kiwanja  chako  kisiuzwe. Njia  kubwa ,  nzuri  na  ya  uhakika  ni  mahakama. Utaratibu  wake  ni  kuwa    utafungua  kesi  mbili  yaani  ndogo  na  kubwa. 

Katika  kesi  kubwa  utakuwa    ukieleza   kilichotokea  kwa  ukamilifu  mpaka  ukashindwa   kulipa  deni   na  ndani  ya  kesi  ndogo   utakuwa  ukiomba  nyumba/kiwanja  chako  kisiuzwe  kwakuwa  wewe si  msababishaji  wa  kilichotokea.  Kesi  ndogo  itafunguliwa  chini  ya  hati  ya  dharula(  certificate  of  urgency)   ili  iweze  kusikilizwa  kwa  muda  mfupi    na  kutolewa maamuzi   ili  kuwahi  wauzaji  kabla  hawajauza. Maamuzi  ya  kesi  ndogo    yaweza  kutolewa  hata    ndani  ya  siku  moja  kutegemea  na  udharula  wenyewe.

Zingatia  kuwa  ikiwa  thamani  ya mkopo  au   eneo  linalotaka  kuuzwa  inaanzia  milioni  arobaini  na  moja  kwenda  mbele    kesi  itafunguliwa  mahakama    kuu    na  ikiwa  chini  ya  hapo  itafunguliwa    baraza  la  ardhi  na  nyumba  la  wilaya.  Pia  zingatia  kesi  ya  namna  hii  hufunguliwa   katika  wilaya    lilipo   hilo  eneo  linalotaka  kuuzwa.  Kwa  kufuata  utaratibu mzuri   waweza kuokoa  nyumba/kiwanja  chako  kisiuzwe  kwa  kuwa  hiyo  nayo  ni  haki  yako  kama  mkopaji.


MWANDISHI   WA   MAKALA  HII   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

Thursday, April 2, 2015

WADAU WA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA MATIBABU MKOANI RUKWA WAPEWA ELIMU YA UTARATIBU WA MIKOPO MBALIMBALI INAYOTOLEWA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa akichangia na kufunga Semina maalum ya siku moja iliyoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwaelimisha wadau wa vituo mbalimbali vya kutolea huduma za matibabu Mkoani Rukwa juu utaratibu wa Mfuko huo katika kutoa mikopo ya vifaa tiba, dawa na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za matibabu. Lengo kuu la utaratibu huo ulioanzishwa na Mfuko wa Bima ya Taifa ni kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake na watanzania kwa ujumla. Semina hiyo imefanyika leo tarehe 02/03/2015 katika ukumbi wa RDC Mkoani Rukwa, Ndugu Pangisa amewaasa wadau hao kuchangamkia fursa hiyo kuimarisha huduma katika vituo vyao.
 Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Rukwa Ndugu Abdiel Mkaro akizungumza katika semina hiyo. Ndugu Mkaro alisema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeanza utaratibu wa kuwakopesha wadau mbalimbali wanaotoa huduma za matibabu Mkoani Rukwa, lakini jambo la kushangaza wengi wao wamekuwa hawatumii fursa hiyo vizuri kwani baadhi yao wamediriki hata kutofuatilia maombi yao na kutelekeza barua zao ambazo wameshakubaliwa. Aliwaasa wadau hao kutumia fursa hiyo ili kuboresha huduma katika vituo vyao.
Mtoa mada mkuu katika Semina hiyo ndugu Yesaya Irira (Kulia) ambaye ni Afisa Mipango na Uwekezaji Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Makao Makuu akizungumza katika Semina hiyo ambapo amesema mikopo hiyo inatolewa kwa vituo vyote vya Serikali, vya Binafsi na vya Kidini kwa kigezo kikuu kuwa kituo hicho kiwe kimesajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutoa huduma kwa wanachama wake. Aliongeza kuwa miongoni mwa taratibu za kupewa mkopo ni pamoja na Mkopaji kujaza fomu ya maombi ambapo kiwango cha Mkopo kitategemea wastani wa madai ya kituo kwa huduma zitolewazo kwa wanachama wa Bima ya Afya ambayo pia yatakuwa dhamana kuu ya Mkopo husika katika madai ya kila mwezi. Kwa Mkopo unaozidi Milioni tano Mkopaji atatakiwa kuweka dhamana yenye thamani ya mkopo na kwa upande wa mkopo wa kifaa tiba hufanyika kuwa dhamana ya mkopo mpaka marejesho ya Mkopo yatakapokamilika.
 Dkt. Dunstan Tendwa, Afisa Mhakiki wa Ubora wa Huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Rukwa akiwa na wadau wengine walishiriki semina hiyo.
 Wadau kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia semina hiyo.
 Bi Safi Julius, Afisa Mipango na Uwekezaji Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na wajumbe wengine waliohudhuria semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa RDC Mkoani Rukwa.
 Sehemu ya wajumbe katika semina hiyo.
Sister Helena Katebela wa Kituo cha Afya Katandala akiuliza swali katika Semina hiyo. Alitaka kujua endapo dawa anazohitaji Mkopaji hazipo kwa wakala wa usambazaji ambaye ni MSD itakuwaje? Alipata jibu kuwa mkopaji huyo ataelekezwa kwa msambazaji mwingine aliyejiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afta tofauti na MSD.